Thursday, March 14, 2013

CHADEMA: Taarifa kwa Vyombo vya Habari, Machi 14, 2013

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 14 MACHI, 2013
Ndugu waandishi wa habari,
Tumewaita hapa leo, ili kupitia kwenu tuweze kutoa taarifa inayohusu kukamatwa kwa mmoja wa viongozi wa chama chetu, Wilfred Lwakatare, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, aliyekamatwa jana tarehe 13 Machi 2013, ofisini kwake makao makuu ya CHADEMA.
Jeshi la polisi linasema limemkamata Lwakatare likimtuhumu kuhusika na mashambulio ya watu mbalimbali kutokana na ushahidi uliopo kwenye walioita, viedo ambayo pia imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwanza, tunapenda kuwaambia umma wa watanzania na watu wote duniani kwamba, CHADEMA hakina nia yoyote ya kuzuia polisi kutenda kazi zake, iwapo watakuwa wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
Bali, tunachoeleza hapa ni jinsi polisi na vyombo vingine vya dola vinavyoshiriki katika kutengeneza paropaganda chafu dhidi ya CHADEMA za kuwahusisha viongozi wa CHADEMA na unyama unaoendelea nchini wa kutesa watu, kupiga, kung’oa kucha na baadaye kuwatekeleza wakiwa nusu mfu.
Mpango huu ulianza katika tukio la kutekwa kwa Dk. Steven Ulimboka, ukaenda kwa Mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi na baadaye kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda; na kwa bahati mbaya sana, kwa namna moja au nyingine, mkakati huu umekuwa ukilihusisha jeshi la polisi katika hatua za utekelezaji wake.
Kuweka kumbukumbu sawa, tunaweza kurejea suala la kuuawa kinyama kwa Mwangosi, unyama uliosimamiwa na kufanikishwa chini ya uangalizi wa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Mara baada ya tukio hilo, jeshi jeshi la polisi kupitia kamishana wake, Paul Chagonja lilitoa kauli kuwa Mwangosi alilipuliwa na kitu alipokuwa anawakimbilia polisi kujisalimisha akitokea kwa wafuasi wa CHADEMA, jambo ambalo limethibitika kuwa halikuwa na ukweli hata kidogo.
Mpaka sasa, jeshi la Polisi halijamchukulia hatua zozote za kisheria Kamhanda aliyesimamia na kufanikisha kifo cha Mwangosi, pamoja na ushahidi wa kuhusika kwake kuwepo wazi.
Aidha, pamoja na ukweli uliobainishwa na tume zote zilizotumwa kuchunguza suala la Nyororo Iringa, kusema Polisi walivunja sheria, walitumia nguvu isiyohitajika, bado mpaka leo hii wanachama 42 wa CHADEMA wanashikiliwa na polisi mkoani Iringa kuhusika na vurugu za Nyololo, Mufindi, Iringa. Waandishi mtakumbuka kuwa Taarifa ya Kamati ya Nchimbi ilitofautiana kabisa na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu nay a MCT. Baada ya kazi ya Tume na Kamati hizo hakuna Taarifa hata mmoja imetolewa na Polisi, walsa hakuna watu waliohojiwa tena ukiaachawaliokamatwa kabla ya Taarifa za Tume hizo. Wala sijaona kwa bahati mbaya vyombo vya habari vikichambua Taaarifa hizo kwa kina,
Katika nyakati mbalimbali, CHADEMA tumefungua jalada Polisi, na nyingine amezifungua Mhe. Lwaklatare mwenyewe akilalamikia mchezo mchafu tunaofanyiwa ikiwa ni barua kuandikwa kwa majina yetu, yenye sura ya kutuchafua. Mojawaopo ikidhaniwa kuandikwa na Rwakatare mwenyewe akiomba Tshs 200 millioni kwa ajili ya vijana anaodhaniwa kuwaleta toka Tarime kwa ajili ya Igunga. Hadi leo Polisi hawajamhoji Lwakatare mwenyewe, wala hatujasikia upepelezi wowte ukifanyika.
Aidha tulitoa Taarifa ya mtu aliyepewa bunduki wakati wa uchaguzi wa Igunga akituhumu kuwa amepewa bastola hiyo kwa lengo la kudhuru wakati wa Kampeni ya Igunga. Tumetoa mpaka nay a Bastola husika na mahali ilipotengenezwa. Polisi hadi leo hawajatoa Tamko lolote kama Bastola hiyo iliyotengenezwa China imesajiliwa kwa jina la nani, na hivi sasa ipo kwa nani. Lakini kwa tukio tu la Lwakatare na picha yake kubandikwa kwenye Mtandao, Polisi tayari wameisha kumkamata. Ni dhahiri kuna mchezo unachezwa dhidi ya CHADEMA, na Polisi kuiingizwa au kwa kujua au kutokujua katika mtego huo.
Sasa hapo mnaweza kujiuliza, hapo haki ipo wapi? Yaani waliotajwa na tume yaani polisi – wapo huru, lakini wanaCHADEMA 42 ambao hawakutajwa popote na tume wanasota gerezani.
Hata katika suala la Dk. Ulimboka, jeshi la Polisi halikutelekeza wajibu wake kikamilifu. Jeshi hilo limekataa kumhoji Dk. Ulimboka na wala kuwahoji baadhi ya watuhumiwa wakuu wanaotajwa kuhusika moja kwa moja katika kumteka Dk. Ulimboka, akiwemo Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka, Afisa wake Ramadhani Ighondo mwengine anayeitwa Nzowa.
Vilevile, kwenye tukio la kutekwa kwa Kibanda, ambalo linafanana kwa kiasi kikubwa na lile la Dk. Ulimboka, Afisa Mtendaji Mkuu wa New Habari Corporation, Hussein Bashe, ametaja kuhusika kwa polisi katika utekaji wa Absalom Kibanda, na baadaye akamtaja Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, lakini mpaka sasa, jeshi la Polisi halijachukua hatua zozote ama kwa waliotajwa au kwa aliyetaja.
Lakini katika hili la Lwakatare CHADEMA kilipata taarifa mapema kuwa upo mkakati unaoratibiwa na kufanikishwa na Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka na genge lake lenye wajumbe mashuhuri, Ramadhani Ighondo na Nzowa linalotaka kukihusisha CHADEMA na njama za kumdhuru Kibanda ili kukidhoofisha kisiasa. Lilipotokea hili la Lwakatare tukasema, sasa kile tulichoambiwa ndiyo hicho kimekuja.
Bahati njema gazeti la Mwananchi la leo linasema Lwakatare anatuhumiwa kupanga njama za kumdhuru Mhariri wa gazeti hilo, Denis Msacky, na kwamba Lwakatare amekamatwa baada ya kuonekana kwenye video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii haraka inayomuonyesha Lwakatare akipanga njama hizo hatujui baadhi ya taarifa zingine ingwa kwa hiki kilichopo kwenye mtandao hakuna popote alipotajwa Msaky. Si nia yangu kuingilia upelelezi wa Polisi, lakini nimesema CHADEMA tumefurahi kwa kuwa iwapo kwa utaratibu huu au wowote ule fursa itapatikana na ukweli wote kutolewa hadharani. Ni imani yangu kuwa zoezi hili litafuata sheria na taratibu zote zilizokwa na Katiba yetu kulinda haki za mtu.
Sasa kutajwa kwa Msacky inawezekana hilo la Kibanda halijaiva, au pengine liko njiani; ama wameona aibu kuliingiza kwa sasa.
Lakini Waandishi wa Habari, mnajua kuwa mara baada ya Kibanda kutekwa, Ridhiwani Kikwete na Nape Nnauye walivyoshangilia kutekwa kwa Kibanda katika mtandao huo huo uliotumika kumkamata Lwakatare bila kuwakamata wahusika hao ambao waliingia kwenye mtandao kwa ID yao wenyewe. Akiandika katika mtandao wake wa face book Ridhiwani alisema: “Na hili la Kibanda mtasema ni kazi ya Ramadhani Ighondo, afisa usalama pale Ikulu?”
Kwanza, kauli hii ya Ridhiwani ilikuwa inathibitisha kwamba aliyepanga njama za kumteka Dk. Ulimboka, ni Ramadhani Ighondo wa Ikulu.
Pili, Ridhiwani alikuwa anataka kuaminisha jamii kwamba katika hili la Kibanda, yeye na kundi lake hawahusiki, bali wanaohusika ni CHADEMA; hivyo akawa anachokoza mjadala ambao ulishapangwa ili baadaye vyombo vya dola viweze kuuchukua, na hivyo ndivyo ilivyotokea.
Tunazo taarifa kutoka vianzio vyetu vya ukakika ndani ya Usalama wa Taifa kuwa baada ya Ridhiwani kuweka andishi lake kwenye facebook, aliingia kiwewe sana hasa baada ya Hussein Bashe kuja juu. Ridhiwani anafahamu nguvu ya Bashe kwenye kufuatilia suala la kutekwa kwa Kibanda na hivyo amemuomba baba yake kuvitumia vyombo vya dola kumuokoa. CHADEMA haijawa na haitakuwa, lakini tuliyoambiwa yametimia, na mengine zaidi yanakuja, kwani kwa Taarifa zetu hiyo yaliyotokea “ni cha mtoto”. Na wala hatutaki kutabiri mbinu zitakazotumika kumwokoa.
Ndugu waandishi wa habari; katika mlolongo wa kuwakamata viongozi wa CHADEMA, yumo Mbunge wa Iringa, Mchungaji Msigwa. Mheshimiwa Msigwa tunaambiwa na watu wetu wamemtafuta kwa muda mrefu sasa. Wanasema sumu anazotema bungeni na kwengineko dhidi ya idara ya usalama ya taifa juu ya tuhuma za kuhusishwa na wizi wa nyara za serikali, zinawanyima usingizi na hivyo wanataka wamnyamazishe.
Wanataka kujua kutoka kwa Msigwa ni nani aliyevujisha na kumpa taarifa zile za ujangiri wa wanyama pori zinazohusisha CCM, usalama wa taifa, polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Msigwa anaonekana kuwa ni jasiri kusemea udhaifu wa idara ya usalama, wanaamini anavyo vitu vingi na wao wangependa wajue ana nini na anapewa na nani.
Tayari Mchungaji Msigwa ameondolewa kwenye kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na kupelekwa Kamati ya Kilimo ili kulinda uchafu wa serikali, wakati yeye ni waziri kivuli wa Maliasili na Utalii na Waziri kivuli anatakiwa kuwa Kwenye Wizara ya Sekta anayoisemea, na wala hajaomba Wizara ya Kilimo.`ni dhahiri syndicate ya mfumo huu wa kutaka kuisambaratisha CHADEMA. Huhitaji kwenda chuo Kikuu chochote, kuelewa hili.
CHADEMA kinafahamu kwa undani, kwamba uzushi huu wa Tape ya “Bukoba Boy”.Tunajua huu umeanzishwa na kuhusisha Usalama wa Taifa, akiwemo Ighondo na wenziwe pale Ada Estate. Huyu Ighondo ambaye anafahamika pia kwa jina la “Rama” tunamfahamu vizuri sana. Aliwahi kufanya kazi ya katibu wa UV-CCM wilaya ya Singida Vijijini, kati ya mwaka 2006 na 2008 na ndiye aliyekuwa akitumia simu na 0713760473 katika mawawsiliano yake na Dr. Ulimboka kwa simu na 0713731610 mpaka takriban dakika 3 kabla ya Ulimboka kutekwa. Gazeti la Mwanahalisi liliandika taarifa ya uchunguzi ya kina ya Jambo hilo.
Rais wetu amenukuliwa na magazeti ya Serikali Addis Ababa akisema kuwa Mwanahalisi ilifungiwa kwa sababu ya ‘kuchochea uasi katika majeshi yetu’ au maneno Kama hayo. Sitaki kumwita Rais wetu wwongo leo lakini kwa kuwa Taarifa hiyo haijakanushwa wala na Rais, wala na Ikulu, tunaamini maneno hayo ni kweli ametamka. Tunamtaka Rais Kikwete atamke maneno hayo hayo hapa nchini. Kwa njia yeyote ili ili Watanzana wengi na hasa wasomaji wa Mwanahalisi, na hata majeshi yetu amba kimsingi ninafahamu walilipenda Gazeti la Mwanahalisi wamsikie kwa masikio yao wenyewe. Taifa linawekwa pabaya sana Rais anapofikia kutoa matamko ya upotoshwaji mkubwa kiasi hicho tena nje ya nchi.
Ndiyo maana tunaposema Idara ya Usalama wa Taifa, ni tawi la CCM, tunaushahidi. Kwa mfano, tunajua jinsi baadhi ya watendaji wajuu wa idara hiyo kama vile, Zoka na vibaraka wake wadogo akiwamo Ighondo, ni radical wa CCM, wenye ushabiki uliopitiliza.
Hata ukiangalia jinsi walivyotekeleza mpango wa utekaji wa Dk. Ulimboka, kwamba walifanya hivyo mbele ya macho ya Dk. Deogratias Michael, haraka utabaini kuwa utekaji huu ulifanywa kwa ushabiki wa kulinda CCM.
Ndugu waandishi wa habari, kutokana na yote hayo hayo sasa tunasema ifuatavyo: Kwamba jeshi la polisi lifanye kazi yake bila ushabiki wa kisiasa au shinikizo la wanasiasa.
Ndugu Waandishi,CHADEMA haiko tayari kuruhusu watu wenye maslahi binafsi kutuchafua mbele ya jamii. Katika hilo, tutapambana na yoyote bila kujali cheo chake, madaraka yake serikalini, fedha alizonazo au madaraka mengine.
Wakati polisi wakitekeleza hilo, tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, ajitokoze hadharani kueleza umma juu ya mgogoro wake na Kibanda. Tunavyofahamu sisi, Kibanda aliteuliwa kuwa mjumbe katika kamati ya kubuni vazi la taifa. Lakini alijitoa na kusema aliyemteuwa yaani - Nchimbi - ambaye wakati huo, alikuwa waziri wa habari, utamaduni na michezo, ndiye aliyeshinikiza polisi kumfungulia kesi ya uchochezi mahakamani.
Hadi sasa hatujapata taarifa za wazi zinazoonyesha kama uadui wa wawili hawa uliisha, na kwamba Nchimbi sasa ndiye waziri wa mambo ya ndani, ambapo polisi wanawajibika kwake. Tuna mashaka kuwa uchunguzi wa tukio lililomkuta Kibanda unaweza kudhoofika.
Kutokana na hayo yote CHADEMA tunasema nini sasa:-
i) CHADEMA katika hatua hii ya awali, tunafuatilia kwa karibu sakata lote la ukamataji wa Lwakatare na kuona kama sheria za nchi, taratibu mbalimbali na misingi ya Haki za Binadamu inafuatwa kuikamilifu.
ii) Tunarudia tena madai yaliyotolewa mara nyingi na CHADEMA, kwa Rais kuandikiwa barua na Mwenyekiti wetu, Iundwe Judicial Commission of Inquiry (Tume Huru ya Kimahakama kuchunguza vifo vyote vyenye utata na sura ya kisiasa). Serikali inaogopa nini kuunda Tume hii huru ili ukweli Ujulikane? Iweje CHADEMA inayotuhumiwa Kupanga njama wanaishinikiza Serikali kuunda Chombo huru na Serikali ndiyo inayopata kigugumizi?

iii) Kwa wale walioumizwa na kujeruhiwa kama kina Ulimboka Kibanda na wengine, tunarudia Tamko letu la kuwa hatuna Imani na uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kuwa viongozi wa Jeshi hilo ni sehemu ya watu tunaowatuhumu kwa kuhusika kwa njia mbalimbali, na Ushihidi wa wazi na Taarifa mbili za Serikali kupingana yaani Taarifa ya Kamati yqa Nchimbi na Tume ya Haki za Binadamu. Tutaiaminije Polisi na Serikali kwa Taarifa ya Kamati ya Nchimbi? Mwendawazimu tu anaweza kuwa na imani baada ya Taartifa zile 3.
iv) Kuokana na upotoshwaji mkubwa, na kutokana na uhakika tulionao mkubwa Mwanahalisi ilifungiwa si kwa sababu yeyote ile, bali kutoka na kukomalia swala la Dr Uliomboka na hasa uhusika wa Ighondu, Afisa Usalama anayefanya kazi Ikulu chini ya Raisi mwenyewe. CHADEMA sasa tunaitaka rasmi Serikali ifungulie Gazeti nla Mwanahali kwa sababu hatuwezi kuendelea kuvumilia uikandamizaji huu wa uhuru wa Habari, ambao sasa unaelekea kuota mizizi nchini kwetu. Na kweli ninawaomba na kuwataka waandishi wote msimame imara, bila kujadili itikadi, au tofauti zetu zozote zile na kusimamia uhuru wa Habari. Tunataka vivyo hivyo, kwa wanaharakati mbalimbali. Waache hofu, eti wanaogopa kuhusishwa na vyama vya Siasa! Haki ni haki na haina rangi ya bendera ya chama chochote.
Ndugu Waandishi Nawashukuru sana
Imetolewa Makao Makuu ya CHADEMA, na,

Dr. Willibrod P. Slaa
KATIBU MKUU - CHADEMA

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...