Thursday, November 11, 2021

Msomaji na Mpiga Debe Wangu Aikwaa Tuzo

Jana niliandika taarifa za msomaji na mpiga debe wangu Joy Zenz, mKenya aishiye uJerumani.

Napenda niseme kuwa juhudi zake za kuwaunganisha akina mama waAfrika waliko Ulaya na kwingineko na kuwahamasisha katika masuala ya maendeleo kwao na kwa bara la Afrika yamemfanya atambuliwe na kutuzwa kwa namna mbali mbali.

Leo nimeona taarifa kuwa ameikwaa tuzo muhimu ya Global Africa Awards. Nimefurahi na ninampongeza kwa dhati msomaji wangu huyu na mpiga debe.

Tuesday, November 9, 2021

WaKenya Wazidi Kukinadi Kitabu


Nimewahi kuandika mtandaoni tena na tena nikiwasifu na kuwashukuru waKenya kwa jinsi walivyokuwa bega kwa bega nami katika utafiti na uandishi wangu.

Huku Marekani, waKenya wamekuwa wasomaji na wapiga debe wangu wakuu kama nilivyotamka, kwa mfano, hapa na hapa.

Sasa amejitokeza mKenya mwingine, Joy Awe, aishiye uJerumani. Yeye ni mwanzilishi na mratibu wa jumuia iitwayo African Women in Europe.

Ameweka picha zake mtandani akiwa na kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, pamoja na ujumbe huu:

Highly recommended book to read especially diaspora or anyone wanting to do business in Africa. Available on Amazon.

Naendelea kuwashukuru waKenya kwa mshikamano nami.

Sunday, November 7, 2021

Simulizi za Wanawake waAfrika Waishio Ulaya


Ninaandika ujumbe huu nikiwa ninavisubiri vitabu viwili vya wanawake waAfrika waishio Ulaya. Napenda nielezee jinsi nilivyopata taarifa za vitabu hivi.

Tarehe 31 Mei hadi 4 Juni mwaka huu nilishiriki mkutano mkubwa mtandaoni, "Trade With Africa Business Summit." Mwandaaji, Toyin Umesiri, alikuwa ameniomba nikazungumzie kitebu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilifanya hivyo, nikijikita katika kuongelea vipengele vya tamaduni vinavyohitaji kuzingatiwa katika biashara baina ya waAfrika na waMarekani.


Kwenye mkutano ule, nilipata kufahamiana na mtoa mada Joy Wanjiru Zenz, mama mKenya aishiye uJerumani na ni mwanzilishi na mwendeshaji wa jumuia ya wanawake waAfrika waishio Ulaya. Alishuhudia jinsi kitabu changu kilivyokuwa kinatajwa na baadhi ya washiriki wa mkutano.

Siku kadhaa baada ya mkutano, Joy nami tuliwasiliana,  akanieleza kuwa wanajumuia wake wamechapisha vitabu kuhusu maisha yao Ulaya. Nilivutiwa na taarifa hii. Ninayafahamu maisha ya waAfrika Marekani, lakini si Ulaya. Ilibidi nimwambie Joy kuwa ninahitaji vitabu hivi. Ninavisubiri kwa hamu.

Saturday, November 6, 2021

Msomaji Wangu Mpya, mTanzania wa Czech

Wiki hii ya kwanza ya Novemba, 2021, nimemmpata msomaji mpya, Corona Cermak, mTanzania aishiye Jamhuri ya Czech. Nilisikia jina lake kwa mara ya kwanza kutoka kwa dada Joy Wanjiru Zenz, mKenya aishiye uJerumani, ambaye aliniambia kuwa kuna huyu mTanzania mwandishi aishiye Czech.

Katika kufuatilia Facebook, YouTube, na Instagram, nimeona shughuli za Corona, za ufundishaji wa kiSwahili na uandishi wa vitabu vya watoto. Vitabu alivyochapisha ni The Rooster's VoiceSauti ya Jogoo, na Grandma Pipi and the Roses.

Juzi nilimwandikia kuwa nimeagiza vitabu vyake Amazon, naye hima akaniletea picha akiwa ameshika kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. alichoagiza hivi karibuni mtandaoni.

Mara tu baada ya kukipata kitabu changu, amekisoma na kukiongelea mitandaoni Instagram na Facebook akiwahimiza watu waendao Marekani, Ulaya, na Tanzania wakisome. Amesema pia kuwa ameagiza kitabu changu cha Matengo Folktales. Ni bahati njema kufahamiana na mwalimu na mwandishi mwenzangu, mTanzania aishiye ughaibuni. Tunategemea kubadilishana mawazo na uzoefu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...