Saturday, February 4, 2012

Wanafunzi Walioenda Tanzania Wameongea Leo

Mwaka jana, niliandika katika blogu zangu kuhusu mizunguko yangu Tanzania na wanafunzi katika programu ya LCCT. Baadhi ya taarifa ni hii hapa na hii hapa.

Baada ya kuwa nao Tanzania kwa wiki tatu, niliwaacha Chuo Kikuu Dar es Salaam, ambapo walisoma kwa muhula moja, kwa mujibu wa programu. Wakisharejea Marekani, wanapata fursa ya kuongelea safari yao, masomo waliyosoma, na maisha yao Tanzania kwa ujumla.

Shughuli hiyo imefanyika leo, Chuoni St. Olaf. Kwa vile wanafunzi hao wanasoma kwenye vyuo hapa Marekani, wanakuwa na upeo wa kufananisha mambo ya Chuo Kikuu Dar na vyuo vyao, kuanzia maisha ya wanafunzi, viwango vya ufundishaji, na kadhalika.







Wanapokuwa Chuo Kikuu Dar, wanafunzi hao wa LCCT wanapata fursa ya kujitolea kama waalimu wasaidizi katika shule ya msingi ya Mlimani. Mwezi Agosti mwaka jana, nilipoenda hapo shule ya msingi kutoa taarifa kuhusu ujio wa wanafunzi hao, walimu walisema mpango huu wa wanafunzi wa ki-Marekani kujitolea pale una manufaa. Kwa mfano, watoto wanapata fursa ya kuboresha ufahamu wao wa ki-Ingereza.



Kila mwaka sisi washauri na waendeshaji wa programu tunapata fursa ya kuwasikia wanafunzi wetu wakielezea mengi wanayojifunza wakiwa Tanzania, na jambo moja la msingi ni kule kuifahamu nchi na jamii ya Tanzania. Wanafunzi hao huwa tumewaandaa vilivyo, kwani wanapaswa kusoma vitabu mbali mbali vinavyohusu historia, siasa, uchumi, na utamaduni wa Tanzania, yakiwemo maandishi ya Mwalimu Nyerere.


Napenda kumalizia kwa kusema kuwa shughuli za kuendesha programu hizi ni za kujitolea. Hivi vikao vyetu, ambavyo vinadumu siku moja nzima na vinaendelea kwa nusu siku ifuatayo, ni vya kujitolea. Hapa Marekani sijaona utamaduni wa posho za vikao kama ilivyo Tanzania. Mnaletewa chakula, saa ifikapo, lakini sijawahi kuona wala kusikia kuhusu vibahasha kama Tanzania. Nimeona niseme hivyo, ili kuonyesha tofauti ilivyo, na papo hapo, hapa Marekani kazi inafanywa kwa roho moja.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...