Saturday, December 10, 2011

Miaka 50 Baada ya Uhuru, Mtoto Albino Anaogopa Kwenda Shule

Jana ilikuwa ni kumbukumbu ya miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika. Nilijaribu sana kuandaa makala kuhusu siku hiyo ya jana, lakini nilipata kigugumizi. Kwa upande moja, ninafahamu kuwa ndoto ya uhuru aliyokuwa nayo Mwalimu Nyerere, ya kuleta ukombozi wa kweli katika nyanja mbali mbali na kujenga taifa linalojitegemea, imezimishwa na sera zilizopo, ambazo zinaimarisha ukoloni mamboleo. Kama ningeandika makala jana kuhusu kumbukumbu za uhuru wa Tanganyika, pangekuwa hapatoshi.

Lakini jambo jingine lililonipa kigugumizi ni kuwa mawazo yangu yalikuwa yanarudi tena na tena kwenye taarifa niliyosoma wiki kadhaa zilizopita, kuhusu mtoto albino wa Ludewa ambaye anaogopa kwenda shule asije akauawa na watu wenye imani za kishirikina. Habari hii niliiweka hapa.

Siku nzima ya jana nilikuwa najiuliza, inakuwaje miaka 50 baada ya uhuru, mtoto huyu anaishi katika hofu ya kuuawa? Tumepiga hatua mbele au nyuma? Enzi za Mwalimu Nyerere, mtoto huyu angekuwa anaenda shule sawa na watoto wengine. Ndoto ya Mwalimu, wakati Tanganyika inapata uhuru, ilikuwa kwamba tupambane na maadui wakuu watatu: ujinga, umaskini, na maradhi. Leo, kushamiri kwa ujinga katika jamii yetu kunatishia maisha ya mtoto huyu albino.

Nimekuja ofisini asubuhi hii nikaona kwenye blogu ya Mtwara Kumekucha taarifa kuhusu mauaji ya albino. Inakuwa kama vile mawazo yetu yamefanana wakati huu. Naileta hiyo taarifa hapa.


5 comments:

Subi Nukta said...

Nadhani tumekumbwa wengina "kigugumizi" cha kuandika kumbukumbu ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania.

Viongozi wanatuhubiria na kutaka tuamini kisha tuhubiri kuhusu "mazuri" ambayo yametendeka Tanzania katika kipindi hiki cha miaka 50, lakini nikilinganisha "mabaya" na "mazuri" mizani yangu inaegemea na kugota chini kabisa kwenye "mabaya" na hiyo ndiyo sababu hasa ya kutokuikashifu nafsi na kuilazimisha kuridhika kisha kuandika na kuhubiri ambacho sikiamini. Ni bora nikaitwa kipofu, asiye na shukrani, asiyetaka kuona na mtu wa ajabu kuliko kufanya kile ambacho nafsi inashuhudia siyo.

Christian Sikapundwa said...

Prf. kwanza nakushukuru kwa pole nyingi,Kama ulivyo sema Mungu ngiye mwamba wa kila kitu.Sasa miaka 50 ya Uhuru mie na timu nzima ya tujifunze tulienda kwenye kitovu cha Kihistoria ya kiashara,Kilwa,ukweli kuna mambo ya kujivunia,na mengine lazima tupigembio.Njiani kuna mzee mmoja jina ninalihifadhi alisema,Mwalimu Nyerere alivyong'atuka aliacha maadui watatu,ila katika miaka 50 ya uhuru kumeongezeka maadui wengine,aliwataja kuwa ni ufisadi,rushwa wizi ,ubadhilifu na ukatili.
Alisema adui ukatili sasa ndiyo namba moja,vikongwe wanawaogopa watoto na wajukuu wao,walemavu wa ngozi wanawaogopa wafanyabiashara na wataka madaraka,watoto wanawaogopa watu wanaowanyanyasa kijinsia sijui miaka 50 ijayo hali itakuwaje kwa vizazi vijavyo. .

Mbele said...

Tangu tulipopata uhuru, Mwalimu Nyerere alitukumbusha kuwa msingi na lengo la maendeleo ni binadamu. Kigezo cha msingi cha maendeleo ni je, huyu binadamu yukoje na ana hali gani?

Kati ya maandishi yake kuhusu masuala haya, Mwalimu Nyerere aliandika kitabu kiitwacho "Binadamu na Maendeleo."

Sasa basi, kukithiri kwa ufisadi, rushwa, wizi, ubadhirifu, na ukatili ni dalili tosha kuwa hatujawa na maendeleo ya kweli, bali tumepiga hatua nyuma.

Kipimo cha maendeleo si maghorofa, barabara, magari yanayopita mitaani, wala pesa. Haya yote yanaweza kuwepo, lakini binadamu waliomo katika nchi husika wakawa si tofauti na hayawani.

Kwa huyu mtoto albino, nchi yetu si nchi ya wanadamu, bali ni kama msitu wa wanyama wakali. Anaishi kwa hofu usiku na mchana.

Goodman Manyanya Phiri said...

@Subi

"Viongozi wanatuhubiria..."

Kwani "kiongozi" ni kitu gani? Si mtu tu kama mimi nawe? Na kwanini tuweke mabegani ya viongozi pekee ufumbuzi wa matatizo yetu?

Kuliko kutoa takwimu, ripoti za polisi au hata lawama kwa viongozi na kwa washirikina wenye kuliabisha taifa la Afrika kwa kuhatarisha maisha ya hawa watoto wetu, tunahitaji sisi kama wanablogu na wasomi wengine tuweke mwezi mzima maalum tukubaliane tutaandika kuhusu hao "Walemavu" wangozi ili umma upate elimu zaidi na uondokane na ujinga kuhusu wananchi hao wenzetu.

[ASK NOT WHAT AFRICA HAS IN 50 YEARS DONE FOR YOU, ASK WHAT YOU HAVE DONE FOR AFRICA IN AS MANY YEARS]

Mbele said...

Mzee Phiri, wazo lako la wanablogu kujimwaga katika kuandika kuhusu suala kama hili nimelipenda. Wanablogu tuna sauti kubwa na tunawafikia watu wengi sana. Kwa hivi, tukijipangia na kutekeleza majukumu ya aina hii, tutafikisha ujumbe kwa umma.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...