Binti m-Kenya Ang'ang'ania Kitabu

Tarehe 11 Juni, nilishiriki maonesho yaliyoandaliwa na African Health Action, kama nilivyoezea katika makala hii. Shughuli za aina hii huwa zina mambo mengi sana, na haiwezekani kuyaelezea yote katika makala ya blogu. Kuna mambo mengine ambayo yanabaki kichwani kama kumbukumbu isiyosahaulika.

Basi, kumbukumbu mojawapo ni jinsi familia moja ilivyokuja kwenye meza yangu, ambapo nilikuwa nimeweka vitabu na maandishi mengine. Katika kutambulishana, walijieleza kuwa wao ni wa-Kenya.

Wakati wakiangalia vitabu, binti yao mkubwa alisema kuwa amesoma kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differenes. Nilipomwuliza alikisoma wapi, alisema amekisoma Duluth. Nilihisi kuwa atakuwa amekipata kupitia kwa wamiliki wa kampuni ya Kili Culture Tours and Safaris, naye alikiri hivyo. Mama Neema, ambaye ni m-Tanzania, na mume wake, ni mashabiki na wapiga debe wakubwa wa vitabu vyangu.

Huyu binti m-Kenya alipokiona kitabu cha CHANGAMOTO, alisema kuwa anakitaka. Wakati huo baba mtu alikuwa analipia vitabu viwili alivyovichagua. Binti alisisitiza kuwa anakitaka hicho pia, na baba alilipia. Jumla ilikuwa yapata dola 35. Kumbuka kuwa hao si matajiri, bali ni wabeba boksi wenzetu.

Kutokana na uzoefu wangu, naweza kusema kuwa kwa ujumla, wa-Kenya wanavithamini vitabu. Nilianza kuona tabia yao hiyo nilipotembelea Kenya kwa mara ya kwanza, mwaka 1989. Wana maduka mengi ya vitabu, na ukiingia humo utawakuta. Siku za kufungua shule, wazazi na watoto wanafurika katika maduka ya vitabu. Ukisoma magazeti ya Kenya, utaona mara kwa mara wana safu ambamo wanaongelea vitabu. Huku Marekani, nawaona wa-Kenya kwenye matamasha ya vitabu.

Mimi mwenyewe kama mwandishi wa vitabu nimeguswa na wa-Kenya kwa namna mbali mbali. Kwa mfano, muda mfupi baada ya kitabu cha Africans and Americans kuchapishwa, gazeti la Mshale, la wa-Kenya, liliandaa shughuli mjini Minneapolis ya kukitambulisha kitabu changu kwa umma. Soma hapa. Soma pia taarifa hii, na hii.

Nikirudi kwenye habari ya binti aliyeng'ang'ania kitabu, naweza kusema kuwa wa-Kenya ndivyo walivyo. Ningeweza kuleta taarifa zingine. Kwa mfano, niliwahi kwenda chuo cha Principia kutoa mhadhara. Binti mmoja wa Kenya aliposikia kuwa nimechapisha kitabu cha ki-Swahili, alitaka kukipata. Baada ya mimi kumpelekea, alikisoma hima, akaniandikia ujumbe kuelezea hisia na mtazamo wake kuhusu kitabu kile. Naona nina sababu ya kusema kuwa wa-Kenya ndivyo walivyo.

Comments

Emmanuel Sulle said…
Aksante Prof kwa hii post nzuri. Ni ukweli huo kwa wa-Kenya maana hata magazeti yanasoma mpaka vijijini tofauti na Tanzania. Bahati mbaya ukiwakuta vijana au wanafunzi wa kitanzania wanasoma gazeti basi wanasoma zile karatasi za mwisho (yaani habari za michezo). Kwa haraka haraka nimepata kuwauliza vijana wengi; majibu yao ni kuwa hawapendi kusoma siasa za Tanzania!
Mbele said…
Ndugu Sulle, shukrani kwa ujumbe wako. Wa-Kenya wamejizatiti kielimu, na wanaendelea kufanya hivyo, tofauti na wa-Tanzania. Matokeo yake yanaonekana kila mahali. Kwa mfano, wa-Kenya wanamiminika Tanzania na kujitwalia ajira, wakati wa-Tanzania wako vijiweni wakingojea ajira milioni ngapi sijui walizoahidiwa na CCM wakati wa kampeni mwaka jana.

Wa-Kenya wamejizatiti tangu zamani hata katika somo la kiSwahili, na hayo niliyaona mwenyewe nilipoanza kutembelea vyuo vikuu vya Kenya mwaka 1989. Ilikuwa dhahiri, tangu wakati ule, kwamba wametutangulia. Matokeo yake ni kwamba leo utawaona wa-Kenya wanafundisha ki-Swahili kwenye vyuo vya ughaibuni.

Kwa mtazamo wangu, muda si mrefu kuanzia sasa wa-Kenya watakuwa wanafundisha ki-Swahili Tanzania.
John Mwaipopo said…
hili la kiswahili haiyumkini litatokea. watanzania tunachuku ujuaji na utumiaji wetu wa kiswahili for granted ilhali wakenya wanakisoma kiswahili shuleni kama wanavosoma lugha zingeni. watanzania wengi tunabofoa (haribu) sana kiswahili katika maandishi na matamshi yetu na hatuna mkosoaji. mkenya anayekijua kiswahili anakikua kweli kweli kuanzia sarufi, miundo, nahau hata fasihi
Anonymous said…
prof.ninapenda sana unavyohimiza watu kusoma vitabu unafanya vizuri lakini ndo yale tuliyokuwa tunayalalamika mzee wetu alituharibu baada ya kuonekana kwamba serikari itafanya kila kitu tumeishachelewa,maana kuna wazazi wanaowapa watoto wao hela za kununulia mitahani ili washinde upo hapo?
Mbele said…
Anonymous, shukrani kwa ujumbe. Nami naamini kuwa kwa mambo fulani, Mwalimu Nyerere alitudumaza, ingawa haikuwa nia yake.

Kwa mfano, alikuwa mtu mwenye uwezo mkubwa wa kutoa hotuba na kujenga hoja, kiasi kwamba watu hatukuweza kuchoka kumsikiliza. Ilikuwa kwamba ikitangazwa kuwa Mwalimu atalihutubia Taifa saa fulani, watu walikuwa wanahama popote walipo ili wawe karibu na redio wamsikilize.

Matokeo yake ni kuwa sisi wa-Tanzania tumebaki kuwa wapenda hotuba, na kila m-Tanzania ni mhutubiaji mkubwa. Kila m-Tanzania ni hodari sana wa kupiga siasa.

Wa-Kenya wanatuelewa vizuri, maana wanajua sisi ni watu wa maneno ila si vitendo.

Hakuna cha maana tunachofanya. Kila siku ni warsha, makongamano, na semina elekezi.

Kwa upande wangu, hapo ndipo alipotuharibu Mwalimu Nyerere, ingawa hakudhamiria hali ije kuwa hivyo.

Lakini, endapo tungemwiga Mwalimu Nyerere kikweli kweli, tungezingatia kuwa yeye alikuwa ni mtafuta elimu makini. Alikuwa anasoma sana, vitabu vya aina mbali mbali. Kuna makumbusho kijijini kwake Butiama, ambapo vitabu vyake maelfu vimehifadhiwa.

Sasa hilo ndilo jambo ambalo wa-Tanzania hawakuiga. Wangeiga, leo wangekuwa wanawika hata mashuleni na vyuoni, na hapangekuwa na hili tatizo la wazazi kuwapa watoto hela za kununulia masuali ya mtihani.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini