Tuesday, December 4, 2012

Wa-Kristu Wasilimu; Wa-Islam Waingia u-Kristu

Dini ni moja ya mada ambazo nazizungumzia sana katika blogu yangu. Leo napenda kugusia tena mada ya mtu kubadili dini. Niliwahi kuandika kuhusu mada hiyo, nikatamka kuwa kubadili dini ni haki ya mtu, kwa mujibu wa dhamiri yake. Soma hapa.

 Dini ni safari ambayo binadamu anasafiri. Kwa wengine ni safari ngumu yenye vikwazo vingi. Kwa wengine ni safari nyepesi, kwa maana kwamba wametulia kabisa katika imani yao. Namshukuru Muumba kwamba mimi ni mmoja wa hao waliotulia, ingawa nilipokuwa kijana nilihangaika na kutetereka kiasi fulani.

Ukiangalia mtandaoni, kama vile YouTube, utaona taarifa nyingi za watu wanaobadili dini, kutoka u-Islam kuingia u-Kristu, kutoka u-Kristu kuingia u-Islam, na kadhalika. Maelfu ya watu wanafanya hivyo muda wote. Katika YouTube utawaona wengi wakitoa ushuhuda kuhusu walivyohamia dini nyingine na nini kiliwafanya wahame.  Kwa mtazamo wangu, hayo ni mambo yao binafsi, baina yao na Muumba. Hayaongezi wala kuteteresha imani yangu.

Hapa chini ni taarifa ya watu kuingia u-Islam hivi karibuni nchini Burundi. Hakuna mwenye haki ya kuwazuia, iwapo watu hao wanajisikia ndani ya moyo wao kuwa kwa kubadili dini wanakuwa karibu zaidi na Muumba. Nawatakia mema katika safari hii ya kiroho.
.

Hapa chini ni taarifa ya wa-Islam kuingia u-Kristu nchini Pakistan. Hakuna mwenye haki ya kuwazuia, iwapo watu hao wanajisikia ndani ya moyo wao kuwa kwa kubadili dini wanakuwa karibu zaidi na Muumba. Nawatakia mema katika safari hii ya kiroho.

2 comments:

Unknown said...

Hali ni hiyohiyo hata Tanzania. Kwenye mihadhara ya Ki-islamu, tunawaona wakristu wakisilimu. Kwenye mikusanyiko ya Ki-injilisti, waislamu pia huingia ukristu.
Pia kuna kuhamahama kulikopindukia kwa madhehebu. Ni jambo la kawaida kukuta familia ya Baba Mkatoliki, Mama Mprotestanti na Watoto wa madhehebu ya kilokole. Kwa hakika, hili ni suala binafsi.

Mbele said...

Ndugu Ado, shukrani kwa mchango wako. Kwa kweli hili ni suala zito, tata, na labda tete pia.

Inaonekana watu wanahangaika. Papo hapo inasikitisha kama watu wanahamahama dini kama vile ni vilabu vya soka. Lakini Mungu ndiye anajua.

Ngoja nijipange kwenda kuhudhuria mihadhara ya wa-Islam na wa-Injilisti nitakapokuwa Tanzania. Labda kuna jambo nitajifunza, liwe linahusu dini au masuala mengine ya jamii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...