Thursday, January 26, 2012

Africonexion: Kampuni Chipukizi

Mwaka 2002 nilisajili kampuni katika jimbo la Minnesota ambayo niliita Africonexion. Nilichagua aina ya usajili iitwayo "sole proprietorship." Yaani mmiliki na mhusika mkuu ni mimi.

Nilianzisha Africonexion kama chombo cha kushughulikia elimu kuhusu tamaduni duniani, kwa kuandika, kuchapisha, na kuuza vitabu, na kutoa mihadhara na ushauri kwa watu binafsi, mashirika, taasisi, makampuni, na kadhalika, kama ninavyoripoti mara kwa mara katika blogu zangu.


Africonexion ni kampuni ndogo sana kwa wakati huu, kwa maana kwamba sina timu ya wafanyakazi au washiriki. Lakini nimeitumia vizuri kama fursa ya kujielimisha, kwa kuzingatia kuwa elimu ni mtaji bora kuliko hata fedha. Shughuli zote ninazofanya, iwe ni kuandika au kutoa mihadhara au ushauri kwa watu binafsi, ni kama shule kwangu. Hii picha hapa kushoto ilipigwa wakati wa maonesho fulani Brooklyn Park, Minnesota.



Ninataka kuipeleka kampuni hii Tanzania na kwingineko. Nimeshaendesha warsha Dar es Salaam, Zanzibar na Pemba, Tanga, na Arusha. Pia nilishiriki maonesho ya elimu na ajira yaliyofanyika Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam. Hapa kushoto naonekana na wadau kwenye meza yangu. Nilishiriki maonesho hayo ili kuwapata wadau wa kujiunga nami, kwani nimejenga msingi mzuri wa uzoefu, na mtandao thabiti, huku Marekani. Lakini, kutokana na shughuli zangu, watu hao inabidi wawe wapenda vitabu na elimu kwa ujumla.

7 comments:

Joachim Mabula said...

Kazi Nzuri Profesa Mbele.

Mbele said...

Shukrani, ndugu Mabula, kwa ujumbe wako. Kazi inayonikabili ni kuwatafuta wa-Tanzania makini katika masuala haya niliyoongelea, au wako tayari kujifunza kwa dhati ili wawemo katika mtandao ninaotaka kuunda.

Subi Nukta said...

Juhudi za kuigwa hizi. Nimeshirikisha wengine ujumbe huu kwenye wavuti.com pia.

Mbele said...

Shukrani sana, Da Subi, kwa kuuweka ujumbe wangu kule wavuti.com. Nimeusoma.

Napenda pia kuchukua nafasi hii kukupongeza kwa mahojiano yako ambayo ripoti yake niliiona Bongocelebrity na nikaisoma hapa.

Subi Nukta said...

Shukrani kwa kuiacha anwani, nime-update.

Shukrani kwa kusoma mahojiano yale.

DAUD YOMBO USHINGE said...

shukrani za dhati, professa mbele,mimi naitwa lushinge daud yombo,miaka 23,mtanzania,muajiriwa serikalini wizara ya mambo ya ndani..kiukweli nimevutiwa sana na wazo lako kweli unaonesha dhairi jinsi gani ulivyo smart,sophisticated,intellectual curios,..ningependa kuwa miongoni mwa wahusika wa mradi wako ingawaje ninaishi remote area sana ambako kuna changamoto nyingi sana ikiwemo kutopata internet access..nna digital camera hivyo nahisi tunaweza kushare mengi sana kwa kupitia habari picha,tafadhali naomba kuwa official member wa AFRICONEXION.aksante.

Mbele said...

Kijana Daud Yombo Ushinge, nimefurahi kupata ujumbe wako. Nitakuwepo Tanzania mwezi wote wa Machi hadi Aprili katikati.

Tufanye mpango wa kukutana. Kama kuna mtu mwingine pia, sawa kabisa. Nitafurahi kukutana, hata kama ni saa tatu, nne, au zaidi, ili kufafanua kila kitu, kuanzia nilikotoka hadi nilipo na wapi naelekea, na hapo mdau utapata fursa ya kuelezea mtazamo wako. Hakuna kisichowezekana.

Jambo muhimu ni umakini wa mhusika au wahusika, sio kupata utitiri wa watu. Mtu mmoja makini anatosha, au wawili. Nimefanya shughuli hizi mwenyewe kwa miaka kumi, bila kutetereka, na watu kwa maelfu wameguswa na kufaidika.

Umesema unakaa mbali. Sijui ni wapi. Mimi nategemea kuwepo zaidi Dar es Salaam. Ukiona katika dhamiri yako kuwa kweli umevutiwa na wazo hili, na uko tayari kujihusisha kwa roho moja, nitakulipia gharama zote ili uweze kuja Dar es Salaam, au tunaweza kupanga kukutana kwenye mji mwingine.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...