Tuesday, October 26, 2010

Mbumbumbu Waache Kugombea Uongozi

Kitu kimoja kinachonikera ni jinsi wakati wa kugombea uongozi, mbumbumbu wengi wanavyojitokeza kuwania uongozi. Halafu, kwa jinsi wapiga kura wengine walivyo mbumbumbu, wanawapigia kura hao mbumbumbu wenzao na kuwawezesha kushinda.

Baada ya hapo, kunakuwa na matatizo mengi. Tatizo moja kubwa ni jinsi hao mbumbumbu wanaoitwa viongozi wanavyojifanya miungu. Hawakubali kukosolewa.

Kwa mfano, gazeti likiwakosoa, wanalitishia au wanazuia lisichapishwe. Kama kuna kitabu kimewakosoa, wanakipiga marufuku. Msimamo wangu ni kuwa watu wasiojiamini au wasioheshimu uhuru wa watu kutoa fikra, wasigombee uongozi.

Nchi inahitaji viongozi wa kweli, ambao wanatambua kuwa wao si miungu, na ambao hawatetereki kwa kukosolewa. Kibaya zaidi ni kuwa hao mbumbumbu wanadhani kuwa wao ndio nchi. Wakikosolewa, wanasema ni hatari kwa usalama wa taifa. Ni usalama wa taifa au ni usalama wa mbumbumbu? Ni taifa gani ambalo linatetereka kwa sababu ya mbumbumbu kukosolewa?

Haya ninayosema nayasema kwa dhati. Mimi mwenyewe ninakosolewa na hata kutukanwa. Kwa mfano, soma hapa, na hapa.

Sioni sababu ya kuwazuia watu wanaofanya hivyo, hata kama ningekuwa kiongozi. Ni muhimu watu wawe huru kutoa mawazo yao. Ingawa tunasema kuwa tutumie lugha ya kuheshimiana, na mimi nakubali hivyo, lakini hatimaye nasema kuwa hata anayetukana anakuwa amepata fursa ya kujieleza. Ni bora iwe hivyo kuliko kuwafunga watu mdomo, kwani madhara ya kuwanyima watu fursa ya kujieleza yanaweza kuwa mazito. Nimefafanua zaidi msimamo wangu huo katika kitabu cha CHANGAMOTO.

Napenda kurudia, mbumbumbu waache kugombea uongozi. Nafasi hizi zinahitaji viongozi, si watu ambao hawajiamini.

4 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Mzizi wa kuwa na wagombea mbumbumbu ni vyama vya kigaidi na mfumo wa kifisadi. Wagombea hawa ni tunda la waramba viatu na wasasi ngawira waliojazana kwenye vyama. Bahati mbaya sana kuna hata mbumbumbu wenye hata masters na PhD kwenye genge hili la wezi. Nchini Kenya mbumbumbu Daniel arap Moi aliweza kuwatumia 'wasomi' kama Prof George Saitoti alivyotaka lakini wao wakashindwa kumtumia. Nchini Tanzania tunao wasomi kama Dk Masumbuko Lamwai, Dk Waridi Kaboro, Dk Daudi Balali na wengine ambao walijirahisi na kukubali kutumiwa na watu wenye elimu ndogo ukilinganisha nao.
Leo tuna wagombea kama JK wanaoogopa hata mdahalo. Nani angeamini kuwa mtu asiyejiamini wala kuwa na lolote kama Kikwete angewageuza tunaodhani wasomi kama Prof. Rwekaza Mukandala, Dk Benson Bana na wasomi wengine nepi kufua nguo zake chafu yaani kuchakachua matokeo ya utafiti kiasi cha kumfurahisha?
Nani angeamini kuwa Rostam Aziz angeweza kuwatumia Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wakidhani wanamtumia? Nani alidhani kihiyo kama Yusuf Makamba angewayumbisha wasomi waliojazana kwenye genge la Mafisadi la CCM?


Watanzania si majuha. Hawatamchagua JK-atachaguliwa na kina Luis Makame, Shimbo, Said Mwema na vijana wake dhidi ya utashi wa watanzania.

Nihitimishe kwa kuwachakazia wananchi kutokubali matokeo yaliyopikwa na kuchakachuliwa kuwapitisha wagombea vihiyo na mafisadi.

Simon Kitururu said...

Kuna mbumbumbu anaweza kuhisi umemtukana kwa hii ATIKO.

Then again,...
...Labda mbumbumbu huwa hawajijui ni MBUMBUMBU kitu kiwezacho kufanya swala zima lisieleweke kwa wahusika.

Nawaza tu kwa sauti!:-(

Mbele said...

Shukrani kwa mawaidha yenu. Mwalimu Nyerere, katika hotuba na maandishi yake, aliongelea sana umbumbumbu. Na hao mbumbumbu alikuwa akielezea tabia zao, maamuzi yao, na vitendo vyao.

Mwalimu hakuwa na tabia ya kuwataja majina, lakini kwa jinsi alivyokuwa anafafanua maelezo yake ilijulikana wazi ni akina nani hao mbumbumbu wenyewe :-)

Simon Kitururu said...

Lakini HAKI YA NANI naamini Mambumbumbu waliokuwa chini ya NYERERE walikuwa hawaelewi anaongea nini.


Naamini angetoa mtihani ili nani awe kiongozi Tanzania katika serekali yake wengi wangefeli .


Ingawa najua pia wasomi kibao BONGO wasifiwao wanaakili na ndio maana wanaitwa WASOMI kunamajibu walikariri ILIKUPASI MITIHANI lakini ukiwaCHALENJI kwenye ISHU aka HOJA unashangaa kuwa hivi ni kweli huyu ni Profesa wa Mchwa lakini haelewi tabia za mchwa hata za kujenga daraja KIMCHWA ili MCHWA wavuke mfereji?




Ni wazo tu zaidi KWA SAUTI baada ya KUMSOMA Prof. ambaye KAMA KAWAIDA kilimbwata asemacho ,aandikacho hunifikirisha.:-(

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...