
Leo baada ya mizunguko kwenye mji wa Apple Valley, niliingia katika duka la vitabu la Half Price Books, ambalo nimeshaliongelea kabla.
Kama ilivyo kawaida hapa Marekani, kwenye duka la vitabu, hawakosekani wateja, na mara kwa mara kunakuwa na msongamano.
Leo nilinunua vitabu vitano. Kimoja ni Three Plays cha Sean O'Casey. Huyu ni mwanatamthilia maarufu wa Ireland. Nilipokuwa nasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, 1973-76, tulisoma tamthilia yake mojawapo iitwayo Purple Dust. Ilituvutia sana. Ingawa nahisi kitabu cha Three Plays ninacho katika shehena ya vitabu vyangu vilivyopo Tanzania, nimeona ni vema nikawa na nakala nyingine. Sean Ocasey alikuwa mtu wa ajabu, kwa jinsi ambavyo alivyokuwa mtoto maskini wa mitaani, akajielimisha mwenyewe hadi kufikia hadhi ya kuwa mwandishi anayeheshimiwa sana duniani.
Kitabu kingine nilichonunua ni Reality, Man and Existence: Essential Works of Existentialism, kilichohaririwa na H.J. Blackham. Kitabu hiki kina maandishi ya Kierkegaard, Sartre, Nietzsche, Jaspers, Buber, na Merleau-Ponty, ambao ni wanafalsafa maarufu sana. Kati ya vitabu vyangu vilivyopo Tanzania, kuna mengi ya maandishi ya wanafalsafa hao na wengine. Hapa Marekani pia nina vitabu vyenye maandishi yao. Lakini sikuona tatizo kununua kitabu hiki cha Reality, Man and Existence, kwa sababu kimekusanya maandishi machache muhimu ya wanafalsafa waliotajwa. Mtu unaweza kusafiri na kitabu hiki, ukajisomea.
Nimenunua pia vitabu viwili vya Robert Louis Stevenson. Kimoja ni The Strange Case of Dr. Jekyll and Mr. Hyde and Other Stories. Kingine ni Treasure Island. Kwa wafuatiliaji wa fasihi ya ki-Ingereza, hadithi ya Dr. Jekyll and Mr. Hyde ni maarufu. Kwetu tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu nchini Tanzania, tulisoma kwa bidii maandishi ya waandishi kama Robert Louis Stevenson. Kwa mfano, tunaikumbuka vizuri Treasure Island.
Kitabu cha tano nilichonunua leo ni A Moveable Feast, cha Ernest Hemingway. Ninayo nakala ya kitabu hiki hapa ughaibuni. Lakini, muda fulani uliopita nilianza kusoma taarifa kuwa limechapishwa toleo jipya la kitabu hiki, na walioandaa toleo hilo ni Mzee Patrick Hemingway na Sean Hemingway. Mzee Patrick Hemingway ni mtoto pekee wa Ernest Hemingway ambaye bado yuko hai. Sean Hemingway ni mjukuu wa Ernest Hemingway. Wameshirikiana kuandaa hili toleo jipya, ambalo limejumlisha baadhi ya mambo ambayo hayakuwemo katika toleo la mwanzo, lililoandaliwa na Mary Hemingway, ambaye alikuwa mke wa mwisho wa Ernest Hemingway. Mimi ni mpenzi mkubwa wa maandishi ya Hemingway, kama nilivyogusia hapa. Nina hamu ya kusoma toleo hili la A Moveable Feast, nione yaliyomo ambayo hayakuwepo katika toleo la mwanzo.

