Monday, August 24, 2015

Nimeimba Wimbo wa Taifa (Tanzania) Mjini Faribault

Juzi tarehe 22 Agosti, katika tamasha la kimataifa mjini Faribault, Minnesota, kulikuwa na muda wa wawakilishi wa nchi mbali mbali kuandamana hadi kwenye jukwaa kuu wakiwa wamebeba bendera za nchi zao. Baada ya kufika jukwaani, kila mmoja alipata fursa ya kusema machache kuhusu nchi yake na bendera yake, na wengine waliimba wimbo wa taifa lao.

Niliweka historia kwa kubeba bendera ya Tanzania, kusema machache kuhusu Tanzania, na kuimba wimbo wa Taifa. Pichani hapa kushoto ninaonekana nikiwa jukwaani na bendera yangu.

Kitendo hiki cha kuiwakilisha Tanzania hakijawahi kutokea mjini Faribault. Wala mimi sijawahi kusimama jukwaani mbele ya umati wa watu, iwe ni Tanzania au kwingineko, na kuimba wimbo wa Taifa peke yangu. Kutokana na upekee wa tukio hili, nimeona niweke kumbukumbu katika hii blogu yangu.

Niliwahi kuandika katika blogu hii nilivyoamua kununua bendera ya Tanzania ili niweze kuitumia katika matamasha na shughuli zingine hapa Marekani. Kwa kuwa katika tamasha la mwaka jana Faribault sikuwa na bendera, niliamua kuitafuta, kwa ajili ya baadaye.


Siku chache kabla ya tamasha la tarehe 22 Agosti nilimfahamisha mratibu wa tamasha kuwa tayari ninayo bendera. Aliniambia kuwa tayari wamepata bendera ya Tanzania.

Nilishangaa na kufurahi kwa mpigo. Niliona wamefanya heshima kubwa kwa Tanzania, nikizingatia kuwa walikuwa wanatarajia kuwa na bendera za nchi ishirini.

Hata hivi, siku ya tamasha, yaani hiyo juzi, nilibeba bendera yangu. Nilipofika kwenye uwanja wa tamasha, niliona wameshatundika bendera, zinapepea. Kwa hivi, yangu nilibaki nayo.

Bendera ya Tanzania pia ilikuwepo, ila kulikuwa na kasoro moja katika kuifunga mlingotini. Upande wa bluu ulikuwa juu, na upande wa kijani ulikuwa chini.

Kwa namna bendera zilivyofungwa, haikuwa rahisi kurekebisha. Na sikuwajulisha waandaaji dosari hiyo, kwa kuzingatia moyo wao wa kuienzi Tanzania. Niliamua kuwa nitatafuta wasaa muafaka, siku zijazo, kuwaelekeza namna ya kuitundika bendera yetu mlingotini.

Siku nzima katika tamasha, nilikuwa na furaha kuiona bendera yetu ikipepea hapo uwanjani, sambamba na bendera za nchi zingine. Niliandika taarifa zaidi katika blogu yangu ya ki-Ingereza.

Ninafanya mambo ya aina hii kwa ajili ya kuwaelimisha watu huku ughaibuni na kujifurahisha mwenyewe. Kama mtu mwingine yeyote, nami nina mambo ninayoyaona muhimu katika maisha yangu, na pia mambo yanayoniletea raha maishani. Hilo suala la bendera ya Taifa, kama nilivyolielezea, naliona kwa mtazamo huo. 

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...