Nimepata Zawadi Murua ya Krismasi Leo

Wafuatiliaji wa fasihi ya ki-Ingereza wanafahamu kuwa juzuu la pili la barua za Hemingway, limechapishwa mwaka huu. Sawa na juzuu la kwanza, hili ni buku kubwa, kurasa 519.

Leo nimepokea kifurushi kutoka Amazon.com. Binti yangu Zawadi aliponiletea nilishangaa, maana sijaagiza kitabu kutoka Amazon kwa miezi kadhaa. Nilipofungua kifurushi sikuamini macho yangu. Ni juzuu hilo nililolitaja. Nimefurahi sana. Nilikuwa natamani kufanya mkakati wa kununua. Lakini Mungu mkubwa, kamwongoza huyu bwana aninunulie hiki hiki ambacho roho yangu ilikuwa inatamani.

Bwana aliyeniletea ni David Cooper, mzazi wa mwanafunzi mmojawapo wa wale waliokuja Tanzania mwezi Januari mwaka huu kwenye kozi ya Hemingway. Baba huyu ni msomaji makini wa Hemingway na waandishi wengine.

Ni huyu bwana, anayeishi Ohio, alipoambiwa na kijana wake kwamba natamani siku moja kwenda Montana kuongea na Mzee Patrick Hemingway, mtoto pekee wa Ernest Hemingway aliebaki, alisema atatusafirisha kwa ndege yake.

Siku ilipofika, yeye na rubani wake walifika Minnesota, wakatuchukua, mimi na wanafunzi wawili, akiwemo yule kijana wake.

Bwana huyu ni kama tumejenga urafiki. Namshukuru sana.
 

Comments

Anonymous said…
Hongera
Mbele said…
Asante sana. Ujumbe wako umenigusa. Nilidhani umma wote unaniona nimechemsha kwa kushangilia zawadi ya kitabu kama vile ingekuwa kreti ya bia. Lakini ndivyo nilivyo.
Anonymous said…
Prof umeanza kuishiwa au tuseme kuzeeka. Huo umma umeongea nao lini kama siyo hisia tu? Yaani ulitaka kila jambo lako binafsi upongezwe? Sikupendezwa na hitimisho lako la jumla kuwa umma tena wote umeona umechemsha. Mbona hakuna hata comment moja inayosema umechemsha kama siyo kuakisi hisia na woga wako? Tujaribu kuwa wavumilivu. Si kila utakachoandika lazima kikubalike kwa wote.
Mbele said…
Wewe anonymous wa pili nenda shule kajifunze ki-Kiswahili. Nilichoandika ni kuwa "nilidhani" sio kwamba nilijua. Hakuna ubaya mtu kuwa na hisia. Na hisia yangu ina msingi kwamba jamii yetu haithamini vitabu. Nimeandika sana katika blogu hii, nikiungana na wataalam mbali mbali wa masuala ya vitabu, ambao wanalalamikia tabia hii ya jamii ya wa-Tanzania kutothamini vitabu. Pita pita katika blogu hii utakuta makala mbali mbali kuhusu jambo hilo.

Sasa watu kama hao wakikuona unashangilia zawadi ya kitabu, hutakosea iwapo utahisi kuwa wanaweza kukudhania umechemsha.

Yamenipata hayo ninayosema. Nilisomea Marekani MA na PhD kwa miaka sita, 1980-86, nikanunua vitabu vingi sana, nikijua kuwa ni nyenzo nitakayohitaji wakati wa kurudi kuendelea kufundisha Chuo Kikuu Dar.

Nilipofika na hiyo shehena ya vitabu, watu walinishangaa kwamba nimekaa Marekani miaka yote hii halafu nikarudi na vitabu badala ya "pick-up" au gari jingine. Kwa lugha rahisi, waliniona nimechemsha.

Hiyo dhana ninayokuambia, kwamba nahisi umma unananishangaa kwa kushangilia namna hii zawadi ya kitabu, kwa maneno maneno mengine, dhana yangu kwamba naweza nikaonekana nimechemsha ina misingi.

Hadi sasa mimi nina vitabu zaidi ya elfu tatu. Na sidanganyi ninaposema kuwa nafurahia kujipatia kitabu kuliko mzinga wa "brandy."

Sasa nawe nipe maelezo yako, unielimishe zaidi.

Vinginevyo, napenda kukuambia kuwa blogu hii ni sehemu ambapo najiwekea mambo yangu binafsi, kuanzia hisia, mawazo, kumbukumbu na kadhalika. Sina deni na mtu, na siombi wala kuhitaji kibali cha mtu. Wala mimi sio bendera kufuata matakwa ya yeyote anayeamua kusoma blogu yangu.

Sasa wewe kutua kijiweni mwangu humu na kudai kuwa nimeishiwa, kama vile unajua kinachoendelea akilini mwangu, ni jambo la kushangaza. Tena husemi kuwa unahisi nimeanza kuishiwa, bali unatamka kama vile una ushahidi, una uwezo wa kuona kilichomo kichwani mwangu.

Ongelea mambo ambayo una uhakika nayo, kama huna uhakika, bali ni hisia, sema kuwa ni hisia.

Narudia, siandiki blogu hii kumpendeza yeyote. Wala sikukukarisha hapa.

Inaonekana hunifahamu kabisa, kwamba, kama profesa, wajibu wangu na mategemeo yangu si kutegemea kupongezwa. Hujui wadhifa na wajibu mmojawapo wa profesa ni kuanzisha au kushiriki mijadala na malumbano, ambamo atapingwa na kupinga hoja. Huwezi ukawa profesa wa kweli ukawa unategemea kupongezwa kwa "kila utakachoandika," au kwamba "kila utakachoandika lazima kikubalike kwa wote." Uhai wa taaluma uko kwenye malumbano.

Kama hufahamu maana ya uprofesa, tafadhali nyamaza, usinifanye nikakushambulia kwa ukali kwa kusema mambo usiyoyajua.

Kama unajiamini, weka wazi jina lako, ili niweze kujua ni nani anayeandika upuuzi kama wako.

Nimalizie kwa kusema kuwa blogu hii si ukumbi wa kiprofesa. Ukitaka kujua mchango wa kiprofesa, kuna machapisho mengi kwenye vitabu na majarida sehemu mbali mbali duniani. Humo utaona sijaishiwa, bali naendelea kufanya utafiti na kutoa mchango wa kitaaluma.
Anonymous said…
Mzee sema ukweli kuwa umeishiwa. Mbona yule Anon wa kwanza ambaye maneno yake "yamekugusa" hukkutaka aandike jina lake?
Kama profesa kwanini usikubali kuwa kuishiwa ni sehemu ya uhalisia wa maisha ya binadamu.Nadhani kwa kusema umeishiwa nimechokoza mjadala ambapo ulipaswa kuonyesha kuwa huajishiwa. Hata hayo machapisho unayotamba nayo siyaoni. Je umeandika vitabu vingapi vya kisomi ukiachia kile unachokipigia debe kila mwaka ulichochapisha mwenyewe? Naomba unisamehe kama nimekukwaza. Haikuwa nia yangu na nashukuru kujua kuwa kumbe sikaribishwi.
Nakutakia mwaka mpya.
Mbele said…
Kitabu changu unachokiwazia sikukiandika kama kitabu cha taaluma. Nimetamka hayo katika kitabu chenyewe, ukurasa wa 4. Nanukuu:

Finally, this booklet is not a scholarly study; it is more like a collection of a traveler's tales, anecdotes, and thoughts.

Kwa watafiti katika taaluma kama "folklore," ambayo ni mmoja ya taaluma ninayoshughulika nayo sana, tunajua kuwa hizo "anecdotes," michapo, na kadhalika, husema ukweli wa jamii pengine kwa usahihi na undani kuliko hata taarifa za utafiti wa taaluma zingine. Ndio maana nikazitumia katika kuandika kitabu hiki. Na nahisi ndio maana kinawagusa watu.

Kwa sababu sikutaka mtu yeyote, awe mhariri au nani, aingilie staili na mtindo wa uandishi wangu wa kijitabu hiki, niliamua kukichapisha mwenyewe. Hakuna aliyeshiriki katika kuandika hata sentensi moja au kurekebisha hata sentensi moja.

Pamoja na mimi kujichapishia kijitabu hiki, kinapendwa na kutumiwa na kupigiwa debe na watu mbali mbali, taasisi, na maprofesa hapa Marekani wa vyuo na masomo mbali mbali wanakitumia katika kozi zao. Huhitaji kufanya juhudi kubwa bali taarifa utazikuta mtandaoni.

Napenda kurudia na kusisitiza, profesa wa kweli hakwaziki na hoja. Hata katika blogu hii, wadau mara kwa mara wanapinga hoja zangu, na hakuna tatizo. Hilo ni jambo jema kabisa, kwani kwa namna hii nami najifunza.

Unakaribishwa kujenga hoja za kupinga hoja zangu, kama wanavyofanya wadau wengine, na mimi sisiti kupinga hoja za wengine ninapoona wamepotoka.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini