Showing posts with label Allah. Show all posts
Showing posts with label Allah. Show all posts

Tuesday, December 11, 2012

Mungu ni Mmoja: Anaitwa Allah, Brahman, Chiuta, Ruwa na Kadhalika

Uzuri wa kuwa na blogu yako ni kuwa hutawaliwi na mtu katika kuamua nini cha kuandika. Uamuzi wote ni wako. Nimesema kabla kuwa katika blogu yangu hii, masuala ambayo yanasemwa kuwa ni nyeti, kama dini, ni ruksa kujadiliwa. Tena sio tu ruksa, bali muhimu kujadiliwa.

Leo napenda kutoa hoja kuwa Mungu ni mmoja: anaitwa Allah, Brahman, Chiuta, Ruwa, na kadhalika, kutokana na kuwepo kwa lugha nyingi hapa duniani. Huyu ndiye aliye juu ya yote, mwenye uwezo wote, kama inavyosemwa katika ki-Arabu, "Allahu akbar." Ni dhana ya msingi katika dini zetu.

Kama wewe ni mu-Islam, halafu unasema kuwa Allah ni tofauti na Mungu wanayemwabudu wa-Kristu, au Mungu wanayemwabudu wa-Hindu, jichunguze upya, kwani utakuwa unasema kuna miungu zaidi ya mmoja. Utakuwa unaongelea kuwepo kwa mungu mwingine zaidi ya Allah. U-Islam hautambui kuwepo kwa Mungu mwingine zaidi ya Allah.

Kama wewe ni m-Kristu, halafu unasema kuwa Mungu unayemwabudu ni tofauti na Allah, basi inabidi ujichunguze, kwa misingi hiyo hiyo. U-Kristu hautambui kuwepo kwa mungu zaidi ya huyu ambaye sisi wa-Kristu tunayemwabudu, ambaye kwa ki-Arabu huitwa Allah. Usishangazwe na jina Allah. Wa-Kristu ambao ni wa-Arabu nao hutumia jina Allah, wakimaanisha Mungu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Huyu Mungu mmoja anatajwa kwa majina mbali mbali kufuatana na lugha. Wa-Tumbuka wa Malawi na Zambia humwita Chiuta. Wa-Hindu humwita Brahman. Wa-Kamba na wa-Kikuyu humwita Ngai. Wachagga humwita Ruwa.

Hoja yangu ni kuwa majina yote hayo yanamtaja Mungu huyu huyu. Muumini anayeamini kuwa kuna Mungu mmoja tu, sherti akubali na azingatie hilo. Ni ushahidi kuwa Mungu alijitambulisha kwa wanadamu duniani kote tangu mwanzo kabisa.

Nimeona nitoe mawazo yangu, kwa uhuru kabisa, kwani ni haki yangu. Kama kuna anayetaka kuyajadili au kuyapinga, namkaribisha kwa mikono miwili kufanya hivyo.

Tuesday, October 16, 2012

Wa-Kristu Tunamwabudu Allah!

Najua kuwa kichwa cha habari hii kitawashtua wengi. Huenda watu watasema nimechanganyikiwa au nimekufuru.  Huenda wako watakaouliza, "Iweje wa-Kristu wawe wanamwabudu Allah?"

Kwa siku kadhaa, nimekuwa nikijuliza suali: Je, wa-Arabu ambao ni wa-Kristu wanatumia jina gani kumtaja Mungu? Ninafahamu kuwa kuna mamilioni ya wa-Arabu ambao ni wa-Kristu, huko Mashariki ya Kati na sehemu zingine za dunia. Sasa je, Mungu wanamwitaje kwa ki-Arabu?

Nimefanya uchunguzi kidogo nikagundua kuwa jina wanalotumia, ni hilo hilo wanalotumia wa-Islam, yaani Allah. Hili ndilo neno lililopo katika ki-Arabu. Katika Biblia ya ki-Arabu, ambayo huitwa "al-Kitab al- Muqadis" yaani Kitabu Kitakatifu, Mungu anaitwa Allah muda wote.

Nilivyogundua hivyo nimetambua jinsi wengi wetu tulivyopotea, kwani tunaamini kuwa Allah ni tofauti na Mungu. Tunalumbana hadi tunatokwa jasho, na povu mdomoni, kwa umbumbumbu wa kutojua lugha. Taarifa iliyonifungua macho ni hii hapa.


Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...