Wednesday, November 3, 2010

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe
. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi
! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

8 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Kila mtu anaiogopa CCM hata wana-CCM wenyewe sema hawana pa kukimbilia wala kuficha nyuso zao. Waliomo ndani ya CCM wapo kwa sababu ima uroho, uinga, kukosa pa kwenda, ufisadi,unafiki, upogo, nyongea na jinai nyingine lakini si kwa mapenzi.
Hata Kikwete mwenyewa hana imani na CCM wala haipendi ni kwa vile ndicho kijiko na kichaka chake.

Muro said...

Haya matatizo yanaletwa na Udini uliopo CCM, CCM Ikisimamisha mgombea Mkristo Inakuwa nzuri sana, Ila ikisimamisha mgombea muislamu inakuwa shida! Hii tumeiona katika Chaguzi za 2000 na 2010. Hali hii sio nzuri kama kweli tunapenda maendeleo ya nchi tuachane na mambo ya udini yanayoletwa na Mwakiyembe na wenzake!

kamala Lutatinisibwa Lutabasibwa said...

Ila matatizo yoote hayo yalilsababishwa na Nyerere mwenyewe asiyetaka kuhojiwa wala kukosolewa

Mbele said...

Ndugu Mhango, kauli yako kuwa hata CCM wanaiogopa CCM naona ina ukweli. Nakumbuka wazito kama Lyatonga Mrema walivyojikuta wakikimbia kutoka CCM. Nakumbuka Horace Kolimba alivyoitwa Dodoma na hakusikika tena. Na hapo juzi, nakumbuka wagombea wote wa CCM walivyofunga midomo na kuacha kabisa kushiriki midahalo. Naona kauli yako ina mantiki, kuwa CCM ni tishio kwa wana-CCM wenyewe :-)

Simon Kitururu said...

Mmmmh!

Peter Chaulo said...

Haisaidii kama sisi wananchi hatutachukua hatua. Ni kua wasomi wazuri na kukubali kwenda barabarani kuandamana na kua na tume huru ya uchaguzi

Tumaini Geofrey Temu said...

Viongozi wa upinzani kama wakula ccm

Unknown said...

Chama katika Kambi ya Upinzani ambacho Mwalimu alitamani kuchukua nafasi ya CCM nakiona kuwa ni ACT Wazalendo.

Umbumbumbu wetu ukija kutuondoka, ndiyo itakuwa mwisho wake!

Najiuliza Mwenyekiti mpya wa CCM, Rais Dkt John Joseph Pombe Magufuli, atatumia dawa ipi kuitibu saratani inayoitafuna Serikali yake!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...