Wednesday, April 3, 2013

Nitafundisha "Midnight's Children," Kitabu cha Salman Rushdie

Nimefundisha fasihi ya India mara nyingi sana, hapa Chuoni St. Olaf, kuanzia mwaka 1991. Nimefundisha maandishi ya watu kama Rabindranath Tagore, Mulk Raj Anand, Raja Rao, R.K. Narayan, Ruth Prawer Jhabvala, Nayantara Sahgal, Anita Desai, na Kamala Markandaya.

Sijawahi kufundisha maandishi ya Salman Rushdie, ambaye ni mwandishi maarufu sana, sambamba na hao niliowataja. Suali moja ambalo nimejiuliza miaka ya karibuni ni je, utafundishaje fasihi ya India bila kumjumlisha Salman Rushdie? Utaachaje kufundisha kitabu cha Rushdie kiitwacho Midnight's Children, ambacho kilipata tuzo maarufu ya Booker?

Mwezi Juni hadi Julai nitafundisha kozi ya wiki sita, katika somo liitwalo "Post-colonial Literature." Nimeamua kufundisha kitabu hiki cha Rushdie. Ni kitabu muhimu kwa namna nyingi, sio tu kwa upande wa sanaa, bali pia kwa jinsi kinavyojumlisha masuala na dhamira mbali mbali ambazo ni muhimu katika fasihi ya India. Ni kitabu chenye upekee kihistoria na kisiasa kwa jinsi kilivyofungamana na tukio moja muhimu sana katika karne ya ishirini, yaani kupatikana kwa uhuru kwa nchi iitwayo India.

Tukio hili la uhuru wa India lilitokea mwaka 1947. Ila kwa bahati mbaya sana, ni tukio lililoandamana na mgawanyiko uliosababisha kuwepo kwa nchi mbili, yaani India na Pakistan. Ni tukio lililoandamana na uhasama, mauaji na ukimbizi wa idadi kubwa sana ya watu, mtafaruku ambao ulikuwa baina ya wa-Hindu na wa-Islam. Tukio hili linakumbukwa kwa majonzi, na limeelezwa sana na waandishi kutoka India na Pakistan.

Kwa vile kitabu cha Midnight's Children kina kurasa nyingi sana, nimeona kuwa nisiweke vitabu vingi katika kozi hii ya wiki sita.  Nawazia kutumia vitabu vingine viwili au vitatu, ambavyo navyo vina kurasa nyingi. Nimeamua tu kutumia haya mavitabu makubwa nione itakuwaje. Kimoja ninachowazia sana ni Half of a Yellow Sun, cha Chimamanda Ngozi Adichie, wa Nigeria. Kingine ni Abyssinian Chronicles cha Moses Isegawa wa Uganda. Bado nina muda wa kufikia uamuzi wa mwisho. Huenda nikatumia The Famished Road, cha Ben Okri, au Wizard of the  Crow, cha Ngugi wa Thiong'o. Uamuzi kamili nitafikia katika siku kadhaa zijazo.

1 comment:

Mbele said...

Nilivyomaliza tu kuandika makala hii, nimeona taarifa kuwa mwandishi Ruth Prawer Jhabvala amefariki leo, akiwa na miaka 85. Niliwahi kufundisha kitabu chake kiitwacho "Heat and Dust."

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...