Thursday, January 20, 2011

Tamko Kuhusu Matamko ya Wa-Tanzania

Tanzania sasa imekuwa nchi ya matamko. Kila kukicha linatolewa tamko kutoka kikundi au jumuia fulani. Katika siku za karibuni, kwa mfano, tumeshasikia matamko kutoka vyama vya siasa, jumuia za kidini, na taasisi mbali mbali, za serikali na zisizo za serikali.

Matamko ya wa-Tanzania yanahusu zaidi masuala tata ya jamii, au migogoro. Yanahusu mambo kama sera za serikali au vitendo vya watendaji mbali mbali, kama vile polisi, au taasisi zingine. Mara kwa mara, matamko yanakuwa na hisia za kulalamika, kuonya, au kutangaza msimamo.

Kila mtu anaweza kuwa na mtazamo wake kuhusu jambo hilo. Binafsi, naliona ni jambo zuri, kwa maana kwamba watu wanatumia uhuru wao wa kuelezea hisia, mawazo na mitazamo yao. Kwa hivi, sishangai kuyasikia matamko hayo. Kila mtu ana haki ya kutoa tamko lake, ili mradi havunji sheria au kuingilia uhuru wa wengine wa kutoa matamko.

Utamaduni wa matamko ni mzuri. Ni bora kuliko tunayoyaona au kuyasikia yakitokea katika jamii za wenzetu, ambao migogoro yao inawapeleka katika kupigana na kuvunjika kwa amani.

Kwa watu wasiopendezwa na jambo, au wenye hasira, fursa ya kujieleza kwa namna yoyote, kama hii ya matamko, ni njia nzuri ya kupooza hisia za kusumbua. Ni aina ya tiba kisaikolojia, hata kama wanayosema katika haya matamko ni upuuzi. Kuzuia uhuru na fursa ya kujieleza ni jambo lenye athari mbaya.

Kwa upande mwingine, utamaduni wa wa-Tanzania wa matamko unanichekesha, kwa jinsi matamko yanavyofumuka kama uyoga au kumiminika kama mvua.

Tungeweza kuendeleza utamaduni wa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana au kuwatumia wawakilishi wetu. Tungeweza hata kufuata utamaduni wa zamani wa mabibi na mababu, kama alivyouelezea Mwalimu Nyerere, kwamba wahenga walikuwa wanakaa chini ya mti na kujadili masuala hadi kukubaliana. Lakini nafurahi nami nimetoa tamko langu.

3 comments:

Emmanuel said...

Aksante Prof. Nitashukuru sana kama watanzania watasikia ujumbe wako na kuufanyia kazi maana tatizo wale wanaokemewa Tanzania wanakuwa kimya kama vile hamna kinachoendelea.

Pia, ninaona hatari ya matamko yenye kupotosha umma na kuhatarisha amani na mshikamano wetu maana watu wengi au makundi kadhaa yameanza harakati za kutoa matamko kwa lengo la kutaka kulikandamiza upande wa pili na kuhadaa wananchi

emuthree said...

Ujumbe murua mkuu. Tunakuwa kama tunaogopana vile...lakini wanasema jinsi gani ya kumfikia mlengwa ili asikie hilo dukuduku...kina vikwazo na ukiacha kwa msaidizi inaweza kabisa isimfikie mlengwa...!

Mbele said...

Ndugu Emmanuel, shukrani kwa ujumbe. Kuhusu matamko yenye kupotosha, nadhani dawa yake ni kutoa matamko ya kusahihisha upotovu. Dawa ya kuua uwongo ni ukweli.

Kwa mfano, hivi majuzi kufuatia tamko la maaskofu kuhusu vurugu zilizotokea Arusha, lilitolewa tamko na jumuia fulani nchini ambamo kulikuwa na dai kuwa maaskofu hawakutoa tamko pale yaliyopotokea mauaji Visiwani, mwaka 2001.

Lakini siku chache zilizopita, watu wameleta ushahidi kupinga dai hilo, na ushahidi wenyewe ni gazeti ambamo kuna tamko ambalo maaskofu walitoa ule mwaka 2001 kuhusu mauaji ya Visiwani.

Sasa hapo utaona kuwa ile jumuia iliyowaandama maaskofu imejifunga kitanzi. Yawezekana hawakujua ukweli au yawezekana walifanya upotoshaji wa makusudi.

Kama hawakujua ukweli, wanayo fursa ya kutoa tamko la kukiri hivyo na kuomba radhi, kwani kukosea ni ubinadamu. Lakini kama hawatafanya hivyo, hata baada ya kuonyeshwa ukweli, itabidi tuwahesabu katika hilo kundi la wapotoshaji umma na wahatarishaji wa amani.

Kama nilivyosema katika ujumbe wangu, watu wana uhuru wa kutoa matamko, isipokuwa wasivunje sheria au kuhujumu haki za wengine. Sasa utaona wazi kuwa kumpakazia mwingine mambo yasiyo ya ukweli ni kumvunjia haki. Na hili halikubaliki.

Uzuri ninaouona katika kuwepo kwa uhuru wa aina ninayoongelea ni kuwa mtu akifurunda katika kutoa tamko lake, ataumbuka yeye pale wengine watakapotoa matamko ya kubainisha ukweli. Nafikiri kwa mtindo huu kila mtu atakuwa anajitahidi kuwa mwangalifu na mkweli.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...