Thursday, October 28, 2010

Mgombea wa CCM Kufanya Mahojiano

Zikiwa zimebaki siku tatu tu hadi uchaguzi ufanyike nchini Tanzania, tumepata habari kuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM atafanya mahojiano na vyombo vya habari. Hii ni tofauti na msimamo wa CCM katika kipindi chote cha kampeni, ambapo wagombea wake walikuwa hawashiriki midahalo.

Wengi wetu tunafahamu kuwa midahalo, mahojiano, na kadhalika, ni mambo muhimu katika jamii inayothamini elimu. Sasa kwa nini CCM haikutambua hilo kabla? Tena CCM ni chama chenye wanachama milioni kadhaa, wakiwemo "wasomi" wengi.

Ni lazima niulize: hao ni wasomi kweli au ni wababaishaji? Ni aibu kuwa hawakuweza kuchangamka kabla na kutambua umuhimu wa midahalo, hadi saa hii ya mwisho, na baada ya Dr. Slaa kuonyesha mfano.

Mimi kama mwalimu, na pia raia ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, nawajibika kuwashutumu CCM kwa kutoonyesha mfano bora, pale walipotamba kuwa mgombea wao hahitaji kushiriki midahalo. Na pamoja na hayo, wagombea wao wote wakawa hawashiriki midahalo. Sijui kama ilikuwa ni fikra zao au ndio nidhamu ya chama. Kama ndio nidhamu ya chama, ni heri nibaki bila chama, kuliko kuwa katika himaya ya udikteta.

Narudia kuushutumu uamuzi wa kutoshiriki midahalo. Na hao wagombea wote nawashutumu kwa kutii amri isiyo na busara kama hiyo. Je, sasa, kwa vile JK ameamua kufanya mahojiano, nao watakimbilia kwenye vyombo vya habari kufanya mahojiano? Akili gani hiyo? Mimi kama mwalimu, lazima niulize: tunawafundisha nini watoto wetu, ambao ni taifa la kesho?

Baada ya kusema hayo, mimi kama raia mwema, ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa, nina masuali kwa mgombea wa CCM. Kwa vile hakuna muda wa kuuliza yote, nitauliza matatu tu.

La kwanza ni kwa nini wale ambao Dr. Slaa amewataja katika orodha yake ya mafisadi hawajampeleka mahakamani hadi leo?

La pili ni je, kwa nini CCM inadai kuwa amani Tanzania inatokana na uongozi wa CCM, wakati CCM inashiriki kikamilifu katika kuhujumu amani, hasa nyakati za kampeni na uchaguzi? Mifano ni mingi, kuanzia Visiwani hadi Bara, na hata ripoti za kimataifa zinathibitisha hilo. Kwa mfano, soma hapa na pia angalia video hizi hapa.

Ukweli ni kitu muhimu sana. Je, CCM haitambui kuwa wanaotunza amani Tanzania kikweli kweli ni sisi mamilioni ya raia ambao si wanachama wa chama chochote cha siasa? Hatuna rekodi yoyote ya kuvuruga amani kama wenzetu wenye vyama wanavyofanya. Kwa nini CCM inafunika ukweli huo?

Suali la tatu ni je, CCM ina maelezo gani kuhusu shutuma alizotoa Mwalimu Nyerere dhidi ya CCM katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania? Kuzifahamu kwa ufupi shutuma hizi, soma hapa.

3 comments:

Subi Nukta said...

Profesa Mbele!
Asante baba!
Asante sana kwa kuongeza kilio chetu tuliotaka mdahalo. Mwanzoni kabisa kwa kampeni hizi niliandika katika wavuti.com umuhimu wa mdahalo, lakini nadhani sisi ni kelele zisizomzuia mwenye nyumba kupata usingizi.
Chama chenye kigeugeu hivi, mara hatutaki mdahalo, mara mdahalo Jumapili baada ya uchaguzi (sijui kwa faida gani, bora wangeita 'tathmini') na sasa wamekubali mdahalo ambao kwa walivyosema, sidhani kama ipo hadhi ya kuita mdahalo bali 'maswali na majibu' tena yanayofanywa na waandishi wa habari tu.
Nimewatoa maanani kwa hili la kuwakosesha wananchi haki ya kumwuliza na kuhojiana na viongozi au wawakilishi wao, kumbe wananiomba ridhaa ya kuwakilisha bila kutaka tuzungumze ili iweje? Kama si dharau hiyo ni nini? Wao waseme tu mimi nisikilize na wananilazimisha kuamini kuwa kila wanachoniwazia ni kizuri bila ya kunipa nafasi ya mimi kujadili uzuri huo? Wanajuaje kuwa wanachodhani kizuri ni kweli nakipenda? ndiyo aina ya mabavu, udikteta na dharau (au vyote kwa pamoja). Hapo CCM wameniudhi kwa kweli hata kama sina maana yoyote kwao, lakini kama mwananchi, nahisi kupunjwa uhuru kamili wa demokrasia. Wasikae warudie upuuzi huu. (ndiyo ni upuuzi).

Christian Bwaya said...

Nadhani huu si mdahalo. Hiki ni kikao cha kujaribu kujibu hoja za washindani wanaotishia madaraka ya CCM hivi sasa. Mwanzoni waliwadharau wakawaona si lolote. Tukitaka kujua si mdahalo, tutizame hadhira iliyoruhusiwa kushiriki (waandishi wateule ambao bila shaka watauliza anachotaka kusikia mgombea wanayemshabikia.)

Nasikitika sana kukubaliana na ulivyosema, kwamba CCM imeonyesha mfano mbaya kwa wana wa taifa hili. Tunajenga taifa lisilotaka kufikiri wala kujadiliana na badala yake tunathamini ghiliba na propaganda.

Christian Bwaya said...

Niliuona "mdahalo" wenyewe. Maswali yaliulizwa na watu walioonekana kuandaliwa kabla. Hiyo tisa. Kumi, ni namna yalivyojibiwa. Kweli kazi tunayo Tanzania.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...