Thursday, August 23, 2012

"The Satanic Verses:" Kitabu Kigumu Kukielewa



The Satanic Verses, kitabu cha Salman Rushdie,  ni kitabu ambacho nimekiona kigumu kukielewa. Nilinunua nakala miaka mingi kidogo iliyopita, nikaanza kusoma, lakini sikufika mbali.

Mtindo aliotumia Rushdie katika kuandika kitabu hiki unahitaji msomaji awe amesoma sana vitabu vingine. Inatakiwa msomaji awe anajua mambo mengi, kuanzia yale ya falsafa hadi ya hadithi na dini. Vinginevyo, ni rahisi kutoka kapa unapojaribu kusoma The Satanic Verses.

Mwandishi maarufu Nadine Gordimer wa Afrika Kusini, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 1991, amegusia suala hili alipoandika kwamba "anyone who actually has read, and been sufficiently literate fully to understand, this highly complex, brilliant novel knows that dominant among its luxuriant themes is that of displacement." Hayo ameyaandika katika insha yake, "Censorship--the Final Solution, the Case of Salman Rushdie," Telling Times, Writing and Living, 1954-2008, uk. 448.

Mimi ni profesa wa masomo ya ki-Ingereza na fasihi yake. Ninasoma na kufundisha maandishi ya waandishi mbali mbali. Hata maandishi mengine ya Rushdie nimesoma, bila tatizo. Lakini, pamoja na uzoefu na ujuzi wangu, kitabu cha The Satanic Verses kimekuwa changamoto kubwa kwangu, kwa jinsi Rushdie anavyoimudu lugha ya ki-Ingereza, na kuiingiza katika ubunifu, mbwembwe, na madoido mbali mbali kama mchawi mahiri wa lugha. Kwa kiasi fulani, nakifananisha kitabu chake hiki na maandishi ya Derek Walcott, mwandishi kutoka St. Lucia, sehemu za Caribbean, ambaye alipata tuzo ya Nobel mwaka 1992. Huyu naye amejikita sana katika historia ya maandishi na anatawala uwanja mkubwa wa waandishi kuanzia wa kale hadi wa leo. Kwa hivi, kuyaelewa maandishi yake, kunahitaji mtu uwe umesoma sana.

The Satanic Verses ni kama mtihani. Sitakubali kushindwa, ingawa ni mtihani mgumu. Pole pole nitafanikiwa kuelewa, kwa namna yangu, alichoandika Rushdie. Msomaji makini yeyote ana uwezo wa kuelewa andiko, kwa namna yake. Ndivyo nadharia ya fasihi inavyofundisha.

2 comments:

Fadhy Mtanga said...

Prof. Mbele nilidhani mimi ndiye mwenye tatizo la uelewa. Nilianza kukisoma mwaka jana mwanzoni. Nikafika mahali nikachoka. Nikakiweka kando. Mwaka huu nimeanza kukisoma tena taratibu ili nijibidiishe kumwelewa.
Ahsante sana kwa kuzungumzia hapa The Satanic Verses. Kwangu nina mengi sana ya kujifunza kuhusu uandishi wa kiubunifu.

Kila la kheri katika kazi zako. Kila mara nafurahi sana kupata wasaa wa kuyasoma maandishi yako.

Mbele said...

Ndugu Mtanga, shukrani kwa ujumbe. Inahitaji unyenyekevu kukiri kuwa jambo fulani hulielewi au umeliona gumu kulielewa. Naweza kusema pia kuwa huu ni ushujaa. Kwa hilo tuko pamoja.

Jambo moja linalofurahisha katika ujumbe wako ni moyo wa kupambana na hicho kitabu, badala ya kukata tamaa. Huo ni ushujaa, na dalili ya kuelimika.

Ishara thabiti ya kuelimika ni kutambua mapungufu yako kiakili na kimtazamo, na kujitahidi muda wote kujifunza. Kwa hilo, tena tuko pamoja.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...