Sunday, September 14, 2014

Wa-Kenya Walitia Fora Tamasha la Afrifest

Tarehe 2 Agosti, lilifanyika tamasha la Afrifest, katika mji wa Brooklyn Park, Minnesota. Tamasha hili hufanyika kila mwaka, likijumuisha wa-Afrika na watu wenye asili ya Afrika waishio Marekani, visiwa vya Caribbean, America ya Kati na Kusini, na sehemu zingine, na pia watu wasio wa-Afrika au wa asili ya Afrika. Wote hao hushiriki, kwa lengo la kufahamiana, kuelimishana, na burudani.

Tamasha huanzia siku moja kabla, jioni, kwa burudani ya muziki, maonesho ya mavazi na kadhalika. Hivyo ndivyo ilivyokuwa tarehe 1 Agosti. Siku inayofuata, tamasha hufanyika nje uwanjani. Kunakuwepo na mabanda ya wafanya biashara, pia watoa huduma mbali mbali. Kunakuwepo muziki, michezo ya watoto, na mechi ya soka. Ndivyo ilivyokuwa mwaka huu kule Brooklyn Park.

Mwaka huu, wa-Kenya walijitokeza kwa wingi kuliko wa-Afrika wa nchi nyingine yoyote. Palikuwa na meza ambapo paliwekwa bidhaa na vitu mbali mbali kutoka Kenya. Bendera ya Kenya ilipepea siku nzima. Ilifurahisha kuona wenzetu walivyoonyesha umakini katika kuitangaza nchi yao.

Jambo hili lilitajwa katika mkutano wa Bodi ya Afrifest Foundation. Mimi mwenyewe nilikuwa na meza ambapo nilikuwa nimeweka vitabu na machapisho yangu mengine. Kati ya watu waliofika hapo mezani walikuwepo wa-Kenya.

Mimi na binti zangu tunakumbuka, kwa mfano, jinsi kijana mmoja alivyofika hapo mezani, akaongea nasi kwa ki-Swahili. Alionekana kijana wa kawaida tu, nasi tulidhani ni mmoja wa wale wanaotaka kuelewa shughuli zangu, kuhusu vitabu vyangu, na kisha wanaenda kwenye meza au mabanda mengine. Bila sisi kutegemea, alinunua vitabu vitatu kabla ya kuondoka.

Thursday, September 11, 2014

Kitabu Kimeingia Katika Chuo Kikuu cha Cincinnati, Marekani

Pamoja na mengine yote, blogu hii ni mahali ninapohifadhi kumbukumbu za shughuli zangu mbali mbali, hasa zile ninazofanya katika jamii, nje ya chuo ninapofundisha. Kumbukumbu hizi ni pamoja na taarifa kuhusu namna vitabu vyangu vinavyotumika katika jamii.

Miezi kadhaa iliyopita, niliona taarifa mpya, ila sikupata fursa ya kuiweka katika blogu hii. Taarifa yenyewe ni kuwa kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kimependekezwa kwa wanafunzi katika chuo cha matibabu cha Chuo Kikuu cha Cincinnati kilichopo katika jimbo la Ohio, hapa Marekani.

Profesa wa programu ya kupeleka wanafunzi Ghana, Dr. Jason Blackard, ambaye picha yake nimeiweka hapa kushoto, ndiye aliyekipendekeza kitabu hiki--pamoja na vingine vitatu--akiwataka wanafunzi kuwa kila mmoja achague kitabu kimojawapo, akisome, halafu aandike ripoti fupi kielezea aliyojifunza. Taarifa hizi zimo katika "syllabus" yake ya programu hiyo ya Ghana.

Simfahamu profesa huyu, na wala hatujawahi kuwasiliana. Ningekuwa na mawasiliano naye, ningependa kujua alizipataje taarifa za kitabu hiki. Najua taarifa ziko tele mtandaoni, lakini najua pia mara kwa mara watu hupata taarifa kutoka kwa wenzao waliokisoma kitabu. Kwa vile nina dukuduku ya kujua, huenda nikawasiliana na profesa huyu.

Tuesday, September 9, 2014

Viongozi wa Afrifest Foundation

Kama wewe ni mtembeleaji wa blogu yangu hii ya hapakwetu au ile ya ki-Ingereza, utakuwa umesoma taarifa zangu kuhusu Afrifest, taasisi iliyoanzishwa hapa Minnesota, Marekani, na makao yake ni hapa hapa.

Hapa kushoto tunaonekana baadhi ya viongozi tunaoendesha Afrifest. Kulia kabisa ni Nathan White, kutoka Liberia, ambaye nikatibu mtendaji wa Afrifest, na ndiye ambaye alianzisha wazo zima la Afrifest, kama anavyoelezea hapa.

Katikati naonekana mimi, m-Tanzania, ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya Afrifest. Nimekuwa mshiriki wa Nathan White tangu mwanzo, pamoja tukapanga na kuendesha tamasha la kwanza la Afrifest, mwaka 2007. Tulipopiga picha hii, afya yangu ilikuwa dhaifu kuliko sasa. Sikumbuki kama maishani mwangu nimewahi kupigwa picha inayonionyesha nikicheka namna hii.

Kusohto kabisa ni Wycliff Chakua, kutoka Kenya. Yeye alijiunga na Afrifest miaka michache iliyopita. Ndiye mweka hazina wa Afrifest.

Tulipiga picha hii tarehe 2 Agosti, wakati wa tamasha la Afrifest lililofanyika Brooklyn Park, Minnesota. Niliandika habari za tamasha hilo mara kadhaa, kwa mfano hapa, hapa, na hapa. Tunao wanabodi wengine ambao hawakuweza kuhudhuria tamasha hili, lakini tuko pamoja katika kushughulikia malengo ya Afrifest ya kuwaunganisha, kuwaelimisha, na kuwaburudisha watu wenye asili ya Afrika popote walipo ulimwenguni, na watu wengine wote wenye mtazamo huo au wanaotaka kufahamu zaidi mambo tunayoyashughulikia.

Kazi zetu katika Afrifest ni za kujitolea. Lakini tunafurahi kuzifanya, na furaha inakuwa kubwa tunapoona jinsi jamii inavyofaidika na shughuli zetu. Utumishi huu kwa jamii unatupa fursa ya kufahamiana vizuri sisi wenyewe na pia kufahamiana na wadau wanaohudhuria matamasha na matukio mengine ya Afrifest. Karibuni kwenye matamasha na matukio haya. Karibuni pia mtutembelee katika Facebook.

Sunday, September 7, 2014

Ninasoma "Shalimar the Clown," Riwaya ya Salman Rushdie.

Salman Rushdie ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa wanaoandika katika ki-Ingereza. Kwa uandishi wake, amepata tuzo zinazoheshimika sana, kama vile "Booker Prize."

Mimi ni mwalimu wa fasihi ya ki-Ingereza. Mara moja moja ninafundisha kozi ya "South Asian Literature," yaani fasihi ya Asia ya Kusini. Katika kozi hii, ninafundisha maandishi ya watu kama Rabindranath Tagore, R. K. Narayan, Raja Rao, Mulk Raj Anand, Anita Desai, Michael Ondaatje, na Salman Rushdie.

Haiwezekani kusoma au kufundisha maandishi yote. Vile vile, kazi mpya za fasihi zinaendelea kuchapishwa. Kwa hivi, kila ninapofundisha kozi ya namna hii, najua kuwa katika orodha yangu kuna waandishi ambao hawamo. Kuna kazi muhimu za fasihi ambazo hazimo. Huu ndio ukweli, ingawa haupendezi.

Uchaguzi wowote wa waandishi au maandishi ambao ninafanya kwa kufundishia katika muhula fulani wa masomo una utata na unazua masuali. Nilipofundisha kozi ya "South Asian Literature" kwa mara ya kwanza, Salman Rushdie hakuwemo. Nilijiuliza kama hii ni sahihi.

Hatimaye, nilianza kutumia maandishi ya Rushdie. Nilianzia na riwaya yake maarufu ya Midnight's Children. Hii sio riwaya rahisi kuisoma, lakini wanafunzi wangu nami tulifanya bidii tukaimaliza. Salman Rushdie anaandika ki-Ingereza ambacho kina mvuto wa pekee, ingawa sio rahisi, kwa mbinu za kila aina. Anadhihirisha ufahamu mkubwa wa ki-Ingereza, falsafa, fasihi, dini, siasa, na tamaduni mbali mbali. Msomaji unajikuta katika kazi kubwa ya kufikiri na kukabiliana na chemsha bongo mbali mbali.

Midnight's Children ilinipa hamasa ya kutumia maandishi ya Rushdie. Muhula huu wa masomo ambao ulianza wiki iliyopita, nitatumia riwaya yake ya Shalimar The Clown. Sikuwa nimeisoma riwaya hii, bali nimeanza, katika kujiandaa kuifundisha. Panapo majaliwa, hapo tutakapokuwa tumemaliza kuisoma na kuijadili, nitaandika habari zake katika blogu hii. Ila napenda kutoa tahadhari kuwa dhana ya kumaliza kusoma kazi yoyote ya fasihi sio dhana yenye ukweli. Ingawa tunaitumia dhana hii, tunajidanganya.


Friday, September 5, 2014

Leo Nimeanza Tena Kufundisha

Baada ya kuumwa kwa miezi mingi, na kuwa katika likizo ya matibabu, leo nimeanza tena kufundisha. Hali yangu inaendelea kuimarika, na ingawa naendelea na matibabu kidogo kidogo, madaktari wameridhia ombi langu kuwa nirudi darasani. Wameniwekea sharti kuwa nisibebe mzigo mkubwa wa kozi za kufundisha, na nisihusishwe na shughuli nyingine ambazo walimu huzifanya, kama vile ushiriki katika kamati mbali mbali na mikutano. Hiyo picha hapa kushoto nimejipiga mwenyewe leo, baada ya kutoka darasani.

Hali itakuwa hiyo kwa muhula mzima, ambao umeanza leo, na utamalizika katikati ya mwezi Desemba. Ninafundisha kozi mbili, ya kwanza ni "South Asian Literature," na ya pili ni "Writing." Katika hiyo kozi ya kwanza, ambayo niliitunga miaka michache iliyopita, nafundisha riwaya kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Riwaya hizo ni, Untouchable, iliyoandikwa na Mulk Raj Anand (India); Twilight in Delhi, iliyoandikwa na Ahmed Ali (India); The Crow Eaters, iliyoandikwa na Bapsi Sidhwa (Pakistan); Shalimar the Clown, iliyoandikwa na Salman Rushdie (India); na Reef, iliyoandikwa na Romesh Gunesekera (Sri Lanka).

Ninapangia kufundisha pia mashairi kutoka katika nchi hizo. Kwa wakati huu, katika kujiandaa, ninasoma kitabu cha mashairi ya Michael Ondaatje kiitwacho The Cinnamon Peeler. Michael Ondaatje alizaliwa Sri Lanka, ila anaishi Canada. Ninafanya pia uchunguzi wa vitabu vya mashairi ambayo nitaweza kuyatumia. Kila ninapofundisha kozi hii, nabadilisha, kwa kiasi fulani, vitabu au waandishi.

Fasihi ya hiyo sehemu ya dunia imejengeka katika historia, siasa, dini, tamaduni, na harakati za watu wa kule tangu miaka elfu tano au zaidi iliyopita hadi kwenye kipindi cha ukoloni, na baada ya kupata uhuru. Waandishi wengi wa India na Pakistan, kwa mfano, wanaelezea janga kubwa lililotokea kabla tu ya kupata uhuru na wakati nchi ilipogawanyika na kuwa nchi hizi mbili, mwaka 1947.

Katika kozi ya "Writing," ninafundisha uandishi bora wa ki-Ingereza. Kadiri miaka ilivyokwenda, nami kujijengea uzoefu zaidi na zaidi wa kufundisha kozi hii, nimekuwa nikitafuta mbinu mpya za kufundisha. Leo nimewaambia wanafunzi kuwa, tofauti na miaka yote iliyopita, na tofauti na wanavyofanya waalimu wengine, muhula huu tutatumia vitabu viwili tu. Kitabu kimoja ni The Trickster, kilichoandikwa na Paul Radin, na kingine ni The Elements of Style, kilichoandikwa na William Strunk Jr. na E.B. White.

Lengo langu katika hii kozi ya uandishi ni kuwafundisha kwanza kabisa namna ya kuandika sentensi bora kabisa ya ki-Ingereza, kama alivyoelekeza mwandishi maarufu Ernest Hemingway, na baada ya hapo tutaendelea hadi kuweza kuandika insha bora kabisa. Nimewaeleza wanafunzi kwamba uandishi bora ni jambo la lazima kwa mafanikio maishani mwao, nikatoa mifano mbali mbali ya namna watakavyohitaji uwezo wa kuandika ipasavyo. Wameona uzito wa hoja na mifano niliyotoa.

Nimefurahi kuwa nimefikia hali ya kuweza kuingia tena darasani, nikizingatia hali yangu kiafya ilivyokuwa mbaya kabla sijalazwa hospitalini. Kwa mara nyingine tena, namshukuru Mungu, na nawashukuru madaktari na wauguzi, familia yangu, marafiki, na wote wanaonitakia mema. Mungu awabariki wote.

Wednesday, September 3, 2014

Matamasha Ninayoshiriki ni Kama Shule

Matamasha ninayoshiriki ni muhimu. Ni kama shule. Ninabadilishana mawazo na wadau mbali mbali. Kuna ambayo ninawaeleza na kuwaelimisha, na wao kuna ambayo wananieleza na kunielimisha. Kuna masuali na majibu, au angalau maelezo, kwa upande wao na wangu.

Hapa kushoto naonekana niko katika mazungumzo mazito na jamaa mmoja kutoka Liberia, aitwaye Ahmed. Tumefahamiana kwa miaka kadhaa. Hapo tulikuwa katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park.



Ninapata fursa ya kukutana na watu wa aina aina. Hapa kushoto niko na mama mmoja ambaye alionekana mkimya, lakini alikuwa na dukuduku ya kujua moja mawili. Ilikuwa katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park.









Hapa kushoto nilikuwa katika mji wa Brooklyn Park, na wa-Marekani Weusi wawili. Huyu aliyekaa pembeni yangu tulikuwa tunafahamiana, lakini huyu mwenye kofia ilikuwa ni mara ya kwanza kukutana. Ilikuwa katika tamasha fulani lililoandaliwa na taasisi ya wa-Afrika, inayoshughulikia masuala ya afya.

Huyu mwenye kofia alikuwa mtu asiye na papara katika kuzungumza, bali mwenye tafakari nzito. Unaweza kujionea jinsi tunavyomsikiliza kwa makini.




Shughuli zangu sifanyii Marekani tu. Hapa kushoto nilikuwa Diamond Jubilee Hall, mjini Dar es Salaam, katika tamasha lililoandaliwa na Tripod Media.

Ninaonekana nikiwahamasisha watoto wa shule kuhusu kufanya bidii shuleni,  nikiwapa mfano wangu mwenyewe na hatua niliyofikia maishani. Kuwaambia watoto kama hao kwamba juhudi niliyofanya shuleni imeniwezesha sasa kuwa mwalimu na mwandishi wa vitabu ni namna ya kuwahamasisha wazingatie shule.



Hapa kushoto niko na jamaa wawili, Diamond Jubilee Hall, Dar es Salaam, katika tamasha la Tripod Media nililotaja hapa juu. Kama unavyoona, tuko katika mazungumzo mazito.










Hapa kushoto, katika tamasha la Afrifest, mjini Brooklyn Park, naonekana nikipata mawili matatu kutoka kwa bwana Bolstad, ambaye alizaliwa na kukulia Tanzania, na wazazi wa-Marekani. Ingawa sasa anaishi Marekani, anajisikia kama m-Tanzania, na ki-Swahili anaongea vizuri sana.

Yeye nami tumefahamiana kwa miaka mingi kidogo, na naguswa na jinsi anavyokipigia debe kwa watu mbali mbali kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Watu wa aina yake wanachangia katika kunifanya niwe na ari ya kuandika zaidi, kwa faida ya walimwengu.

Tuesday, September 2, 2014

Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania Kuhusu Katiba Mpya

Tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania kuhusu Katiba Mpya

JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA

TAMKO LA JUKWAA LA WAKRISTO TANZANIA KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA


Sisi, wajumbe wa Jukwaa la Wakristo Tanzania, tuliokutana tarehe 27 hadi 28 Agosti, 2014, Dar es salaam , tumepata fursa ya kutafakari, kujadili na kujielimisha kwa kina yaliyomo katika Rasimu ya pili ya Katiba na mjadala unaoendelea katika Bunge Maalum la Katiba. Baada ya mjadala wa kina, tunatoa tamko letu kama ifuatavyo:

Tunaipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikusanya Maoni ya WANANCHI kuhusu mabadiliko hayo na kutuletea Rasimu yenye maoni mengi ya Watanzania bila kujali dini zao, upande wa Muungano walikotoka, hali zao za kimaisha, jinsi na kabila.

Pia tunaipongeza Tume kwa kuandaa nyaraka na kumbukumbu mbalimbali kama Randama, Nyaraka zenye maoni ya wananchi, picha, tafiti mbalimbali na hata orodha ya watu walioshiriki kutoa maoni katika Tume. Tume pia iliweza kuandaa Tovuti iliyokuwa na kumbukumbu za Tume na Maoni yote
yaliyotolewa. Kazi hii ni ushahidi kuwa Tume iliandaa Rasimu kwa weledi na kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kwa kuzingatia maoni ya WANANCHI.

Tume imedhihirisha kuwa, ilitenda KIZALENDO na, kwa mantiki hiyo, wajumbe wote bila kujali vyama vyao, dini zao na upande wa Muungano walikotoka, waliweza kujadili kwa uwazi na kweli na mwisho wakaridhiana katika kila Ibara iliyopendekezwa. Hili linatufundisha kuwa Katiba ni MARIDHIANO na si jambo la maslahi ya kisiasa, bali ni suala la maslahi ya WANANCHI.

Tunaamini kuwa kila Mjumbe wa Kamati ya kukusanya maoni ya WANANCHI aliheshimu kiapo chake na hivyo kufanya kazi waliyokabidhiwa kwa uaminifu na uadilifu na ya kwamba hawakushawishiwa au kupokea rushwa kutoka kwa kundi, dini au chama chochote cha siasa wakati wa zoezi hili.

Baada ya Tume kuwasilisha Rasimu kwenye Bunge Maalum la Katiba, Taifa likaanza kushuhudia “uasi wote na uovu wa wanadamu wapingao kweli kwa uovu” (Warumi 1:18). Katika mijadala ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) yakaanza kujitokeza mambo mengi yasiyo ya maslahi kwa WANANCHI, na ukiukwaji wa sheria na kanuni. Mambo kadhaa yanadhihirisha hili:

Tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifungwa bila sababu za msingi kutolewa wakati mchakato unaendelea. Hali hii imefanya zile nyaraka na kumbukumbu zilizoandaliwa kwa ajili ya rejea na kuwezesha mjadala wa Rasimu ya Katiba kuendelea katika mwanga na ufahamu wa nyaraka hizo kutowezekana kabisa. Kwa sababu hiyo, tumeona Bunge Maalumu la Katiba likiendelea kupotosha takwimu na taarifa mbalimbali ambazo WANANCHI hawawezi kuzipata kwa ajili ya kuoanisha baina ya kinachojadiliwa Bungeni na kilichomo katika Rasimu na viambatanisho vyake vyote. Tunajiuliza jambo hili limefanywa na nani na kwa maslahi ya nani?

Bunge la Katiba limeshindwa kusimamia Kanuni kama ambavyo zilipendekezwa na kuridhiwa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Kushindwa huku kusimamia kanuni kumesababisha vurugu ndani ya Bunge Maalumu na kumekwamisha matarajio ya wananchi kupata Katiba bora ya nchi yetu. Matumizi ya ubabe na wingi wa Wabunge wa Chama Tawala (CCM), badala ya Kanuni za Bunge na maridhiano, kumefanya mchakato wa Katiba kuhodhiwa na Chama Tawala dhidi ya maslahi ya WANANCHI.

Mijadala katika Bunge Maalumu la Katiba imekuwa ya kejeli, matusi, vitisho, ubabe na kupuuza hata kupotosha maoni yaliyotolewa na Wananchi kwa Tume. Hali hii imelifanya Bunge Maalumu la Katiba kupuuzwa na hivyo kupoteza heshima na hadhi yake. Matokeo yake baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wakaamua kususia vikao vya bunge na wengine kuendelea, bila kukumbuka kuwa KATIBA NI MATOKEO YA TENDO LA MARIDHIANO NA SI SUALA LA MASLAHI YA KIKUNDI CHA WATU WACHACHE.

Hatua iliyofikiwa ni dhahiri, Mjadala wa BMK unaoendelea umeondoa kwa kiasi kikubwa maoni yaliyotolewa na wananchi kuhusu muundo wa Muungano, kupunguza mamlaka ya Rais, uwajibikaji na uwajibishwaji wa wabunge, ukomo wa ubunge, n.k., na kuwezesha maoni na maslahi ya Chama Tawala kwa uongozi wa kikundi cha wanasiasa wachache wasio na uaminifu na uadilifu wa kutosha kuwekwa kama mapendekezo ya Katiba mpya kwa nia ya kulinda maslahi binafsi au ya makundi na kuhalalisha ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na maadili ya uongozi bora.
Baada ya kujadili na kuona haya na mengine mengi, Jukwaa la Wakristo Tanzania lina maoni yafuatayo;

1. Kwamba Serikali (Wizara ya Katiba na Sheria) irudishe tovuti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba na nyaraka zake zote kwa ajili ya wananchi kuendelea kuona kazi waliyoifanya, kujifunza na kujadili Rasimu ya Katiba kwa uwazi.

2. Kwamba maoni ya wananchi hayawezi kufutwa na kudharauliwa na Chama Tawala. Hivyo basi, Bunge Maalumu la Katiba linaloendelea lijadili na kuboresha tu maoni yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na sio kufanya mabadiliko katika Katiba ya mwaka 1977.

3. Kwamba mchakato wa Katiba usimamishwe ili kupisha majadiliano, maelewano na maridhiano muafaka, uchaguzi mkuu na wa serikali za mitaa. Na mabadiliko ya Katiba ya 15 ya mwaka 1977 yafanyike kuwezesha chaguzi kufanyika kwa uwazi na haki. Pia, kuweka kifungu kitakacholinda Rasimu ya pili na kumtaka kiongozi ajaye kuendelea na mchakato wa Katiba.

4. Kwamba baada ya Bunge Maalum la Katiba kuanza shughuli zake tena, Mwenyekiti wa Bunge hilo afanye kazi kwa mujibu wa kanuni na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba badala ya kutumia ubabe na kiburi cha wingi wa wajumbe wa Chama cha Mapinduzi katika Bunge la Katiba.

5. Kwamba wananchi waendelee kusoma na kujadili maoni yaliyoko katika Rasimu ya pili ya Katiba, na kufuatilia kitakachokuwa kinajadiliwa kwenye Bunge la Katiba ili kuwawezesha kupiga kura ya maoni wakiwa na uelewa wa kutosha kabisa kuhusu ni nini kipo kwenye “Katiba inayopendekezwa”. Wananchi pia wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwa nia ya kuwawezesha kupiga kura ya maoni.

6. Kwamba tunaomba Tume ya Mabadiliko ya Katiba ihuishwe na kupewa mamlaka kisheria ili kuiwezesha kujibu maswali yanayojitokeza na kutoa ufafanuzi kwa Bunge Maalumu la Katiba na wananchi kwa jumla hadi Katiba Mpya itakapokamilika na kukabidhiwa rasmi.

Jukwaa la Wakristo Tanzania na Watanzania wote wanaoitakia nchi yao mema, tunakuomba Mheshimiwa Rais kwamba AMANI ya nchi yetu sasa imo mikononi mwako hasa katika kipindi hiki cha kuandikwa kwa Katiba Mpya. Tunakuomba uahirishe mchakato unaoendelea ili uepushe ishara za aina mbalimbali za kuanzisha sintofahamu nchini mwetu na hali yoyote inayoweza kuathiri vibaya mshikamano, umoja na amani ya Taifa letu.

Ifahamike kuwa WANANCHI wa Tanzania wako juu ya Wajumbe wa Chama cha Mapinduzi. Kwa mantiki hiyo, tunakuomba uepushe WANANCHI wa Tanzania kuhamasishwa kukikataa Chama cha Mapinduzi kwa kuwa tu Chama hicho kimeyapuuza na kimekataa Maoni yao waliyotoa kwa dhati baada ya kuaswa na kuhimizwa kufanya hivyo na viongozi wa nchi.

“Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye yasiyowapasa. Wamejawa na udhalimu wa kila namna, uovu na uuaji, na fitina, na hadaa; watu wa nia mbaya, wenye kusengenya, wenye kusingizia, wenye kumchukia Mungu, wenye jeuri, wenye kutabakari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao, wasio na ufahamu, wenyekuvunja maagano, wasiopenda jamaa zao, wasio na rehema; si hivyo tu, bali wanakubaliana nao wayatendao”. (Rejea Warumi 1: 28-32)

IKUMBUKWE KUWA RASIMU YA PILI YA KATIBA NI WARAKA HALALI NA RASMI NA NDIYO MAWAZO YA WATANZANIA NA TUNAHIMIZA KUWA KATIBA NI YA WANANCHI NA INAHITAJI MARIDHIANO NA SIO UBABE.

Imetolewa leo Agosti 28, 2014
Na MKUTANO WA JUKWAA LA WAKRISTO
Tanzania Episcopal Conference (TEC) The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT)
Christian Council of Tanzania (CCT) The Seventh Day Adventists (SDA)

CHANZO: Wavuti

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...