Kitabu Changu Kutafsiriwa kwa kiSomali

Mara moja moja, katika miaka kadhaa iliyopita, nimekuwa nikiwazia kufanya mpango wa kutafsiriwa kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kwa kiSomali. Niliwazia lugha hiyo kwa kuwafikiria waSomali waishio Marekani. Hapa kuna waSomali wengi kuliko sehemu yoyote duniani ukiachilia mbali Somalia yenyewe. Jimbo hili la Minnesota ninapoishi linaongoza kwa kuwa na waSomali wengi.

Nimekuwa na mahusiano ya miaka mingi na waSomali wa Minnesota, hasa katika miji ya Faribault na Minneapolis. Nimehusika katika kuwashauri kuhusu maisha ya hapa Marekani, mifano ikiwa ni mihadhara yangu Mankato na Faribault.

WaSomali ambao wamesoma kitabu changu wanakipenda sana na wananikumbusha tunapokutana. Mmoja wao ni rafiki yangu Mohamed Dini. Huyu ndiye tumekubaliana akitafsiri kitabu hicho. Yeye ni mmoja wa waSomali wachache sana wanaotambulika katika fani hiyo hapa Minnesota. Kazi hiyo itaanza mwezi huu.

Ni faraja kubwa kwangu kwamba tafsiri hii itakapochapishwa itapunguza kwa kiasi kikubwa matatizo yanayowakabili waSomali Marekani, ambayo ni mara dufu kuliko yanayowakabili waAfrika wengine wengi. Tofauti na waAfrika wengi, waSomali wengi hawajui kiIngereza ambayo ndio lugha ya Marekani. Vile vile, waSomali ni waIslam, dini ambayo ni ya wachache hapa Marekani, na sehemu nyingi hakuna yale ambayo waIslam wanahitaji kwa mujibu wa dini yao. Kuna juhudi zinafanyika, lakini bado hazijatosheleza.

Ninangojea kwa hamu maendeleo ya shughuli hii hadi ifikie lengo.

Comments

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini