Saturday, October 1, 2022

Nimekutana na Wasomaji Wangu

Leo mjini Burnsville, Minnesota, nilikutana na wasomaji wangu wawili: Sarah B. Kamsin mwenye asili ya Sudan ya Kusini na Brighid McCarthy kutoka Marekani. Sarah ndiye aliyeandaa mkutano.

Sarah na mimi tumefahamiana tangu Julai 2019, aliponikuta kwenye maonesho ya vitabu mjini Blaine, Minnesota, akaipatia kitabu cha "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences." 

Baadaye Sarah alichapisha kitabu cha mashairi yake kiitwacho  "Vita, Babel, Cauliflower," ambacho nilikisoma nikakifurahia, na kisha nikakiandikia uhakiki. Unaweza kuona kisehemu cha uhakiki wangu kwenye tovuti ya Amazon. Sarah ana kipaji kikubwa cha utunzi wa mashairi ya kiIngereza.

Katika maongezi yetu ya leo, nimefahamu kuwa baada ya kusoma kitabu changu cha "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences," Sarah  alianza kumwelezea rafiki yake wa miaka mingi Brighid juu yangu na kitabu hiki..

Kutokana na hayo, Brighid alifurahi sana kukutana nami leo. Alikuwa na nakala ya kitabu, kikiwa kimepigiwa mistari kwenye vifungu na sentensi nyingi, kuashiria kuwa amekuwa akisoma kwa uangalifu na tafakuri tele. Nilishangaa anavyokumbuka hata mambo madogo yaliyomo kitabuni.

Tuliongea kwa masaa matatu, na muda mwingi tuliongelea tofauti za tanmadunni nilizozielezea kitabuni. Lakini pia tuliongelea uwezekano wa kushirikiana katika utatuzi wa mahitaji mbali mbali katika jamii za Afrika Mashariki, kama vile elimu na maji. Tumefurahi kugundua kuwa wote tayari tumekuwa tukifanya hayo. Brighid, kwa mfano amekuwa akifanya shughuli hizi Arusha. Tumehamasika kufanya zaidi.

2 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kwa mwandishi kukutana au kupata mrejesho wa wasomaji wako ni tunu kuliko hata fedha. Kwani, ni ushahidi kuwa unaathiri maisha ya jamii kama ambavyo umekusudia. Hata ukikutana au kupata ujumbe kwa mtu anayechukia au kupingana na mawazo yako bado ni tunu. Kazi yako hata hivyo ni pevu hata kama imetoka muda mrefu. Nadhani, unapaswa kuja na chapisho la pili juu ya mada ile ile kwa kuliborosha au kuhusisha na mrejesho wa wasomaji wako.

Mbele said...

Ndugu Mhango, shukrani kwa ujumbe wako. Nami nina msimamo huo huo uliouelezea vizuri namna hiyo.

Money in African and American Culture