Monday, February 13, 2012

Mitaani Mbinga, 2011

Mwaka jana, tarehe 2 Agosti, nilipita Mbinga, mji mkuu wa wilaya yangu, nikapiga picha kadhaa. Hapa kushoto ni kituo cha mabasi. Hapo ndipo unapandia mabasi ya kwenda Mbamba Bay na Songea. Hapo pia unapanda mabasi au magari mengine yanayoenda vijijini katika wilaya hiyo.






Hapa kushoto ni mtaa mojawapo wa pembeni, karibu na kituo cha mabasi, upande wa barabara iendayo Songea.












Hapo ni mtaa mwingine, sehemu ya bondeni kutoka kituo cha mabasi.












Huo nao ni mtaa wa pembeni. Udongo wa Mbinga ni kama inavyoonekana pichani, sawa na ilivyo katika eneo lote kuanzia Songea hadi karibu na Mbamba Bay. Kahawa inastawi katika udongo huo, na hapa Mbinga kuna kiwanda cha kusindikia kahawa.

Siku zijazo ninapangia kuleta picha za mashamba ya kahawa, ngano, na kadhalika, ambayo yanazipendezesha sehemu za vijijini katika wilaya ya Mbinga.


Huo ni mtaa mwingine upande wa chini kutoka kituo cha mabasi. Mbinga ya leo sio kama ya miaka kumi au ishirini iliyopita. Ingawa nafika hapo karibu kila mwaka, daima naona mambo mapya. Kwa mfano, hoteli nzuri zinaongezeka. Mwaka jana nilifikia kwenye hoteli ambayo iko hapa kwenye dishi la satalaiti.






Mbinga ni mji ulio karibu na nyumbani kwangu Litembo. Kama unatoka Songea, ukitaka kufika Litembo, unapita hapa Mbinga na kuelekea mbele, juu milimani. Wilaya ya Mbinga kwa ujumla ina hali ya vuguvugu na pia baridi, na kadiri unavyoelekea milimani zaidi, baridi inaongezeka. Katika hiyo picha tumevaa kwa kufuata hali hiyo, nami nimejihami na jaketi la Shidolya Safaris ya Arusha.

Baadhi ya ndugu zangu wanaishi hapa Mbinga. Hapo kushoto niko na binamu yangu Remigius Komba ambaye anaishi hapo. Tulikutana hapo kituoni bila kutegemea. Hapa nyuma yetu unayaona magari yamepakia, tayari kwa safari. Hayo ndio magari ninayopanda kwa safari ya kutoka hapa Mbinga kwenda Litembo. Ingawa niko ughaibuni, ninapofika hapo Mbinga nagundua kuwa madereva na utingo wananifahamu vizuri.

5 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Ahsante kwa kumbukumbu hii ninajivuna sana kwa kuona sehemu zile nilizokulia/ishi. Mimi nilijisahau nilipofika Lundo mwaka 2007 nilisahau kupiga picha kule: shule niliyosema ya kwanza, hospital, hata nyumba niliyoishi tangu kachanga...Nasikitika sana..

Anonymous said...

Safi sana, Ndo mitaa yetu ya kujinafasi hapo. Mimi nilisoma hapo Kigonsera (Caigo), Litumbandyosi, Kingole, Luhagala, Nchweka. Kuna beach nzuri sana pale Mbambabay hakuna Duniani labda kidogo pale Punta del Elste-South Amerca. Halafu ukisimama pale Litembo kwa mbele yake unaona ng'ambo ya ziwa nyasa- Nkata bay. Nyumbani kuzuri nataka nirudi maana nimepotea huku ughaibuni.
Lete picha nyingine za huko Beatiful country.

Mbele said...

Ni kweli, Yasinta, kwamba kama ulipitiwa ukasahau kupiga picha mahali, inaumiza. Pole.

Shukrani, Anonymous, kwa yote uliyosema. Nina picha nyingi za kwetu. Utazipenda. Kama wanavyosema, kaa mkao wa kula.

Mimi nilisoma ile shule ya karibu na Kigonsera, Seminari ya Likonde, 1967-70. Kigonsera imesomesha watu maarufu wengi, kuanzia Rais Mkapa, hadi mwandishi Mbunda Msokile (marehemu), ambaye alisoma sekondari ya Kigonsera miaka ile ile niliyosoma Likonde.

Ufukwe pale Mbamba Bay ni moto wa kuotea mbali. Umetulia na unapendeza sana. Ukiwa kijijini pangu, ukapandisha mlimani kidogo tu, unaliona Ziwa Nyasa na nchi ya Malawi. Tena, usiku unaona mioto inamulika kule Malawi. Nadhani pale ndio Nkata Bay.

Yasinta Ngonyani said...

Anonymous! nimefurahi kusikia ulisoma Litumbandyosi, Kingole Luhagala kwani mimi asili yangu ni Litumbandyosi na pia nimesoma /ishi Kingole je unaweza kusema wewe ni nani?

Anonymous said...

Hata mim nimesoma mbinga shule ya msingi mazoez huko ndiko nilipokulia napapenda sana watu wake wana upendo mno daima nitapakumbuka

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...