Friday, September 16, 2011

Nimetua Indianapolis

Nimerejea kutoka Tanzania tarehe 6 mwezi huu, na tayari nimeshaanza mizunguko. Leo alasiri nimetua Indianapolis, Indiana, kuhudhuria mkutano wa Africa Network, mtandao wa vyuo vya hapa Marekani ambao lengo lake ni kuhamasisha na kuendeleza masomo yahusuyo Afrika. Tunajenga mikakati ya ushirikiano katika utafiti, ufundishaji, na kubadilishana uzoefu wa aina mbali mbali. Hatimaye tunataka kuendeleza ushirikiano baina ya vyuo vyetu hivi na vyuo vya Afrika, kwa mfano kwa kupeleka wanafunzi na watafiti Afrika na kupokea wanafunzi na watafiti kutoka Afrika.

Nimekuwa mwanabodi wa bodi ya Africa Network tangu ilipoanza, miaka mitano iliyopita. Ni shughuli ya kujitolea, lakini napenda shughuli za aina hiyo. Kuna mambo mengi yanayonivutia katika mikutano yetu, kwa mfano kukutana na walimu ambao wanaandaa programu za kupeleka wanafunzi Afrika na kuwapa ushauri na mawaidha.

Thursday, September 15, 2011

Kitabu Kipya cha Haji Gora Haji

Kama ilivyo kawaida ninapokuwa Dar es Salaam, mwaka huu nilizungukia mara kadhaa maeneo ya Chuo Kikuu Dar es Salaam. Katika duka la vitabu la Taasisi ya Uchunguzi wa Ki-Swahili, ambako nilienda kuangalia vitabu, nilifurahi kuona kitabu kipya cha Haji Gora Haji kiitwacho "Siri ya Ging'ingi," ambacho kilichapishwa na Taasisi hiyo mwaka 2009. Nimeanza tu kukisoma.

Nilikuwa sijakisikia kitabu hiki na nilikinunua hima. Haji Gora Haji ni mtafiti na mwandishi maarufu katika masuala ya ushairi utamaduni na lugha ya ki-Swahili. Upeo wa fikra zake na kina cha uchambuzi wake ni hazina isiyomithilika.

Haji Gora Haji ni mzaliwa wa kisiwa cha Tumbatu. Hakusoma katika hizi shule tunazosomea sisi wengine. Elimu yake aliipatia katika madrasa, kisha akafanya kazi mbali mbali, kama vile uvuvi na ubaharia.

Nimebahatika kuonana naye mjini Zanzibar na kufanya mahojiano naye. Ni mtaalam aliyebobea, mwenye mengi ya kutufundisha. Nina vitabu vyake kadhaa, na napangia siku zijazo kuandika makala kuhusu mchango wake uliotukuka katika sanaa na taaluma. Kwa mfano, mbali na vitabu vyake vya tenzi na mashairi, amefanya utafiti wa kina na kuandika "Kamusi ya Kitumbatu," ambayo ni hazina kubwa.

Kitu kimoja kilichonivutia sana katika kamusi hii ni jinsi ilivyosheheni majina ya aina mbali mbali za samaki na viumbe vingine vya baharini. Yeyote anayedhani kuwa ki-Swahili hakina msamiati wa taaluma kama hii aangalie kamusi hii. Atatambua alivyopotoka.

Tuesday, September 13, 2011

Mdau Kaleta Wadau Wengine


Kama nilivyowahi kuandika, tarehe 31 Agosti nilitembelewa na mdau Renatus Mgusii, ambaye anaonekana nami katika picha hapa kushoto. Ni mtu wa pekee kwangu, kwani ni msomaji makini wa vitabu vyangu. Ametumia hela zake nyingi kuvinunua na anapenda kuongelea yaliyomo. Pia ni mfuatiliaji wa blogu zangu. Ni wazi kuwa alivutiwa na mazungumzo yetu, hadi akaamua kuwaleta marafiki zake tuonane.


Wageni hao, ambao ni Mariana Ilieva na mumewe, aliwaleta tarehe 3 Septemba, pale Lion Hotel, Sinza. Mariana ni mkurugenzi wa Evin School of Management kwa upande wa Tanzania. Anajua lugha za ki-Bulgaria, ki-Rusi, ki-Swahili na ki-Ingereza. Mume wake, anayeonekana pichani, kulia kabisa, ni daktari m-Tanzania. Tuliongea mengi kuhusiana na taaluma na shughuli zetu sote wanne, na uwezekano na umuhimu wa kushirikiana. Ni jambo la kufurahisha kukutana na watu makini kama hao.

Sunday, September 11, 2011

Nyumba za Ibada Mjini Songea

Kama ilivyo katika miji mingine ya Tanzania, na hata katika vijiji vingi, mjini Songea kuna nyumba za ibada za dini mbali mbali, nami huvutiwa ninapoziona. Ni faraja kuona jinsi wa-Tanzania tulivyo na jadi ya kuishi pamoja bila kujali tofauti za dini. Picha hizi zinazoonekana hapa ni za baadhi ya nyumba za ibada zilizopo katikati ya mji wa Songea.

Hapa kushoto ni kanisa ambalo nalikumbuka tangu nilipofika Songea kwa mara ya kwanza, kwenye mwaka 1963 mwanzoni, nilipokuwa nakwenda kuanza darasa la tano katika Seminari ya Hanga. Kila ninapopita karibu na kanisa hili kumbukumbu hizi zinarudi akilini mwangu.






Hapa kushoto ni kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Songea. Nimewahi kuhudhuria misa katika kanisa hili.












Hapa kushoto ni msikiti. Sioni shida kupiga picha makanisa, lakini sina hakika kuhusu misikiti. Niliwahi kupiga picha msikiti mmoja katika mji fulani mkubwa Tanzania na dakika chache baadaye walikuja watu kunihoji kwa nini nimefanya hivyo. Nilifanya kazi kubwa kuwapa maelezo, na bado haikuwa rahisi kuwaridhisha. Lakini mimi natafuta kumbukumbu na taarifa hizi kwa nia njema, kama nilivyoelezea hapa. Sisiti kukiri kuwa navutiwa na taswira za misikiti.

Hapo nje ya msikiti niliwaona watu wakiuza vitu mbali mbali, kama vile vitabu. Nilivutiwa na uwepo wa vitabu, kwani tangu mwanzo wake, dini ya Islam ilikuwa inahimiza elimu. Inavyoonekana, hata dhana ya madrasa ilimaanisha mahali pa kufundishia taaluma mbali mbali, sio dini tu. Kama kumekuwa na upotoshaji, umetokea baadaye.

Friday, September 9, 2011

Hoteli ya Masista, Mbamba Bay

Mwaka huu nilipotembelea Mbamba Bay, tarehe 2 hadi 4 Agosti, nilifikia katika hoteli ya St. Bernadetha ambayo ni ya masista wa Kanisa Katoliki. Ni mradi wao katika kuendeleza huduma kwa jamii. Papo hapo, kuwepo kwa hoteli hii ni kivutio kwa utalii.

Ukiwa mjini Mbamba Bay, hoteli hii inaonekana vizuri, kwani iko kilimani. Ukiwa hapo hotelini, unaliona Ziwa Nyasa vizuri na mji wa Mbamba Bay chini yako.

Hoteli hii ni nzuri kwa kila hali, kuanzia mazingira hadi huduma za malazi na chakula. Ni aina ya hoteli ambayo unategemea kuiona katika miji mikubwa, si mji mdogo kama huu.

Wednesday, September 7, 2011

wa-Marekani Wajifunza u-Islam Kalenga

Mwaka huu, wanafunzi niliowaleta Tanzania kutoka Marekani wamepata fursa ya kujifunza kuhusu u-Islam kutoka kwa wahusika wa dini hiyo. Nilitaka wapate fursa hiyo, ili wapate mwanga angalau kidogo kuhusu dini hiyo, na pia waifahamu Tanzania kama nchi yenye dini mbali mbali, na waweze kujua tunavyoishi pamoja.

Mimi kama m-Kristo, ninaweza kuelezea masuala ya u-Kristo Tanzania kwa kiwango cha kuridhisha. Vile vile, kutokana na juhudi zangu za kujielimisha kuhusu dini mbali mbali, ningeweza kutoa maelezo kuhusu u-Islam, kama ninavyofanya ninapofundisha fasihi.

Lakini niliona ni muhimu kuwapa wanafunzi hao fursa ya kukutana na kujifunza kutoka kwa viongozi wa dini ya ki-Islam. Fursa nzuri ilijitokeza tulipokuwa Kalenga, mkoani Iringa, kwenye Makumbusho ya Mkwawa. Hiyo ilikuwa ni tarehe 11 Agosti. Baada ya ziara ya makumbusho, niliona msikiti, nikamwambia mkurugenzi wa makumbusho, ndugu Nicholaus Kulanga, kuwa ningependa kuonana na imam wa msikiti, ili anisaidie kuwaelimisha wanafunzi wangu kuhusu u-Islam. Mkurugenzi aliahidi kututambulisha.

Siku ya pili, alasiri, tulienda tena Kalenga, tukapata fursa ya kuongea na Imam Zuberi Suleiman. Nilimweleza lengo na madhumuni yangu, yaani kuwapa wanafunzi wangu fursa ya kuelewa kidogo kuhusu u-Islam, kwani fursa za aina hiyo ni nadra Marekani, na wa-Marekani wengi hawaelewi chochote au wana mawazo potofu kuhusu u-Islam.

Imam, anayeonekana pichani amevaa kanzu na kofia, alivutiwa na ombi hilo, akatuongoza hadi kwenye msikiti wa mwanzo wa Kalenga. Wakati anajiandaa kuongea nasi, alimwita pia mwenzake, ambaye ni Ustaadh Maneno, akajumuika nasi.

Imam na Ustaadh walitoa maelezo ya chimbuko la u-Islam na misingi yake kwa ufasaha kabisa. Hata mimi ambaye ninaelewa mambo kadha wa kadha kuhusu u-Islam nilipata mwanga mpya. Imam alinionyesha kitabu kiitwacho "Tafsiri ya Sehemu ya Kumi ya Mwisho ya Qur'an Tukufu." Nilivutiwa na kitabu hiki, na nitakinunua.

Sote tulifurahi kupata fursa hii ya kuongea. Nilijisikia vizuri pale Imam na Ustaadh waliposema wamefurahishwa kuwa nafahamu mengi kuhusu u-Islam. Wakati tunaagana, Ustaadh Maneno aliwapa majina mapya hao wanafunzi: huyu mvulana jina lake ni Abdi Karim na huyu dada jina lake ni Bi Aisha. Jambo hili lilitufurahisha wote, tukacheka kwa furaha. Niliwaeleza hao wanafunzi heshima ya majina hayo katika u-Islam, na kuanzia siku ile nimekuwa nikiwaita kwa majina hayo.

Tumejenga uhusiano mzuri hapo Kalenga. Mwakani, Insh'Allah, natawapeleka wanafunzi wengine hapo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...