Tuesday, December 11, 2012

Mungu ni Mmoja: Anaitwa Allah, Brahman, Chiuta, Ruwa na Kadhalika

Uzuri wa kuwa na blogu yako ni kuwa hutawaliwi na mtu katika kuamua nini cha kuandika. Uamuzi wote ni wako. Nimesema kabla kuwa katika blogu yangu hii, masuala ambayo yanasemwa kuwa ni nyeti, kama dini, ni ruksa kujadiliwa. Tena sio tu ruksa, bali muhimu kujadiliwa.

Leo napenda kutoa hoja kuwa Mungu ni mmoja: anaitwa Allah, Brahman, Chiuta, Ruwa, na kadhalika, kutokana na kuwepo kwa lugha nyingi hapa duniani. Huyu ndiye aliye juu ya yote, mwenye uwezo wote, kama inavyosemwa katika ki-Arabu, "Allahu akbar." Ni dhana ya msingi katika dini zetu.

Kama wewe ni mu-Islam, halafu unasema kuwa Allah ni tofauti na Mungu wanayemwabudu wa-Kristu, au Mungu wanayemwabudu wa-Hindu, jichunguze upya, kwani utakuwa unasema kuna miungu zaidi ya mmoja. Utakuwa unaongelea kuwepo kwa mungu mwingine zaidi ya Allah. U-Islam hautambui kuwepo kwa Mungu mwingine zaidi ya Allah.

Kama wewe ni m-Kristu, halafu unasema kuwa Mungu unayemwabudu ni tofauti na Allah, basi inabidi ujichunguze, kwa misingi hiyo hiyo. U-Kristu hautambui kuwepo kwa mungu zaidi ya huyu ambaye sisi wa-Kristu tunayemwabudu, ambaye kwa ki-Arabu huitwa Allah. Usishangazwe na jina Allah. Wa-Kristu ambao ni wa-Arabu nao hutumia jina Allah, wakimaanisha Mungu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Huyu Mungu mmoja anatajwa kwa majina mbali mbali kufuatana na lugha. Wa-Tumbuka wa Malawi na Zambia humwita Chiuta. Wa-Hindu humwita Brahman. Wa-Kamba na wa-Kikuyu humwita Ngai. Wachagga humwita Ruwa.

Hoja yangu ni kuwa majina yote hayo yanamtaja Mungu huyu huyu. Muumini anayeamini kuwa kuna Mungu mmoja tu, sherti akubali na azingatie hilo. Ni ushahidi kuwa Mungu alijitambulisha kwa wanadamu duniani kote tangu mwanzo kabisa.

Nimeona nitoe mawazo yangu, kwa uhuru kabisa, kwani ni haki yangu. Kama kuna anayetaka kuyajadili au kuyapinga, namkaribisha kwa mikono miwili kufanya hivyo.

10 comments:

Unknown said...

Ni kweli.... kule kwetu tunaita SAPANGA, na ninarafiki yangu yeye huita NGURUVI, lakini sisi wote tunamaanisha yuleyule Mungu, yuleyule Allah!!!!!!

Anonymous said...

Ni kweli mungu ni mmoja tu na anatambulika kwa majina mengi kutokana na mgawanyiko wa makabila kuwepo kwa lugha nyingi hapa duniani naamini kama pangekuwa na lugha moja hapa duniani pasingekuwa na hayo malumbana naamini pia pangekuwa na dini moja tu

Anonymous said...

Duh! Daah! Prof. Huu ni mtihani mkubwa. Wahenga walituambia, "akili ni nywele, kila mtu ana zake." Wenzetu wakatuambia, " a rose by any other name, will smell the same." Labda nizungumzie, kuelewa kwangu kama Muislamu. Allah ana majina 99 yanayokunjua "attributions" Zake. Hata hivyo huyu Allah anayekubalika na kuaminika akilini mwangu, pengine siye Allah anayekubalika akilini kwa mwingine. Na katika hali hiyo hiyo, Mungu mmoja anayekubalika na kuaminika katika ummoja na upweke wake siyo ummoja na upweke unaokubalika na kuaminika na mwingine. Kwa mantiki hii, Mungu anabaki kuwa mmoja yule yule, lakini Mungu wa imani yangu, kwa vyovyote vile siye yule wa imani ya mwenzangu. Nafikiri kwa picha hii ndio maana pana tofauti ya madhehebu na jinsi za kuwabudu. "Ninachokiabudu sicho anachokiabudu na wala ninavyoabudu, sivyo anavyoabudu. Anabaki na dini yake, nami nabaki na yangu. Ahlan wa sahalan.

Mbele said...

Anonymous wa December 11, shukrani kwa ujumbe wako. Ni kweli kuwa lugha imechangia kutuvuruga. Utawakuta wahubiri wana vipaaza sauti wakihutubia kwa jazba kwamba mungu wao ndio wa kweli na yule wa wengine si mungu wa kweli. Hapo ndipo nikaona bora nami nijitose katika haya malumbano, ila si kwa kumbeza au kumtukana yeyote, bali kuwa kujenga hoja bila jazba.

Anonymous wa December 12, shukrani kwa maoni na mawaidha yako. Yanafikirisha. Ni ukweli unavyosema, kwamba katika akili ya mtu kama mimi ambaye ni m-Kristu, ukiniambia namwabudu Allah au Brahman, nitafadhaika. Labda kwa vile mimi nimeanza kujijengea mawazo haya niliyoeleza katika blogu hii, huenda sitafadhaika sana, kwa vile nimeanza kutambua kuwa majina ya Mungu ni suala la lugha.

Lakini ukimwambia m-Kristu wa kawaida kuwa anamwabudu Allah, nadhani atakuja juu kiasi kwamba patakuwa hapatoshi, au kama wengine wanavyosema, patachimbika. Suluhisho ni kuweleza kuwa waKristu waArabu hutumia jina la Allah katika sala zao na katika tafsiri yao ya Biblia.

Umwambie mu-Islam wa kawaida wa Bagamoyo au Tunduru kuwa anayemwabudu ni huyu huyu anayeitwa Ruwa au Chiuta, napo patakuwa hapatoshi. Ni tatizo pande zote. Kama unavyosema, ni mtihani mkubwa.

Na hiyo hoja yako kuhusu tofauti za jinsi ya kuabudu ni kweli. Kama vile kulivyo na tofauti za tamaduni na lugha, tofauti hizo zinahusika pia katika kumwelewa au kumwelezea Muumba. Kila lugha ina dhana zake, na maneno ya lugha moja aghalabu hupishana na maneno ya lugha nyingine. Hivyo hata ufahamu wetu wa huyu Mungu hutofautiana.

Lakini kwa mtazamo wangu, Mungu mwenyewe anabaki ni huyu huyu mmoja.

Anonymous said...

asante sana mheshimiwa Profesa Mbele naona hapo huyo anon wa december12 ndio wale wenye akili mgando samahani kama nimetumia lugha ya ukali,Kama unavyosema Mungu huyuhuyu ndo huyo mmoja Allah,Chiuta,Ruwa,Ngai,Ruhanga nk hivyo basi wengine kuwatoa kwenye akili mgando ni kazi kweli

Mbele said...

Nchini Malaysia, serikali ilizikamata nakala za Biblia zaidi ya 20,000 kwa vile zilitumia jina "Allah" katika kumtaja Mungu. Serikali ilidai kuwa ni u-Islam peke yake ndio unaostahili kutumia jina "Allah." Taarifa ni hii hapa.

Kwa upande wa Tanzania, umbumbumbu juu ya masuala ya lugha unachangia kuwepo kwa malumbano baina ya baadhi ya wa-Islam na baadhi ya wa-Kristu.

Anonymous said...

sasa mbona Wakiristu wa Arabuni wanamwita ALLAH?

Mbele said...

Ndugu Anonymous wa Desemba 18, hilo ndilo suala ambalo Malaysia nadhani hawakuzingatia.

Niongezee tu kuwa nilileta mada hii kwa makusudi, nikiamini kuwa itawashtua au kuwakera watu kifikra, kisha wajitokeze kutoa msimamo.

Nilitegemea utokee mjadala mkali, sawa na ile mijadala ya vijiweni wanakolumbana kuhusu kama Yesu ni Mungu au la.

Khalfan Abdallah Salim said...

Mungu ni mmoja. Hii ni itikadi ya ambayo ni rahisi kuisema na ni muhimu ifahamike tofauti na mfanano wa itikadi hii baina ya dini mbalimbali. Prof Sengo, alipata kusema kuwa 'utu uzima ni kujua mfanano katika tofauti na tofauti katika mfanano."

Kwa kuwa si mjuzi wa dini zote, nitoe maelezo machache kama maoni yangu. Katika Uislamu, itikadi ya Mungu mmoja maana yake ni kuamini kuwa kuwa huyo ndiye muumba, huyo ndiye mwenye kusamehe dhambi, huyo ni yule ambaye hajazaa wala hajazaliwa na hafanani na yeyote, huyo ni yule ambaye hunufaisha watu na hufanyia watu majaribu kwa mateso na mazito. Huyo ni yule ambaye anapaswa kuombwa pekee, kutegemewa na kuabudiwa pekee. Hii ndio dhana ya Mungu mmoja katika Uislamu, na waislamu wanaposema wanamuabudu Allah ni kwa maana hii.

Niwazi kuwa twaweza wote tukasema Mungu ni mmoja, jina lake Allah lakini sifa za huyu Allah ni tofauti na hayo wasemayo waislamu juu ya Mungu mmoja (Alla). Hakika hii, nadhani ndiyo iliyopelekea wamalay, waone kuruhusu neno 'Allah' kutumiwa na wasio waislamu, italeta sintofahamu ya kiitikadi japo kijuu juu ni kweli kutumia jina hilo kilugha maana yake ni Mwenyezi Mungu Mmoja lakini kisifa kuna tofauti kubwa!

Je Ukristo, Uhindu, Uyahudi unasemaje juu ya sifa za Mungu mmoja (Allah)?

Mbele said...


Ndugu Khalfan Abdallah Salim

Samahani, sikumbuki kama niliuona ujumbe wako. Hii ndio sababu ya mimi kukosa kuuongelea.
Hata mimi si mjuzi wa dini zote, hasa tukizingatia kuwa ziko nyingi na zinaendelea kuchipuka. Ila kwetu wa-Kristu, ufahamu wetu wa Mungu ni huu huu unaoelezea.

Tatizo ni kuwa wasio wa-Kristu wanatushutumu kwa mambo ambayo hawayaelewi ipasavyo. Kwa mfano, tunaposema Yesu ni mwana wa Mungu, hatumaanishi sawa na mimi au Shaabani wa Bagamoyo tulivyooa na kuzaa watoto. Inahitaji mtu uwe umelelewa katika u-Kristu kuweza kujua kuwa tunaposema Yesu ni mwana wa Mungu, tunatumia dhana hiyo "kiteolojia" si "kibailojia."

Vivyo hivyo, tunavyoongelea Utatu Mtakatifu, yaani uwepo wa nafsi tatu za Mungu, hatumaanishi kuna miungu watatu. Hakuna m-Kristu ambaye haelewi kuwa kuna Mungu mmoja tu. Hii dhana ya nafsi tatu ni ya kiteolojia. Kama mtu umekulia katika u-Kristu, huwezi hata siku moja kudhani kuwa u-Kristu unaongelea miungu watatu.

Wako wanaodai kuwa sisi "tunamshirikisha" Mungu, yaani tunasema Mungu ana washirika. Ukweli kwamba hatufanyi hivyo. Hii dhana ya Utatu imefungamana kabisa na dhana ya Umoja. Mungu ni mmoja.

Kuhusu u-Hindu, kwa miaka mingi nilikuwa naangalia jinsi wa-Hundu walivyo na miungu wengi. Lakini katika kusoma kwa makini mafundisho ya wanateolojia wa dini hiyo, nimegundua kuwa dini hiyo pia inamtambua na kumwamini Mungu ambaye ni juu ya yote, yaani "Supreme."

Kwetu ambao si wa-Hindu, ambao hatukulelewa katika u-Hindu, inaweza kuwa tatizo kufahamu undani wa imani yao hiyo, kwani bado tunachokiona ni miungu wengi. Ni hivyo hivyo kwa wale ambao hawakulelewa katika u-Kristu. Wanachoona wao ni kuwa Mungu wetu kazaa mtoto na kwamba ana washirika.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...