Tuesday, September 5, 2017

Wadau Wanauliza Wanilipe Kiasi Gani

Siku chache zilizopita nilileta taarifa katika blogu hii kuhusu mwaliko niliopata kutoka Red Wing, kwenda kuongelea utamaduni wa hadithi. Tarehe 31 Agosti, wameniletea ujumbe kuniulizia iwapo kiwango cha malipo yangu ni kiasi gani. Huu ni utaratibu wa kawaida hapa Marekani. Mtu akialikwa kuhutubia, analipwa. Viwango vya malipo hutofautiana kulingana na umaarufu wa mwalikwa.

Suala la malipo ni tata kwangu, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Kipaumbele changu ni kutoa huduma kwa jamii. Malipo ni matokeo. Ninatoa mihadhara kwa wenye uwezo wa kunilipa na kwa wasio na uwezo wa kunilipa. Sipendi kuchukua pesa maadam tu ni pesa. Lazima nijiridhishe kuhusu uhalali wa hizo pesa.

Kwa msingi huo, ninatafakari ulizo kutoka Red Wing kuhusu malipo. Mwaliko wa Red Wing unahusu hadithi za jadi za wahenga wetu. Si hadithi zangu, kwa sababu sikuzitunga mimi. Ni urithi wetu wa tangu zamani. Sina hati miliki. Suala la kupokea malipo ni tata. Wale walionisimulia hadithi zilizomo katika kitabu cha Matengo Folktales, kwa mfano, hawakuwa na utamaduni wa kulipwa, na sikuwalipa.

Hata hivyo, nitakwenda Red Wing si kusimulia hadithi tu, bali pia kuongelea utamaduni wa kusimulia hadithi. Nitatoa elimu kuhusu suala hilo, kuanzia chimbuko la usimuliaji wa hadithi hadi kuhusu mchango wa hadithi katika jamii. Itakuwa kama darasa la fasihi simulizi. Kwa upande huo, kulipwa hakuna dosari.

Jambo la ziada ni kwamba kutoka hapa mjini Northfield ninapoishi hadi Red Wing ni mwendo wa saa moja. Nitatumia muda kuandaa mambo ya kusema na nitaingia gharama za safari. Ninaona ni sahihi kupokea malipo.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...