Thursday, April 18, 2013

Mlima Longido, Tanzania

 Hakuna mtu ambaye anaweza kuzitembelea au kuziona sehemu zote za nchi yetu au nchi yoyote nyingine. Hii ni sababu moja ya mimi kuweka kwenye blogu hii picha za sehemu mbali mbali. Nataka wengine nao wafaidike angalau kidogo na kupanua ufahamu wao. Yawezekana, pia, wakahamasika kwenda kujionea.

Leo naleta picha za mlima Longido. Mlima huu uko Tanzania ya kaskazini, baina ya mji wa Longido na Namanga. Unaonekana vizuri kabisa kutoka kwenye barabara itokayo Arusha kwenda Namanga. Picha hizi nilizipiga mwishoni mwa Januari, mwaka huu, nikiwa safarini kutoka Namanga kwenda Longido. Baada ya kuondoka Namanga, picha ya kwanza niliyopiga ni hiyo hapa kushoto.
Muda mfupi baadaye, nilipiga picha hii inayoonekana kushoto.
 Baadaye kidogo nilipiga picha hii hapa kushoto.
Tulivyozidi kukaribia Longido, nilipiga picha hii hapa kushoto.

Nimeshauona mlima Longido mara nyingi, katika miaka zaidi ya ishirini iliyopita, wakati nikisafiri baina ya Tanzania na Kenya. Nimewahi kuutaja mlima huu katika ujumbe huu hapa.

Kitu kimoja kinachonivutia ni jinsi mlima huu unavyoonekana wakati unapoukaribia kutokea Namanga. Ile sehemu iliyochomoka inanifanya niwazie pembe ya kifaru. Picha ninayopata ndio hiyo. Lakini mwaka huu, nimetambua vizuri kwamba ile pembe ya kifaru inabadilika kabisa na kuwa mwamba unaoonekana hapa kushoto. Mwaka huu ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuangalia kwa makini taswira hii na kujionea jinsi pembe ya kifaru inavyotoweka na kuwa mwamba uliosimama, ukiwa na sura tofauti.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...