Thursday, September 27, 2018

Nimenunua Tena Tungo Zote za Shakespeare

Tarehe 24 Septemba, nimenunua tena kitabu cha tungo zote za William Shakespeare.  Nilikinunua katika duka la Half Price Books mjini Apple Valley nilipotoka Burnsville kuangalia kitabu changu kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Ingawa tayari nina vitabu vinne vyenye tungo zote za Shakespeare, sikuona tatizo kununua hiki pia. Kuwa na nakala mbali mbali za kitabu cha tungo za Shakespeare kuna mantiki nzuri kwa sababu tungo hizo zimehaririwa kwa namna mbali mbali. Hii imekuwa ni sehemu ya historia ya uchapishaji wa tungo za Shakespeare.

Mara kwa mara neno linaloonekana kwenye nakala fulani si lile linaloonekana kwenye nakala nyingine au limeandikwa kwa namna tofauti na lilivyo katika nakala nyingine. Hali hiyo ni ile inayoonekana katika miswada ya tungo za zamani, sehemu mbali mbali ulimwenguni, ikiwemo za huku kwetu, kama zile za Liongo Fumo.

Tofauti hazikwepeki, kwa sababu uandishi katika enzi za Shakespeare ulikuwa tofauti na wa leo. Leo kitabu kikichapishwa, tunategemea ni nakala sahihi ya mswada ulivyoridhiwa na mwandishi. Wakati wa Shakespeare, hapakuwa na utaratibu huo. Watu walikuwa wananakili andiko walivyoweza, na tofauti mbali mbali zilijidhihirisha kutoka kwa mnukuzi hadi mwingine.

Kadhalika waigizaji wa tamthilia majukwaani walikuwa wanatamka, pengine bila kujitambua, maneno yaliyofanana sauti, ingawa maneno ya mwandishi yalikuwa tofauti. Hiyo nayo ni sababu ya waandishi kuandika maneno tofauti.

Kwa hali hiyo, ni busara kuwa na nakala tofauti za kitabu hiki cha tungo zote za Shakespeare. Hata mtu ukiwa na kitabu cha tamthilia mojawapo tu, ni busara kuwa na nakala zilizohaririwa na wahariri tofauti wa kitabu hicho.

Faida nyingine ni kwamba baadhi ya nakala hizi zina maelezo ya wahariri juu ya mambo mbali mbali, yakiwemo maana za maneno na semi. Maelezo haya ni msaada mkubwa kwetu, kwani ki-Ingereza cha wakati wa Shakespeare kina tofauti nyingi na kiIngereza cha leo.

Monday, September 24, 2018

Nimekikuta Kitabu Changu Barnes and Noble

Baada ya kusikia kwamba kitabu changu kimewekwa sehemu maalum katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoandika katika blogu hii, leo nimeenda Burnsville kuangalia. Hapa kushoto linaonekana duka hilo, ambalo nimelitembelea mara kadhaa.





Hapa kushoto ndio mwonekano wa kabati ambapo huwekwa vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka. Kitabu changu kinaonekana hapo chini. Duka lolote la Barnes and Noble huwa na vitabu vingi sana. Ni kama maktaba. Kwa hiyo, kitabu kuuzwa humo si jambo la ajabu. Hakunaajabu yoyote kwa kitabu changu kuuzwa Barnes and Noble. Kama nilivyoandika juzi, kitab changu hich kimekuwepo kwenye mtandao wa Barnes and Noble kwa muda mrefu.





Kitu cha pekee ni uamuzi wa mhudumu wa duka kukipendekeza kwa wateja, kama inavyooneka hapa chini ya kitabu:

Short and sweet. A wonderful read about the differences between Africans and Americans. I feel wiser to the world after reading it.
Tafsiri yangu:
Kifupi na kitamu. Andiko la kupendeza ajabu kuhusu tofauti za tamaduni baina ya waAfrika na waMarekani. Najiona nimejiongezea werevu mbele ya dunia baada ya kukisoma.

Ninafurahi kwa sababu huyu mhudumu, mwenye uzoefu katika maktaba amesema hivyo. hudumu wa maktaba hapa Marekani ni msomaji wa vitabu. Anapopendekeza kitabu hawezi kupendekeza kiholela. Aanajua kuwa wadau wanaofika humo ni wa kila aina. Wengine ni wasomi waliobobea. Anaweka heshima yake rehani, kwani wadau wakinunua wakaona si kitabu bora, ataaibika yeye kabla ya mwandishi. Hiyo ni sababu ya wazi ya mimi kufurahi.

Friday, September 21, 2018

Kitabu Kimeingia Barnes and Noble

Kwa wasomaji wa vitabu hapa Marekani, jina la Barnes and Noble si geni, kwani ni jina la kampuni inayomiliki maduka mengi ya vitabu yaliyoko nchi nzima. Maduka ya Barnes and Noble ni maarufu kiasi kwamba watu wanapoongelea maduka ya vitabu, huwazia kwanza Amazon na Barnes and Noble.

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mhudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville, mwendo wa nusu saa kutoka hapa ninapoishi. Ameandika:

Hi Joseph. Just letting you know I put your book on the staff recommendation display at the Barnes and Noble Burnsville where I work. The book about cultural differences between Africans and Americans. I really enjoyed it!

Tafsiri yangu:

Jambo Joseph. Nakufahamisha tu kwamba nimeweka kitabu chako sehemu vinapoonyeshwa vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville ambapo ninafanya kazi. Kile kitabu juu ya tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani. Nilikifurahia sana!


Bwana huyu aliyeniandikia ujumbe alikuwa mhudumu wa duka la vitabu la hapa Chuo cha St. Olaf,  na ndipo alipokisoma kitabu changu. Yeye na wahudumu wenzake tulikuwa tukipenda kuongea. Kwa kuwa walikuwa wamesoma kitabu changu, walipokuwa wanaenda kujisaidia walipenda kusema, "kuchimba dawa," usemi waliouona kitabuni. Tulikuwa tukicheka. Nilikuwa nikivunjika mbavu na kujisikia raha kuwasikia hao wazungu wakiwa wa-Swahili namna hiyo. Niliona kitabu changu kimewagusa.

Nimefurahi kusikia kuwa kitabu changu kimeingia Barnes and Noble namna hiyo. Nasema ”namna hiyo” kwa maana ya kitabu kuwemo dukani, kwani, kwa miaka, kimekuwepo kwenye mtandao wa Barnes and Noble. Sitaki kusema mengi, nisije nikawa nahesabu vifaranga kabla havijaanguliwa, kama isemavyo methali ya ki-Ingereza. Nitasubiri nione.

Monday, September 10, 2018

Mdau Wangu Mpya

Juzi, tarehe 8, nilikwenda Coon Rapids, Minnesota, kuhudhuria uzinduzi wa jarida liitwalo L Magazine. Jarida hilo linalohusu zaidi masuala ya uandishi, uchapishaji, na uuzaji wa vitabu, limeanzishwa na Bi Bukola Oriola mwenye asili ya Nigeria anayeishi hapa Minnesota.

Kati ya watu waliohudhuria ni Dr. Artika Tyner, rafiki wa karibu wa Bi Oriola. Dr. Tyner ni "Vice President for Diversity and Inclusion" wa Chuo Kikuu cha St. Thomas. Anaonekana pichani akiwa ameshika tuzo alizopewa hiyo juzi kwa mchango wake kwa jamii.

Alipotambulishwa kwangu kwenye meza nilipoweka vitabu vyangu, tuliongea kiasi kuhusu shughuli zake na zangu. Alinunua vitabu vyangu, zikiwemo nakala 9 za Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Vile vile alielezea hamu yake ya kuendelea kuwasiliana nami ili tutafakari namna ya kushirikiana katika programu zinazohusu Afrika na watu wenye asili ya Afrika yaani wanadiaspora.

Nilitambua kuwa Dr. Tyner ni mmoja wa waMarekani Weusi ambao wana mapenzi ya dhati na Afrika. Hata mavazi yake yanaashiria hivyo. Ametembelea Afrika na anahamasisha programu za kupeleka watu Afrika. Dr. Tyner ni mtu maarufu, na kwa upande wangu kigezo kimoja ni kwamba ameshatoa mhadhara wa TED kuhusu elimu na mabadiliko ya jamii.


Ninafurahi kumpata mdau huyu mpya. Ninategemea kuendelea kubadilishana naye mawazo na uzoefu na kufanya shughuli mbali mbali za kuelimisha.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...