Ugali wa Yanga

Ukitamka ugali wa Yanga, utawachokoza wa-Tanzania waliokulia enzi za Mwalimu Nyerere. Utawakumbusha wakati ambapo walilazimika kula ugali wa njano. Kilikuja kipindi ambapo nchi ilikuwa na upungufu wa chakula, na Nyerere alipokea unga wa njano kutoka Marekani. Kwa shingo upande na masononeko, wa-Swahili walitumia unga huo, maarufu kama Yanga, na mpaka leo hawajamsamehe Nyerere kwa kuwalisha Yanga.

Wa-Tanzania walipolalamikia unga huo, Mwalimu Nyerere alijibu kwa ukali kuwa wasiotaka Yanga ni watu wasio na shida. Naomba wadau wenzangu wa wakati ule wanisahihishe kama nimepotosha.

Sio kwamba tulikula Yanga miaka yote ya utawala wa Mwalimu Nyerere, na sio kwamba Mwalimu Nyerere alitaka Yanga ndio iwe chakula cha wa-Tanzania, au kwamba aliifurahia hali hiyo. Nawaomba wadau wanikumbushe ni mwaka upi au miaka ipi ambayo tulipata dhiki hiyo ya kula Yanga.

Je, tunalitafsiri vipi suala la unga wa Yanga? Kwa mtazamo wangu, kuna kipengele muhimu cha tofauti za tamaduni. Tofauti hizi zinajitokeza katika mambo mengi, na kwa namna nyingi, likiwamo hili suala la vyakula.

Tofauti za tamaduni zinaweza kuathiri kukubalika au kutokukubalika kwa bidhaa. Kwa mfano, namna bidhaa inavyotangazwa katika jamii au utamaduni fulani na kuwavutia watu inaweza ikawachefua watu wa jamii na utamaduni tofauti.

Hata rangi zinaweza kuibua hisia tofauti katika tamaduni mbali mbali. Rangi ya bidhaa inayowavutia watu wa utamaduni fulani inaweza kuwachefua watu wa utamaduni tofauti. Mfanyabiashara anaweza kuhujumu biashara yake kwa vile tu ameitangaza kwa kutumia rangi fulani au bidhaa yenyewe ina rangi isiyokubalika katika jamii fulani.

Katika utamaduni wetu wa-Swahili, ambao tunakula ugali, unga wa manjano haukubaliki. Kama ni unga wa mahindi, tunataka uwe mweupe. Hii ndio jadi tuliyozoea. Ni sehemu ya utamaduni wetu. Wengine wanatumia unga wa muhogo au ulezi. Lakini Yanga haikubaliki.

Lakini Marekani, Yanga iko kila mahali, sambamba na unga mweupe. Mwanzoni, katika kuishi kwangu Marekani, nikienda dukani, nilikuwa naikwepa kabisa Yanga. Lakini kidogo kidogo nilianza kuitumia, hadi nikafikia hatua ya kuupenda kabisa ugali ya Yanga.

Uamuzi wa kuleta Yanga Tanzania haukuzingatia suala la tofauti za tamaduni. Sijui ni nani aliyefanya uamuzi ule, lakini naamini haukuwa kwa nia mbaya. Kilichokosekana ni elimu sahihi. Nahisi wangejua wangeweza kubadilisha na kuleta unga mweupe. Hapangetokea manung'uniko, wala jazba za Mwalimu Nyerere.

Suala la ugali wa Yanga ni kielelezo kidogo cha masuala yanayoikabili dunia katika utandawazi wa leo, na masuala haya yatazidi kuongezeka kwa kadri dunia inavyozidi kuwa kijiji. Katika maandishi, warsha na mihadhara, najaribu kuelezea masuala hayo. Ni muhimu sana, kama ninavyosisitiza katika kitabu cha Africans and Americans. Elimu hii kama ingefanyika ipasavyo, ingetuepushia matatizo yaliyojitokeza wakati wa Mwalimu Nyerere, na pia ingepunguza jazba ambazo bado zipo kuhusiana na suala la kulishwa Yanga.

Comments

Mwaka 1984-85. Hali ya chakula nchini haikuwa nzuri na unga wa Yanga ulikomboa watu.

Wakati ule ulikuwa wakati wa vijiji vya Ujamaa na ilibidi uende kufanya kazi za umma - kuchimba barabara, kukusanya mawe kwa ajili ya ujenzi wa shule; na shughuli zingine za kimaendeleo kabla hujaupata huo unga wa Yanga...Kule kwetu Usukumani, unga huu ulikuwa hautolewi bure!

Nadhani watu waliuchukia unga huu kwa sababu - pengine kutokana na kutotunzwa vizuri na pengine safari ndefu ya kutoka huko ulikotoka, ulikuwa umeoza - funza kibao na ulikuwa unanuka sana. Kwa hali uliyokuwa nayo huko ulikotoka bila shaka ulifaa kwa kulishia nguruwe na au kutupwa tu baharini!

Kusema kweli mpaka hii leo mimi siupendi unga huu ingawa wanangu wanaupenda sana na kila tunapokwenda kununua mahindi mabichi au unga basi wao ni lazima watachagua unga wa njano. Bado sijawasimulia hadithi hii kwani sitaki kuwakatisha tamaa!

Tunavyo vyanzo vingi sana vya maji na kama tungekuwa makini na kuwekeza sawasawa katika kilimo cha umwagiliaji pengine tusingekuwa tunasumbuliwa na ukosefu wa chakula. Pengine sera za Kilimo Kwanza zitatuokoa!

Kumbukumbu nzuri Mwalimu Mbele!
Unknown said…
Nimefurahi mno kujua Historia ya taifa langu .

Je? Unga huo ilikuwaje Hadi uitwe yanga ? Kuna uhusiano na timu ya yanga?
Unknown said…
Nimefurahi mno kujua Historia ya taifa langu .

Je? Unga huo ilikuwaje Hadi uitwe yanga ? Kuna uhusiano na timu ya yanga?
Joseph said…
Ndugu Unknown, kia cha unga kuitwa Yanga ni ile rangi ya njano, na uhusiano na timu ya Yanga ulikuwa hiyo rangi.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini