Thursday, August 2, 2012

Kwenye Baa Hakuna Udini

Katika wiki sita zilizopita, nimepata fursa ya kuichunguza nchi yangu kwa karibu. Kitu kimoja kilichonigusa, ingawa sio kigeni, ni kwamba kwenye baa hakuna udini. Niliamua niandike makala hii kuhusu jambo hilo, kwani naona linasisimua.

Nimezunguka Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Songea, na kwa vile baada ya shughuli zangu za mchana napenda jioni kuvinjari baa, nimejikuta nikijumuika na wa-Islam na wa-Kristu katika baa kwenye miji hiyo. Kilichobadili hali hiyo ni ujio wa Mwezi Mtukufu.

Lakini kabla ya hapo wa-Islam na wa-Kristu tulikuwa tunajumuika vizuri kabisa huko baa. Hatubaguani bali tunakaribishana. Tunaongea; tunapiga soga; tunajenga mahusiano mema. Kwenye baa moja Tanga, nilipata fursa ya kuongea na meneja, ambaye ni mu-Islam. Mada yetu ilikuwa ulabu.

Nilianza mimi, kwa kusema kuwa katika dini yetu, hatukatazwi kunywa pombe. Tunakatazwa kulewa. Meneja naye akaionyesha kidole bia yangu na kuniambia kuwa kwa mu-Islam, ile bia yangu ni haram. Muislam haruhusiwi kuinywa hata kidogo.

Tuliongelea mitazamo ya dini zetu kwa ustaarabu na kuheshimiana hadi mwisho. Tulielimishana. Maongezi yale yalitufanya tuelewane na kufahamiana. Kwenye baa hakuna udini.

Kinachoshangaza ni kuwa katika nchi hii hii kwenye nyumba za ibada hatujumuiki watu wa dini mbali mbali. Tunatengana kabisa. Ni ajabu. Lakini je, Mungu amewakataza wa-Islam wasihudhurie ibada za wa-Kristu? Je, Mungu ametukataza wa-Kristu tusihudhurie ibada za wa-Islam?

Sio hilo tu. Kuna nyumba za ibada nchini mwetu ambako wahubiri wanaeneza udini na wanakazana kukashifu dini za wengine. Je, Muumba anayakubali hayo? Inakuwaje kwenye baa kuwe ndiko sehemu tunakoheshimiana watu wa dini mbali mbali, wakati kwenye hizo nyumba za ibada mafundisho ni ya kujenga chuki na uhasama? Inakuwaje kwamba kwenye baa ndiko kuna busara kuliko kwenye hizo nyumba za ibada? Ni ajabu kweli kwamba ni bora mtu aende baa, kuliko kwenye hizi nyumba za ibada. Tulifikaje hapo?

7 comments:

Simon Kitururu said...

Umeniwazisha sana tu Prof.!Na siku hizi kirahisi wapayukao sana neno AMANI unaweza kukuta ndio waanzisha VITA yani!:-(

Simon Kitururu said...

Ila kwa ujumla mie naamini Tanzania hatuna Serekali yenye nguvu sasa hivi ndio maana kuanzia , UDINI ,...tatizo la MALAWI.... tukiachilia mbali mapungufu kidhaifu ambayo hayahitaji hata misaada kama tuaminishwavyo yafanyavyo TANZANIA imelala!:-(

Anonymous said...

Prof, unapaswa ujue kuwa kuna Waislamu jina(wengi wao wamezaliwa tu na wazee wa Kiislamu) na Waislamu waliosoma dini yao. Uislamu si dini ya kuzaliwa kama ulivyo ukristo na baadae kwenda kubatizwa. Uislamu ni matendo. Ni sawa na kusema Waislamu ndio magaidi. Matendo ya watu ndio yanayowapelekea kujulikana imani zao. Hao unaowaona kwenye vilabu vya pombe wanakunywa wanaitwa "wanafiki". Katika Uislamu hao ni wabaya kuliko makafiri. Katika Quran tunaambiwa kuwa wanafiki watakuwa wa mwanzo kuingia motoni na watakuwa chini kabisa. Angalia aya hii:
4:145 The Hypocrites will be in the lowest depths of the Fire: no helper wilt thou find for them;
Kwahiyo hilo naomba ulijue.
Kuhusu ubaguzi wa kidini, upo sehemu nyingi ikiwemo chuo kikuu Dar. Walimu wengi walioonekana kuwa ni Waislamu wa kweli pale chuoni, walikuwa wakipata vitisho na kuitwa wakiulizwa masuali kuhusiana na misimamo yao.Pia bahati mbaya katika shule za Wakristo iko ubaguzi wa dini.Nakumbuka niliwahi kuwatembelea vijana wa Kiislamu katika shule za bara na walikuwa wakilalamikia kuwa walikuwa wanalazimishwa kwenda kusafisha mabanda ya nguruwe na wakizuiliwa kusali.

Mbele said...

Ndugu Anonymous, shukrani kwa changamoto yako. Hapa kijiweni pangu ni sehemu ya fikra huru, kwa hivi jisikie nyumbani.

Nina dukuduku na masuali kadhaa kutokana na kauli zako. Kwanza umesema kuwa u-Islam ni matendo. Kama ni hivyo, basi wale wa-Islam ninaojumuika baa angalau wana hii dalili moja kuwa ni wa-Islam, kwani matendo yao ni pamoja na kuwa sambamba na binadamu wenzao bila ubaguzi, bila udini. Nimeeleza hayo katika makala yangu.

Umewaita hao "wanafiki." Hapo nashindwa kukubali, kwa sababu anayemjua mnafiki ni Muumba peke yake. Binadamu hana upeo wa kumjua binadamu mwenzake kiasi hicho, na akijipa wadhifa wa kumhukumu mwenzake namna hii, naona anajifanya yeye ana uwezo wa Muumba. Katika dini zetu, hiii huitwa kufuru.

Napendekeza kuwa sote tuwe makini na suala hilo la kuwahukumu wenzetu, kwani tunajiweka katika hatari ya kutotambua uwezo na wadhifa wa Mungu (Allah).

Umesema pia kuwa "Katika Uislam hao {wanafiki} ni wabaya kuliko makafiri. Mimi nakunywa nao baa na sijaona ubaya wao. Ni watu wazuri, ambao tunakaa nao pamoja kwa amani. Siwaogopi, bali nawaogopa wale ambao wamejiaminisha kuwa wao ni waIslam safi kabisa, (yaani akina Boko Haram, Al Shabab na wengine) na wanatuvizia ili watulipue huko baa. Hao ndio nawaogopa.

Unafanya vema kunukuu Quran. Waumini tunapaswa kurejea kwenye misahafu, ili tusipotee njia. Lakini Quran ni kitabu cha Allah. Anayeongea ni Allah. Na mwenye ufahamu kamili ni Allah.

Tukisoma aya kama hiyo uliyonukuu, haimaanishi kuwa sisi binadamu tunaweza kumtambua nani mnafiki, ingawa ametajwa katika Quran. Mwenye uwezo wa kumtambua mnafiki na kumwadhibu ni Allah. Kama nilivyosema hapo juu, wanadamu tujihadhari na hiki kishawishi cha kujitwalia mamlaka ambayo hatuna, kwani sisi ni viumbe dhalili mno.

Makala yangu iliongelea suala la kutokuwepo udini katika baa. Sikujiingiza katika kuongelea uwepo au kutokuwepo kwa udini sehemu zininge katika jamii ya Tanzania. Tukitaka kuongelea suala hilo kwa upana, basi, tutataja sehemu nyingi, taasisi nyingi, za wa-Kristo na za wa-Islam.

Kwa mfano hatuwezi kufumbia macho udini uliopo Visiwani, ambako makanisa zaidi ya ishirini yamechomwa moto. Hilo nalo itabidi tulijumlishe katika uchambuzi. Tusimpendelee mdini m-Kristu, wala mdini mu-Islam.

Umetoa mfano wa wa-Islam kushurutishwa kwenda kusafisha mabanda ya nguruwe. Kama hilo limetokea, na jambo la kulaaniwa na yeyote anayeheshimu imani za wanadamu wote. Papo hapo, nami nimesikia kuwa kuna sehemu fulani Tanzania ambako m-Kristu akionekana anakula wakati wa Mwezi Mtukufu ananyanyaswa.

Hiyo nayo ni hujuma, kwani Mwezi Mtukufu ni wa wa-Islam, sio wa-Kristu. Mimi m-Kristu nikienda sehemu ya aina ile, nahitaji kuona hoteli ambapo naweza kupata chakula. Naziheshimu dini zote, na nategemea nami kuheshimiwa kutokana na imani yangu.

Tutafakari mambo hayo kwa uwazi. Napenda kugusia pia hoja yako ya mwanzo kabisa, kwamba kuna waIslam jina, yaani ni kwamba tu wamezaliwa na wazee wa ki-Islam. Naona hii ni hoja muhimu.

Sasa basi, wale wa-Islam waliosema wataendesha kampeni nchi nzima ili kushinikiza sensa iwe na kipengele cha dini, walikuwa na huu upeo wa kupambanua waIslam na wa-Islam jina? Au maana yao ilikuwa kwamba kila Hassan, Maryam, Mustafa, na Zubeda ni mu-Islam?

Na je, wakati ule wa mgogoro wa shule ya Ndanda, tulipoambiwa waIslam wananyanyaswa pale, palikuwa pamefanyika uchambuzi na kubaini kuwa wale wote walikuwa ni wa-Islam au walikuwepo pia wa-Islam jina? Tufanye uchambuzi huo nchi nzima?

Anonymous said...

Prof,
Hao jamaa wanaojiita Waislamu na kisha ukawakuta baa hawana matendo mema kwa mujibu wa Uislamu. Uislamu uko very clear unaposema katika aya tofauti kuwa "wale walioamini na kisha wakafanya matendo mema". Matendo mema katika Uislamu Uislamu yako very clear na baadhi yake yanafanana na matendo mema ya dini nyengine. Matendo mauvo pia yako wazi. Sasa kunywa pombe ni katika mambo yaliyokatazwa katika Uislamu. Sasa mtu anaekunywa pombe anakuwa ni mnafiki. Wanafiki wanajulikana wazi katika Uislamu. Quran imetufahamisha wanafiki ni nani na katika hadithi za Mtume(SAW) zimeweka alama zote za wanafiki.(Ukipenda na nikipata nafasi naweza kukuelezea alama hizo)
Kwako wewe hao jamaa unaokunywa nao hawana makosa, lakini katika Uislamu hao wana makosa.
Kauli yako hii nahisi ni sawa na wale wanaowahifadhi Al Qaeda kule Pakistan. Wanawahifadhi kwasababu wanawaona hawana makosa, Wanaona wanaenda nao msikitini, wanafunga nao na wanawapatia misaada. Wao wanahisi Al Qaeda kushambulia Wamarekani au kushambulia watu wanaotofautiana nao wakiwemo Mashia, kwao wao sio makosa hayo. Lakini haya ni makosa katika Uislamu. Kwahiyo it does not matter kwamba wewe unamuona mtu ni mwema machoni mwako. Kama mtu anafanya matendo yalitokatazwa katika Uislamu na akajiita Muislamu, Uislamu hauna jina la kumuita mtu huyo isipokuwa ni mnafiki. Huyo ni muovu mbele ya Uislamu. Huyo ni muovu kuliko kafiri. Kwasababu huyo ni adui "miongoni mwenu"(Chui alievaa ngozi ya paka au mbuzi).

Kwa kuwa uko nje muda mwingi inaonekana hujui kinachoendelea Zanzibar. Unachokijua ni kile ulichosoma kwenye magazeti.Sijui kama katika taaluma hili ni sawa kuongelea kitu ambacho hujakifanyia utafiti. Mtu kama wewe uliesoma usifanye analysis kwa kauli za kusikia.Ukitaka kujua kilichotokea Zanzibar, ama njoo ufanye utafiti au uliza watu walioshuhudia. Usiwe "simplistic" kiasi hicho. Mimi nakuheshimu sana kwa elimu yako. Na napata tabu sana kuona wakati mwengine unavyochambua mambo kama watu wanaotaka kuuza magazeti yao.

Alshabab, Boko Haram na wengineo kama hao ni makundi ya wanafiki. Matendo yao ni maovu.

Inaonekana hii mada unaipanua zaidi na zaidi. Kwa bahati mbaya nasikitika sina muda mwingi wa kuandika, lakini kwa ufupi sisi Waislamu tunatakiwa tuwaogope watu wote ambao matendo yao hayaendani na mafundisho ya dini ya Kiislamu

Anonymous said...

profesa Mbele asante sana,hilo mimi nilikuwa silijui kwamba kumbe kwenye baa watu wa dini tofauti tunapendana asante kumbe kusoma ni kuelimika hilo nalo nimelipata ni kweli pamoja na huyo anon kupinga lakini baa ndio kuna upendo zaidi kuliko kwenye nyumba za ibada maana kwenye nyumba za ibada kumejaa vitisho mara kwenda motoni,mara sijui nini.asante sana yaani leo umenipa kitu ambacho sikukitegemea.ni mimi mwislamu ni siyekuwa wa kuzaliwa.vipi bado upo songea dar utapita lini?

Mbele said...

Ndugu Anonymous wa kwanza, ungefanya vema kutusaidia sisi wengine kufahamu yaliyotokea Zanzibar.

Kama Muumba amekupa fursa ya kuishi na kufahamu jambo, unawajibika kuwamegea wengine, kwani chochote tulicho nacho kinatoka kwa Muumba, na ni dhamana.

Kama tunakubaliana, hebu tupe angalau dondoo kuhusu ukweli wa yaliyojiri Zanzibar.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...