Tuesday, August 4, 2015

Mwandishi Seenaa Aongelea Kitabu Chake Mjini Minneapolis

Juzi Jumapili, nilipata ujumbe wa Facebook kutoka kwa rafiki yangu Peter Magai Bul wa Sudan aishiye Chicago kwamba kuna rafiki yake mwandishi, Seenaa Godana-Dulla Jimjimo, anakuja Minneapolis kuongelea kitabu chake, The In-Between: The Story of African-Oromo Women and the American Experience. Jana, baada ya kumaliza kufundisha na kupumzika kidogo nilikwenda Minneapolis kumsikiliza mwandishi huyu.

Ukumbi ulijaa watu, na karibu wote ni wa-Oromo wanaoishi hapa Minnesota. Nilifurahi kuonana na wanawake wawili na mwanamme mmoja ambao niliwahi kuwafundisha hapa chuoni St. Olaf. Tulifurahi kukutana.

Walikuwepo wazungumzaji watatu ambao waliongelea masuala yanayowahusu wa-Oromo kama vile ukandamizwaji wanaofanyiwa na jeshi la Ethiopia, harakati zao za ukombozi dhidi ya Ethiopia, unyanyaswaji na ukandamizwaji wa wanawake katika jamii ya wa-Oromo. Mzungumzaji mmojawao aliongelea juu ya mwandishi Seenaa na kitabu chake.

Baada ya hapo, mwandishi Seenaa alikaribishwa kuongea. Alielezea mambo muhimu yalyoathiri maisha yake, msukumo alioupata kwa mama yake katika elimu, kujitambua na kujiamini. Aligusiia umuhimu wa wa-Oromo kujituma katika kupigania haki zao na haki na usawa kwa wanawake, akawasihi viongozi wa dini wawe mstari wawemo katika kuihamasisha jumuia katika harakati hizo.  Kufuatia maongezi hayo, mwandishi alijibu masuali ya wasikilizaji.

Hatimaye mwandishi alikaribishwa kusaini vitabu vyake. Watu wengi tulijitokeza tukapanga foleni ya kununua vitabu ili kusainiwa. Nilipokaribia mezani, wanafunzi wangu walinizuia kulipia kitabu, wakalipia wao. Wakati wa kusaini, mwandishi alifurahi sana kuniona, kwani alishaelezwa habari zangu na Peter Magai Bul. Tulifurahi, tukapiga picha kabla na baada ya kusaini.

Nimeanza kukisoma kitabu. Nina hamu ya kujua mawazo na mtazamo wa dada huyu kuhusu masuala yanayowahusu wa-Oromo kuanzia kwao Oromia hadi huku ughaibuni. Inavyoonekana, kwa mujibu wa utangulizi wa kitabu, mwandishi anakwenda mbali ya kuwaongelea wa-Oromo tu. Kwa mfano, kuhusu suala la haki za wanawake, anawaongelea wanawake kwa ujumla, si wa-Oromo tu.

Niliguswa kuona jinsi shughuli ya kukutana na mwandishi na kuongelea kitabu ilivyowavutia watu wengi namna hii. Nilivutiwa na usikivu wao kwa wazungumzaji na masuali waliyouliza. Imenifanya nitambue kuwa hao wenzetu wameelimika na wanathamini elimu. Nimebaki ninajiuliza iwapo wanadiaspora wa ki-Tanzania tuna mwamko huo huo.

2 comments:

mandela pallangyo said...

napenda sana mwaalimu anavyoshirikisha mawazo. napenda sana unapokuwa karibu na waandishi wengine. inatupa hamasa. napenda sana kuandika lakini naona siku za karibuni nitaachana na fani hii kisha niendelee kuchimba madini

Mbele said...

Ndugu Mandela Pallangyo,

Shukrani kwa ujumbe wako. Ninajisikia vizuri kuongea na waandishi chipukizi na kuwapa yale ambayo nayafahamu, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii. Huyu dada Seenaa niliyemwongelea hapa alifurahi sana kukutana nami ile siku tulipokusanyika kusikiliza maongezi juu ya kitabu chake. Alikuwa ameambiwa na yule Peter wa Chicago habari zangu.

Siku ya pili yake, yaani tarehe 5, Seenaa nami tulikutana tena, tukaongea kirefu. Nilipata wasaa wa kumhamasisha kwa hili na lile, hasa kwa vile nilishaanza kusoma kitabu chake. Baadaye, yeye, dada mwingine, na mimi tulienda kuangalia mechi ya kabumbu kati ya timu za wa-Oromo. Tulizungumza kirefu zaidi.

Kwa mawazo yangu, Seenaa atakuja kuwa maarufu katika uandishi na katika harakati za ukombozi, hasa ukombozi wa wanawake. Ni jasiri. Anatoka katika familia ya ki-Islam, lakini amekuwa akipambana na mila desturi ambazo zinadaiwa kuwa ni za ki-Islam, lakini yeye anaziona ni kipingamizi kwa haki za wanawake.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...