Mwaka jana, tarehe 2 Agosti, nilipita Mbinga, mji mkuu wa wilaya yangu, nikapiga picha kadhaa. Hapa kushoto ni kituo cha mabasi. Hapo ndipo unapandia mabasi ya kwenda Mbamba Bay na Songea. Hapo pia unapanda mabasi au magari mengine yanayoenda vijijini katika wilaya hiyo.
Hapa kushoto ni mtaa mojawapo wa pembeni, karibu na kituo cha mabasi, upande wa barabara iendayo Songea.Huo nao ni mtaa wa pembeni. Udongo wa Mbinga ni kama inavyoonekana pichani, sawa na ilivyo katika eneo lote kuanzia Songea hadi karibu na Mbamba Bay. Kahawa inastawi katika udongo huo, na hapa Mbinga kuna kiwanda cha kusindikia kahawa.
Siku zijazo ninapangia kuleta picha za mashamba ya kahawa, ngano, na kadhalika, ambayo yanazipendezesha sehemu za vijijini katika wilaya ya Mbinga.
Huo ni mtaa mwingine upande wa chini kutoka kituo cha mabasi. Mbinga ya leo sio kama ya miaka kumi au ishirini iliyopita. Ingawa nafika hapo karibu kila mwaka, daima naona mambo mapya. Kwa mfano, hoteli nzuri zinaongezeka. Mwaka jana nilifikia kwenye hoteli ambayo iko hapa kwenye dishi la satalaiti.
Mbinga ni mji ulio karibu na nyumbani kwangu Litembo. Kama unatoka Songea, ukitaka kufika Litembo, unapita hapa Mbinga na kuelekea mbele, juu milimani. Wilaya ya Mbinga kwa ujumla ina hali ya vuguvugu na pia baridi, na kadiri unavyoelekea milimani zaidi, baridi inaongezeka. Katika hiyo picha tumevaa kwa kufuata hali hiyo, nami nimejihami na jaketi la Shidolya Safaris ya Arusha.Baadhi ya ndugu zangu wanaishi hapa Mbinga. Hapo kushoto niko na binamu yangu Remigius Komba ambaye anaishi hapo. Tulikutana hapo kituoni bila kutegemea. Hapa nyuma yetu unayaona magari yamepakia, tayari kwa safari. Hayo ndio magari ninayopanda kwa safari ya kutoka hapa Mbinga kwenda Litembo. Ingawa niko ughaibuni, ninapofika hapo Mbinga nagundua kuwa madereva na utingo wananifahamu vizuri.

