Sunday, February 5, 2012

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

(Makala hii nilishaichapisha katika blogu yangu. Ninaichapisha tena, wakati huu CCM inapoazimisha miaka 35 ya kuwepo kwake)

--------------------------------------------------------------------------------------------------------

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

2 comments:

Anonymous said...

NIMEJARIBU KUSOMA HAYO MANENO NIKABAKIA KUWA MWENYE DONGE , NA CHA KUSIKITISHA ZAIDI SIJUI HILI DONGE LANGU NIANZE KULIELEZEA VP, LAKINI NITAJARIBU.KWA KWELI CHA KUJIULIZA JEE WAKATI WA UONGOZI WA MWALIMU NCHI ILIKUWA NA MAENDELEO YA KIASI GANI?MM NAONA ILE SIASA YAKE YA UJAMAA NDIO ILIKUWA CANCER NA WALIO KUWA WANACHAMA WA CCM NI WAGONJWA WA MARADHI HAYO. MAANA MPAKA HII LEO WANA CCM WANA FALSAFA ZA KIMWALIMU MWALIMU TU. KUWA WAO NI WAO TU NA WALOBAKI NI WA KUFUATA TU.MM KITU KIMOJA KINANIUDHI NI KUWA TUNAPENDA SANA KUMUADHIMISHA NYERERE KWA KITU GANI ALISEMA WAKATI WAKE NA TUKACHUKUA MANENO YAKE KAMA NI YA BUSARA, LAKINI UKICHUNGUZA NI SAWA NA SUNGURA ALIPOSEMA SIZITAKI MBICHI HIZI ALIBAKIA KUNYOOESHEA WENGINE KWA KUWATOA MAKOSA ILHALI NA YY MWENYEWE ALIKUWA NI CHANZO KIKUBWA CHA TANZANIA KUZIDI KWENDA CHINI.JAMANI MNAKUMBUKA MIEZI 18 YA NJAA ALIPOSEMA NI BORA TUWE NA CHAKULA KIDOGO TUGAWANE KULIKO CHAKULA KINGI TUKAGOMBANIA? SASA NANI ANGOMBANIA CHAKULA KINGI
NAAM JEE NA MNAKUMBUKA WAKATI WA WAHUJUMU UCHUMI? LAKINI MYONGE MNYONGENI NA HAKI YAKE MPENI, KITU NNCHOMSIFU NI KUHAKIKISHA TANZANIA NZIMA INALUGHA MOJA YA TAIFA, NA AKATILIA MKAZO KWA HILO NA FAIDA YAKE TUNAIYONA. WATANZANIA TUNARINGIA KISWAHILI CHETU.

Mbele said...

Shukrani kwa mchango wako. Mwalimu Nyerere angalau alikuwa na uchungu na nchi. Alikuwa na uchungu na rasilimali zetu na maisha ya wananchi. Kwa kweli, aliyokuwa anajaribu kufanya, ilikuwa ni kwa lengo la kuikwamua jamii ya waTanzania kutokana na ukoloni na ukoloni mambo leo. Alikuwa na dhamiri ya kweli ya kuiweka nchi katika kiwango cha kujitegemea, na kuiweka jamii katika haki na usawa, kuanzia kwenye nyanja za uchumi.

Ni kutokana na imani yake hiyo ndio akawa ana aina fulani ya kiburi, na kile wengine wanachoita udikteta. Bahati nzuri ni kuwa alikuwa na akili na ushawishi mkubwa kwa wananchi wa kawaida, ambao ndio wengi. Kuhusu akili yake, Mzee Ruksa alituambia kuwa Nyerere alikuwa ni mlima, na wengine vichuguu. Sidhani kama kuna ubishi hapo, kwani hata kwa kukumbuka tu alivyokuwa anatoa hotuba zake na kujenga hoja, na kwa kusoma maandishi yake, hilo linajitokeza wazi.

Tatizo la hao CCM wa leo ni kuwa wamejifanya nao wanajua na wanang'ang'ania kushika hatamu kama alivyofanya Mwalimu Nyerere, wakati akili yao ni ya wasi wasi, na hawana uchungu na nchi. Wameukumbatia ukoloni mambo leo na ufisadi.

Hapa ndipo ilipo tofauti kati ya Nyerere na hao watu. Kijuu juuu, inaonekana wamekaa kiMwalimu Mwalimu, lakini tofauti kati yao na Mwalimu ni kubwa. Wakati Mwalimu alitaka kujenga nchi na kulinda rasilimali zake ili ziwafaidie wananchi, hao CCM hawana huruma na nchi.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...