Saturday, September 17, 2011

Mkutano wa "Africa Network" Umefana

Mkutano wa Africa Network hapa Indianapolis umefana sana. Hapa kulia anaonekana Dr. Tom Benson, mwanzilishi wa Africa Network, ambaye alitukusanya watu kadhaa miaka mitano iliyopita tukaunda bodi ya Africa Network. Ni miaka mitano sasa na Africa Network inaendelea kupiga hatua.





Tumetafakari masuala mengi, kuanzia ujasiriamali, ufundishaji, hifadhi za nyaraka na kumbukumbu nyingine, taasisi zinazohusika na masomo yahusuyo Afrika, kuandaa na kutekeleza mipango ya kupeleka wanafunzi Afrika, utafiti, na shughuli za kujitolea.






Kama kawaida, ni fursa ya watafiti na walimu wa vyuo mbali mbali kukutana na kubadilishana mawazo. Kama inavyotokea katika kila mkutano, wengine tulifahamiana kabla na wwngine ni wapya.








Kati ya watu wapya niliowakuta na kufahamiana nao ni Bernard Woma ambaye ni msanii kutoka Ghana. Anaonekana katika picha hapa kushoto, mbele kabisa, amevaa kofia. Anaendesha kituo nchini Ghana ambapo anawafundisha wageni sanaa na utamaduni wa kutumia ala za kiasili za muziki na mambo kadha wa kadha mengine. Hebu jionee mwenyewe anavyoimudu kazi hapa.







Hapa kushoto naonekana nikiwa na mtoa mada mmojawapo, wakati tulipokuwa tunatoa mada zatu.











Hapa kushoto naonekana nikitoa mada yangu, "Engaging with Somali Immigrants in Minnesota." Niliongelea uzoefu nilioupata katika jimbo la Minnesota, jimbo ambalo lina wakimbizi na wahamiaji wengi kutoka Somalia na nchi zingine za Afrika, hasa Liberia. Kitu kimoja nilichowatajia wasikilizaji ni ripoti inayopatikana hapa, ambayo ni utafiti waliofanya wanafunzi wa Idara ya Siasa, Chuo cha St. Olaf, katika mji wa Faribault kuhusu masuala yanayowahusu wa-Somali ambao wanaishi katika mji ule. Utafiti huu ulikuwa ni njia nzuri ya kuwapa wanafunzi uzoefu wa kufanya utafiti katika jamii na kujifunza kuhusu masuala ya watu wa utamaduni tofauti na wao. Ripoti hii imenigusa kwa namna ya pekee kutokana na jinsi inavyothibitisha namna ufundishaji wetu unavyoweza kuwekwa katika misingi mipya kwa kuwapa wanafunzi kufanya utafiti katika jamii. Pia ripoti hii inaonyesha jinsi viongozi na wadau mbali mbali wa jamii wanavyoutambua mchango wangu katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wanajamii wa miji kama Faribault ambayo ina idadi kubwa ya hao wahamiaji na wakimbizi. Sina sababu ya kuficha faraja ninayoipata kwa kuona viongozi na wadau hao wanakipigia debe kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nashukuru kwamba kina mchango muhimu kwa watu wanaokabiliwa na masuala magumu ya jamii.

Kitu kimoja ambacho ni cha pekee sana ni kuwa tumepata pia fursa ya kuona sanaa za kale za Ife, Nigeria, ambazo kwa sasa ziko katika jumba kuu la makumbusho mjini Indianapolis. Hizo ni sanamu za shaba na "terra cota." Zimeletwa na zinaonyeshwa hapa Indianapolis kwa mpango maalum kutoka hifadhi ya Taifa ya Nigeria.

2 comments:

Emmanuel said...

Thanks Prof,

Those are great moments and great activities...Thanks for keeping us posted.
God bless you

Mbele said...

Thanks, Emmanuel, for reading my post. Best wishes.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...