Monday, April 25, 2022

Mdau Wangu Makini Katutembelea

Leo hapa Chuoni St. Olaf alifika mama mmoja kutoka Togo ambaye anaishi kwenye mji wa mbali kiasi kutoka hapa nilipo. Alimleta binti yake kwenye programu fulani ya wanafunzi. 

Mama huyu ni mdau wangu hodari, kwa maana kwamba ni msomaji wa tangu zamani wa vitabu vyangu na maandishi mengine, na ni mfuatiliaji wa shughuli zangu za kuelimisha jamii. 

Kwenye haya matamasha, huwa sikosi kuwaona waAfrika  wa nchi kama vile Somalia,  Kenya, Ethiopia, Uganda, Sudani, Congo, Nigeria, Togo, Liberia au Ghana. Ninafurahi kuwa wadau kutoka nchi zote hizo wamenunua na wamevutiwa na kitabu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.



Friday, March 18, 2022

Nimekutana na Mdau Wangu Mwingine

Leo nilienda Mall of America kukutana na Tanya, mjumbe wa bodi ya shule za Osseo District. Tulifahamiana miezi kadhaa iliyopita, siku nipotoa mhadhara kwa Rotary Club of Brooklyn Park. Alikuwa mmoja wa wahudhuriaji, na nilimfahamu siku hiyo kama mjumbe wa bodi ya shule za Osseo District.

Nilikuwa nimemwomba tukutane, kwa sababu nilikuwa na mambo ya kumwuliza. Moja ni kuhusu uwezekano wa kujenga uhusiano baina ya shule za Osseo District na shule ya Bukoba, Tanzania, ambayo uongozi wake uliniomba niwatafutie uwezekano huo hapa Marekani.. 

Jambo jingine nililotaka kuongea naye ni muendelezo wa yale machache tuliyogusia siku ya mhadhara wangu, ambao yanahusu kuzuia au kutatua migogoro inyotokea shuleni. Tulikuwa tumakubaliana kwamba tofauti za tamaduni zinachangia tatizo hilo.

Jambo la tatu ni kuwa nilitaka kumpa nakala ya Chickens in the Bus: Embracing Cultural differences. Nilishampa Africans and Americans: Embracing Cultural Differences baada kukutana mara ya kwanza. Ilikuwa ni furaha leo kusaini hiki kitabu na kumkabidhi. Huyu namhesabu kama mdau wangu muhimu.

Tumeongea mengi yanayohusu shule, kuhusu migogoro mashuleni itokanayo na tofauti au changamoto za tofauti za tamaduni na kadhalika. Tumegundua kuwa kwa ujumla tuna mitazamo inayofanana. Tumekubaliana kushirikiana kwa dhati siku zijazo katika kutafuta njia za kutatua changamoto zilizopo.
 

Saturday, March 12, 2022

 WADAU WA UTALII KWENYE MHADHARA WANGU ARUSHA

Tarehe 8 Januari, 2022, nilitoa mhadhara Arusha, mada ikiwa "challenges of cultural differences," yaani changamoto za tofauti za tamaduni. Hii ni mada ambayo naiongelea na kuiandikia sana. Mwandaaji wa mhadhara alikuwa mama Ama, mMarekani Mweusi. Walihudhuria watu wa mataifa mbali mbali, lakini zaidi kutoka Marekani na Tanzania. Tuilkaa kwa takriban saa tatu.
Baadhi ya waTanzania waliohudhuria ni vijana wa kampuni ya utalii iitwayo Rift Valley Cultural Tourism, ambayo makao yake ni Karatu. Kupitia kwa mkurugenzi wa kampuni, wote walikuwa wamepata nakala za kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences," na walikuwa wamekisoma. 

Waliposikia kuwa ninatoa mhadhara, waliamua kuhudhuria. Tulifurahi kukutana. Baada ya mhadhara, tulipiga hii picha inayoonekana hapa juu; baadhi yao wameshika kitabu changu. Wadau wa utalii ni wanufaika wa moja kwa moja wa kitabu hiki. Hii ilidhihirika mwaka 2007 wakati mkurugenzi wa J.M. Tours aliponunua nakala kadhaa akawapa madreva waongoza watalii wake wasome. 

Walikifurahia kwa msingi kwamba kiliwawezesha katika kushughulika na watalii. Niliandika kuhusu hilo kwenye makala yangu, "My Arusha Readers."
Ninawapongeza Rift Valley Cultural Tourism kwa kutambua fursa na kuitumia. Niko tayari kuwa nao bega kwa bega katika masuala ya utalii na utamaduni, kubadilishana uzoefu na kuelimishana. 

Mbali ya vitabu vyangu, ambavyo vinapatikana mtandaoni, nawakaribisha kwenye chaneli yangu ya YouTube.

Saturday, February 12, 2022

MTanzania Ughaibuni Aongelea Kitabu cha "Matengo Folktales"

 

Wiki za hivi karibuni nimepata kufahamiana na dada Corona Cormak, mTanzania aishiye Jamhuri ya Czech. Ni mwandishi mahiri wa vitabu vya watoto, ambavyo nimesoma nikavifurahia. Pia ni msimuliaji hodari wa hadithi.

Wiki hii, katika ukurasa wake wa Instagram, Coriona ameandika uchambuzi wake wa kitabu changu Matengo Folktales. Ameandika hivi:

I will start with a big smile. This book Matengo Folktales by John Mbele @africonexion. Took me way back into those days of story telling. Three stories in this book were so vividly. The Monster in the Rice, The Tale of two women and the Tale of Katigija. The sound of the songs in these stories is what I am still trying to remember. These songs were always sang with everyone when the stories were narrated. This is what is missing in story telling these days. We let our children just listen to the story without them taking part.

However, I am quite shocked with the amount of killing in every story. At least I don't remember the killing part. For example the Tale of two women, I remember this part when the woman was told to lick the wounds. And in Katigija Tale I remember the grandma singing when she brought the food to the child and the Monster in the Rice field, I remember how the children kept on disappearing.

My son was shocked when I told him The tale of Monster in the Rice. He was like, what a story, what a family 🙈🤣
Beautiful written and I like the comment section. This helps one to understand why these stories were what they were.
Now I need someone to sing those songs for me 🥳🤗
 
Tafsiri ya juu juu ya kiSwahili ni hivi:

Nitaanza na tabasamu kubwa. Kitabu ni "Matengo Folktales" cha [Joseph] Mbele. Kilinirudisha kwenye siku zile za usimuliaji hadithi. Hadithi tatu katika kitabu hiki zilisisimua: “Jitu Katika Shamba la Mpunga,” “Kisa cha Wanawake Wawili” na "Hadithi ya Katigija.” Najaribu kukumbuka sauti za nyimbo katika hadithi zile. Nyimbo hizi daima ziliimbwa na wote wakati hadithi zinasimuliwa. Hicho ndicho kinachokosekana katika usimulizi wa hadithi leo. Tunawafanya watoto wetu wasikilize tu bila wao kushiriki.

Lakini, nimeshtushwa na idadi ya mauaji katika kila hadithi. Sikumbuki sawasawa sehemu ambapo mauaji yenyewe yanatokea. Kwa mfano, "Kisa cha Wanawake Wawili," nakumbuka pale mwanamke anapoambiwa kulamba vidonds. Na katika “Hadithi ya Katigija” nakumbuka bibi anavyoimba wakati anamletea mtoto Katigija chakula, na katika “Jitu Katika Shamba la Mpunga” nakumbuka jinsi watoto walivyokuwa wanapotea. Mtoto wangu alishtuka nilipomsimulia “Kisa cha Jitu Katika Shamba la Mpunga.” Alishangaa ni hadithi gani hiyo, na ni familia gani hiyo.
 
Kitabu kimeandikwa vizuri na nilipendezwa na maelezo kuhusu hadithi. Yanasaidia kuelewa kwa nini hadithi ziko zilivyo. Sasa nahitaji mtu wa kuniimbia nyimbo zilozomo.

 

 

Wednesday, February 9, 2022

Vitabu Viko Chuoni Mbeya

 

Tarehe 27 hadi 29 Januari, 2022, nilikuwa mgeni wa Catholic University College of Mbeya. Nilikuwa nimealikwa kutoa mhadhara juu ya “Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.” Lakini nilijikuta katika shughuli zingine pia, ikiwemo mazungumzo na waalimu na pia mkuu wa chu

 

Katika mhadhara wangu, niliibua masuala ambayo nimeyaongelea katika vitabu vyangu Africans and Americans: Embracing Cultural Differences na Chickens in the Bus: More Thoughts on Cultural Differences. Lengo langu kuu lilikuwa kuanzisha jadi ya kutafakari changamoto za tofauti za tamaduni katika ulimwengu wa utandawazi wa leo.

Tafakari hii inapaswa iwe endelevu. Kuchangia hilo, nilikabidhi nakala za hivi vitabu vyangu viwili kwa ajili ya maktaba ya chuo. Baadaye mkurugenzi  wa maktaba ameniandikia ujumbe wa shukrani kwa kupewa vitabu hivyo. 

Saturday, December 25, 2021

Krismasi Katika Fasihi

Pamoja na mambo mengine, fasihi inaweza kubeba tafakari au taswira ya yale tunayokutana nayo maishani.Leo, siku ya Krismasi, napenda kuanzisha tafakari juu ya fasihi na Krismasi. Kwa upande wangu, kazi za fasihi ninazozikumbuka wakati huu wa Krismasi ni hizi:

1) "A Christmas Carol" (hadithi ya Charles Dickens)
2) "Journey of the Magi" (shairi la T.S. Eliot)
3) "Christ Climbed Down" (shairi la Lawrence Ferlinghetti)

Kazi hizi zote zina mambo mengi yanayohusu Krismasi na pia yanayogusa hisia kwa umahiri wa sanaa. KiIngereza kilivyotumika katika "Journey of the Magi," kwa mfano, kinagusa sana, na ubunifu wa simulizi yake ni wa kusisimua. Ninajiona mwenye bahati kuifahamu lugha hiyo vizuri sana, kwa undani kabisa, na ninafaidi uhondo.

Kwa upande mwingine, shairi la Ferlinghetti linasisimua kwa jinsi linavyokejeli kugeuzwa kwa Krismas kuwa si tukio la kidini bali la kibiashara. Kwa maana hiyo, Ferlinghetti anatukumbusha yale waliyoandika akina Marx na Engels katika "Communist Manifesto" kuhusu namna ubepari unavyohujumu na kunajisi mambo mbali mbali.

Huu ni wakati wa muafaka kwa wapenzi wa fasihi kutafuta tungo hizi, na zingine, kuzisoma au kurudia kuzisoma, na kuzitafakari.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...