Furaha ya Kusainiwa Kitabu

Wapenzi wa vitabu wakishajipatia nakala ya kitabu cha mwandishi fulani, huguswa pale mwandishi anaposaini kitabu hicho. Aghalabu mwandishi huandika ujumbe mfupi kwa mteja huyu na kasha kuweka sahihi. Ni jambo linalowagusa sana wasomaji. Mimi mwenyewe, kama mwandishi, nimeshasaini vitabu vyangu vingi. Ninazo baadhi ya picha za matukio haya kutoka miaka iliyopita.

Msomaji makini na mwanablogu Christian Bwaya hivi karibuni ameelezea vizuri katika blogu yake, hisia zake baada ya kujipatia kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differencesambacho nilikuwa nimekisaini:

Namshukuru kwa dhati mwandishi wa kitabu hiki, Prof. Mbele kwa kunitumia kitabu hiki bila malipo, tena kwa gharama zake. Si jambo linalowatokea wengi. Ni furaha iliyoje hatimaye nimekipokea leo asubuhi. Naanza kukisoma kitabu hiki kwa mara nyingine, safari hii kikiwa na saini ya mwandishi. Ni upendeleo na muujiza wa pekee kunitokea katika siku za hivi karibuni. Ni lazima nimshukuru kwa dhati. Asante sana Profesa.

Utamaduni wa kusaini na kusainiwa vitabu nimeuzoea. Hata juzi tarehe 2 Agosti, niliposhiriki tamasha la Afrifest kule Brooklyn Park, Minnesota, nikiwa na vitabu vyangu, wadau kadhaa walionunua vitabu vyangu waliomba kusainiwa.

Hapa kushoto anaonekana mdau akiniangalia wakati nasaini nakala ya Matengo Folktales, ambayo alikuwa amenunua hapo.
Baada ya kusainiwa nakala yake, aliona furaha ya ziada kupiga picha nami huku akiwa ameshika kitabu hicho. Hiyo nayo ni kawaida hapa Marekani; wadau wakishanunua kitabu na kusainiwa, wanapenda kupiga picha na mwandishi, ikiwezekana.

Mdau huyu, aitwaye Adrian, m-Marekani Mweusi, alinifahamu tangu miaka kadhaa iliyopita. Alikuwa anasoma katika chuo fulani mjini Minneapolis. Kulikuwa na mkutano wa kitaaluma, nami nilikuwa mmoja wa wanajopo, nikitoa mada. Adrian alivutiwa sana. Halafu, alinisikiliza tena mwaka jana, nilipokuwa naongea katika jopo la watu wawili, nikiwa na Profesa Mahmud el-Khati, m-Marekani Mweusi, tukiongelea mbele ya umati, mahusiano baina ya wa-Afrika na wa-Marekani Weusi.

Adrian ni msomi kijana makini. Tayari naona nyota yake imeanza kung'ara katika medani ya uongozi katika jamii. Nina imani atafika mbali katika jamii ya wa-Marekani weusi na Marekani kwa ujumla.
Hapa kushoto ni picha nyingine, kutoka hiyo hiyo juzi katika tamasha la Afrifest, nikiwa na mdau kutoka Liberia, ambaye alikuwa amenunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nami nikiwa nimekisaini. Inaonekana aliguswa sana, na hakuweza kujizuia kuniwekea mkono wake begani pangu.

Suala hili la kusaini au kusainiwa vitabu linastahili  kutafakariwa. Naamini lina vipengele kadhaa muhimu, kama vile kiutamaduni, kisoshiolojia, kisaikolojia, na kifalsafa. hata katika maduka ya vitabu hapa Marekani, aghalabu utaona vimepangwa vitabu vya mwandishi vikiwa na ujumbe "Signed copy." Jambo hili linaisukuma akili yangu kutaka kulielewa zaidi. Ningependa kujifunza zaidi kuhusu suala hili, kwa kusoma maandishi mbali mbali na kufanya tafakari mwenyewe.

Comments

Jamani! Hongera SANA. Nasikitika nami ningepiga picha nawe na vyote viwili maana ninavyo vyote hivyo...
Mbele said…
Dada Yasinta, asante kwa kauli yako. Nashukuru pia kwa jinsi ambavyo umekuwa mstari wa mbele katika kuelewa ninachojaribu kuwajulisha walimwengu katika hivi vitabu vyangu.

Mungu si Athmani, huenda tukakutana Ruhuwiko. Nami huwa natembea na nakala za hivi vitabu. Tukikutana, tutapiga hiyo picha.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini