Monday, September 22, 2014

Tamko la CHADEMA Kuhusu Migomo na Maandamano ya Amani

TAMKO LA CHAMA JUU YA UTEKELEZAJI WA AZIMIO LA MKUTANO MKUU KUHUSU MIGOMO NA MAANDAMANO YA AMANI NCHI NZIMA

Ndugu waandishi wa habari

Tunapenda kuanza mkutano huu kwa kutoa salaam za amani kwa Watanzania wote, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Amani Kimataifa, ambayo huadhimiswa Septemba 21, ya kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu kama ilivyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ni ‘The Right Of People’s to Peace’.

Tumekutana nanyi hapa siku hii mahsusi ya kuazimisha amani kimataifa, tukiwa na ujumbe maalum kwa Watanzania kuwaeleza namna ambavyo watawala wa Serikali ya CCM, wanavyohatarisha amani ya nchi yetu kwa kuvunja haki za msingi za Watanzania huku pia wakififisha matumaini ya wananchi.

Tunataja maneno hayo mawili HAKI na MATUMAINI kwa makusudi kabisa kwa sababu hayo ndiyo ndiyo msingi wa amani na utulivu wa kweli mahali katika taifa ambalo linajali na kuzingatia maendeleo na ustawi wa wananchi wake.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere katika moja ya hotuba zake kali kuonesha namna ambavyo walioko madarakani wanahatarisha amani na utulivu wan chi, aliwahi kusema kuwa ni hatari sana iwapo wananchi wakipoteza matumaini kwa viongozi wao huku pia hawaoni haki ikitendeka. Mwalimu alikwenda mbali na kusema Watanzania watakuwa ‘wapumbavu’ wakikubali viongozi waendelee kwenda kinyume na maslahi au matakwa ya wananchi wao.

Kama wananchi hawapati haki na wanapoteza matumaini na viongozi wao, hakuwezi kuwa na amani na utulivu. Itabaki amani inayoimbwa na CCM majukwaani wakati haki za msingi ndani ya nchi zikiminywa na kukiukwa.

Ni vigumu kuwa na amani au utulivu wa dhati iwapo haki za kisiasa (mf; kukutana, kuandamana n.k), haki za kiuchumi (kuwa na maisha bora) haki za kijamii (kupata elimu bora na bure, matibabu bora na bure, maji safi na salama), n,k, huku ufisadi na ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma, ukiongezeka na UWAJIBIKAJI ukiwekwa kapuni.

Ndugu waandisi wa habari, ninyi pia ni mashahidi wa namna ambavyo utawala huu wa CCM ambao umeshapoteza kabisa ushawishi wa kisiasa kwa wananchi, umezidi kuminya haki ya kupata taarifa huku pia ikiendelea kutumia sheria za kikoloni kuminya uhuru wa habari nchini.

Hali hii imewafanya waandishi makini wanaozingatia miiko na maadili ya taaluma yao, kuwa wahanga wa vitendo viovu vya watawala, wakiwemo askari polisi kama ilivyodhihirika hivi karibuni mbele kabisa ya milango ya wakubwa wa Jeshi la Polisi na Wizara ya Mambo ya Ndani. Ikiwa ni mwendelezo wa matukio ya namna hiyo ambayo yalifikia hatua ya juu pale askari walipomuua kikatili Mwandishi Daudi Mwangosi, Septemba 2, 2012, huko Nyololo, Iringa.

Tungependa pia kutumia nafasi hii Siku ya Amani Kimataifa, kuwatia moyo ninyi waandishi wa habari kuendelea kutekeleza wajibu wenu wa kijamii (social responsible journalism) kwa kuzingatia maslahi na matakwa ya wananchi, tukiungana na Watanzania wengine wanaothamini na kutambua uhuru wa habari kama moja ya mihimili muhimu katika ujenzi wa demokrasia na hatimaye maendeleo na ustawi wa wananchi wote.

CHADEMA inaungana na Watanzania wote ambao wako sambamba nanyi katika kuheshimu wajibu, majukumu na taaluma yenu, hususan katika kipindi hiki ambapo vyombo vya habari na waandishi wanaojipambanua kwa umakini wa kuwatumikia Watanzania, kama ilivyo kwa watu wengine makini kwenye makundi mbalimbali ya kijamii, wanalazimika kupitia kwenye ‘bonde la kifo’ linalotengenezwa na watawala waliopoteza uhalali na ushawishi wa kisiasa, wakikabiliwa na hofu ya anguko kubwa kutoka madarakani.

Katika siku hii ya leo, tukiunganisha na mfululizo wa matukio ya vyombo vya dola kugeuka kuwa adui wa raia na mali zao, ikiwemo kushambulia waandishi wakiwa kazini, tunao wajibu wa kuwataka watawala kutambua wajibu wa kitaaluma na uhuru wa waandishi wa habari kwa ajili ya kuweka misingi ya amani na utulivu unaotokana na haki na matumaini.

CHADEMA ni moja ya wadau wa habari ambao wameweka saini kukubaliana na Azimio la Dar es Salaam Juu ya Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji (DEFRI), ambalo iwapo Serikali ya CCM ingekuwa imelikubali, kulithamini na kulizingatia, leo hii lingeweza kuwa moja ya nyaraka zinazotutambulisha duniani kama taifa linalotukuza haki, matumaini, uhuru na uwajibikaji kwa ajili ya wananchi.

Tumeomba kukutana nanyi leo ili tuweze kutoa kauli juu ya Siku ya Amani Kimataifa, sambamba na yanayoendelea kuhusu Azimio la Mkutano Mkuu wa Chama; kufanya maandamano na migomo ya amani nchi nzima isiyo na ukomo kupinga ufisadi unaofanywa na Bunge Maalum la Katiba, kupinga uchakachuaji wa maoni ya wananchi unaoendelea kufanyika mjini Dodoma na uvunjifu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Katika muktadha huo wa Siku ya Amani Kimataifa, tungependa kuelezea uhalali wa maandamano na migomo hiyo ya amani kama ifuatavyo;

Maandamano; Haki na Wajibu wa kikatiba;

Kwanza kabisa, Watanzania wote wanawajibika kwa mujibu wa Katiba ya Nchi, Ibara ya 27 (1)-(2), ambayo inasema;

“(1) Kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano, mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na wananchi, na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

(2) Watu wote watatakiwa na sheria kutunza vizuri mali ya mamlaka ya nchi na ya pamoja, kupiga vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu, na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Azimio la Mkutano Mkuu wa Chama la kufanya maandamano na migomo ya amani nchi nzima lilizingatia takwa hili la Katiba ya Nchi. Kinachoendelea huko Dodoma ni uharibifu na ubadhirifu wa mali na rasilimali za umma. Ule ni ufisadi. Kwa sababu Katiba Mpya haitapatikana kwa namna ile bunge linavyoendelea Dodoma. Hata Rais Jakaya Kikwete amekubali hilo mbele ya viongozi wenzake. Ni wajibu wetu sote kupinga Bunge la Katiba kuendelea.

Pamoja na ubovu wake ilionao, Katiba ya Nchi, katika Ibara ya 20 (1), imetoa haki kwa mtu au watu kuwa huru kukutana, kuchanganyika na kushirikiana na watu wengine kutoa mawazo hadharani.

Mikutano ya hadhara, migomo na maandamano hayo ya amani ya CHADEMA ni sehemu ya mikusanyiko, ambayo ni haki ya kikatiba ya kila mtu au kikundi cha watu.

Mbali ya haki hiyo kuwekwa bayana kwenye Katiba ya nchi, upo utaratibu ambao umewekwa wa kuhakikisha haki hiyo inatekelezwa na wanayoitaka katika kuhakikisha wanatoa mawazo yao kupitia mikusanyiko ya aina mbalimbali.

Utaratibu ambao unavihusu vyama vya siasa mahsusi umefafanuliwa vizuri kisheria, kupitia Sheria ya Vyama vya Siasa ya Mwaka 1992, kifungu cha 11 ambacho kinasema hivi;

“11. —(1) Every party which has been provisionally or fully registered shall be entitled-a) to hold and address public meetings in any area in the United Republic after giving notification to the police officer in-charge of the area concerned for purposes of publicizing itself and soliciting for membership;”

“…(4) When a political party is desirous of holding a meeting or procession in any open public place in any area it shall, not less than forty eight hours before the meeting, submit a written notification of its impending to the police officer in charge of the area in which the meeting is to take place is situated.

(5) The written notification referred to in subsection (4) shall specify—a) the name of the political party submitting the notification; b) the place in and time at which the meeting is to take place; c) the agenda or purpose in general of the meeting;”.

Ndugu waandishi wa habari Vipo vifungu vingine kwenye Police and Auxiliary Service Act ambavyo navyo vinaweka utaratibu wa kisheria kwa makundi mbalimbali ya kijamii, vikiwemo vyama vya siasa, kutekeleza haki hiyo, ambapo kifungu cha 43 (1) kinasema;

“Any person who is desirous of convening, collecting, forming or organizing any assembly or procession in any public place shall, not less than forty eight hours before the time when the assembly or procession is scheduled to take place, submit a written notification of his impending assembly or procession to the police officer in charge of the area specifying; (a) the place and time which the meeting is to take place, (b) the purpose in general of the meeting; and (c) such other particulars as the Minister may from time to time, by notice published in the Gazette, specify.”

Taarifa zote za CHADEMA ambazo zimetolewa kwa ajili ya mikutano, migomo na maandamano ya amani kwa Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali kwenye ngazi za majimbo, wilaya na mikoa zimezingatia wajibu wa kikatiba, matakwa ya kisheria.

Wakati watu wetu wakitimiza matakwa ya kisheria, Jeshi la Polisi kupitia barua mbalimbali, mbali ya kukiri kuwa maandamano yetu ni ya amani, limekuwa likitoa amri ambazo hazina msingi wa kisheria kuzuia mikutano na maandamano hayo. Raia mtiifu kwa nchi yake hawezi kutii amri isiyotokana na msingi wa kisheria. Kwa sababu ni batili.

Hivyo tunapenda kuwataarifu kuwa maandamano yetu ya kupinga ufisadi, uchakachuaji kwenye mchakato wa Katiba na uvunjwaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba yako pale pale kuanzia kesho Jumatatu, Septemba 22 na kuendelea itakuwa ni wiki ya maandamano.

Ni vyema utaratibu huu tukaueleza na ueleweke vyema kwa sababu Jeshi la Polisi nchini linatumia mamlaka lisilokuwa kikatiba wala kisheria, kuzuia haki ya kikatiba ya wananchi kukusanyika na kuandamana dhidi ya jambo ambalo linafanyika kinyume na maslahi au matakwa ya wananchi.

Wanachama wetu katika maeneo mbalimbali kama ambavyo tutawaonesha kwa ushahidi hapa wa barua, wamefuata utaratibu huo wa kisheria ambao unawataka kuwasilisha barua za TAARIFA kwa Jeshi la Polisi, kuwataarifu polisi kuhusu kusudio la kufanya mkutano au kuandamana.

Tunaomba kusisitiza kuwa barua hizo ni za kutoa TAARIFA. Si kuomba KIBALI.

Pamoja na wanachama wetu katika maeneo mbalimbali ya nchi kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi, bado wamekataliwa kutekeleza wajibu na haki yao hiyo ya kikatiba kwa kisingizio cha kunyimwa KIBALI.

Neno KIBALI, limekuwa likitumiwa na Jeshi la Polisi katika hali ile ile ya matumizi mabovu ya madaraka na mamlaka wasiyokuwa nayo kisheria wala kikatiba. Hakuna mahali popote kisheria ambapo wananchi au chama cha siasa kinatakiwa kuomba kibali ili waweze kukusanyika au kuandamana.

Jambo la pili ambalo tungependa kuzungumza hapa ni kusisitiza kuwa tunaendelea na uratibu wa maandamano ya nchi nzima, ambayo sasa tumepanga yaendelee kuanzia kesho Jumatatu.

Tunafanya hivyo kwa sababu ni wajibu na haki yetu ya kikatiba, baada ya kuwa tumefuata utaratibu wa kisheria ambao ni kutoa taarifa kwa mamlaka husika. Tunapenda kuwaambia Jeshi la Polisi kuwa matumizi ya neon hilo ‘kibali’ ni ubatili kisheria na si sahihi kutii amri isiyokuwa na msingi katika sheria.

Kulaani kupigwa waandishi wa habari

Tunatumia fursa hii, kwa mara nyingine tena, kutoa kauli ya chama kulaani kwa nguvu zote kitendo cha Jeshi la Polisi kupiga waandishi wa habari waliokuwa wakitimiza wajibu wao siku ya Alhamis wakati Mwenyekiti wa Chama Taifa, Freeman Mbowe alipoitikia wito wa jeshi hilo.

Kitendo hicho cha askari wa Jeshi la Polisi kuwashushia kipigo waandishi wa habari mbele ya macho, masikio na milango ya wakubwa wa jeshi hilo na Wizara ya Mambo ya Ndani, ni wazi kimetupeleka hata nyingine katika kutaka mabadiliko makubwa ya kimfumo na kisheria kuhusu utendaji na usimamizi wa Jeshi la Polisi nchini.

Kitendo hicho kinachopaswa kulaaniwa na kila mpenda demokrasia na maendeleo, anayeamini katika uhuru wa maoni na fikra mbadala, kilitokea siku moja tu baada ya Makamu wa Rais (mkuu wa nchi kwa wakati huu) kuwa amekutana na Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini pamoja na Vyombo vya Dola, akitoa wito kuwepo na maelewano kati ya pande hizo mbili wakati wa utekelezajiwa majukumu yao.

Tangu juzi tumemtaka Makamu wa Rais kujitokeza hadharani kuuambia umma wa Watanzania kama alitoa maelekezo mengine baada ya kuachana na wanahabari, ambayo ndiyo yaliyotekelezwa na askari siku iliyofuata!

Tumemtaka pia IGP Ernest Mangu kutoa kauli ya hatua zipi amechukua hadi sasa dhidi ya matukio mbalimbali ya askari polisi kushambulia waandishi wakiwa kazini, huku tukimkumbusha tukio la kuuwawa kikatili kwa Daudi Mwangosi katika mazingira yale yale kama ya juzi Makao Makuu ya Polisi.

Ikiwa ni sehemu ya hatua za haraka, tunawashauri vyombo vya habari nchini vikiwa kama mhimili wa nne, kuchukua hatua zifuatazo katika kuupigania mhimili huo upate hadhi na heshima unayostahili;

1. Kufuatilia na kuhakikisha kwa hatua za kinidhamu zimechukuliwa dhidi ya wale wote waliohusika katika kuwashambulia na kuwapiga waandishi wa habari walipokuwa kazini wakitimiza wajibu wao.

2. Kufungua mashtaka; private prosecution kama sheria inavyoelekeza.

3. Kukusanya ushahidi wa wazi uliopo na kufungua kesi za madai, kudai fidia.

Imetolewa leo Septemba 21, 2014 na; Kigaila Singo Benson Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda

Maandamano ya CHADEMA, Bunge la Katiba, na Polisi

Kwa muda wa siku kadhaa, tumesikia kuhusu azma ya CHADEMA kufanya maandamano katika nchi nzima kupinga vikao vinavyoendelea Dodoma kwenye Bunge la Katiba. CHADEMA inasema kuwa kuendelea kwa vikao hivi ni ufujaji wa fedha za wananchi.

Sehemu mbali mbali za nchi, polisi wamekuwa wakifanya juu chini kuzuia maandamano hayo kwa sababu hii au ile. Walioko kwenye hilo Bunge, polisi, na waziri mkuu Mizengo Pinda, wanaendelea kudai kuwa vikao hivi vya Bunge ni halali kwa mujibu wa sheria.

Wazo hili limenifanya nami niandike kifupi mtazamo wangu. Kama raia wa Tanzania, ninayo haki sawa na raia wenzangu, kutoa maoni kuhusu suala hilo na masuala mengine yanayohusu nchi yetu. Wale wanaodhani kuwa kwa vile ninafanya kazi Marekani, na nimekaa huku kwa miaka mingi, basi nimechukua uraia wa Marekani, napenda kuwaambia kuwa dhana hii haina ukweli wowote.

Sijawahi kuwazia kuchukua uraia wa Marekani wala nchi nyingine yoyote. Kwa hivi, nina haki sawa na m-Tanzania aishiye Dar es Salaam, Korogwe au Tunduru kujiingiza katika masuala yanayohusu nchi yetu. Nina haki ya kupigania haki Tanzania, ninapoona haki inakiukwa.

Hii hoja kwamba vikao vinavyoendelea Dodoma ni halali kisheria siipingi. Lakini ni sherti tuzingatie pia kuwa kama ni sheria tu, hata utawala wa makaburu ulikuwa umejengeka katika misingi ya sheria. Ndio maana, waliopinga ukaburu, yaani ANC, PAC, na wengine; akina Nelson Mandela, Robert Sobukwe, na wengine, walionekana wahalifu.

Vikao vinavyoendelea Dodoma ni halali kisheria, lakini hoja ya wapinzani, hasa CHADEMA, kwamba vikao hivi ni ufujaji wa hela za wananchi, ni hoja muhimu.  Wao wanaongelea suala la haki na maslahi ya umma. Panaweza pakawa na jambo ambalo ni sawa kisheria, kama ilivyokuwa wakati wa ukaburu, lakini sheria hiyo ikawa haiendani na haki wala maslahi ya umma.

Polisi wa Tanzania wanapozuia maandamano ya CHADEMA ya kupinga vikao vinavyoendelea Dodoma wanafanya kosa. Kuendelea kwa vikao sio sababu ya kuwazuia watu kutumia uhuru na haki yao ya kuandamana kwa amani.

Polisi wanaposema vikao vinavyoendelea Dodoma ni halali kisheria watambue pia kuwa wananchi bado wana haki zao, ikiwemo haki ya kuandamana kwa amani. Polisi hawana sababu ya kuhujumu haki hiyo, kama wanavyofanya.

Polisi wanapaswa wazingatie kuwa katika nchi yoyote inayoheshimu haki za binadamu, wajibu wa polisi ni kuweka ulinzi kwenye mikutano na maandamano ya amani, ili kuhakikisha kuwa wahusika wanayo fursa kamili ya kutumia haki yao ya kukutana na kuandamana kwa amani. Huu ndio ustaarabu.

Inasikitisha kuwa mambo yanaenda kinyume Tanzania, kwani tumefikia mahali sasa ambapo polisi wamejitwalia jukumu la kutoa vibali vya mikutano na maandamano. Hiyo sio kazi yao. Hawana wadhifa wa kuingilia uhuru na haki ya watu ya kukutana na kuandamana kwa amani. Ila wana wajibu wa kulinda amani kwenye mikutano na maandamano.

Kinachokubalika ni kimoja, kwamba wanaoandaa wawafahamishe polisi kabla ya mkutano au maandamano kwa mujibu wa sheria, ili polisi waende wakaweke ulinzi. Kama kuna watu wanataka kuvuruga mikutano au maandamano, ni wajibu wa polisi kuwashughulikia hao wavurugaji, sio kuwashughulikia wanaokutana au kuandamana kwa amani.

Sunday, September 21, 2014

Jibu Langu kwa "Anonymous" Aliyenikosoa Leo

Hapa naleta maoni ya "anonymous," aliyoyatoa leo kwenye taarifa niliyoleta jana kuhusu dhuluma za polisi dhidi ya waandishi wa habari.  Taarifa niliyoweka hii jana ni hii hapa. Baada ya maoni ya "anonymous", nami nimejaribu kuweka jibu langu chini yake, ikashindikana. Kwa hivi, nimeweka hapa maoni yale ya "anonymous" na jibu langu. Mdau karibu ujisomee: ----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------- Anonymous said...

Naona na wewe umejiunga katika kundi la wanaharakati ambao wanajiita waandishi. kwa taarifa yako huyo Isango anafanya kibarua (sio ajira rasmi) gazeti la Tanzania Daima na huyo Badi pia anapeleka picha (si muajiriwa rasmi kwa muda mrefu tu, sababu hazijulikani) na wote walikuwa wanakaidi amri halali ya polisi. Nani kasema uhuru wa habari hauna mipaka? Mbona nyie huko Snowden na wikileaks hamuwaachii wafanye watakalo? Babu usijivunjie heshima yako ndogo uliyonayo
Anonymous said...
Tanzania Daima, kukuongezea tu, ni la Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema. Hata mwangosi hakuwahi kuwa mwandishi wa habari (hakuwa na taaluma kama walivyo badi na Isango) bali ni mwanaharakati kama ambavyo wewe unataka kuelekea

-------------------------------------------------------------------------------------------------------------------------

Anonymous, kwanza nikushukuru kwa kufika hapa kwenye blogu yangu, kusoma taarifa, na kuweka maoni.

Taarifa niliyoleta sikuiandika mimi, wala picha sio zangu. Mwishoni mwa taarifa ile, nimetaja chanzo: "Maisha Times." Mjumbe hauawi.

Taarifa za polisi kuwapiga waandishi ziliripotiwa katika magazeti na blogu mbali mbali, na pia katika televisheni,na kila mahali ilisemwa kuwa polisi waliwapiga waandishi. Umejaribu kuelezea kuwa Isango na Badi si waandishi, kwa msingi kuwa si waajiriwa rasmi.

Kigezo cha kuwa mwandishi sio kuajiriwa au kuajiriwa rasmi. Wako pia wanaofanya uandishi bila kuajiriwa. Mimi mwenyewe ni mfano hai, kwani nimeandika katika magazeti ya Tanzania na ya Marekani, bila kuajiriwa nayo.

Katika mazingira haya, jina "waandishi," linawajumlisha  hata wapiga picha na wanablogu kama walikuwepo.

Hoja yako ya kuwaweka kando akina Isango na Badi, eti kwa vile hawajaariwa rasmi na eti kwa vile Badi anapeleka picha haina uzito.

Hao waandishi waliopigwa na polisi walivunjiwa haki zao za kibinadamu, ambazo zimeelezwa katika tangazo la kimataifa la haki za binadamu (ki-Ingereza tangazo hili hujulikana kama "The Universal Declaration of Human Rights"). Soma kifungu hiki:

Article 19.
•Everyone has the right to freedom of opinion and expression; this right includes freedom to hold opinions without interference and to seek, receive and impart information and ideas through any media and regardless of frontiers.

Kwa wale ambao hawajui ki-Ingereza, kifungu hiki kinatamka kuwa kila binadamu anayo haki ya kujieleza na kutoa mawazo yake, na haki hii inajumlisha pia haki ya kuwa na mawazo au mtazamo bila kuzuiwa, na anayo haki ya kutafuta, kupata, na kusambaza taarifa, mawazo na mitazamo kwa kutumia vyombo vyovyote bila mipaka. Hapa nimetumia neno vyombo nikimaanisha magazeti, televisheni, blogu, redio na kadhalika.

Tangazo halisemi mtu awe ana ajira rasmi kama mwandishi ndipo aweze kutafuta na kusambaza habari. Isango na Badi wanayo hiyo haki, sawa na wewe na mimi.

Kuhusu mipaka ya uhuru wa habari, binafsi, sipendi kuwawekea watu mipaka. Naheshimu uhuru wa kila mtu kujiwekea mipaka yeye mwenyewe. Hata kwenye hizi blogu zangu, yaani hii ya "hapa kwetu" na ile ya ki-Ingereza, naweka maoni yoyote ambayo watu wanaleta. Sijawahi kuzimisha maoni ya mchangiaji yeyote. Ninachozingatia ni kuwa mtu amejaribu kujenga hoja, na pia kuwa watu hupishana kwa akili na ufahamu.

Ndio maana hata mawazo yako nimeyaweka hapa, ingawa sikubaliani nayo. Kuna wengine wamewahi hata kujenga hoja za kunikebehi au kunitukana, lakini sikuwazimisha, ingawa uwezo wa kufanya hivyo ninao. Ningekuwa siheshimu haki hiyo, ningeweza hata kuweka blogu zangu katika mfumo ambao hauruhusu maoni. Ziko blogu za namna hiyo, lakini kwangu milango iko wazi.

Iwapo mtu anaona mwandishi amevuka mpaka, tunazo njia za kistaarabu za kushughulikia suala hilo. Kwa mfano tunazo mahakama.

Kama polisi waliona waandishi wa habari wamevunja sheria, au wamekaidi hicho unachokiita "amri halali," wangewakamata na kuwafikisha mahakamani. Picha zinaonyesha kabisa kuwa hao akina Isango walishakamatwa na polisi, na haingekuwa vigumu kuwapeleka mahakamani.

Lakini polisi waliamua kutumia njia isiyo ya ustaarabu, yaani kuwapiga. Huu si ustaarabu. Polisi wanavunja haki za binadamu, wanajifedhehesha, na wanaifedhehesha nchi.

Unasema, katika sentensi yako ya kwanza kuwa mimi nimejiunga na kundi la wanaharakati wanaojiita wandishi. Mimi siwajui hao unaowaita wanaharakati. Sijajiunga, na sihitaji kujiunga nao.
Nina historia yangu; nimeelimishwa na kujielimisha hadi nikafikia mtazamo nilio nao sasa, na kadiri ninavyoendelea kujielimisha, ninaweza nikafikia kuwa na mawazo tofauti. Ni uhuru wangu na haki yangu.

Sikuanza leo kutetea haki za waandishi. Kwa mfano, mwaka ule kitabu cha Dr. Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai kilipopigwa marufuku na serikali ya Tanzania, nilipinga sana kitendo cha serikali, hasa huko mtandaoni. Na nilikuwa nafanya hivyo nikijitambulisha kwa jina langu kamili, wala sikuandika kama "anonymous." Nilitetea haki ya Hamza Njozi ya kutoa mawazo na fikra zake.

Tafuta kitabu alichoandika Njozi baada ya hicho cha Mwembechai, utaona kuwa katika "Utangulizi" amenishukuru kwa kutetea haki yake.

Msimamo wangu ulikuwa kwamba kama serikali haikuafiki aliyoandika Njozi, basi iandike kitabu chake, na kama polisi hawakuafiki, nao waandike kitabu chao, na yeyote mwingine mwenye msimamo tofauti anaandike kitabu chake. Katika hali hii ya mawazo na fikra mbali kukutanishwa au kugonganishwa, ukweli utajitokeza.

Siafiki dhana yako ya kuwapa polisi wadhifa wa kutuwekea mipaka ya uhuru wetu wa kutafuta habari na kuzisambaza. Hali hii itakuwa ni janga kubwa.
Kuhusu Mbowe kumilikia gazeti la "Tanzania Daima," ni jambo la kumshukuru, kwani anatoa fursa ya watu kupata na kupashana habari, mitazamo, na taarifa, kama linavyoelekeza tangazo la kimataifa nililonukuu hapa juu. Ungekuwa mtu mwenye ufahamu, ungetambua hilo.

Kuhusu Snowden, mimi sina mamlaka yoyote kuhusu mambo ya aina hii hapa Marekani. Kwa vile sio raia wa nchi hii, na sijawahi hata kuwazia kuwa raia, sipigi kura. Mpiga kura angalau ana uwezo fulani, ingawa ni mdogo sana, wa kuathiri mwelekeo wa nchi yake.

Binafsi, namshukuru Snowden na WikiLeaks, kwa kufichua uovu katika siasa na uongozi wa nchi. Wenye visa na Snowden na WikiLeaks ni wale wanaotawala nchi, na ndio wenye mamlaka, sio mimi.

Nimalizie na usemi wako kwamba nisijivunjie heshima. Kati yako na mimi, ni nani anayejivunjia heshima? Wewe unayewapa polisi wadhifa wa kutuamulia mipaka ya uhuru wetu, au mimi ninayezingatia tangazo la kimataifa la haki za binadamu?

Saturday, September 20, 2014

Dhuluma za Jeshi la Polisi Tanzania Kwa Waandishi wa Habari


 Askari wa Jeshi la Polisi wa kuzuia ghasia wakiwazuia kwa mbwa Waandishi wa habari kufanya kazi yao.


Askari wa Jeshi la Polisi wa kuzuia ghasia wakimpa kipigo cha mbwa mwizi Mwandishi wa habari Bwn. Josephat Isango


Muendelezo wa Jeshi la Polisi nchini kuwanyanyasa, kuwatisha waandishi wa habari na kuwafanya wasitekeleze wajibu wao ipasavyo, ilijidhihirisha wazi jana makao makuu ya jeshi hilo, baada ya waandishi kupigwa, kukimbizwa na mbwa ili wasichukue taarifa za kuhojiwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Tukio la kupigwa na kudhalilishwa kwa waandishi wa habari lilitokea jana, limetokea ikiwa ni siku moja baada ya Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama nchini kushirikiana na waandishi wa habari katika kufanya kazi kwa ajili ya kulinda amani ya nchi.
Waandishi waliyopigwa na Polisi hiyo jana ni Josephat Isango anayeandikia gazeti la Tanzania Daima huku Yusuph Badi ambaye ni mpiga picha wa magazeti ya serikali, akipigwa na ‘kusakiziwa’ mbwa ili wamuume.
Dalili za waandishi wa habari kuzuiwa kufanya kazi yao zilianza kujionesha mapema jana wakati Mbowe alipowasili katika makao makuu ya Jeshi la Polisi, ambako waandishi walizuiwa wasiingie katika eneo hilo kwa ajili ya kuchukua picha na maelezo ya kiongozi huyo.
Akiwa anawaongoza askari wake katika amri ya kushambuliwa kwa waandishi wa habari hiyo jana, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, Paul Chagonja, alisikika mara kwa mara akiwaagiza vijana wake wawaondoe waandishi na hata kuwasakizia mbwa.
Chagonja, alisikika mara kadhaa akitoa amri kwa askari kuwa wawafungulie mbwa ili waweze kujeruhi angalau mtu mmoja kutoa funzo ili wafuasi wa CHADEMA waliokuwa kwenye lango kumsubiri Mbowe waondoke.
“Waondoeni wote msiwaruhusu hata hao waandishi kuingia humu, ninyi askari wa mbwa mnafanya nini hapo wakati watu wamejazana mlangoni wapelekeeni hao,” alisikika akisema Kamishna Chagonja.
Mara baada ya maelekezo hayo ya Kamishna Chagonja, askari waliokuwa na mbwa walianza kuwakimbiza wafuasi wa CHADEMA na waandishi wa habari.
Katika hali ya kustaajabisha, askari watatu kwa pamoja walimfuata Josephat Isango, aliyekuwa akitoka katika lango kuu na kuanza kumshambulia kwa rungu na mateke hali iliyowafanya waandishi wa habari kuingilia kati kwa ajili ya kumnusuru.
Baada ya waandishi kumnusuru Isango, kipigo kiligeukia kwa Mwandishi Yusuph Badi, ambaye wakati akishambuliwa alianguka chini huku askari wenye mbwa wakiwaachia kwa ajili ya kumshambulia.
Kilichomnusuru Badi asiumwe na mbwa hao ni kamera aliyoishika mkononi na kujikinga ili asidhurike, kitendo hicho cha kujikinga kilisababisha kuharibika kwa kifaa hicho.
Wakizungumza baada ya hali kutulia, Badi na Isango, walieleza kuwa kilichofanywa na jeshi la Polisi ni kuminya uhuru wa utendaji kazi wa waandishi katika kuuhabarisha umma wa watanzania juu ya mambo yaliyokuwa yakitokea.
“Ni jana tu wameambiwa namna ya kutoa ushirikiano na vyombo vya habari, lakini leo wanatupiga na kutusakizia mbwa hii si haki na viongozi wetu wanapaswa waangalie mara mbili mbili namna ya kushirikiana na jeshi hili,” alisema Badi.
Jeshi la Polisi limekuwa na kawaida ya kuwanyanyasa, kuwapiga na hata kuwaua waandishi wa habari pale wanapotekeleza wajibu wao wa kukusanya habari.
Tukio linalokumbukwa zaidi la ukatili wa askari wa jeshi hilo kwa waandishi wa habari ni mauaji ya Mwandishi wa kituo cha Televisheni ya Chanel ten mkoani Iringa, Daudi Mwangosi, mauaji yaliyotokea Septemba 2 mwaka juzi katika Kijiji cha Nyololo Mufindi mkoani Iringa wakati mwandishi huyo akiwajibika kukusanya habari.

CHANZO: Blogu ya MAISHA TIMES

Sunday, September 14, 2014

Wa-Kenya Walitia Fora Tamasha la Afrifest

Tarehe 2 Agosti, lilifanyika tamasha la Afrifest, katika mji wa Brooklyn Park, Minnesota. Tamasha hili hufanyika kila mwaka, likijumuisha wa-Afrika na watu wenye asili ya Afrika waishio Marekani, visiwa vya Caribbean, America ya Kati na Kusini, na sehemu zingine, na pia watu wasio wa-Afrika au wa asili ya Afrika. Wote hao hushiriki, kwa lengo la kufahamiana, kuelimishana, na burudani.

Tamasha huanzia siku moja kabla, jioni, kwa burudani ya muziki, maonesho ya mavazi na kadhalika. Hivyo ndivyo ilivyokuwa tarehe 1 Agosti. Siku inayofuata, tamasha hufanyika nje uwanjani. Kunakuwepo na mabanda ya wafanya biashara, pia watoa huduma mbali mbali. Kunakuwepo muziki, michezo ya watoto, na mechi ya soka. Ndivyo ilivyokuwa mwaka huu kule Brooklyn Park.

Mwaka huu, wa-Kenya walijitokeza kwa wingi kuliko wa-Afrika wa nchi nyingine yoyote. Palikuwa na meza ambapo paliwekwa bidhaa na vitu mbali mbali kutoka Kenya. Bendera ya Kenya ilipepea siku nzima. Ilifurahisha kuona wenzetu walivyoonyesha umakini katika kuitangaza nchi yao.

Jambo hili lilitajwa katika mkutano wa Bodi ya Afrifest Foundation. Mimi mwenyewe nilikuwa na meza ambapo nilikuwa nimeweka vitabu na machapisho yangu mengine. Kati ya watu waliofika hapo mezani walikuwepo wa-Kenya.

Mimi na binti zangu tunakumbuka, kwa mfano, jinsi kijana mmoja alivyofika hapo mezani, akaongea nasi kwa ki-Swahili. Alionekana kijana wa kawaida tu, nasi tulidhani ni mmoja wa wale wanaotaka kuelewa shughuli zangu, kuhusu vitabu vyangu, na kisha wanaenda kwenye meza au mabanda mengine. Bila sisi kutegemea, alinunua vitabu vitatu kabla ya kuondoka.

Thursday, September 11, 2014

Kitabu Kimeingia Katika Chuo Kikuu cha Cincinnati, Marekani

Pamoja na mengine yote, blogu hii ni mahali ninapohifadhi kumbukumbu za shughuli zangu mbali mbali, hasa zile ninazofanya katika jamii, nje ya chuo ninapofundisha. Kumbukumbu hizi ni pamoja na taarifa kuhusu namna vitabu vyangu vinavyotumika katika jamii.

Miezi kadhaa iliyopita, niliona taarifa mpya, ila sikupata fursa ya kuiweka katika blogu hii. Taarifa yenyewe ni kuwa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimependekezwa kwa wanafunzi katika chuo cha matibabu cha Chuo Kikuu cha Cincinnati kilichopo katika jimbo la Ohio, hapa Marekani.

Profesa wa programu ya kupeleka wanafunzi Ghana, Dr. Jason Blackard, ambaye picha yake nimeiweka hapa kushoto, ndiye aliyekipendekeza kitabu hiki--pamoja na vingine vitatu--akiwataka wanafunzi kuwa kila mmoja achague kitabu kimojawapo, akisome, halafu aandike ripoti fupi kielezea aliyojifunza. Taarifa hizi zimo katika "syllabus" yake ya programu hiyo ya Ghana.

Simfahamu profesa huyu, na wala hatujawahi kuwasiliana. Ningekuwa na mawasiliano naye, ningependa kujua alizipataje taarifa za kitabu hiki. Najua taarifa ziko tele mtandaoni, lakini najua pia mara kwa mara watu hupata taarifa kutoka kwa wenzao waliokisoma kitabu. Kwa vile nina dukuduku ya kujua, huenda nikawasiliana na profesa huyu.

Tuesday, September 9, 2014

Viongozi wa Afrifest Foundation

Kama wewe ni mtembeleaji wa blogu yangu hii ya hapakwetu au ile ya ki-Ingereza, utakuwa umesoma taarifa zangu kuhusu Afrifest, taasisi iliyoanzishwa hapa Minnesota, Marekani, na makao yake ni hapa hapa.

Hapa kushoto tunaonekana baadhi ya viongozi tunaoendesha Afrifest. Kulia kabisa ni Nathan White, kutoka Liberia, ambaye nikatibu mtendaji wa Afrifest, na ndiye ambaye alianzisha wazo zima la Afrifest, kama anavyoelezea hapa.

Katikati naonekana mimi, m-Tanzania, ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya Afrifest. Nimekuwa mshiriki wa Nathan White tangu mwanzo, pamoja tukapanga na kuendesha tamasha la kwanza la Afrifest, mwaka 2007. Tulipopiga picha hii, afya yangu ilikuwa dhaifu kuliko sasa. Sikumbuki kama maishani mwangu nimewahi kupigwa picha inayonionyesha nikicheka namna hii.

Kusohto kabisa ni Wycliff Chakua, kutoka Kenya. Yeye alijiunga na Afrifest miaka michache iliyopita. Ndiye mweka hazina wa Afrifest.

Tulipiga picha hii tarehe 2 Agosti, wakati wa tamasha la Afrifest lililofanyika Brooklyn Park, Minnesota. Niliandika habari za tamasha hilo mara kadhaa, kwa mfano hapa, hapa, na hapa. Tunao wanabodi wengine ambao hawakuweza kuhudhuria tamasha hili, lakini tuko pamoja katika kushughulikia malengo ya Afrifest ya kuwaunganisha, kuwaelimisha, na kuwaburudisha watu wenye asili ya Afrika popote walipo ulimwenguni, na watu wengine wote wenye mtazamo huo au wanaotaka kufahamu zaidi mambo tunayoyashughulikia.

Kazi zetu katika Afrifest ni za kujitolea. Lakini tunafurahi kuzifanya, na furaha inakuwa kubwa tunapoona jinsi jamii inavyofaidika na shughuli zetu. Utumishi huu kwa jamii unatupa fursa ya kufahamiana vizuri sisi wenyewe na pia kufahamiana na wadau wanaohudhuria matamasha na matukio mengine ya Afrifest. Karibuni kwenye matamasha na matukio haya. Karibuni pia mtutembelee katika Facebook.

Sunday, September 7, 2014

Ninasoma "Shalimar the Clown," Riwaya ya Salman Rushdie.

Salman Rushdie ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa wanaoandika katika ki-Ingereza. Kwa uandishi wake, amepata tuzo zinazoheshimika sana, kama vile "Booker Prize."

Mimi ni mwalimu wa fasihi ya ki-Ingereza. Mara moja moja ninafundisha kozi ya "South Asian Literature," yaani fasihi ya Asia ya Kusini. Katika kozi hii, ninafundisha maandishi ya watu kama Rabindranath Tagore, R. K. Narayan, Raja Rao, Mulk Raj Anand, Anita Desai, Michael Ondaatje, na Salman Rushdie.

Haiwezekani kusoma au kufundisha maandishi yote. Vile vile, kazi mpya za fasihi zinaendelea kuchapishwa. Kwa hivi, kila ninapofundisha kozi ya namna hii, najua kuwa katika orodha yangu kuna waandishi ambao hawamo. Kuna kazi muhimu za fasihi ambazo hazimo. Huu ndio ukweli, ingawa haupendezi.

Uchaguzi wowote wa waandishi au maandishi ambao ninafanya kwa kufundishia katika muhula fulani wa masomo una utata na unazua masuali. Nilipofundisha kozi ya "South Asian Literature" kwa mara ya kwanza, Salman Rushdie hakuwemo. Nilijiuliza kama hii ni sahihi.

Hatimaye, nilianza kutumia maandishi ya Rushdie. Nilianzia na riwaya yake maarufu ya Midnight's Children. Hii sio riwaya rahisi kuisoma, lakini wanafunzi wangu nami tulifanya bidii tukaimaliza. Salman Rushdie anaandika ki-Ingereza ambacho kina mvuto wa pekee, ingawa sio rahisi, kwa mbinu za kila aina. Anadhihirisha ufahamu mkubwa wa ki-Ingereza, falsafa, fasihi, dini, siasa, na tamaduni mbali mbali. Msomaji unajikuta katika kazi kubwa ya kufikiri na kukabiliana na chemsha bongo mbali mbali.

Midnight's Children ilinipa hamasa ya kutumia maandishi ya Rushdie. Muhula huu wa masomo ambao ulianza wiki iliyopita, nitatumia riwaya yake ya Shalimar The Clown. Sikuwa nimeisoma riwaya hii, bali nimeanza, katika kujiandaa kuifundisha. Panapo majaliwa, hapo tutakapokuwa tumemaliza kuisoma na kuijadili, nitaandika habari zake katika blogu hii. Ila napenda kutoa tahadhari kuwa dhana ya kumaliza kusoma kazi yoyote ya fasihi sio dhana yenye ukweli. Ingawa tunaitumia dhana hii, tunajidanganya.


Friday, September 5, 2014

Leo Nimeanza Tena Kufundisha

Baada ya kuumwa kwa miezi mingi, na kuwa katika likizo ya matibabu, leo nimeanza tena kufundisha. Hali yangu inaendelea kuimarika, na ingawa naendelea na matibabu kidogo kidogo, madaktari wameridhia ombi langu kuwa nirudi darasani. Wameniwekea sharti kuwa nisibebe mzigo mkubwa wa kozi za kufundisha, na nisihusishwe na shughuli nyingine ambazo walimu huzifanya, kama vile ushiriki katika kamati mbali mbali na mikutano. Hiyo picha hapa kushoto nimejipiga mwenyewe leo, baada ya kutoka darasani.

Hali itakuwa hiyo kwa muhula mzima, ambao umeanza leo, na utamalizika katikati ya mwezi Desemba. Ninafundisha kozi mbili, ya kwanza ni "South Asian Literature," na ya pili ni "Writing." Katika hiyo kozi ya kwanza, ambayo niliitunga miaka michache iliyopita, nafundisha riwaya kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Riwaya hizo ni, Untouchable, iliyoandikwa na Mulk Raj Anand (India); Twilight in Delhi, iliyoandikwa na Ahmed Ali (India); The Crow Eaters, iliyoandikwa na Bapsi Sidhwa (Pakistan); Shalimar the Clown, iliyoandikwa na Salman Rushdie (India); na Reef, iliyoandikwa na Romesh Gunesekera (Sri Lanka).

Ninapangia kufundisha pia mashairi kutoka katika nchi hizo. Kwa wakati huu, katika kujiandaa, ninasoma kitabu cha mashairi ya Michael Ondaatje kiitwacho The Cinnamon Peeler. Michael Ondaatje alizaliwa Sri Lanka, ila anaishi Canada. Ninafanya pia uchunguzi wa vitabu vya mashairi ambayo nitaweza kuyatumia. Kila ninapofundisha kozi hii, nabadilisha, kwa kiasi fulani, vitabu au waandishi.

Fasihi ya hiyo sehemu ya dunia imejengeka katika historia, siasa, dini, tamaduni, na harakati za watu wa kule tangu miaka elfu tano au zaidi iliyopita hadi kwenye kipindi cha ukoloni, na baada ya kupata uhuru. Waandishi wengi wa India na Pakistan, kwa mfano, wanaelezea janga kubwa lililotokea kabla tu ya kupata uhuru na wakati nchi ilipogawanyika na kuwa nchi hizi mbili, mwaka 1947.

Katika kozi ya "Writing," ninafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza. Kadiri miaka ilivyokwenda, nami kujijengea uzoefu zaidi na zaidi wa kufundisha kozi hii, nimekuwa nikitafuta mbinu mpya za kufundisha. Leo nimewaambia wanafunzi kuwa, tofauti na miaka yote iliyopita, na tofauti na wanavyofanya waalimu wengine, muhula huu tutatumia vitabu viwili tu. Kitabu kimoja ni The Trickster, kilichoandikwa na Paul Radin, na kingine ni The Elements of Style, kilichoandikwa na William Strunk Jr. na E.B. White.

Lengo langu katika hii kozi ya uandishi ni kuwafundisha kwanza kabisa namna ya kuandika sentensi bora kabisa ya ki-Ingereza, kama alivyoelekeza mwandishi maarufu Ernest Hemingway, na baada ya hapo tutaendelea hadi kuweza kuandika insha bora kabisa. Nimewaeleza wanafunzi kwamba uandishi bora ni jambo la lazima kwa mafanikio maishani mwao, nikatoa mifano mbali mbali ya namna watakavyohitaji uwezo wa kuandika ipasavyo. Wameona uzito wa hoja na mifano niliyotoa.

Nimefurahi kuwa nimefikia hali ya kuweza kuingia tena darasani, nikizingatia hali yangu kiafya ilivyokuwa mbaya kabla sijalazwa hospitalini. Kwa mara nyingine tena, namshukuru Mungu, na nawashukuru madaktari na wauguzi, familia yangu, marafiki, na wote wanaonitakia mema. Mungu awabariki wote.

Wednesday, September 3, 2014

Matamasha Ninayoshiriki ni Kama Shule

Matamasha ninayoshiriki ni muhimu. Ni kama shule. Ninabadilishana mawazo na wadau mbali mbali. Kuna ambayo ninawaeleza na kuwaelimisha, na wao kuna ambayo wananieleza na kunielimisha. Kuna masuali na majibu, au angalau maelezo, kwa upande wao na wangu.

Hapa kushoto naonekana niko katika mazungumzo mazito na jamaa mmoja kutoka Liberia, aitwaye Ahmed. Tumefahamiana kwa miaka kadhaa. Hapo tulikuwa katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park.



Ninapata fursa ya kukutana na watu wa aina aina. Hapa kushoto niko na mama mmoja ambaye alionekana mkimya, lakini alikuwa na dukuduku ya kujua moja mawili. Ilikuwa katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park.









Hapa kushoto nilikuwa katika mji wa Brooklyn Park, na wa-Marekani Weusi wawili. Huyu aliyekaa pembeni yangu tulikuwa tunafahamiana, lakini huyu mwenye kofia ilikuwa ni mara ya kwanza kukutana. Ilikuwa katika tamasha fulani lililoandaliwa na taasisi ya wa-Afrika, inayoshughulikia masuala ya afya.

Huyu mwenye kofia alikuwa mtu asiye na papara katika kuzungumza, bali mwenye tafakari nzito. Unaweza kujionea jinsi tunavyomsikiliza kwa makini.




Shughuli zangu sifanyii Marekani tu. Hapa kushoto nilikuwa Diamond Jubilee Hall, mjini Dar es Salaam, katika tamasha lililoandaliwa na Tripod Media.

Ninaonekana nikiwahamasisha watoto wa shule kuhusu kufanya bidii shuleni,  nikiwapa mfano wangu mwenyewe na hatua niliyofikia maishani. Kuwaambia watoto kama hao kwamba juhudi niliyofanya shuleni imeniwezesha sasa kuwa mwalimu na mwandishi wa vitabu ni namna ya kuwahamasisha wazingatie shule.



Hapa kushoto niko na jamaa wawili, Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam, katika tamasha la Tripod Media nililotaja hapa juu. Kama unavyoona, tuko katika mazungumzo mazito.










Hapa kushoto, katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park, naonekana nikipata mawili matatu kutoka kwa bwana Bolstad, ambaye alizaliwa na kukulia Tanzania, na wazazi wa-Marekani. Ingawa sasa anaishi Marekani, anajisikia kama m-Tanzania, na ki-Swahili anaongea vizuri sana.

Yeye nami tumefahamiana kwa miaka mingi kidogo, na naguswa na jinsi anavyokipigia debe kwa watu mbali mbali kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Watu wa aina yake wanachangia katika kunifanya niwe na ari ya kuandika zaidi, kwa faida ya walimwengu.

Tuesday, September 2, 2014

Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania Kuhusu Katiba Mpya

Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu Katiba Mpya

JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA

TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA


Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:

Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya Maoni ya WANANCHI kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila.

Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume. Tume pia iliweza kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na Maoni yote
yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa Rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya WANANCHI.

Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda KIZALENDO na, kwa mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni MARIDHIANO na si jambo la maslahi ya kisiasa, bali ni suala la maslahi ya WANANCHI.

Tunaamini kuwa kila Mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya WANANCHI aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.

Baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa WANANCHI, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili:

Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa mbalimbali ambazo WANANCHI hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa Bungeni na kilichomo katika Rasimu na viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na kwa maslahi ya nani?

Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu. Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya WANANCHI.

Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake. Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa KATIBA NI MATOKEO YA TENDO LA MARIDHIANO NA SI SUALA LA MASLAHI YA KIKUNDI CHA WATU WACHACHE.

Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na maslahi ya Chama Tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;

1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.

2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na Chama Tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.

3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.

4. Kwamba baada ya Bunge Maalum la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.

5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.

6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.

Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.

Ifahamike kuwa WANANCHI wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe WANANCHI wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu Chama hicho kimeyapuuza na kimekataa Maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi.

“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenyekuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)

IKUMBUKWE KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NI WARAKA HALALI NA RASMI NA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA KATIBA NI YA WANANCHI NA INAHITAJI MARIDHIANO NA SIO UBABE.

Imetolewa leo Agosti 28, 2014
Na MKUTANO WA JUKWAA LA WAKRISTO
Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT)
Christian Council of Tanzania (CCT) The Seventh Day Adventists (SDA)

CHANZO: Wavuti

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...