Mwalimu Nyerere Aliongelea Uozo Katika CCM

Mwalimu Nyerere aliongelea uozo katika CCM. Kwa mfano, wakati alipokuwa anajiandaa kung'atuka uenyekiti wa CCM, alizunguka nchi nzima akikagua uhai wa CCM. Wakati wa ziara hiyo, inaonekana Mwalimu alitatizwa na yale aliyoyaona. Aliwahi kusema kuwa kuna watu ndani ya CCM ambao hata mtihani juu ya Azimio la Arusha hawawezi kupasi.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe
. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Mwalimu Nyerere aliongelea hayo miaka yapata ishirini iliyopita. Leo hali ikoje? Kwa mtazamo wangu, uozo aliosemea Mwalimu umeongezeka. Hayo yamekuwa mawazo yangu tangu zamani. Kwa mfano, soma hapa.

Comments

...na ni katika uozo huo vyama vinavoitwa vya kishenzi vitaingia madarakani...

hata kama si wakati huu, watu watachoka na miaka michache ijayo watu watafanya kweli
malkiory said…
Asante Profesa Mbele kwa changamoto hii. Mpiganaji Chacha, umenena kwa hili, siku za mwizi ni arobaini tu.
Mbele said…
Shukrani kwa mchango wenu. Ingekuwa wa-Tanzania wana utamaduni wa kusoma vitabu, wangeshafahamu vizuri hayo aliyoandika Mwalimu Nyerere, na mengine mengi.

Matokeo yake ni kuwa CCM haingeweza kutamba kama inavyotamba. Umbumbumbu wa wa-Tanzania ndio unaoipa CCM fursa ya kutamba.

Kwa mfano, wakati wa mkutano mkuu wa CCM kule Dodoma mwaka huu, nilikuwa Tanzania. Kati ya mengi niliyoyasikia kutoka Dodoma ni wimbo uliosema kuwa wapinzani kuingia Ikulu haiwezekani.

Utaona kuwa fikra hii ni kinyume kabisa na msimamo wa Mwalimu Nyerere. Lakini kwa vile ni mambo ya vitabuni, watu hawayajui.
Anonymous said…
Masanga umenena unaposema, "Ingawa Mwalimu Nyerere ndiye mwanzilishi wa sera na falsafa nyingi zilizotufikisha hapa tulipo lakini atabakia kuwa msema kweli ambaye hakuogopa kukemea pale alipoona mambo hayaendi sawa; na madondoo haya mawili ni ushahidi mzuri."

Mungu alitupenda kwa kutujalia kiongozi kama yeye. Tanzania tunaingia maji marefu...ila msingi aliotuachia nadhani utatuvusha. Mungu Ibariki Afrika. Mungu Ibariki Tanzania.

Majaliwa
emuthree said…
Rejea za mwalimu Nyerere zinaeleza mengi, lakini nasikitika kusema zinatumika kama `siasa' ya kuficha `madoa yetu' yaliyosababishwa na uchafu.
Ndio hatupendi yaitwe uchafu, ukisema hivyo unaweza kubandikwa kosa la `kukashifu' lakini Nyerere hakuogopa akatumia neno `kansa'
Nani aiyeogopa kansa, kansa ni ugonjwa hatari, na kutibika kwake ni kuwahiwa...sasa kwanini atumie neno hilo,...kansa, inavyoachwa ndivyo inavyoumiza na mwishowe ikifikia pabaya haitibiki!
Sasa je kansa hiyo imegundulika, na kama bado imefikia hatua gani? Tusisubiri ifikie pabaya...hilo neno lina maana zaidi ya `siasa'....
Ni hayo tu. Tuendelee kuilea hiyo kansa, ...
Mbele said…
emu-three, shukrani kwa mchango wako. Ningekuwa na hela nyingi, ningenunua vitabu vya Mwalimu Nyerere, halafu ningevipeleka mashuleni na kuwahimiza watoto wetu wavisome na kuvitafakari.

Mimi mwenyewe nashukuru nilipata fursa ya kuvisoma. Hata nilipokuwa nasomea digirii ya juu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, nilipata fursa ya kutafakari maandishi ya Mwalimu Nyerere. Kwa mfano, nilifanya uchambuzi na kuandika makala kuhusu "Azimio la Arusha."

Baadhi ya walimu wangu walikuwa Marehemu Profesa Gilbert Gwassa na Marehemu Profesa Haroub Othman.
Unknown said…
Nimefurahia sana nukuu hiyo kutoka kwa Mwalimu. Watu wenye uchungu na nchi hii wapo, hata kama ni wa kuheshabu. Watu hawa wapo CCM na nje ya CCM. Inawezekana kabisa kwamba wale walio na uchungu huo na wapo CCM pengine wanavuta subira kuona watayarekebisha vipi makansa kibao yaliyojaza kwenye chama hicho ... kama alivyosema Mwalimu. Walio nje ya chama hicho wana nafasi nzuri zaidi ya kuyasema kwa uwazi na kuyakemea ili kwamba Watanzania tuamke. Utamaduni wa sisi kusoma vitabu bado uko chini sana. Ukituambia ngoma, harusi, ulabu ... tuko juu. Kumbe basi ili kuleta mapinduzi ya kweli ndani ya CCM na katika nchi nzima kwa ujumla ni kusaidiana kuelimishana kupitia njia zote zilizopo. Najua kuna utata kuhusu matumizi ya ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu ... hasa kutokana na sakata la hivi karibuni ... lakini kama ni ujumbe wa kuelimisha na si wa uchochezi kwa nini usitumwe? Siku hizi simu za mkononi zipo kila kona ya nchi yetu na habari inaweza kusambaa kwa kasi sana kupitia njia hiyo. Tuko pamoja.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini