Monday, August 7, 2017

Global Minnesota Wameniletea Kifuta Jasho

Juzi, tarehe 5, niliandika katika blogu hii kwamba nilikuwa nimepata barua ya shukrani kutoka Global Minnesota, kufuatia mhadhara niliotoa. Leo, bila kutegemea, nimepata cheki kutoka kwao, kama kifuta jasho.

Sikutegemea, kwani tangu mwanzo waliponialika kutoa mhadhara na hata baada ya mhadhara, sikuwa na hata fununu kwamba kuna kifuta jasho. Nami sikufikiria wala kutegemea. Nilichojali ni kufanya kazi waliyoniomba kufanya, yaani kujadili mada ya "African Folktales to Contemporary Authors."

Ninaongozwa na nasaha ya wahenga kwamba tenda wema nenda zako; usingoje shukrani. Kama nilivyosema katika blogu hii, mengine ni matokeo. Sijawahi kukataa mwaliko wa kwenda kutoa mhadhara kwa sababu ya malipo.

Watu wanaonihimiza nisitoe huduma bila malipo ninawaambia kuwa kuna baraka katika kuwasaidia watu. Fursa ya kutoa mhadhara ni ya manufaa kwangu, kwani inaniongezea uzoefu na kuniwezesha kujitathmini ufahamu wangu, hasa katika kipindi cha masuali na majibu. Vile vile matangazo ya mhadhara yanayoandaliwa na kusambazwa na wale wanaonialika yananiongezea kufahamika.

Mara nyingi, huwezi kujua watu unaowahutubia ni akina nani katika jamii. Nimeshuhudia baada ya mhadhara watu wakijitokeza na kujitambulisha kwangu na kuniuliza iwapo nitakuwa tayari kuhutubia kwenye taasisi au jumuia zao. Mwaliko moja unazaa mialiko mingine. Ninasema hayo ili kuwashawishi wale wanaosita kutoa huduma bila kuahidiwa malipo. Hakuna hasara, bali ni faida.

2 comments:

Emmanuel Kachele said...

Hongera sana Profesa Mbele. Ninavyozidi kufuatilia katika blogu yako hii ndivyo ninazidi kujihisi niko darasani kwa wakati fulani. Ni kweli, Wahenga walisema 'Tenda wema uende zako'. Hawakukosea kwa sababu kukaa kusubiri malipo kwa binadamu unaweza kukaa kusubiri na usipate kitu kabisa. Hili ni somo pia hata kwangu. Mimi kama blogger chipukizi ninaendesha blogu ya Kielimu, na kwa sasa natoa hudumu, lakini sijali sana kuhusu kulipwa mtandaoni au na mtu. I know one day, God will work for me!
Good day Profesa!

Mbele said...

Ndugu Emmanuel Kachele

Shukrani kwa kutembelea hapa kwetu na kuandika ujumbe. Tunakubaliana kwa hiyo falsafa. Huwa ninawashangaa watu ambao dhana yao ya malipo ni pesa tu. Kumbe, mtu unaweza kujibadili fikra ukawa na dhana tofauti na pana zaidi.

Kwa upande wangu, ninapofanikiwa kuwaelimisha watu wakaridhika au kuwafurahi, nami ninafurahi. Ninafurahi kuwa nina uwezo na kipaji cha aina hiyo. Furaha yao ni furaha yangu. Furaha ina manufaa katika akili na afya yangu. Ni malipo tayari. Kama ni pesa, zinakuja bila mimi kuzikimbiza. Mfano ni hiki kifuta jasho kutoka Global Minnesota.

Halafu, kama unavyosema, Mungu mwenyewe anaangalia matendo yetu. Analipa mema na mabaya tufanyayo, na hapotezi kumbukumbu, wala hadanganyiki. Sisi wa-Kristu tunafundishwa kuwa kadiri tunavyotoa, ndivyo tunavyopewa.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...