Sunday, October 28, 2012

Taarifa kwa Umma Kuhusu Hatma ya MwanaHalisi

Leo 28 Oktoba 2012

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Bidamu (THRD-Coalition), wadau wanaounda mtandao huu na mwanachama mwanzilishi wa Mtandao likiwa ni shirika lenye majukumu ya ya kutetea uhuru wa habari kusini mwa Afrika (MISA-Tan) tunaendelea kwa pamoja kuonyesha kusikitishwa kwetu kwa kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi.

Kwa mara kadhaa sasa tunawakutanisha tena lengo likiwa ni kuendelea kuishawishi serikali ilifungulie gazeti la Mwanahalisi. Kwa vile hoja yetu ya kutaka kuliona gazeti la Mwanahalisi likiwa mitaani haijatimia basi na sisi kwa upande wetu kazi yetu bado haijatimia.

Tunatambua umuhimu wa kuheshimu sheria za nchi, lakini kwa upande mwingine tunaona kwamba ipo haja ya sisi watetezi wa haki za binadamu kupitia kwenye vyombo vya habari na pia kwenye mashirika mengine yanayounda mtandao huu kuishawishi serikali kuachana na sheria gandamizi ambazo ni za kidikteta kama sheria hii ya magazeti ya mwaka 1976 ambayo hukiuka misingi ya haki za binadamu na utawala bora. Pia kwamba maendeleo ya kiteknolojia na kisiasa hapa nchini yanaiweka rehani sheria hiyo gandamizi.

Tumebaini kuwa kufungiwa kwa gazeti la Mwanahalisi siyo tu kwamba kunawaathiri kwa kiwango kikubwa wasomaji wake ndani na nje ya nchi bali pia kunaathiri uhuru wa kutafuta, kupata na kueneza habari, kunawaathiri waajiriwa wa gazeti hilo na familia zao na pia kunaiweka katika hati hati hata kampuni nzima ya Halihalisi ambayo ndiyo mchapishaji wa gazeti hilo.

Tunaendelea kusisitiza kuwa sababu walizotumia viongozi wa wizara ya habari kulifungia gazeti la mwanahalisi sio za kweli kwani kilichoandikwa na Mwanahalisi ni ukweli mtupu ambao hivi karibuni umethibitishwa na tamko la Dr Steven Ulimboka.

Pia, hivi karibuni Dkt Stephen Ulimboka, kupitia kwa wakili wake Mheshimiwa Nyaronyo Kicheere aliweka wazi kwamba Afisa wa Usalama wa Taifa Ramadhan Ighondu alihusika katika kutekwa kwake kwa kuwa mazingira yote kabla na baada ya tukio yanaonyesha wazi kuwa Ramadhani Ighondu ni mdau katika tukio hili.

Kinachoshangaza zaidi ni kwamba baadala ya serikali kutoa tamko kwamba sasa imepata uhakika kwamba afisa wake alikiuka kanuni za ajira yake na ingeaza rasmi kuwasaka washirika wa afisa hiyu jambo hilo halijatokea mpaka sasa huku gazeti hili lililosidia kubainisha ushahidi likifungiwa. Zaidi, tulitegemea serikali ingemkana afisa huyo kwamba siyo mwajiriwa wake katika idara hiyo, kama hivyo ndivyo ilivyo, au vinginevyo tungeitarajia serikali itangaze kwamba inachukua hatua za kisheria dhidi ya afisa huyo ambaye ametajwa kuhusika katika makosa ya jinai kinyume cha utaratibu wa mwajiri wake. Pia tungetemea Jeshi la polisi lingetumia fursa hii kumkamata mshukiwa huyu wa Usalama wa Taifa na kulisadia Jeshi la Polisi kuwapata wale waliotekeleza udhalimu huu dhidi ya Dr Steven Ulimboka. Kwa namna yoyote vitendo vya aina hiyo vinaiabisha serikali na haviwezi kuwa sehemu ya utawala bora ambao serikali yetu imekuwa ikitangaza kwamba inauzingatia.

Mpaka sasa kumekuwapo na matamko mbali mbali kutoka kwa wadau, viongozi wa kiroho, mabalozi na hata Baraza la Habari Tanzania (MCT) likiwa peke yake na hata kwa kushirikiana na wadau wengine wakilaani kufungiwa kwa gazeti hili lakini serikali imeendelea kuwa kaidi katika hili.

Tunachosisitiza
1. Kwa Serikali
Tunaendelea kuwasihi viongozi wa nchi waone sasa umuhimu wa kukutana na viongozi wa Hali Halisi na kujadili namna ya kulifungulia gazeti hili kwani tayari Dr Steven Ulimboka ameshaweka wazi kilichoandikwa na Mwanahalisi ni cha kweli kabisa. Serikali itambue kuwa suala hili sio dogo katika anga za kidemokrasia na haki za binadamu kwani ubabe wa baadhi ya viongozi serikalini leo unaweza iweka nchi pabaya siku za usoni.

2. Vyombo vya Habari
Vyombo vya habari pamoja na taasisi mbalimbali katika tasnia ya habari tuweke tofauti zetu pembeni na kuungana kwa pamoja katika hili na kuhakisha kuwa ukandamizaji wa uhuru wa habari kama huu wa wazi wazi haupati nafasi katika enzi hizi za uwazi na ukweli. Vyombo na taasisi mbalimbali za habari bado mna nafasi na uwezo mkubwa katika kuhakisha gazeti la Mwanahalisi halipotei katika tasnia ya habari hapa nchini.

3. Jumuiya ya Kimataifa
Kwa kuwa mmekuwa wadau wakubwa wa maendeleo na utekelezaji wa haki za binadamu hapa nchini, tukiwa tunaendelea kuuthamini mchango wenu, tunawasihi muendelee kuishawishi serikali kwa njia za kidiplomasia kuhusu suala la kuheshimu kazi za watetezi haki za binadamu na uhuru wa habari. Nafasi zenu za kidiplomasia na uhusiano mkubwa mlionao na nchi ya Tanzania inaweza pia kutumika kushawishi viongozi wa Tanzania walifungulie gazeti la Mwanahalisi.

Kutokana na hali ilivyo ya uvunjifu wa haki za watetezi wa haki za binadamu ikiwamo haki ya kutoa habari, MISA-Tan, mwanachama wa THRD-Coalition anaehusika na uhuru wa habari inaandaa mkutano wa siku moja utakaowakutanisha wadau mbalimbali katika tasnia ya habari ili kujadili hatma ya gazeti la Mwanahalisi na uhuru wa habari nchini.

Mwisho Tunawasihi wanaharakati, watanzania wote wasichoke wala wasirudi nyuma katika azma hii ya kutetea haki, uhuru na ulinzi kwa haki na watetezi wake.

CHANZO: KATUNEWS BLOG

Thursday, October 25, 2012

Mdau Profesa Aliyenihamasisha Kuandika Kitabu

Leo nimekutana na rafiki yangu wa siku nyingi, Profesa John Greenler wa Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Alikuja hapa Chuoni St. Olaf na binti yake. Kama umesoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, utaona nimemtaja Profesa Greenler kwenye ukurasa wa "Acknowledgements."

Profesa huyu tulifahamiana miaka yapata kumi iliyopita kwenye mikutano ya washauri wa programu ya Associated Colleges of the Midwest (ACM) ambayo hupeleka wanafunzi Tanzania. Miaka ile yeye alikuwa anafundisha Chuo cha Beloit. Wakati wa kupanga na kutathmini hali ya program kila mwaka, nachangia kwa namna ya pekee masuala yanayohusu tofauti za tamaduni, ambayo ni changamoto kwa wa-Marekani na wa-Tanzania.



Kwenye mikutano yetu hiyo, nilikuwa, na bado niko, mstari wa mbele kufafanua matukio mbali mbali na mambo mengine wanayokumbana nayo wanafunzi katika kuishi na wa-Tanzania.

Profesa Greenler alipochukua fursa ya kupeleka wanafunzi Tanzania, aliniomba niandike mwongozo angalau kurasa hata tatu tu, wa masuala hayo, ili yamsaidie katika safari yake. Nililitafakari ombi lake, hatimaye nikaanza kuandika.

Wakati muswada ukiwa bado katika hali duni, bila marekebisho ya kutosha, watu mbali mbali hapa Marekani wanaopeleka wageni Tanzania waliuchangamkia, wakawa wanautumia. Nilipogundua hivyo, nilifadhaika, kwa sababu muswada haukuwa umekamilika,  na haukufanana na hadhi na ujuzi wangu. Niliona ni sherti nifanye juhudi kuurekebisha bila kuchelewa. Baada ya kazi ngumu ya miezi kadhaa nilichapisha kitabu, Februari 2005.




Leo nimemkumbusha Profesa Greenler alivyonihamasisha katika suala hili, na nikamsisitizia binti yake kuwa habari ndio hiyo. Tumefurahi sana kukutana na kukumbushana mambo ya Bongo. Ameniambia tena kuwa yeye na familia yake wanaikumbuka sana Tanzania na wanaipenda.

Amenielezea pia kuhusu wanafunzi wa ACM aliowapeleka Tanzania miaka ile, na ambao wanaendelea kuwa na uhusiano na Tanzania. Hili ni jambo la kawaida, na sisi tunaohusika na programu hizi tunafarijika tunapoona kuwa zimechangia kujenga mahusiano baina ya watu wa nchi hizi mbili.

Hata hivi, kwa kuzingatia kuwa profesa huyu ni kati ya wa-Marekani wengi sana ambao ni wapenzi wa Tanzania, ilibidi nimwambie kuhusu maandamano na vurugu Zanzibar na Dar es Salaam, ambayo yanachafua jina la Tanzania. Miaka yote iliyopita ilikuwa rahisi na heshima kuinadi Tanzania kama nchi ya amani na utulivu, lakini ni sherti kusema ukweli unaojitokeza sasa.

Monday, October 22, 2012

Ngoma Nzito Marekani: Tanzania Je?

Pamoja na mapungufu yake yote, siasa Marekani ina mambo kadhaa ya kupigiwa mfano. Kinachonivutia zaidi ni mijadala inyofanyika baina ya wagombea kabla ya uchaguzi. Leo, kwa mfano, tumeshuhudia pambano la tatu baina ya Obama na Romney

Mijadala ya namna hii inawapa wapiga kura fursa ya kuwasikiliza wagombea. Vile vile naiona kama namna ya kuwaheshimu wapiga kura.

Mfumo wa Marekani unatambua kuwa wapiga kura wana haki ya kuwasikia wagombea wakiongelea masuala kadha wa kadha katika kupambanishwa na wapinzani wao.

Ninakerwa ninapokumbuka mambo yalivyo kwetu Tanzania. Ninakerwa nikikumbuka jinsi CCM ilivyotoroka midahalo mwaka 2010. Ni dharau kwa wapiga kura. Tatizo ni jinsi wapiga kura wengi walivyo mbumbumbu, wasitambue kuwa hili lilikuwa dharau. Walipiga kura kama vile hawajadharauliwa.

Hebu fikiria mambo yangekuwaje ule mwaka 2010 iwapo Kikwete angepambana na Slaa katika midahalo mitatu hivi, ambayo ingeonekana katika televisheni na kusikika redioni. Lakini tulinyimwa fursa hii, kutokana na maaumzi muflisi ya CCM.

Hakuna sababu yoyote kwa nini siku zijazo tusifanye kama wa-Marekani wafanyavyo. Watangazaji makini wa redio na televisheni tunao, ambao wanaweza wakaendesha mahojiano nasi tukapata fursa nzuri ya kuwabaini wababaishaji na kuwatupilia mbali.

Saturday, October 20, 2012

Mtume Hatetewi kwa Dhulma na Ujinga

Mtume Hatetewi Kwa Dhulma Na Ujinga

Uislamu Na Shari'ah Zake

Imekusanywa Na: ‘Uthmaan Beecher

Imefasiriwa Na: Abu Suhayl

Shukrani njema zinamstahili Allaah, rahmah na amani zimuendee Mtume wetu Muhammad, na aali zake na maswahaba zake na Waislamu wote. Ama baada ya hayo

Hakuna Muislamu ambaye anaweza kukubaliana na kutukanwa, kudhalilishwa, kudhauruliwa na kusingiziwa mambo mabaya Mtume wetu mpendwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ma-Imaam wa Ahlus-Sunnah kama Imam Maalik, al-Layth, Ahmad, na Ash-Shaafi’iy, wamekubaliana kwa pamoja kwamba yeyote atakayemvunjia heshima, kumtukana au kumdhalilisha au kumtia ila Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakuwa amekufuru, na adhabu inayomstahili kwa yule anayeishi katika dola ya Kiislamu na akafanya hivyo ni kifo, adhabu ambayo itakuwa katika mikono ya mtawala wa Kiislamu.

Hapana shaka kwamba mashambulizi ya aina hii kwa Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yatasababisha hasira na kukata matumbo ya kila Muislamu kutokana na mapenzi yao kwa Allaah, Mtume wake na Dini yake. Lakini Muislamu aliye mkweli, muadilifu na muaminifu hawezi kuruhusu kuchukuliwa na hasira na jazba na kujibu mashambulizi haya kwa matendo ya kihuni ambayo yanakusanya matendo ambayo Allaah na Mtume wake wameyakataza. Zaidi atakuwa kama katika matendo mengine na subra, kisha anayarejesha mambo hayo katika Qur-aan na Sunnah na ufahamu wa Maswahaba na Ma’ulamaa walioshikana barabara na elimu. Hivyo Muislamu anakuwa na subira na anaithibitisha miguu yake kwa elimu na anajisalimisha kwa hukumu za Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah anasema:

“Enyi mlioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Mtume mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya ‘Aakhirah. Hivyo ni (njia) bora na matokeo mazuri zaidi.” [An-Nisaa 4: 59].

Al-Haafidhw Ibin Kathiyr ametaja kuwa maana ya “wenye madaraka katika nyinyi.” kwa mujibu wa Ibn ‘Abbaas, Mujaahid na ‘Atwaa na wengine katika Salaf, inakusudiwa “Maulamaa”. Na Ibn Kathiyr amesema inakusudiwa Ma’ulamaa na watawala na hapa inakusudiwa Ma’ulamaa wa Ahlus-Sunnah Wal-Jamaa’ah.

Ambacho kimetokea siku chache zilizopita katika ardhi za Waislamu na sehemu nyingine kama hatua za kupinga filamu inayoshambulia Uislamu na kumtukana Mtume wetu mpendwa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yanapingana na muongozo wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Tunatakiwa tukumbuke kuwa mashambulizi haya si mapya. Allaah Ametaja katika Qur-aan kuwa Mitume Wake (‘Alayhimus Salaam) walishambuliwa na kutukanwa, watu wao waliwaita vichaaa, wendawazimu na hata kuwaita wachawi. Allaah Anasema:

“Basi ndio hivyo hivyo, hakuwajia kabla yao Mtume ila walisema: Huyu ni mchawi au mwendawazimu.” [Adh-Dhaariyaat 51: 52].

Na haya yametokea kwa Mitume kuanzia Nuwh (‘Alayhis Salaam) mpaka kwa Mtume wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Katika kipindi cha maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuna ambao walikuwa wakimtusi na kumkashfu hadharani. Ka’ab bin Ashraf Al-Yahuwdiy aliyekuwa Madiynah alikuwa akiimba mashairi ya kumkashifu Mtume na kuimba mashairi mabaya kuhusu wanawake wa Kiislamu. Na Makkah alikuwepo ‘Abdullaah bin Khatal ambaye alikuwa na waimbaji wawili wa kike ambao walikuwa wakiimba mashairi ya kumkejeli Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

Aliporudi toka safari ya Makkah kuja Madiynah Ka’ab bin Al-Ashraf akaanza kuimba mashairi ya kumtukana. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwauliza Maswahaba zake, “Nani atakayemdhibiti Ka’ab bin Al-Ashraf? Kwani amemdhuru Allaah na Mtume Wake.” Na hapa ni pale Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa katika dola yake na yeye alikuwa ndiye kiongozi na Ka’ab alikuwa akiishi chini ya mamlaka yake hapo Madiynah. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwaambia Maswahaba zake kwenda kuwaadhibu majirani zake, rafiki zake au familia yake kwa yale aliyokuwa akifanya Ka’ab bin Al-Ashraf. Wala hakuuadhibu ukoo wake wa Banu Nadhwiyr au kuwaadhibu Mayahudi wengine wa Madiynah.

Yeyote mwenye akili iliyosalimika hawezi kukubaliana na hili kwani halikubaliani na mantiki achilia mbali maandiko ya Kitabu na Sunnah.

Alichofanya kama mtawala Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuadhibu Ka’ab ambaye ndiye aliyekuwa anafanya kosa hilo.

‘Abdullaah bin Khatal alikuwa Makkah na alikuwa na waimbaji wawili wa kike aliowafundisha kuimba nyimbo za kumkejeli na kumkashifu Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na wakati huo Mtume alikuwa ni kiongozi na hakuwahi kamwe kuwashambulia makafiri wa Madiynah au miji au vijijiji vingine kama malipo ya matusi ya ‘Abdullaah bin Khatal kwake yeye. Pia hakuwaamrisha Maswahaba zake kuishambulia Makkah au watu wa Makkah kwa sababu ya ‘Abdullaah bin Khatal.

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na subira na hakuwakandamiza watu au kuchupa mipaka. Alikuwa na subira na alikuwa muadilifu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipoiteka Makkah na jeshi lake, akaamrisha asidhuriwe yeyote ambaye hatopigana nao, isipokuwa kikundi kidogo cha watu ambao aliwataja kwa majina.

Hapa Mtume alikuwa na nguvu, ameiteka Makkah na alikuwa na nguvu na miongoni mwa aliowataja ni ‘Abdullaah bin Khatal na waimbaji wake wawili wa kike. Hakuamrisha majirani zake wala familia yake kuadhibiwa. Hakuamrisha mali za ukoo wake kuharibiwa. Alichoamrisha ni kuuawa ‘Abdullaah bin Khatal na waimbaji wake wawili wa kike.

Hii ni mifano miwili tu ya jinsi Mtume alivyofanya na watu waliomtukana akiwa hai. Alikuwa ni muadilifu na subira. Hakumkandamiza mtu wala kumdhulumu na hawa watu walimlaani, wakamtukana, wakamdhalilisha na kumkashifu akiwa hai (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Sasa matendo haya ya haya makundi na wajinga wengine walioathiriwa na hayo makundi wameyapata wapi kwa kutazama mwenendo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)?

Mmeona wapi kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Maswahaba zake walikwenda katika miji mingine na kuandamana, na kuua watu wasiokuwa na hatia, kuharibu mali zao kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya Ibn al-Ashraf na Ibn Al-Khatal wakiwa Makkah na Madiynah?

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na subira na uadilifu. Na uadilifu ni kukiweka kila kitu mahali pake. Na haya tunayayona toka kwa watu Misr, Yemen, Libya na nchi zingine katika mashariki ya kati ni ukandamizaji, dhulma na kuvunja Sunnah. Allaah Anasema:

“Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake (Mtume Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo.” [An-Nuwr 24: 63].

Kinachofafanua zaidi tofauti katika muongozo wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wale Waislamu ambao wanachukuliwa na jazba na upotevu ni Hadiyth ya ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ambayo imesimuliwa na Al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad na wengineo, walipokuja kundi la Mayahudi kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia “As-Saamu ‘Alaykum” (kifo kiwe juu yako). ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alielewa walichosema hivyo akawajibu “Wa ‘alaykum As-Saam wa la‘ana.” (Na kifo na laana ziwe juu yenu). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Taratibu ee ‘Aaishah, bila shaka Allaah Anapenda upole katika mambo yote.” ‘Aaishah akasema “Ee Mtume wa Allaah! Hukuwasikia waliyoyasema?” Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema, “Nimeshawajibu (kwa kusema) “Wa ‘Alaykum.” (Na juu yenu pia.” Na Dini yetu haiendi kwa hisia na jazba. Muislamu ambaye anampenda kiukweli Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atafuata muongozo na Sunnah zake.

“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Ghafuwrur-Rahiym (Mwingi wa Kughufiria - Mwenye Kurehemu.” [Al-‘Imraan 3: 31].

Tuzizingatie nukta zifuatazo:

- Maandamano haya ambayo yameenea katika ardhi za Waislamu na yameeingia mpaka Kuwait ni bida’a kama walivyosema wanachuoni wa Ahlus Sunnah waljama’a kama Shaykh Ibn Baaz, Shaykh al-Albaani, Shaykh Ibn ‘Uthaymini na walivyoyafafanua. Ni matendo ya kuwapinga na kupambana na viongozi wa Kiislamu na ni katika njia za Makhawaariji. Makundi ya kisiasa wanayaruhusu na kuyatetea kwani ni njia ya kupambana na watawala wa Kiislamu na ndio njia ya kuchukua madaraka.

Tumeona jinsi vijana waliojawa na hamasa walivyochukua hatua kuingia mitaani katika maandamano haya na kupambana na polisi na kusababisha uharibifu kwa mali na si mali za balozi -ambacho pia kitendo hichi ni ukandamizaji lakini mali za Waislamu pia!! Na hii ndio inaitwa kumlinda Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Haiwezekani kwa Muislamu kumtetea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukandamizaji wakati Allaah Ametuamrisha kuwa waadilifu:

“Enyi mlioamini! Kuweni wasimamizi madhubuti kwa ajili ya Allaah mkitoa ushahidi kwa uadilifu. Na wala chuki ya watu isikuchocheeni kutokufanya uadilifu. Fanyeni uadilifu; hivyo ni karibu zaidi na taqwa. Na mcheni Allaah; hakika Allaah Khabiyr (Mjuzi wa undani na ukina wa mambo) kwa myatendayo.” [Al-Maaidah 5: 8].

Al-Haafidhw Ibn Kathir amesema: “Usiache chuki zako kwa watu zikufanye ukaacha kuwafanyia uadilifu. Fanya uadilifu kwa kila mtu akiwa ni rafiki au adui.”

Shaykh wa Uislamu Ibn Taymiyyah amesema:

“Kwani watu hawakutofautiana kuhusiana na ukweli kwamba mwisho wa dhulma ni mbaya na una madhara na mwisho wa uadilifu ni mzuri wenye kupendeza.” Kwa ajili hiyo pamesemwa: Allaah atalisaidia taifa ambalo linafanya uadilifu hata kama watakuwa ni makafiri na hatolisaidia taifa litakalokuwa linafanya dhulma hata kama taifa hilo litakuwa limeamini.” [Majmu’u Al-Fataawaa 28/63].

Jua kwamba kuwaadhibu watu wengine kwa makosa ya mtu mwingine sio uadilifu Allaah Anasema:

“Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Je, nitake ghairi ya Allaah kuwa ni Mola, na hali Yeye ni Mola wa kila kitu? Na wala nafsi yoyote haitachuma (ubaya) ila ni dhidi yake. Na wala hatobeba mbebaji (mzigo yake ya dhambi) mzigo (wa dhambi) wa mwengine. Kisha kwa Mola wenu Pekee ndio marejeo yenu, Atakujulisheni kwa yale mliyokuwa ndani yake mkikhitilafiana kwayo.” [Al-‘An’aam 6: 164].

Makundi ya kisiasa wanatumia maandamano haya na matukio kama haya kama jukwaa na mimbari za kuenezea mashaka na hila zao kwa watu ili watu wawageuke watawala.

- Maandamano haya ambayo Ma’ulamaa wamesema ni bid’ah yametumika kama ngao kujificha kwa wale walio katika Manhaj ya Khawaarij kuua wasio na hatia. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema “Yeyote katika Waislamu atakayeua mtu ambaye anaishi kwa mkataba au makubaliano (na Waislamu) hatoonja harufu ya pepo japokuwa harufu ya pepo inasikika umbali wa mwendo wa miaka 40.” [Al-Bukhaariy].

Na katika Hadiyth nyingine amesema:

“Mkataba wa amani kwa Waislamu ni mmoja, yeyote atakayeuvunja mkataba wa amani na usalama kwa Muislamu mwengine ni juu yake laana ya Allaah, Malaika na watu wote.”

Al-Haafidhw Ibn Hajr (Rahimahu Allaah) amefafanua:

“Maneno mkataba wa amani kwa Waislamu ni mmoja’ ina maana kuwa kumpa mtu uhakika wa usalama wa amani ni sahihi (unakuwa mkataba umefungika). Kama mmoja wao atampa mkataba wa amani kafiri ni haramu kwa yeyote yule kuuvunja.”

Makafiri wanaoishi na kufanya kazi katika nchi za Waislamu wamepewa mkataba wa amani kwa hiyo kuwashambulia ni kupambana na kuwapinga watawala wa Kiislamu na kitendo cha usaliti na dhulma.

Shaykh Twaariq As-Subay’i amesema kwamba kama Muislamu atampa amani asiyekuwa Muislamu, hata kama huyo Muislamu atakuwa ni mwanamme au mwanamke, muungwana au mtumwa, na hata akiwa amepewa amani kwa ishara tu au kama amepewa amani kwa makubaliano ya kibalozi au kwa kumpa viza kuingia katika nchi -mtu huyo atakuwa amepewa mkataba wa amani na usalama wa maisha yake. Ni haramu kwa Waislamu kumdhuru. Na Muislamu atakayemdhuru ataangukia katika laana za Allaah, na Malaika na watu wote.

- Ukitazama wanaoongoza maandamano haya utawakuta wote ni katika viongozi wa vyama vya kisiasa. Na ushahidi kuwa hakuna katika Wanachuoni wa Ahlus-Sunnah ambaye amejihusisha na haya maandamano yatosha kuwa dalili kwa mtu mwenye akili, kama ambavyo Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) alivyotumia hoja kama hii dhidi ya Makhawaarij kwamba hakuna hata Swahaba mmoja aliye pamoja nao aliposema: “Bila shaka nimekuja kwenu kutoka katika Maswahaba wa Mtume wa Allaah na hakuna hata Swahaba mmoja aliye pamoja nanyi.”

Tunaona Waislamu wakiandamana, wakipambana na polisi wakiharibu mali na mambo mengine mabaya zaidi ya yote hayo yanafanyika kwa jina la kumtetea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutokana na filamu iliyotengenezwa na mtu mmoja anayeishi Marekani. La kusataajabisha hakuna hata mmoja anayechukizwa na Misikiti yenye makaburi ndani ambapo asiyekuwa Allaah anaabudiwa kama Msikiti wa Badawi, Zaynab na Al-Husayn?! Dhambi kubwa kabisa mtu anayoweza kuifanya inafanyika katika ardhi za Waislamu na watu wanashambulia mali na haki za watu kwa kitu ambacho hawana mamlaka nacho au uwezo wa kufanya chochote kukizuia!

Allaah Anasema:

“Hakika Allaah Haghufuri kushirikishwa; na Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amebuni dhambi kuu.” [An-Nisaa 4: 48].

Kwa hiyo Waislamu hawa na makundi haya wanataka kumtetea Mtume kwa kufanya dhulma na na uonevu - lakini uko wapi utetezi wa Allaah na Tawhiyd yake kutokana na shirk zinazofanywa na Waislamu katik ardhi ya Waislamu wenyewe!

Jua kwamba Allaah Ametuamrisha kuwa na subira na uvumilivu na Ametukataza kufanya dhulma na uonevu. Na hakuna uadilifu katika matendo tunayoyaona toka kwa kaka zetu na dada zetu wa Misr, Yemen, Tunisia, Morocco, Sudan na nchi nyingine ambapo haya yanatokea. Matendo haya ni matendo ya ujinga, dhulma, upotevu na kuiacha Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Aliyetengeneza filamu hii chafu anaishi Marekani na Marekani ni nchi ambayo ina kanuni zake inazotumia kutawala raia wake. Jambo hili halipo katika mikono ya sisi watu wa kawaida na hatuna uwezo wa kufanya lolote kulihusu. Jambo muhimu kwetu na subira na kushikamana na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na hii ni njia bora zaidi ya kumtetea Mtume zaidi ya haya tunayoyaona yakifanywa na makundi haya na wafuasi wao.

Na ni muhimu kuzingatia kuwa subira yetu na uvumilivu wetu na kushikamana kwetu na Sunnah wakati wa hali kama hizi wakati hatuna uwezo wa kuzikabili si alama ya udhalili au unyonge. Makundi yaliyopotea ndiyo yamewaingiza vijana katika fikra hizi kuwa ukikosa uwezo wa kuchukua hatua ni sawa na kutochukua hatua, huu ni usaliti na upotevu.

Ibn Mas’uwd amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiswali katika Ka’abah na alipokuwa akisujudu mmoja kati ya wafuasi wa Abu Jahl alimuwekea matumbo ya ngamia mgongoni kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati Ibn Mas’uwd akiwa anamtazama. Ibn Mas’uwd amesema: “Nilikuwa natazama lakini sikuwa na cha kufanya. Laiti ningekuwa na nguvu na uwezo (wa kumzuia).” [Al-Bukhaariy].

Hili linatuonyesha kwamba wakati hatuna uwezo kutokana na kuwa na miili dhaifu, au kukosa uwezo au kuna kitu kinakuzuia hakuna aibu kwa hilo, kama ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyoshindwa kuwasaidia Yaasir, ‘Ammaar na mama yake ‘Ammaar (Radhiya Allaahu ‘anhum) alipowaona wakiteswa kwa sababu ya kumuamini Allaah. Hivyo akawaambia: “Fanyeni subra enyi watu wa nyumba ya Yaasir, kwani mmeahidiwa pepo.” [Al-Mastadrak Al-Haakim (3/383), Al-Hilyah (1/140), na vingine. Tazama vilevile Swahiyh Siyrat An-Nabawiyyah cha Shaykh Al-Albaanee (uk. 154-155)].

Haya tumayoyaandika hapa si kwa ajili ya kuitetea filamu hiyo. Hiyo filamu nasi tunaiona kuwa ni matusi yenye kuudhi kama watu wengine. Lakini tunafanya hivi kama njia ya kumtetea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Dini yetu dhidi ya wale wenye kuchupa mipaka, na wale wanaocheza na hisia za Waislamu na vijana na kuwaita katika njia za upotevu. Huu ni wito wa kuwa na subra na kuwa na uadilifu na kushikama na Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haya ndiyo yaliyokuwa ynahitajika kuelezewa na kufafanuliwa. Allaah ni mjuzi zaidi.

Rahmah na amani zimuendee Mtume wetu Muhammad na aali zake na Maswahaba zake wote. Na shukrani njema zinamstahili Allaah.

CHANZO: ALHIDAAYA

Friday, October 19, 2012

Ziara Chuoni Lake Forest

Juzi nilienda chuoni Lake Forest, maili kadhaa kaskazini ya Chicago. Nilishinda pale jana yote. Hapa kushoto ni picha ya Student Center, ambamo wanafunzi hupata chakula na kupumzika. Nilienda na profesa kutoka chuo cha Wheaton, kutathmini programu ya Area Studies. Hii ni programu ambayo inampa mwanafunzi fursa ya kusoma masomo mbali mbali kuhusu sehemu moja ya dunia, kama vile Mashariki ya Kati, Amerika ya Kusini, Afrika, au Asia. Anasoma masomo kama historia, siasa, uchumi, na hata lugha ya sehemu husika. Pia, ikiwezekana, anaenda kusoma katika sehemu hiyo.

Utaratibu wa kutathmini programu na idara mbali mbali za masomo ni wa kawaida katika vyuo vya Marekani. Hufanyika baada ya miaka kadhaa; yaweza kuwa saba, au kumi, na kadhalika.

Shughuli ya kutathmini programu huhitaji mtu usome taarifa mbali mbali zinazoelezea malengo na utaratibu wa masomo hayo, ratiba za masomo, na tathmini kutoka kwa wanafunzi waliosoma masomo hayo. Pia kuna taarifa kuhusu wafundishaji, elimu yao, masomo wanayofanyia utafiti, mihadhara ya kitaamula waliyotoa, vitabu na machapisho mengine waliyoandika, na kadhalika.

Shughuli za kusoma taarifa tulizifanya kabla ya kufanya ziara. Ziara ilitupa fursa kamili ya kuongea na walimu, wakuu wa idara, na mkuu wa kitivo. Kwa siku chache zijazo, kazi yetu sisi wawili itakuwa ni kuandika ripoti yetu na kutoa mapendekezo.

Shughuli hii imeniwezesha kuifahamu vizuri programu ya Area Studies ya chuo cha Lake Forest. Hii haikuwa mara yangu ya kwanza kutembelea chuo hiki. Niliwahi kualikwa na chuo hiki mwaka 2003, kutoa mhadhara ulioitwa "Neo Colonialism and African Development."

Kumbe, dunia ni mzunguko. Mkuu wa programu ya Area Studies, profesa ambaye anasema karibu atastaafu, alinikumbusha mhadhara niliotoa. Anakumbuka hata baadhi ya hoja zangu, na anasema anazitumia katika kufundisha. Yeye ni profesa wa somo la biashara, ambaye anazingatia kipengele cha utamaduni katika mahusiano ya kibiashara hapa duniani. Ametembelea nchi yapata 20 katika utafiti wake. Nilifurahi kuongea na profesa huyu, ambaye aliniambia anazingatia niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Tuliongea kirefu kwa siku zote mbili nilizokuwa chuoni hapo.

Tuesday, October 16, 2012

Wa-Kristu Tunamwabudu Allah!

Najua kuwa kichwa cha habari hii kitawashtua wengi. Huenda watu watasema nimechanganyikiwa au nimekufuru.  Huenda wako watakaouliza, "Iweje wa-Kristu wawe wanamwabudu Allah?"

Kwa siku kadhaa, nimekuwa nikijuliza suali: Je, wa-Arabu ambao ni wa-Kristu wanatumia jina gani kumtaja Mungu? Ninafahamu kuwa kuna mamilioni ya wa-Arabu ambao ni wa-Kristu, huko Mashariki ya Kati na sehemu zingine za dunia. Sasa je, Mungu wanamwitaje kwa ki-Arabu?

Nimefanya uchunguzi kidogo nikagundua kuwa jina wanalotumia, ni hilo hilo wanalotumia wa-Islam, yaani Allah. Hili ndilo neno lililopo katika ki-Arabu. Katika Biblia ya ki-Arabu, ambayo huitwa "al-Kitab al- Muqadis" yaani Kitabu Kitakatifu, Mungu anaitwa Allah muda wote.

Nilivyogundua hivyo nimetambua jinsi wengi wetu tulivyopotea, kwani tunaamini kuwa Allah ni tofauti na Mungu. Tunalumbana hadi tunatokwa jasho, na povu mdomoni, kwa umbumbumbu wa kutojua lugha. Taarifa iliyonifungua macho ni hii hapa.


Sunday, October 14, 2012

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

(Katika kumkumbuka Mwalimu Nyerere, naileta makala yangu, "Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM," ambayo nimeshaichapisha katika hii blogu yangu mara kadhaa)

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

Saturday, October 13, 2012

Leo Nimehudhuria Tamasha la Vitabu Twin Cities

Leo nilikuwa mjini St. Paul, kushiriki Twin Cities Book Festival. Kama nilivyowahi kuelezea, maonesho haya hufanyika kila mwaka, wakati kama huu. Nililipia ushiriki wangu nikitumia jina la "Africonexion" ambalo ni jina la kikampuni changu ambacho nimekuwa nikikijenga pole pole.










Tofauti na miaka iliyopita, maonesho ya leo yalifanyika sehemu iitwayo State Fairgraounds. Miaka iliyopita maonesho haya yalikuwa yakifanyika Minneapolis Community and Technical College, mjini Minneapolis. Miji ya St. Paul na Minneapolis inagusana, na mgeni huwezi kujua mpaka ni wapi.










Kama kawaida, watu walikuwa wengi, tangu kuanza kwa maonesho hadi kumalizika.

















Kama ambavyo nimesema tena na tena, inavutia kuona jinsi wa-Marekani wanavyothamini matamasha ya vitabu. Wanaanza kufika hata kabla milango haijafunguliwa. Vijana, wazee, wake kwa waume wanahudhuria. Pia wako wanaokuja na watoto. Nimeongea na watoto kadhaa waliofika na wazazi wao kwenye meza yangu. Baba mmoja alifika na binti wawili wadogo, labda umri wa miaka kumi hivi. Baba ni mzungu, na hao mabinti ni weusi. Mmoja alisema anataka kununua kitabu changu cha Matengo Folktales. Mimi nilidhani kuwa baba yake ndiye atalipa. Lakini haikuwa hivyo. Mtoto alitoa hela yake akanipa. Nilipomwambia baba yake kuwa sikutegemea hivyo, baba alisema "ndio ana hela yake ya kulipia." Nilivyomwangalia, niliona kama ni mtoto wa miaka yapata kumi tu.









Nilichelewa kufika, dakika kama 45 hivi, lakini halikuharibika neno. Nilipanga vitabu vyangu mezani, nikaanza kuongea na wadau. Kitu kimoja cha pekee ni kuwa kwa nyakati tofauti, zilikuja familia mbili kutoka Bemidji, mji ambao uko upande wa kaskazini wa Minnesota. Nilifurahi kuwasikia wanatoka Bemidji. Niliwaeleza kuwa nimeshafika kule. Jambo la pili, ambalo liliwashangaza ni pale nilipowaeleza kuwa mimi ni mpenzi wa mwandishi Hemingway, na kwamba Bemidji ndio nyumbani kwa Mary Walsh, mke wa mwisho wa Hemingway. Niliwaeleza kuwa Hemingway na Mary Walsh walisafiri pamoja nchini Kenya na Tanganyika, baina ya mwaka 1953-hadi 1954. Pia niliwaeleza kuwa lengo langu moja ni kwenda Bemidji na kutafuta habari za mama huyu.

Thursday, October 11, 2012

Mwandishi Mo Yan Apata Tuzo ya Nobel

Nimesoma taarifa mtandaoni sasa hivi kuwa mwandishi Mo Yan wa China ameikwaa tuzo ya Nobel katika fasihi kwa mwaka huu. Sikuwahi kusikia jina la mwandishi huyu. Hili si jambo la kujivunia.

Ni kweli kuwa kuna waandishi wengi sana maarufu hapa duniani. Sio rahisi kwa mtu kuwa amesoma au anasoma maandishi ya wale wote wanaopata tuzo ya Nobel.

Kwa mfano, mwaka 2006 tuzo ya Nobel katika fasihi aliitwaa Orhan Pamuz wa u-Turuki. Sidhani kama niliwahi kusikia hata jina lake kabla. Nilijisika vibaya kuwa sina hata ufahamu wa mwandishi huyu. Hatimaye nilijikakamua nikanunua kitabu chake kimojawapo. Nadhani kwa sasa ninavyo viwili, ila bado sijapata wasaa wa kuvisoma.

Inapotokea habari ya mwandishi kupata tuzo kama hii ya Nobel, nchi zingine hufanya hima kutafsiri maandishi ya washindi hao, iwapo lugha yao ni tofauti. Watatafsiri maandishi ya Mo Yan katika lugha zao.

Tanzania hatuna utamaduni huo. Tunadanganyana kuwa sisi ni mabingwa wa ki-Swahili, ambacho kwa kweli hatukitumii kwa nidhamu itakiwayo. Hatufundishi ki-China, ki-Jerumani, ki-Rusi, na kadhalika. Hata ki-Arabu, lugha ambayo imekuwemo nchini mwetu kwa miaka zaidi ya elfu, hatufundishi. Kwa hivyo, utajiri wa uandishi uliomo katika lugha hizi hautufikii.

Kamati inayotoa tuzo ya Nobel imetamka kuwa maandishi ya Mo Yan yamejengeka katika "hallucinatory realism." Kwa vile hii dhana imeandikwa ki-Ingereza, nafahamu fika inamaanisha nini. Lakini ukiniuliza niitafsiri kwa ki-Swahili, nitababaika, pamoja na kwamba ni msomi wa kiwango cha juu. Huu ni ushahidi wa tatizo nililoongelea hapa juu, linalotusibu wa-Tanzania. Tukiambiwa tuelezee dhana kama hii ya "hallucinatory realism" kwa ki-Swahili, tutabaki tunahangaika.

Wednesday, October 10, 2012

Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Juu ya Kifo cha Daudi Mwangosi


TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA(THBUB) YATOA TAARIFA YAKE YA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI

Mwenyekiti wa Tume Ya Haki za Binaadamu na Utawala Bora Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri Ramadhan Manento (katikati) akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani jijini Dar es Salaam Oktoba 10,2012 wakati akitoa muhtasari wa taarifa ya Uchunguzi wa Tume yake kuhusu tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi kilichokea Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo. Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mahfoudha.A. Hamid na kulia ni Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Tume hiyo Florida Kazora.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri Ramadhan Manento akionyesha taarifa kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu Muhtasari wa wa Taarifa ya tume yake ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa,.
Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mahfoudha.A. Hamid akijibu moja ya Swali kutoka kwa Mwandishi wa Habari (hayupo pichani) leo jijini Dar es Salaam kuhusu Muhtasari wa wa Taarifa ya tume yake ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa.
Waandishi wa Habari wakiwa kwenye ukumbi wa mkutano wa ofisi ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora jijini Dar es Salaam wakati wa kutoa Muhtasari wa wa Taarifa ya tume yake ya Uchunguzi wa tukio lililopelekea kifo cha Mwandishi wa habari wa kituo cha Chanel Ten Daudi Mwangosi kilichotokea Septemba 2, 2012 kijijini Nyololo, Wilaya ya Mufindi, Mkoani Iringa.Picha na Mwanakombo Jumaa - MAELEZO.

MUHTASARI WA TAARIFA YA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YA UCHUNGUZI WA TUKIO LILILOPELEKEA KIFO CHA DAUDI MWANGOSI KILICHOTOKEA SEPTEMBA 2, 2012 KIJIJINI NYOLOLO, WILAYA YA MUFINDI, MKOANI IRINGA


  1. UTANGULIZI
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ni idara huru ya serikali iliyoundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 129(1)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7  ya mwaka 2001. Jukumu kubwa la Tume ni kulinda, kutetea na kuhifadhi haki za binadamu nchini.  Katika kutekeleza jukumu hilo Tume imepewa mamlaka ya kupokea malalamiko (kwa njia mbalimbali) kutoka kwa mtu yeyote au kuanzisha uchunguzi wake yenyewe endapo itaona kuna uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Kwa kuzingatia majukumu hayo, Tume ilianzisha uchunguzi wake yenyewe baada ya vyombo vya habari kutoa taarifa ya tukio la kifo cha Daudi Mwangosi. Tume iliunda timu ya watu watatu iliyoongozwa na Mhe. Kamishna Bernadeta Gambishi akisaidiwa na maafisa wawili, Bwana Gabriel Lubyagila na Bwana Yohana Mcharo. Timu hiyo ilifanya uchunguzi wake kuanzia tarehe 13-19 Septemba, 2012.

Katika uchunguzi uliofanywa, Tume ilizingatia zaidi masuala ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Hivyo basi, Tume ilitilia maanani Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sheria mbalimbali za nchi na mikataba ya kimataifa na ya kikanda inayohusu haki za binadamu ambayo Tanzania imeridhia.

Kwa kuzingatia matakwa ya sheria ya Tume Na. 7 ya mwaka 2001, baada ya uchunguzi huo kukamilika, Tume imeandaa taarifa yake na kuiwasilisha kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.

Taarifa ya uchunguzi wa Tume imegawanyika katika sehemu kuu nne, ambazo ni:
    1. Maelezo ya viongozi, watendaji na wananchi waliohojiwa
    2. Uchambuzi wa taarifa/vielelezo vilivyopokelewa kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya haki za binadamu
    3. Matokeo ya uchunguzi
    4. Maoni na mapendekezo.

Kwa kuwa tukio la kifo cha Daudi Mwangosi liligusa hisia za jamii, Tume imeona ni vyema kukutana na wawakilishi wa vyombo vya habari  ili kutoa taarifa yake.

2.0 MATOKEO YA UCHUNGUZI
Katika uchunguzi wake Tume imebaini kuwa:
    1. Tarehe 02/09/2012 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kiliruhusiwa na Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Mufindi (OCD) kufanya mikutano ya ndani na kuzindua matawi mapya.  Lakini jioni ya tarehe 01/09/2012 Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa (RPC), alizuia CHADEMA kufanya mikutano iliyoruhusiwa na OCD ambaye ni Officer In-charge wa polisi wa eneo husika kama sheria inavyotaka.
    1. Viongozi wa CHADEMA walikuwa na mazungumzo na Mkuu wa Polisi Mkoa Upelelezi (RCO) na kuruhusiwa kufungua matawi yao bila ya kuwa na mikutano ya hadhara.
    1. Msajili wa vyama vya siasa aliwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa.
    1. Wakati shughuli za uzinduzi wa tawi la Nyololo ukiendelea, RPC alifika katika eneo hilo na kuamuru viongozi wa CHADEMA wakamatwe; na kuwa wafuasi wa CHADEMA walipinga kukamatwa kwa viongozi wao.
    1. RPC aliamuru kupigwa kwa mabomu ya machozi ili kuwatawanya wananchi waliokusanyika katika ofisi za tawi hilo la CHADEMA.
    1. Baada ya mabomu ya machozi kupigwa, wananchi walitawanyika na kukimbia ovyo; na kuwa marehemu Daudi Mwangosi alizingirwa na askari, aliteswa na hatimaye inadaiwa alipigwa bomu na kufa hapo hapo.
    1. Daudi Mwangosi aliuwawa umbali wa takriban mita 100 kutoka ilipo Ofisi ya CHADEMA tawi la Nyololo.
    1. Katika tukio hilo wananchi kadhaa walijeruhiwa kwa mabomu, wakiwemo Mwandishi wa Habari wa Nipashe, Bwana Godfrey Mushi, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake CHADEMA Wilaya ya Mufindi, Bibi Winnie Sanga na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mufindi, Asseli Mwampamba aliyekuwa akifanya jitihada za kumuokoa marehemu Daudi Mwangosi.

Kutokana na hayo yote, Tume imejiridhisha kuwa tukio lililopelekea kifo cha Daudi Mwangosi limegubikwa na uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

2.1 Uvunjwaji wa Haki za Binadamu
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977, sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Azimio la Kimataifa la Haki za Binadamu (Universal Declaration of Human Rights of 1948), Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za kiraia na kisiasa (International Covenant on Civil and Political Rights of 1966) na Mkataba wa mataifa ya Afrika kuhusu Haki za Binadamu na Watu (African Charter on Human and Peoples Rights of 1981), Tume imejiridhisha kuwa Jeshi la Polisi limevunja haki zifuatazo:
    • Haki ya kuishi,
    • Haki ya kutoteswa na kupigwa,
    • Haki ya usawa mbele ya sheria na
    • Haki ya kukusanyika na kutoa maoni.

CHADEMA ni chama cha siasa ambacho kina usajili wa kudumu.  Chini ya sheria ya vyama  vya siasa (Cap. 258 RE. 2002), vyama vya siasa vyenye usajili vimeruhusiwa kufanya maandamano na kuwa na mikutano ya kujitangaza baada ya kutoa taarifa kwa “Afisa wa Polisi” wa eneo husika.  Baada ya taarifa kutolewa chama husika kinatakiwa kipewe ulinzi na “security agencies” (mawakala wa usalama).

2.2 Ukiukwaji wa Misingi ya Utawala Bora
Ili pawepo utawala bora mamlaka zote za serikali ni lazima zifuate utawala wa sheria.  Uchunguzi umebaini kuwa kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a) na (b) na sheria ya Polisi (Sura ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli za CHADEMA wakati yeye hakuwa “Officer In-charge” wa polisi wa eneo husika. Kwa maana hiyo amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo.  Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka, hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.

Aidha, hatua ya Msajili wa vyama vya siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa ndani ya barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa pia ni kinyume na sheria ya vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002) Kifungu cha 11(a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake bila ya kuingiliwa.

Ibara ya 8(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelezea kwamba Tanzania ni nchi inayofuata misingi ya demokrasia na Haki ya Kijamii, aidha ibara 18(b) na (c) ya Katiba inaeleza kuwa kila mtu anayo haki ya kufanya mawasiliano (kutoa maoni/habari) na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake.  Haki hii imekiukwa kwa kiasi kikubwa na Jeshi la Polisi katika tukio la Nyololo Mufindi kwa kuwa waandishi wa habari na wafuasi wa CHADEMA walizuiwa na Polisi kufanya shughuli zao za kupata habari na za kisiasa.  Huu ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa kuwa hali hiyo inazorotesha au inafifisha uhuru wa habari.

3.0 MAONI NA MAPENDEKEZO
Kwa kuzingatia Sheria ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Na. 7 ya mwaka 2001 Kifungu cha 15(2)(c) na 28 Tume inapendekeza yafuatayo:
    1. Kamati za ulinzi na usalama za Mkoa na Wilaya ziwe makini na vitendo vya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utalawa bora vinavyofanywa na mamlaka mbalimbali kwenye maeneo yao.  Aidha, kamati hizo zihusike moja kwa moja na usalama wa wananchi na mali zao kwa kujadili masuala yote ya kiusalama kabla hatua hazijachukuliwa na vyombo vinavyotekeleza sheria.
    1. Viongozi wa CHADEMA na wafuasi wao waepuke malumbano na vyombo vya dola kwa kutii maagizo yanayotolewa na vyombo hivyo bila shuruti.  Pale wanapogundua kuwa pana uonevu au upendeleo ni vyema busara ikatumika ili kuepusha madhara makubwa yanayoweza kutokea.
    1. Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Mfano, Jeshi la Polisi lilizuia mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huo huo Chama cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wakifanya uzinduzi wa Kampeni huko Zanzibar.  Aidha, rai ya Msajili wa vyama vya siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA walishurutishwa na Polisi kutii rai hiyo.
    1. Demokrasia ya mfumo vya vyama vingi iheshimiwe na kulindwa.
    1. Elimu ya vyama vya siasa na sheria ya Polisi kuhusu vyama vya siasa itolewe kwa askari polisi ambao wanaonekana kutozifahamu kabisa.

4.0 HITIMISHO
Jukumu la kulinda amani na utulivu ni wajibu wa kila mtanzania, mkulima na mfanyakazi, viongozi wa serikali na watumishi wa umma wote wanapaswa kuwa wazalendo wa kweli wakati wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.  Tume inatoa wito kwa watanzania wote kuheshimu haki za binadamu na kutekeleza kwa vitendo misingi ya utalawa bora.  Kwa kufanya hivi Taifa letu litaendelea kuwa na amani na utulivu.  Tume inatoa rai kwa jeshi la polisi kutekeleza wajibu wake mkuu wa ulinzi na usalama wa raia bila kutumia jazba.

Kuwepo kwa vyama vya siasa ionekane kuwa ni kukuwa kwa demokrasia na sio kuwa ni upinzani kwa chama tawala.

....................................................
Jaji Kiongozi (Mstaafu) Amiri R. Manento

MWENYEKITI
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA

OKTOBA 10, 2012

CHANZO: MICHUZI-MATUKIO

Tuesday, October 9, 2012

Programu za Kupeleka Wanafunzi Nje

Leo hapa chuoni St. Olaf, tumefanya shughuli ya kutangaza programu zinazowapeleka wanafunzi kwenye masomo nje ya chuo hapa Marekani na nchi za nje. Ni shughuli ambayo tunafanya kila mwaka, wakati kama huu. Tunawapa wanafunzi fursa ya kuzifahamu programu hizi. Mimi ni mshauri wa program ya ACM Tanzania, ACM Botswana, na Lutheran Colleges Consortium for Tanzania (LCCT).









Chuo cha St. Olaf kinaendesha programu nyingi sehemu mbali mbali duniani. Pia kinashiriki katika programu za vyuo na taasisi nyingine, kwa maana kwamba wanafunzi wa chuo hiki wanayo fursa ya kujiunga na programu zile. Kuna programu za mwezi mmoja, muhula mmoja, na hata mwaka.


















Chuo cha St. Olaf ni maarufu hapa Marekani kwa programu zake hizi za kupeleka wanafunzi nje. Wanafunzi wengi huja kusoma hapa kwa sababu ya fursa hizo. Nami kama mdau mkubwa wa masuala ya kujenga mahusiano baina ya mataifa na tamaduni mbali mbali nimejizatiti sana katika shughuli ya ushauri wa programu hizi. Mara kwa mara ninawapeleka wanafunzi Tanzania. Ni jambo lenye manufaa makubwa kwa wanafunzi hao, kwa Tanzania, kwa Marekani na bila shaka kwa ulimwengu kwa ujumla. Wanafunzi hao wanapata fursa ya kufanya masomo na wanafunzi wa kiTanzania, kufahamiana na wa-Tanzania, na kujipanua upeo kitaaluma na kimtazamo. Pia, ni lazima niseme kuwa wanaingiza hela nyingi za kigeni katika hazina ya Tanzania, kwa visa wanayolipia ubalozini, masomo wanayolipia mahali kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na mizunguko ya kitalii wanayofanya vipindi vya mapumziko.











Kwa upande wangu, shughuli hii ya leo, kama ilivyo kawaida kila mara, ni fursa ya kuonana na wanafunzi wengi na kuwaeleza habari za Tanzania na Botswana, na habari za masomo yanayotolewa katika programu husika katika nchi hizo. Ni fursa ya kujibu masuali yao mbali mbali na kuwavutia wajiandikishe kwenye programu hizi.

Saturday, October 6, 2012

Nimejipatia iPad

Pamoja na kuwa mimi ni mmoja wa wale watu wa zamani tuliozaliwa na kukulia kijijini na ambao tunababaishwa na hizi tekinolojia zinazofumuka kwa kasi, nimejipatia kifaa kiitwacho iPad siku chache zilizopita. Nimenunua iPad Wi-Fi+3G. Nilishinikizwa na binti yangu Zawadi. Ndiye anayenisukuma niende na wakati.

Tangu ninunue kifaa hiki, yapata wiki mbili zilizopita, nimekuwa katika kujifunza namna ya kukitumia, maana kina mambo mengi sana. Angalau naweza kutembelea mitandao, kutuma na kupokea barua pepe, na kupiga picha na kisha kuziangalia. Hata video najua namna ya kupiga.

Kitu ninachotaka kukifanya hima ni kuingiza vitabu pepe kwenye hii iPad, nikianzia na kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho wadau wanakipata mtandaoni, pamoja na vitabu vyangu vingine, kwa njia hiyo.





Kidogo najisikia vibaya kwamba nilikiweka kitabu hiki katika muundo wa kitabu pepe na wadau wanakinunua, wakati mimi mwenyewe sikuwa na kifaa cha kuingizia vitabu pepe wala sikuwahi hata kuona kinakuwaje katika umbo la kitabu pepe. Nimejisikia kama mpishi ambaye anawapikia wengine lakini yeye mwenyewe hata kuonja haonji. Sasa, na hii iPad yangu, ngoja nikae mkao wa kula, kwa vitabu vyangu na vya wengine.

Unaweza Kushindwa Mtihani wa Dini Yako

Siku za hivi karibuni kumekuwa na zogo kubwa Tanzania kutokana na wanafunzi kushindwa mtihani wa dini yao. Sikufuatilia vizuri undani wa kisa hicho na siwezi kukiongelea. Badala yake, napenda tu kuongelea suala la kinadharia la mtu kushindwa mtihani kuhusu dini yake.

Tunapokuwa kanisani au msikitini, kwenye mihadhara ya dini au madrassa ya dini, tunafundishwa dini yetu kwa maana ya kwamba tunaelekezwa tuelewe dini inasema nini ili tuwe waumini bora. Suala ni kutujenga kiimani na kimaisha kwa mujibu wa dini yetu, kutokana na yale anayofundisha padri, imam au sheikh.

Mambo ni tofauti tunapokuwa shuleni au chuoni. Mimi ni mwalimu, na ingawa sifundishi dini, napenda kusema kuwa darasani hatufundishi kwa lengo la kujenga imani ya watu kwenye dini yao. Labda kabla sijaenda mbali, nifafanue kuwa naongelea kiwango cha chuo. Kwenye madarasa ya mwanzo, ambako tunawafundisha watoto, naamini tunategemewa kuwafundisha dini kwa lengo la kuwafanya wawe waumini bora.

Lakini, lengo langu hapa ni kuongelea ufundishaji wa dini vyuoni. Kwenye chuo, kazi yetu ni kutafakari na kuchambua dini, kuhoji na kudadisi. Tunawajibika kutafakari historia ya dini husika, mafundisho yake, mwelekeo wake, athari zake katika jamii na kadhalika.

Chuoni tunapaswa sio tu kusoma na kuongelea yaliyomo katika misahafu na yaliyosemwa na watetezi wa dini husika, bali tunapaswa pia kusoma na kutafakari yaliyosemwa na wapinzani wa dini. Kwa mfano, ni wajibu kutafakari kauli kama zile za Karl Marx kwamba dini ni kama bangi ya jamii yenye matatizo. Darasani tunapaswa kujadili kauli za aina hiyo kwa makini, na kila mwanafunzi anawajibika kutumia akili yake ili kujenga hoja zake.

Kwa hivyo, hata kama mtu ni muumini bora wa dini yako, mtu ambaye umeelewa na kukubali kila kinachosemwa kanisani au msikitini, ukija kwenye mtihani unaweza kufeli. Kwa msingi huo huo, kwa vile darasani ni mahali pa kuchambua na kutafakari masuala, kama mtihani ni wa dini ya u-Islam, muislam anaweza kufeli na m-Kristu akafaulu. Vile vile, kwenye mtihani wa dini ya u-Kristu, mu-Islam anaweza akafaulu na m-Kristu akafeli.

Napenda kutoa mfano ambao unaweza kufafanua hoja yangu. Nakumbuka tulipokuwa shuleni, mkoani Ruvuma, mbali kabisa na pwani, tulikuwa tunajiamini kwamba pamoja na kuwa ki-Swahili si lugha yetu ya kwanza, tuna uwezo wa kufaulu mitihani ya ki-Swahili kuliko vijana wa pwani ambako ki-Swahili ni lugha yao ya kwanza. Kama nakumbuka vizuri, matokeo ya mitihani yalidhihirisha jambo hilo, nasi tukawa tunawacheka vijana wa pwani.

Basi, katika mitihani ya dini mambo ni hayo hayo. Watu tusijiaminishe kuwa kwa vile sisi ni waumini wa dini fulani, basi ni lazima tufaulu mtihani wa dini hiyo. Ukweli ni kuwa kwa vile shuleni au chuoni somo la dini linakuwa katika mkabala wa ki-taaluma, hata mtu asiye na dini anaweza kufaulu mtihani wa dini na sisi waumini tukafeli.

Friday, October 5, 2012

Mkutano wa Cheetah Development

Jana jioni nilihudhuria shughuli ya Cheetah Development mjini St. Paul. Cheetah Development ni mtandao wa watu wanaojishughulisha na miradi ya maendeleo Afrika Mashariki, hasa Tanzania. Nilijulishwa kuhusu mtandao huu na rafiki yangu Mzee Paul Bolstad, ambaye anaonekana kushoto kabisa hapa pichani.
Yeye na huyu mwingine ni marafiki wa tangu zamani. Wote ni wapenzi wakubwa wa Tanzania. Mzee Bolstad alizaliwa na kukulia Tanzania, na huyu mwenzake walikuwa wote katika programu ya Peace Corps Tanzania walipokuwa vijana.
Walihudhuria watu wengi Kulikuwa na hotuba na maonesho ya shughuli mbali mbali za Cheetah Development.





































Kikundi cha kwaya kiitwacho imuka, kutoka Bukoba, ambacho kiko katika ziara hapa Marekani, kilitoa burudani.













Tulikutana wa-Tanzania kadhaa, tukabadilisha mawazo na kupiga michapo.

Wednesday, October 3, 2012

Museum Africa, Johannesburg

Nilipokuwa Johannesburg, mwezi Juni, nilitembelea sehemu kadhaa za jiji hilo. Hiyo ilikuwa ni tarehe 17. Kwenye kitongoji cha Newton niliweza kuona taasisi kadhaa, mojawapo ikiwa Museum Africa. Hili ni jumba la makumbusho ambamo wamehifadhi vitu vingi vya kihistoria. Kwa mfano, kuna picha nyingi sana na maelezo kuhusu siku za mwanzo kabisa za Johannesburg, kwa mfano usafiri ulivyokuwa, simu, nyumba ya mwanzo ya ibada, na idara ya mwanzo kabisa ya zimamoto, ambayo haikuwa na vifaa tunavyovijua leo. Ni kumbukumbu murua sana kwa yeyote anayeithamini historia.






Museum Africa sio kumbukumbu pekee eneo hili la Newton. Ziko nyingine pia. Ukiingia humo ukakaa saa moja, mbili, au zaidi ukiangalia na kusoma yaliyomo, utatoka ukiwa umeelimika sana. Insh'Allah nitaleta taarifa zaidi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...