Wednesday, July 4, 2012

Ninatalii Tanga

Kwa siku kadhaa sasa nimekuwa mtalii katika mji wa Tanga. Kama wanavyojua ambao wamefika mjini hapa, Tanga ni mji uliotulia sana, ukifananisha na Dar es Salaam, ambao ni mji wa kero nyingi na wajuaji wengi pia.

Jana mchana nilikuwa nimekaa nje ya hoteli ambapo nimefikia. Hapo nje kuna viti vingi na meza, kwani ni sehemu ya wateja kujipatia vyakula na vinywaji. Alipita muuza gazeti nami nikatoa pochi yangu nikanunua magazeti mawili. Muuza gazeti akaenda zake.

Dakika chache baadaye, alipita mtu mmoja akanisogelea na kuniambia kuwa pochi yangu iko chini ya kiti nilichokalia. Nikaangalia, nikaiona. Huyu jamaa hakusimama, bali aliendelea na safari yake, ila najua alinisikia nilipomshukuru. Ingekuwa hajaniambia, sijui mambo yangekuwaje, maana nina hakika ningesimama na kuondoka, bila kujua pochi iko wapi. Pochi ilikuwa na kadi za hela (credit cards), vitambulisho, na kadhalika.

Nimeshapita mitaa kadhaa ya hapa mjini, ambayo nilikuwa siifahamu. Vile vile, nimeona ilipo shule ya Galanos, ambayo ina historia na umaarufu wa pekee sio Tanga tu bali nchini. Nilipokuwa nasoma Mkwawa High School, 1971-72, tulikuwa tunaisikia sana shule ya Galanos.

Insh'Allah leo au kesho nitaenda maktaba ya Tanga, ambayo nimeshaitembelea mara kadhaa. Nitapenda kuona hali yake ya sasa. Mara ya mwisho nilipopita hapo niliona kuwa inahitaji ukarabati mkubwa. Ilijengwa na wakoloni wa ki-Ingereza. Mwalimu Nyerere, ambaye wapika majungu wa Tanzania wanakazana kumbeza, alizienzi maktaba, sambamba na suala zima la elimu. Lakini leo, wa-Tanzania tumepania zaidi kuwekeza katika baa kuliko maktaba au shule. Huko maktabani wa-Tanzania hawaonekani, labda wawe wanafunzi wanaojiandaa kwa mitihani.

Watu wa Tanga walikuwa na bahati ya pekee ya kujengewa maktaba kubwa namna hii. Wangeitumia vizuri, pia kuiwekea vitabu na majarida, leo wangekuwa mbali sana kielimu, ukifananisha na sehemu nyingine za nchi.Lakini sijui ni wangapi katika mji huu wenye mazoea ya kusoma katika maktaba hii.

Ninajiona ni mtalii hapa Tanga. Mbali ya kuangalia sehemu mbali mbali za mji, ninalipia malazi, chakula, vinywaji, usafiri, na huduma zingine kadha wa kadhaa. Ni faraja kubwa kutambua kuwa pesa ninazotumia hapa zinachangia uchumi wa mji huu. Ni pesa ambazo ninaolipwa kule Marekani, ambako nafanya kazi wakati huu. Wazo hili la kuchangia uchumi wa hapa nchini linanifanya nijisikie vizuri.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...