Sunday, April 26, 2009

Migogoro ya Kitamaduni Sehemu ya Kazi

Kadiri dunia inavyozidi kuwa kijiji, kwa maana kwamba umbali kutoka sehemu moja hadi nyingine unazidi kupoteza umuhimu, na mawasiliano baina ya watu yanazidi kuwa rahisi, na kukutana uso kwa uso inazidi kuwa rahisi, tutakuwa na kazi kubwa ya kujizatiti kukabiliana na tofauti za tamaduni duniani.

Watu wa kila utamaduni wana namna yao ya kufikiri, kuelewa, kufanya mambo, kuongea, na kadhalika. Wao kwa wao wanaelewana. Lakini dunia ya leo si ya watu kukaa na wenzao wanaoelewana tu, bali ni ya kukabiliana na watu wa tamaduni tofauti. Haijalishi kama uko Dar es Salaam, Tokyo, au Los Angeles. Mchanganyiko wa watu wa tamaduni mbali mbali unazidi kuziathiri sehemu zote za dunia.

Hapa Marekani, nimeona juhudi inayofanyika ya kujizatiti na hali hiyo. Sehemu za kazi, kwa mfano, kutokana na kuwa na wafanyakazi kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wahusika wanaanza kuelewa umuhimu wa kujielimisha na kuelimishana kuhusu tofauti za tamaduni, ili kuzuia migogoro na kuboresha mahusiano kazini.

Mimi mwenyewe, kutokana na utafiti na uandishi wangu kuhusu masuala hayo, nimekuwa napata fursa za kwenda sehemu mbali mbali kuchangia mawazo na uzoefu wangu. Kwa mfano, tarehe 14 Februari, 2008, nilialikwa kwenye mji wa Minneapolis na kampuni ya RBC Wealth Management kutoa ushauri na uzoefu mbele ya timu ya uongozi wa kampuni hiyo.

Kampuni hii, kama kampuni zingine nyingi, ina mchanganyiko wa wafanyakazi kutoka sehemu mbali mbali duniani, wakiwemo waAfrika. Mazungumzo yangu yalihusu umuhimu wa kujifunza kuhusu tamaduni mbali mbali na mbinu za kukabiliana na hali hiyo, ili tuwe na maelewano na ufanisi mahali pa kazi na duniani kwa ujumla.

Pamoja na mazungumzo hayo, kampuni iliagiza nakala za kutosha za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, kwa watendaji waliohudhuria. Nilitambua kuwa kampuni hii inayo jadi ya kutafuta elimu kwa njia ya vitabu. Walinionyesha vitabu ambavyo walikuwa tayari wanavyo na wanavitumia, kwa lengo hilo hilo la kuelewa namna ya kushughulikia masuala yatokanayo na tofauti baina ya wafanyakazi. Kitabu kimoja walichonionyesha ni A Peacock in the Land of Penguins.

Hili ni fundisho kwetu waTanzania. Ni muhimu tuamke. Kama vile ilivyo Marekani na sehemu zingine duniani, waTanzania wanavyo vyuo, makampuni, na taasisi mbali mbali ambamo watu wa tamaduni mbali mbali wanashughulika. Kwa mfano, katika vyuo hivi na taasisi kuna watu wa kujitolea wanaotoka Marekani, Ulaya na sehemu zingine. Je, waTanzania wanaoendesha taasisi hizi wameshawahi kuwazia suala la elimu kwa wafanyakazi wote kuhusu tofauti za tamaduni? Mahusiano baina ya waTanzania na wageni katika sehemu hizo za kazi yakoje?

Kuna vile vile makampuni na taasisi za kigeni Tanzania, zenye wafanyakazi wananchi na wageni. Wahusika wana mkakati wowote wa kutoa elimu kuhusu tofauti za tamaduni?

Ukweli ni kuwa, mara kwa mara tunasikia taarifa za migogoro katika sehemu za kazi nchini Tanzania. Ninapoziangalia taarifa hizi, naona kuwa baadhi ya migogoro hii chanzo chake ni tofauti za tamaduni, au inachochewa na hizo tofauti za tamaduni. Tabia au kauli ya mgeni inaweza kuwaudhi waTanzania, ambao wanaichukulia kwa msingi wa utamaduni wa kiTanzania, na papo hapo, tabia au kauli ya mTanzania inaweza kumwudhi mgeni, kwa vile naye anaichukulia kwa misingi ya utamaduni wake. Shutuma zinatokea pande zote mbili. Nimeona, kwa mfano, waTanzania daima wanatoa malalamiko kuhusu ubaguzi. Sina hakika kama muda wote suala ni ubaguzi, bali nahisi kuwa wakati mwingine ni tofauti za tamaduni. Na wageni nao wanayo malalamiko mengi kuhusu waTanzania, ambayo msingi wake ni kutoelewa tofauti za tamaduni. Bila kuelimishana, magomvi hayo yataendelea na ufanisi sehemu za kazi utakuwa wa matatizo.

Je, waTanzania tunajizatiti vipi na masuala hayo ya dunia ya leo ambayo inazidi kuwa kijiji? Ninapenda sana kutafakari masuala hayo na kutoa mchango kwa kadiri niwezavyo. Nimeanza kuendesha semina nchini Tanzania. Ninajiandaa kufanya semina hizo mwaka huu pia. Kwa taarifa zaidi, yeyote anaweza kuwasiliana nami, kwa anwani hii: info@africonexion.com

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Nimenukuu "Tabia au kauli ya mgeni inaweza kuwaudhi waTanzania, ambao wanaichukulia kwa msingi wa utamaduni wa kiTanzania, na papo hapo, tabia au kauli ya mTanzania inaweza kumwudhi mgeni, kwa vile naye anaichukulia kwa misingi ya utamaduni wake. Shutuma zinatokea pande zote mbili. Nimeona, kwa mfano, waTanzania daima wanatoa malalamiko kuhusu ubaguzi. Sina hakika kama muda wote suala ni ubaguzi, bali nahisi kuwa wakati mwingine ni tofauti za tamaduni. Na wageni nao wanayo malalamiko mengi kuhusu waTanzania, ambayo msingi wake ni kutoelewa tofauti za tamaduni. Bila kuelimishana, magomvi hayo yataendelea na ufanisi sehemu za kazi utakuwa wa matatizo".Ni kweli kabisa hii yote inatokana na kutoelewana kitamaduni. Asante kwa kutuelimisha ni furaha kubwa kupata elimu hii. Nakutakia semina njema.

Mbele said...

Dada Yasinta, shukrani kwa ujumbe wako. Nawe unayo mengi ya kuchangia, kwani una uzoefu mkubwa. Tukichanganya uzoefu wako kama mwanamke na uzoefu wa aina yangu, tutaweza kutoa semina za nguvu huko mbele ya safari. Napendekeza tukaanzie Mfaranyaki, kwani semina nyingi zinafanyika Dar es Salaam, Arusha na kwingineko.

Cha zaidi ni kuwa miaka hii ya karibuni nimeanza kujenga hoja kwamba ili tufanikiwe katika kujielimisha haya masuala ya utamaduni, inabidi tufanye juhudi maisha yote. Semina ninazotoa ni kianzio tu, kuwaamsha watu ili wajenge tabia ya kujielimisha katika maisha yao yote kuhusu masuala haya.

Nasisitiza hivi kwa sababu, hata baada ya kukaa na waMarekani miaka mingi, bado naona ninayo mengi ambayo siyaelewi katika utamaduni wao. Na wao vile vile, hawawezi kusema wananielewa kikamilifu. Kwa hivi, hii elimu haina mwisho. Ndio kitu ambacho nataka waTanzania kule nyumbani wafahamu.

Yasinta Ngonyani said...

Kwa elimu hii uliyonayo kwa kweli nakuhakikishia wataelewa tu na kama hawataelewa basi hakuna maana.Nashukuru sana kwa kuniamini kuwa nami naweza kufanya hiyo kazi. Kusema kweli ningependa.

Bennet said...

Hali hii inanikuta (ga) sana ninapoenda sehemu za vijijini, mimi ni mtu niliyezaliwa mjini na kukulia mjini maisha yangu yote, baada ya kufika miaka 15 Baba yangu (marehemu) alikuwa ananipeleka kijijini likizo zangu zote na kuniacha mwenyewe wiki 2 - 4. Nilikuwa simwelewi na ilikuwa inaniudhi sana hasa kazi zile za shamba, mazingira na vyakula vya kule ingawa nilijifunza mengi sana.

Nilikuja kumwelewa baada yakuniambia inabidi nisomee kilimo/mifugo, maana sasa hivi muda mwingi ninakuwa na wanavijiji huko mashambani hasa misimu ya kilimo. ingawa ninawajua sana tabia zao na saikolojia lakini bado naendelea kujifunza na wao wanajifunza kwangu pia

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...