Ninapokuwa katika miji kama Dar es Salaam, napatikana mitaa ya u-Swazi, kama inavyoonekana katika picha hii, iliyopigwa Sinza, bondeni ukifuata barabara inayopita mbele ya Lion Hotel. Kwa wale wasiojua, neno u-Swazi linamaanisha sehemu wanazoishi wananchi wa kawaida.
Hapo kushoto kuna baa na sehemu ya kitimoto ambapo nimeshakuwa mteja mara kadhaa. Picha hii inaonyesha jinsi mwenye kitimoto anayotangaza biashara yake. Tofauti na zamani, anaweza kuagiza nyama kutoka bucha kwa kutumia simu, na anaweza kuchukua oda za wateja kwa simu pia.Pamoja na umaarufu wake, kuna hisia tofauti, michapo, na utani kuhusu kitimoto, mambo ambayo yanaweza kufanyiwa utafiti kama sehemu muhimu ya utamaduni wa leo wa m-Tanzania.