Thursday, February 23, 2012

Dini Inayoenea kwa Kasi Kuliko Zote Tanzania

Mara kwa mara ninawasikia watu wakiongelea suala la dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania, Afrika au duniani kwa ujumla. Kila mtu ana mtazamo wake. Wengine wanatoa pia takwimu, ambazo sijui kama ni za kweli au ndoto. Ni mchezo wa kuringiana nani zaidi kwa kutumia takwimu, wakati dini ni suala la mtu binafsi. Wala hutaingia ahera kwa msingi kuwa dini yako hapa duniani ilikuwa na wafuasi wengi kuliko dini nyingine.

Kwa mtazamo wangu, dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania ni ufisadi na ushirikina. Ufisadi na ushirikina huo unaendelea kushamiri kiasi kwamba unajitokeza hata kwenye nyumba za ibada za dini mbali mbali. Hebu tutafakari hilo.

6 comments:

Rachel Siwa said...

Haswa umenena kaka,Ufisadi na Ushirikina upo mpaka nyumba za Ibada.

tz biashara said...

Ufisadi na ushirikina umekomaa zaidi ktk ngazi za juu yaani viongozi wetu.Na ukiangalia kwa umakini hakuna kiongozi alie kuwa mtu wa dini yaani kufuata maandiko ya dini ambayo ndio muongozo bora ktk jamii.Nauhakika ktk kila dini kuna maandiko mazuri na yakuongoza jamii bila ya ushirikina.

Sasa ikiwa kiongozi hana mapenzi na mungu na kuendekeza ushirikina,je jamii yetu itakuwaje?Kwasababu naamini mungu ni mmoja na ndie alie tuumba na kama tuna matatizo tunahitaji kumuomba mola muumba.Na hivo basi yeyote anae endekeza ushirikina basi sio kipenzi cha mwenyezi mungu.Na kama huna mapenzi na mwenyezi mungu basi hutaona vibaya kufanya ufisadi kwakuwa hutoijali jamii yako inayokutegemea na kutafuta njia za mkato ili kujibinafsisha.

Na kingine Profesa kunajingine ambalo ni lakusikitisha na ni POMBE.Hivi sasa kila mita chache utakazo tembea mitaani hukosi kuona maduka ya kuuza pombe.Na wala hakuna wakati maalum ila ni kuanzia asubuhi mpaka usiku wa manane.Yaani tutajaaliwa na kizazi ambacho ni walevi watupu na hakuna wakulijenga TAIFA tena.

Haya mambo matatu USHIRIKINA,UFISADI na POMBE ni hatari kwa jamii.Watu wanaendekeza starehe kupita kiasi na wala hafikirii kutafuta maisha na matokeo yake akigutuka anaona amechelewa kwa hiyo la kufanya ni short cut "mganga"

Mbele said...

Asanteni sana Rachel na tz biashara kwa maoni yenu. Nafarijika kuwa hata kama sikujenga hoja kinaganaga, angalau tunakubaliana kuhusu mwelekeo wa kila nilichosema.

tz biashara, napenda kuongezea hapo kwenye hoja zako. Ukizingatia kuwa janga la mauaji ya albino, na janga la watu kuchunwa ngozi au kunyofolewa sehemu za mwili chimbuko lake ni ushirikina halafu uzingatie kuwa viungo hivi vinauzwa kwa bei kubwa sana, ni wazi kuwa wanaohusika ni hao wenye pesa, kuanzia wanasiasa na vigogo mbali mbali, hadi hao tunaowaita wafanyabiashara wakubwa.

Hao ndio wanunuaji, maana sitegemei muuza chipsi wa Magomeni anazo shilingi 500,000 za kununulia ngozi ya binadamu. Hao vigogo naamini ndio chanzo cha kuendelea kwa mauaji ya albino na watu kuchunwa ngozi au kunyofolewa viungo.

Hao tunaowaita viongozi wetu ni matatizo. Hebu fikiria, tuliwahi kusikia jinsi mtu alivyokuwa anakatiza ndani ya Bunge usiku wa manane akinyunyizia kitu kwenye viti vya waheshimiwa. Ni aibu kabisa kwa nchi yetu, lakini sidhani kama hata serikali imechukua hatua.

Pombe, kama tz biashara unavyosema, ni balaa jingine. Kama Taifa, inaonekana hatutambui kuwa tunawekewa hii mipombe nchi nzima ili akili zetu zikongoroke na mafisadi waendelee kuchota rasilimali zetu. Pombe nyingi namna hii zinaharibu akili, na taifa ambalo limeharibika akili sijui litaishia wapi.

Lakini hakuna msisimko wa kuelimishana kuhusu madhara ya pombe. Badala yake, promosheni za pombe ziko kila mahali. Na sasa tumeingia awamu ya mashindano ya kuonja pombe. Hatimaye huenda tukawa na mashindano ya kunywa, na takayepiga maji hadi kupoteza fahamu ndio atatangazwa mshindi.

mlengela daudi said...

Prof nini maana ya 'ahera'?

Mbele said...

Ndugu Mlengela, nilidhani ahera ni huko ambako wa-Kristu tunakuita mbinguni. Ila sasa, baada ya suali lako, nimeona nitafakari zaidi. Na kutafakari huko ni kwa njia ya mzunguko, ambamo naleta masuala tofauti kidogo.

Kama wa-Islam wanamwabudu Allah na sisi wa-Kristu tunamwabudu Mungu, sina hakika kama Mungu ndiye Allah au vipi. Labda wataalaam watatuelimisha hapo.

Ukisema wa-Islam wema wanafika mbinguni, sijui kama watakubali, au watasema wanafika ahera. Na ukisema wa-Krsitu wema wanafika ahera, sijui kama watakubali, au watasisitiza kuwa wanafika mbinguni. Nawasubiri wataalam wa malumbano watuelimisha.

Wa-Swahili wakianzisha mada hizi, hulumbana hadi majogoo kuwika, wakati huenda hili ni suala la lugha tu. Kwa msingi wa lugha, "Allah," Mungu, au God ni yule yule, sawa na ilivyo katika ki-Latini ""Deus." Napo hapo naomba watalaam wanielekeze.

Kwenye noti za dola za ki-Marekani unakuta pameandikwa "In God we Trust." Kwangu mimi dhana hii sio tofauti sana na dhana ya ki-Islam ya "Allah u akbar."

Lakini napo nawasubiri wataalam wa malumbano wajimwage ulingoni. Mimi nachochea fikra tu.

Kuhitimisha, ni kuwa sijajibu suali lako, maana naliona ni suali tata. Nilichofanya ni kuongezea masuali juu ya suali lako.

tz biashara said...

AHERA...
Ahera ni maisha tunayategemea kuwa ni ya milele.Sisi wanaadamu tumezaliwa hapa duniani ikiwa ni maisha ya kupita tu na ni mwenyezi mungu peke yake ndie mwenyekujua sisi tunaishi kwa muda gani.Na tutakapokufa tutazikwa na wengine huchoma moto maiti na kutupa baharini majivu.Na ndio maana tunaambiwa tutubu pale ukiwa hai kwasababu ukifa huwezi tena kutubu madhambi yako hata kama utaombewa na ulimwengu mzima.

Sasa akhera ni sehemu ya maisha ya milele ambayo makazi yako hutegemea mazuri yepi uliyoyafanya duniani au mabaya yapi uliyoyafanya duniani.Na kama hukumtii mwenyezi mungu kwa yale aliye tuagiza tuyafanye na yepi tusiyafanye basi malipo yako ni mabaya "moto"Maana siku ya mwisho wa dunia "kiama"ni siku ambayo ya kufufuliwa wanaadamu wote na kufikishwa mbele ya mahakama kuu ambayo hakuna kuchakachua kila kitu ni haki.

Ndio maana mwenyezi mungu alituletea wajumbe wake kuja kutuletea ujumbe ambao tuufate lakini wanaadamu sisi ni watu wa kujisahau wengine wanajiona kama hawafi.

Na kwamimi muisilamu naamini mungu ni mmoja tu hakuna miungu.Waisilamu hupenda kutumia ALLAH subhana wataala yaani mungu kwasababu allah (sw) ni neno la kiarabu ambalo huwezi kuongeza herufi au kupunguza na hubakia kama ilivo allah kutokana na literature ya kiarabu inasemekana ni bora ktk lugha hapa duniani au tajiri kwa lugha nyingine.Kwasababu hata waarabu wakristo wakifanya ibada zao makanisani hutumia allah (sw).

Kwahivo ahera ni maisha ya milele tunayokwenda kuishi baada ya siku ya mwisho wa dunia.Na kabla siku ya mwisho hakuna kiumbe chochote kitakachobaki duniani kila kiumbe hai kitakufa na ndio kiama kitatokea.

Haya ni mafundisho ya kiisilamu sasa sijui dini nyingine wataitafsiri vipi akhera.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...