Saturday, April 13, 2013

Maonesho ya Elimu na Huduma za Jamii, Brooklyn Park

Leo nimeshiriki maonesho ya elimu na huduma za jamii yaliyoandaliwa na African Career, Education & Resource, Inc (ACER). Maonesho haya yalifanyika katika shule ya Park Center, Brooklyn Park, Minnesota. Wadau wa huduma kama afya, ajira, elimu, na malezi ya vijana, walikuwepo, kutoa elimu na ushauri, na hasa kuifahamisha jamii kuhusu huduma wanazotoa.
Nilipata fursa ya kukutana na watu ambao tunafahamiana, na wengine ambao hatukuwa tunafahamiana.








Huyu dada anayeonekana kwenye picha ya juu kabisa na hapa kushoto alikuwa mwanafunzi wangu hapa Chuoni St. Olaf, miaka 13 iliyopita. Asili yake ni Ethiopia. Ni shabiki mkubwa wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences




Kati ya hao tunaofahamiana, ambao tumekutana leo, ni Dr. Alvine Siaka kutoka Cameroon, ambaye ni mratibu wa African Health Action. Mwingine ni Rita Apaloo, kutoka Liberia, ambaye ni mratibu wa jumuia iitwayo African Women Connect. Rita naye ni shabiki wa kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences

Kati ya watu ambao tumefahamiana leo ni dada Iqbal Duale, m-Somali, ambaye ni mtaalam wa elimu ya jamii.  Tulielezana shughuli zetu kwa jamii, tukaona zinahusiana. Taasisi anayofanyia kazi inaitwa Planned Parenthood.  Tutawasiliana zaidi, Insh' Allah.

 Kama kawaida, kwenye mikusanyiko kama hii, tulipata fursa ya kubadilishana mawazo. Tuliongelea shughuli tunazofanya, changamoto zake na malengo yake, na umuhimu wake kwa jamii. Kitu kimoja cha kuvutia na kutia moyo ni kuwa pamoja na changamoto zote na magumu, kila moja wetu ana msimamo thabiti kuwa hakuna kulegea, kurudi nyuma, wala kukata tamaa. Changamoto hizi ni kama chachu kwetu.

Taasisi iliyoandaa maonesho ya leo, yaani ACER, niliitaja siku chache zilizopita, katika ujumbe wangu kuhusu mkutano wa bodi ya taasisi ya Afrifest. ACER na Afrifest tumeamua kushirikiana, nami niliamua kuhudhuria maonesho ya leo kama njia ya kujenga uhusiano huo.

Mimi ni mwenyekiti wa bodi ya taasisi ya Afrifest. Papo hapo, nilienda nikiwa nimejisajili kwa jina la kampuni ya Africonexion. Nilikuwa na meza, kama inavyoonekana hapa kushoto, ambapo niliweka vitabu na machapisho yangu mengine, nikapata fursa ya kuongea na wadau waliofika hapo. Wengine wana wadhifa katika taasisi zinazoshughulikia masuala ninayoshughulikia, yaani ya elimu kuhusu tofauti za tamaduni. Uzuri wa kukutana namna hiyo ni kuwa tunajenga msingi wa kushirikiana siku zijazo.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...