Saturday, March 30, 2013

Wa-Marekani Watua kwa Mama Lishe, Usa River

Mwezi Januari mwaka huu, nilipokuwa Tanzania nikifundisha kozi ya Hemingway, niliandaa fursa mbali mbali za kuwawezesha wanafunzi, ambao ni wa-Marekani, kushiriki katika utamaduni wa wa-Tanzania, ili kujifunza. Tulikuwa tumefikia Colobus Mountain Lodge, iliyomo pembeni mwa Arusha National Park. Siku moja, mara tu baada ya wanafunzi hao kuwasili nchini niliwapeleka kwenye mji mdogo wa Usa River, ili wakazunguke na kujionea. Niliamua kuwasafirisha katika dala dala, tukiwa tumebanana. Usafiri ule ulikuwa kitu kipya kabisa kwao, lakini niliona ni muhimu kwao, wajifunze. Tulifika Usa River, tukazunguka mitaa kadhaa, na kisha tukasogea tena pembeni mwa barabara kuu. Hapo wanafunzi walimwona mama lishe akiwa kazini, wakapanga foleni kujipatia chipsi mayai.



Kwao hili lilikuwa jambo jipya, ila walifurahia hicho chakula. Niliridhika sana kwamba wanafunzi walipata fursa hiyo ya kujionea na kufaidi huduma ya mama lishe, kwani ni sehemu muhimu katika utamaduni wa Tanzania ya leo.











Wanafunzi walikuwa wengi zaidi ya hao wanaoonekana pichani. Mama lishe alifanya kazi kubwa ya kuwahudumia. Wala hiyo haikuwa mara yao ya mwisho kuja hapa. Walifika tena, na kama tungekaa siku nyingi eneo hili la Usa River, wangefika tena na tena.

Kwa vile wengi wanaosoma blogu hii ni wa-Tanzania, naomba tukumbushane tu kuwa mbali ya elimu inayotokana na safari za aina hii, kwa wageni na wenyeji, na mbali na fedha nyingi inayoingia katika hazina ya nchi, shughuli hizi za kuwapeleka wanafunzi Tanzania ni zinachangia kipato cha watu wa kawaida, kama vile mama lishe, dobi, mwenye nyumba ya kulala wageni, na muuza ndizi sokoni. Safari hii, hata vinyozi nao walijipatia biashara.

Tuesday, March 26, 2013

Ufundishaji Wangu wa Maandishi ya Achebe

Nimefundisha maandishi ya Chinua Achebe kuanzia miaka ya sabini na kitu. Kabla sijahitimu na shahada ya kwanza Chuo Kikuu Dar es Salaam, mwaka 1976, huenda nilifundisha Things Fall Apart katika shule za sekondari nilikopelekwa kufanya mazoezi ya kufundisha, yaani sekondari ya wasichana Iringa, 1974, na sekondari ya Kinondoni, 1975. Sina hakika.

Lakini baada ya kuhitimu shahada ya kwanza, mwaka 1976, nilipata fursa za kufundisha Things Fall Apart, nikianzia na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa mhadhiri. Mwaka 1980, chini ya mkataba wa ushirikiano baina ya Tanzania na Burundi, nilifundisha kwa wiki kadhaa katika Chuo Kikuu cha Burundi. Kitabu kimojawapo kilikuwa Things Fall Apart

Uzoefu huu ulinifanya niandike mwongozo wa Things Fall Apart, ili kuelezea mambo ambayo waandishi wengine hawajayaweka wazi.  Ilikuwa ni fursa kwangu kuwaelezea wanafunzi na walimwengu namna ninavyoichukulia riwaya hii ya Things Fall Apart. Kwa maelezo zaidi ya historia hii, soma hapa. Sihitaji kuficha ukweli kwamba mwongozo huu ni maarufu na wengi wanautumia.

Baada ya kuja kufundisha chuo cha St. Olaf, mwaka 1991, nimefundisha Things Fall Apart na maandishi mengine ya Achebe. Kuna muhula fulani nilitunga kozi nzima juu ya maandishi ya Achebe tu. Tulisoma riwaya zake kadhaa, na pia insha baadhi ya insha zake, zikiwemo "The Novelist at Teacher," "Colonialist Criticism," na "An Image of Africa." Tulisikiliza pia baadhi ya mahojiano yake. Ingekuwa muda unaruhusu, tungesoma pia mashairi yake.

Ni wazi kwamba Things Fall Apart ni moja ya riwaya ambazo nimezifundisha sana. Kila ninapoifundisha, nazua masuala mapya na tafakari mpya. Hiyo ni tabia ya fasihi. Hata misahafu ina tabia hiyo, ingawa wako watu wanaodai kuwa misahafu haibadiliki. Binafsi, kutokana na uzoefu wangu wa kusoma na kutafakari fasihi na maandishi mengine, siamini kwamba kuna andiko lolote, hata msahafu, ambalo haliguswi na mabadiliko, kuanzia na mabadiliko ya lugha na maana zake, ambayo hayakwepeki. Nimegusia suala hilo katika mwongozo wangu.

Monday, March 25, 2013

Achebe wa Enzi za Ujana Wetu

Sisi tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu tunaikumbuka picha ya Chinua Achebe inayoonekena hapa kushoto. Ndio picha iliyokuwepo kwenye jalada, upande wa nyuma wa kitabu cha Things Fall Apart. Kwa bahati nzuri, ninayo nakala ya miaka ile ya Things Fall Apart. Niliipata miaka ya karibuni, nikaona niwe nayo, angalau kujikumbusha enzi za ujana wetu. Ninazo pia nakala za matoleo ya hivi karibuni, lakini ile ya zamani niliiona kama lulu.

Kuanzia mwaka 1966 hadi 1970 nilikuwa mwanafunzi wa sekondari, seminari ya Likonde. Wakati huo riwaya ya Things Fall Apart ilikuwa maarufu. Tulivijua pia vitabu vya watoto ambavyo Achebe alikuwa ameandika. Navikumbuka viwili: The Sacrificial Egg and Other Short Stories na Chike and the River. Shule yetu ilikuwa na maktaba kubwa na nzuri sana. Nidhamu ya kusoma ilikuwa kali, chini ya usimamizi wa mapadri waliokuwa waalimu wetu.

Miaka ile ile, Achebe alichapisha riwaya ya No Longer at Ease na Arrow of God na A Man of the People. Tulikuwa tunamsoma Achebe sambamba na Cyprian Ekwensi. Baadhi ya vitabu vya Ekwensi ambavyo tulivisoma ni Burning Grass, na People of the City na Jagua Nana. Hao wawili walikuwa kama mafahali wawili kutoka Nigeria katika uwanja wa uandishi.

Katika seminari ya Likonde, mwalimu wangu wa ki-Ingereza alikuwa Padri Lambert Doerr OSB, m-Jerumani, ambaye sasa ni askofu mstaafu pale Peramiho. Sidhani kama nimewahi kukutana na mtu anayesoma vitabu kama yeye. Alituwekea amri kwamba tusome angalau kitabu kimoja cha hadithi ya ki-Ingereza kwa wiki. Kitabu kimoja ilikuwa ni kiwango cha chini, lakini usikae wiki bila kumaliza angalau kitabu.

Padri Lambert alikuwa na mtindo wa kugawa daftari kwa kila mwanafunzi ambamo tulipaswa kuelezea kuhusu vitabu tulivyosoma, au ambavyo tulidai tumesoma. Wakati wowote alikuwa anaitisha daftari lako, ili akusikie ukimweleza habari ya kitabu chochote ulichokiorodhesha humo. Kumdanganya ilikuwa haiwezekani, wala huthubutu. Matokeo ya hayo ni kuwa kila mmoja wetu alisoma vitabu vingi sana, na ufahamu wetu wa ki-Ingereza ulikuwa mkubwa kabisa. Achebe, kwa uandishi wake wa kuvutia, alichangia kwa kiasi kikubwa kutufanya tupende kusoma.

Toleo Jipya la "Kioo cha Lugha"

Siku chache ziilizopita, nilipata nakala ya jarida la Kioo cha Lugha, kutoka Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Mimi ni mwanakamati katika kamati ya uhariri wa jarida hilo. Ni furaha kubwa kwangu kushirikiana na wanataaluma wenzangu katika mambo ninayoyapenda. Masuala ya la lugha, fasihi, utamaduni, na falsafa yana nafasi ya pekee katika maisha yangu.















Toleo hili la Kioo cha Lugha lina makala nyingi, kama inavyoonesha katika picha hii hapa kushoto. Wanaodhani kuwa ki-Swahili kina mapungufu katika kuelezea taaluma mbali mbali, watafakari upya suala hilo, hasa kwa kusoma machapisho kama yale yatokayo katika Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, ambayo ni ya taaluma mbali mbali. Niliwahi kugusia suala hilo katika ujumbe huu hapa.

Friday, March 22, 2013

Buriani, Chinua Achebe

Msiba mzito umetufika leo, wasomaji wa fasihi na walimwengu kwa ujumla. Chinua Achebe amefariki, akiwa na umri wa miaka 82.

Maarufu kama muasisi wa fasihi ya ki-Ingereza katika Afrika, Chinua Achebe ametoa mchango mkubwa katika uandishi, mchango ambao uliiweka Afrika mahala pazuri katika ramani ya fasihi ya dunia.

Tangu alipochapisha riwaya yake maarufu, Things Fall Apart, hadi kufariki kwake, Achebe ameandika riwaya, hadithi fupi, na insha kuhusu fasihi, uandishi, siasa na utamaduni. Amefanya mahojiano mengi, ambayo, kwa bahati nzuri yanapatikana mtandaoni au katika vitabu na majarida.

Achebe aliamini kwa dhati kuwa jukumu la msanii ni kuwa mwalimu wa jamii. Yeye mwenyewe amezingati wajibu huo tangu ujana wake, alipochapisha Things Fall Apart, hadi kurariki kwake. Amewafundisha waAfrika mengi kuhusu jamii yao, udhaifu na uwezo wao, na amewafundisha walimwengu kuwaona wa-Afrika kwa mtazamo tofauti na ule wa wakoloni. Amewafundisha walimwengu maana ya ubinadamu, ambayo inavuka mipaka ya kabila, taifa, dini, jinsia au nchi.

Sikupata fursa ya kukutana uso kwa uso na Chinua Achebe, bali nimesoma na kufundisha maandishi yake mara kwa mara. Nashukuru pia kuwa nilipata wazo la kuandika mwongozo wa Things Fall Apart. Kwa namna hiyo ya kusoma na kutafakari maandishi yake, najiona kama vile nami nimekutana na mwandishi huyu. Nimalizie tu kwa kusema kwamba kwa mchango wake mkubwa kwa walimwengu, Achebe atakumbukwa daima.

Wednesday, March 20, 2013

Tamko la CCM Mkoa wa Vyuo Vikuu

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkoa maalum wa vyuo vikuu, kanda ya Dar es salaam, umefanya kikao cha kujadili mipango na mikakati mbalimbali ya kuimarisha Mkoa huo na Chama kwa ujumla. Pamoja na Ajenda hiyo, pia kikao hicho:-

· Kimelaani vikali matukio ya kuvamiwa, kudhuru mwili na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa Dini na wanahabari. Mkoa umesikitishwa sana na tukio la kushambuliwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006 Ndugu Absalom Kibanda.

· Lakini pia, kimevitaka vyombo vya Dola kuwakamata, kuwashikilia na kuwachukulia hatua za kisheria wote waliothibitika kuhusika na matukio ya namna hiyo bila kuangalia Itikadi za Kivyama, Cheo ama Kundi. Na pia kuyataka makundi ya kijamii, wanaharakati na wanasiasa kuacha kuingilia/kuvuruga kwa namna yeyote taratibu za kisheria na kiusalama.

· Pia, kuwataka wanausalama kumhoji kwa kina Dr Slaa juu ya tuhuma zake dhidi ya Kurugenzi ya Usalama wa Taifa (TISS) na kumtaka kuthibitisha madai yake kuwa baadhi ya watendaji wa taasisi hiyo muhimu na nyeti wanaripoti kwake kinyume cha utaratibu, kanuni na maadili ya taasisi hiyo.

Kwani tuhuma hizo ambazo Dr Slaa amekuwa akizisema mara kwa mara tangu kipindi cha Kampeni za Urais Mwaka 2010 zimeanza kuaminika, lakini pia zimepelekea wananchi sasa kukosa imani na Taasisi hiyo na zaidi kupoteza imani juu ya uwezo wa serikali kuwalinda na kuwahakikishia Usalama wa maisha yao, ambapo ni jukumu la kikatiba la serikali.

Imetolewa na:- Daniel Zenda.

Katibu wa Wilaya Dar es salaam.

-----------------------------------------------------------------

Hili hapa juu ndilo tamko la CCM mkoa wa vyuo vikuu. Nami kwa mtindo wa majibizano ya blogu, nimejibu hivi:

Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2010, mheshimiwa mmoja wa ngazi ya juu kabisa katika CCM alitamka kwamba CHADEMA wamepeleka vijana wao nje kwa mafunzo ya kuhujumu amani na kwamba vijana hao wameshaingia nchini baada ya mafunzo hayo.

Kauli hii ya mheshimiwa wa CCM ilinishtua, kwa maana mbali mbali, hasa kwa vile ilikuwa inajenga hisia kuwa Tanzania haina ulinzi wa kufaa, na kwamba kama kuna idara ya usalama wa Taifa, basi idara hiyo haiko makini.

Je, nyinyi CCM wa vyuo vikuu mlimsikia mheshimiwa huyu, na je, hamkutambua kuwa amewaambia walimwengu, wakiwemo maadui, kwamba nchi yetu haina ulinzi imara?

Je, mlitoa tamko la kutaka mheshimiwa huyu akamatwe na ahojiwe? Leo mnasema Dr. Slaa ahojiwe, kwa nini msimwunganishe na huyu mheshimiwa wa CCM?

Nyinyi CCM wa vyuo vikuu mnanitia kichefuchefu kwa jinsi mlivyokosa umakini. Mimi nilikuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu Dar kuanzia 1973 na wakati ule nilikuwa katika Umoja wa Vijana wa TANU (TANU Youth League)

TANU Youth League hatukuwa vikaragosi wa TANU. Tulikuwa makini katika kudumisha fikra za mapinduzi, na mara kwa mara tulikuwa tunawapinga wazee wa TANU. TANU yenyewe haikuwa ina msimamo kama wetu, na Nyerere alikiri hivyo. Lakini alituachia tufanya tulivyoamini.

Kwa mfano, tulikuwa tunaendesha jarida liitwalo "Maji Maji," na nendeni maktaba mkaone. Mtaona kuwa hatukuwa vikaragosi wa TANU, kama vile nyinyi mlivyo vikaragosi wa CCM. Wala hamjaonyesha uwezo wowote wa kutafakari masuala ya mwelekeo wa nchi.

Kwa mfano, mnashindwa hata kutafakari suali la msingi la, Je, CCM ni chama cha mapinduzi?

Ingekuwa nyinyi ni wasomi, angalau mngepitia "Azimio la Arusha," "Mwongozo," na maandishi mengine, mkafahamu dhana ya Mapinduzi ambayo wa-Tanzania tulianza nayo enzi za Nyerere, halafu mfananishe na sera za CCM, ambazo ni sera za kuhujumu Mapinduzi.

Kwa kweli, nyinyi CCM wa vyuo vikuu ni mfano hai wa jinsi viwango vya elimu vilivyoporomoka.

Mkitaka kujibizana nami, mjitokeze kwa majina yenu, sio "anonymous," kwani itakuwa ni fedheha ya ziada iwapo wasomi mnajificha namna hiyo. Kwenye mijadala, wasomi tunajitokeza wazi wazi. Nawasubirini.



Saturday, March 16, 2013

Dunia Bila U-Islam

Wiki hii nimenunua vitabu kadhaa. Kimojawapo ni A World without Islam, kilichotungwa na Graham E. Fuller. Na hiki ndicho kitabu ninachotaka kukiongelea hapa.

Nilipokiona kitabu hiki katika duka la vitabu la hapa chuoni St. Olaf, nilivutiwa na jina la kitabu, nikajiwa na duku duku ya kufahamu ni kitabu cha aina gani, na kinaongelea nini. Dhana ya dunia isiyokuwa na u-Islam ilikuwa ngeni kwangu, kwa kuzingatia jinsi dunia ya leo ilivyo na jinsi u-Islam ulivyo na nguvu duniani. Dunia bila u-Islam ingekuwaje?

Ninahisi kuwa hadi hapo, wewe msomaji nawe tayari umeshapata mawazo au hisia fulani. Kama wewe ni mu-Islam, labda umeshaanza kuhisi kuwa kitabu hiki kimeandikwa na adui wa u-Islam. Labda unahisi kuwa kitabu hiki ni mwendelezo wa vita vya Msalaba ("Crusades"). Labda unahisi kuwa ni njama za makafiri dhidi ya u-Islam. Na kama wewe ni mmoja wa wale wanaoitwa wa-Islam wenye msimamo mkali, labda tayari unatamani yafanyike maandamano kulaani kitabu hiki, kama yalivyofanyika maandamano dhidi ya kitabu cha Satanic Verses cha Salman Rushdie.

Kama wewe si mu-Islam, labda ni m-Kristu, huenda una hisia zako pia. Na mimi kama m-Kristu nilikuwa na hisia zangu. Kusema kweli, nilipokiona hiki kitabu, nilihisi kuwa kitakuwa kimeandikwa na mtu ambaye ana ugomvi na u-Islam, na kwamba labda anataka kutueleza kuwa dunia ingekuwa bora endapo u-Islam haungekuwepo.

Hakuna ubaya kuwa na hisia au duku duku, ili mradi mtu uwe na tabia ya kufuatilia ili kujua ukweli. Unapokiona kitabu kama hiki, na hujakisoma, wajibu wako ni kukisoma ili ujue kinasema nini. Sio jambo jema katika taaluma kwa mtu kukumbana na kitu usichokifahamu, halafu ukaendelea na maisha yako bila duku duku ya kujua. Dukuduku hii huitwa "intellectual curiosity" kwa ki-Ingereza.

Duku duku hii ndio inayomtofautisha mtu aliyeelimika na yule asiyeelimika. Mtu aliyeelimika ni yule anayejitambua kuwa upeo wake ni finyu, na kuwa anawajibika kutafuta elimu muda wote. Nimeanza kukisoma kitabu hiki, na tayari nimegundua kuwa anachosema mwandishi si kile nilichodhania, ni tofauti kabisa na kile ambacho labda nawe ulidhania.

Kati ya hoja zake muhimu ni hizi: a) Vita vya Msalaba ("Crusades") vingekuwepo kwa vyo vyote vile, hata bila u-Islam. b) Ukristu wa ki-Orthodox wa Mashariki ungeinukia kuwa na nguvu sana na ungepambana na nchi za Magharibi. c) "Magaidi" wanaojilipua kwa mabomu wangekuwepo, kwani ingawa wengi wanahusisha jambo hili na wa-Islam, ukweli ni kuwa walioanzisha jambo hili ni Tamil Tigers, ambao ni wa-Hindu, kule Sri Lanka.

Inavyoonekana, hiki ni kitabu kimojawapo ambacho kinaelimisha sana. Kinatoa tahadhari mbali mbali kwa wale wanaouwazia u-Islam kwa ubaya.  Kwenye jalada lake, kitabu kimesifiwa sana na maprofesa Akbar S. Ahmed, Reza Aslan, na John L. Esposito, ambao ni wataalam wakubwa wa masuala hayo. Napendekeza tukisome kitabu hiki, kama ninavyopendekeza vitabu vingine katika blogu hii.

Thursday, March 14, 2013

CHADEMA: Taarifa kwa Vyombo vya Habari, Machi 14, 2013

CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 14 MACHI, 2013
Ndugu waandishi wa habari,
Tumewaita hapa leo, ili kupitia kwenu tuweze kutoa taarifa inayohusu kukamatwa kwa mmoja wa viongozi wa chama chetu, Wilfred Lwakatare, Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama, aliyekamatwa jana tarehe 13 Machi 2013, ofisini kwake makao makuu ya CHADEMA.
Jeshi la polisi linasema limemkamata Lwakatare likimtuhumu kuhusika na mashambulio ya watu mbalimbali kutokana na ushahidi uliopo kwenye walioita, viedo ambayo pia imesambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwanza, tunapenda kuwaambia umma wa watanzania na watu wote duniani kwamba, CHADEMA hakina nia yoyote ya kuzuia polisi kutenda kazi zake, iwapo watakuwa wanafanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
Bali, tunachoeleza hapa ni jinsi polisi na vyombo vingine vya dola vinavyoshiriki katika kutengeneza paropaganda chafu dhidi ya CHADEMA za kuwahusisha viongozi wa CHADEMA na unyama unaoendelea nchini wa kutesa watu, kupiga, kung’oa kucha na baadaye kuwatekeleza wakiwa nusu mfu.
Mpango huu ulianza katika tukio la kutekwa kwa Dk. Steven Ulimboka, ukaenda kwa Mwandishi wa habari, Daudi Mwangosi na baadaye kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Absalom Kibanda; na kwa bahati mbaya sana, kwa namna moja au nyingine, mkakati huu umekuwa ukilihusisha jeshi la polisi katika hatua za utekelezaji wake.
Kuweka kumbukumbu sawa, tunaweza kurejea suala la kuuawa kinyama kwa Mwangosi, unyama uliosimamiwa na kufanikishwa chini ya uangalizi wa kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Mara baada ya tukio hilo, jeshi jeshi la polisi kupitia kamishana wake, Paul Chagonja lilitoa kauli kuwa Mwangosi alilipuliwa na kitu alipokuwa anawakimbilia polisi kujisalimisha akitokea kwa wafuasi wa CHADEMA, jambo ambalo limethibitika kuwa halikuwa na ukweli hata kidogo.
Mpaka sasa, jeshi la Polisi halijamchukulia hatua zozote za kisheria Kamhanda aliyesimamia na kufanikisha kifo cha Mwangosi, pamoja na ushahidi wa kuhusika kwake kuwepo wazi.
Aidha, pamoja na ukweli uliobainishwa na tume zote zilizotumwa kuchunguza suala la Nyororo Iringa, kusema Polisi walivunja sheria, walitumia nguvu isiyohitajika, bado mpaka leo hii wanachama 42 wa CHADEMA wanashikiliwa na polisi mkoani Iringa kuhusika na vurugu za Nyololo, Mufindi, Iringa. Waandishi mtakumbuka kuwa Taarifa ya Kamati ya Nchimbi ilitofautiana kabisa na Taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu nay a MCT. Baada ya kazi ya Tume na Kamati hizo hakuna Taarifa hata mmoja imetolewa na Polisi, walsa hakuna watu waliohojiwa tena ukiaachawaliokamatwa kabla ya Taarifa za Tume hizo. Wala sijaona kwa bahati mbaya vyombo vya habari vikichambua Taaarifa hizo kwa kina,
Katika nyakati mbalimbali, CHADEMA tumefungua jalada Polisi, na nyingine amezifungua Mhe. Lwaklatare mwenyewe akilalamikia mchezo mchafu tunaofanyiwa ikiwa ni barua kuandikwa kwa majina yetu, yenye sura ya kutuchafua. Mojawaopo ikidhaniwa kuandikwa na Rwakatare mwenyewe akiomba Tshs 200 millioni kwa ajili ya vijana anaodhaniwa kuwaleta toka Tarime kwa ajili ya Igunga. Hadi leo Polisi hawajamhoji Lwakatare mwenyewe, wala hatujasikia upepelezi wowte ukifanyika.
Aidha tulitoa Taarifa ya mtu aliyepewa bunduki wakati wa uchaguzi wa Igunga akituhumu kuwa amepewa bastola hiyo kwa lengo la kudhuru wakati wa Kampeni ya Igunga. Tumetoa mpaka nay a Bastola husika na mahali ilipotengenezwa. Polisi hadi leo hawajatoa Tamko lolote kama Bastola hiyo iliyotengenezwa China imesajiliwa kwa jina la nani, na hivi sasa ipo kwa nani. Lakini kwa tukio tu la Lwakatare na picha yake kubandikwa kwenye Mtandao, Polisi tayari wameisha kumkamata. Ni dhahiri kuna mchezo unachezwa dhidi ya CHADEMA, na Polisi kuiingizwa au kwa kujua au kutokujua katika mtego huo.
Sasa hapo mnaweza kujiuliza, hapo haki ipo wapi? Yaani waliotajwa na tume yaani polisi – wapo huru, lakini wanaCHADEMA 42 ambao hawakutajwa popote na tume wanasota gerezani.
Hata katika suala la Dk. Ulimboka, jeshi la Polisi halikutelekeza wajibu wake kikamilifu. Jeshi hilo limekataa kumhoji Dk. Ulimboka na wala kuwahoji baadhi ya watuhumiwa wakuu wanaotajwa kuhusika moja kwa moja katika kumteka Dk. Ulimboka, akiwemo Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka, Afisa wake Ramadhani Ighondo mwengine anayeitwa Nzowa.
Vilevile, kwenye tukio la kutekwa kwa Kibanda, ambalo linafanana kwa kiasi kikubwa na lile la Dk. Ulimboka, Afisa Mtendaji Mkuu wa New Habari Corporation, Hussein Bashe, ametaja kuhusika kwa polisi katika utekaji wa Absalom Kibanda, na baadaye akamtaja Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, lakini mpaka sasa, jeshi la Polisi halijachukua hatua zozote ama kwa waliotajwa au kwa aliyetaja.
Lakini katika hili la Lwakatare CHADEMA kilipata taarifa mapema kuwa upo mkakati unaoratibiwa na kufanikishwa na Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jack Zoka na genge lake lenye wajumbe mashuhuri, Ramadhani Ighondo na Nzowa linalotaka kukihusisha CHADEMA na njama za kumdhuru Kibanda ili kukidhoofisha kisiasa. Lilipotokea hili la Lwakatare tukasema, sasa kile tulichoambiwa ndiyo hicho kimekuja.
Bahati njema gazeti la Mwananchi la leo linasema Lwakatare anatuhumiwa kupanga njama za kumdhuru Mhariri wa gazeti hilo, Denis Msacky, na kwamba Lwakatare amekamatwa baada ya kuonekana kwenye video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii haraka inayomuonyesha Lwakatare akipanga njama hizo hatujui baadhi ya taarifa zingine ingwa kwa hiki kilichopo kwenye mtandao hakuna popote alipotajwa Msaky. Si nia yangu kuingilia upelelezi wa Polisi, lakini nimesema CHADEMA tumefurahi kwa kuwa iwapo kwa utaratibu huu au wowote ule fursa itapatikana na ukweli wote kutolewa hadharani. Ni imani yangu kuwa zoezi hili litafuata sheria na taratibu zote zilizokwa na Katiba yetu kulinda haki za mtu.
Sasa kutajwa kwa Msacky inawezekana hilo la Kibanda halijaiva, au pengine liko njiani; ama wameona aibu kuliingiza kwa sasa.
Lakini Waandishi wa Habari, mnajua kuwa mara baada ya Kibanda kutekwa, Ridhiwani Kikwete na Nape Nnauye walivyoshangilia kutekwa kwa Kibanda katika mtandao huo huo uliotumika kumkamata Lwakatare bila kuwakamata wahusika hao ambao waliingia kwenye mtandao kwa ID yao wenyewe. Akiandika katika mtandao wake wa face book Ridhiwani alisema: “Na hili la Kibanda mtasema ni kazi ya Ramadhani Ighondo, afisa usalama pale Ikulu?”
Kwanza, kauli hii ya Ridhiwani ilikuwa inathibitisha kwamba aliyepanga njama za kumteka Dk. Ulimboka, ni Ramadhani Ighondo wa Ikulu.
Pili, Ridhiwani alikuwa anataka kuaminisha jamii kwamba katika hili la Kibanda, yeye na kundi lake hawahusiki, bali wanaohusika ni CHADEMA; hivyo akawa anachokoza mjadala ambao ulishapangwa ili baadaye vyombo vya dola viweze kuuchukua, na hivyo ndivyo ilivyotokea.
Tunazo taarifa kutoka vianzio vyetu vya ukakika ndani ya Usalama wa Taifa kuwa baada ya Ridhiwani kuweka andishi lake kwenye facebook, aliingia kiwewe sana hasa baada ya Hussein Bashe kuja juu. Ridhiwani anafahamu nguvu ya Bashe kwenye kufuatilia suala la kutekwa kwa Kibanda na hivyo amemuomba baba yake kuvitumia vyombo vya dola kumuokoa. CHADEMA haijawa na haitakuwa, lakini tuliyoambiwa yametimia, na mengine zaidi yanakuja, kwani kwa Taarifa zetu hiyo yaliyotokea “ni cha mtoto”. Na wala hatutaki kutabiri mbinu zitakazotumika kumwokoa.
Ndugu waandishi wa habari; katika mlolongo wa kuwakamata viongozi wa CHADEMA, yumo Mbunge wa Iringa, Mchungaji Msigwa. Mheshimiwa Msigwa tunaambiwa na watu wetu wamemtafuta kwa muda mrefu sasa. Wanasema sumu anazotema bungeni na kwengineko dhidi ya idara ya usalama ya taifa juu ya tuhuma za kuhusishwa na wizi wa nyara za serikali, zinawanyima usingizi na hivyo wanataka wamnyamazishe.
Wanataka kujua kutoka kwa Msigwa ni nani aliyevujisha na kumpa taarifa zile za ujangiri wa wanyama pori zinazohusisha CCM, usalama wa taifa, polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Msigwa anaonekana kuwa ni jasiri kusemea udhaifu wa idara ya usalama, wanaamini anavyo vitu vingi na wao wangependa wajue ana nini na anapewa na nani.
Tayari Mchungaji Msigwa ameondolewa kwenye kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira na kupelekwa Kamati ya Kilimo ili kulinda uchafu wa serikali, wakati yeye ni waziri kivuli wa Maliasili na Utalii na Waziri kivuli anatakiwa kuwa Kwenye Wizara ya Sekta anayoisemea, na wala hajaomba Wizara ya Kilimo.`ni dhahiri syndicate ya mfumo huu wa kutaka kuisambaratisha CHADEMA. Huhitaji kwenda chuo Kikuu chochote, kuelewa hili.
CHADEMA kinafahamu kwa undani, kwamba uzushi huu wa Tape ya “Bukoba Boy”.Tunajua huu umeanzishwa na kuhusisha Usalama wa Taifa, akiwemo Ighondo na wenziwe pale Ada Estate. Huyu Ighondo ambaye anafahamika pia kwa jina la “Rama” tunamfahamu vizuri sana. Aliwahi kufanya kazi ya katibu wa UV-CCM wilaya ya Singida Vijijini, kati ya mwaka 2006 na 2008 na ndiye aliyekuwa akitumia simu na 0713760473 katika mawawsiliano yake na Dr. Ulimboka kwa simu na 0713731610 mpaka takriban dakika 3 kabla ya Ulimboka kutekwa. Gazeti la Mwanahalisi liliandika taarifa ya uchunguzi ya kina ya Jambo hilo.
Rais wetu amenukuliwa na magazeti ya Serikali Addis Ababa akisema kuwa Mwanahalisi ilifungiwa kwa sababu ya ‘kuchochea uasi katika majeshi yetu’ au maneno Kama hayo. Sitaki kumwita Rais wetu wwongo leo lakini kwa kuwa Taarifa hiyo haijakanushwa wala na Rais, wala na Ikulu, tunaamini maneno hayo ni kweli ametamka. Tunamtaka Rais Kikwete atamke maneno hayo hayo hapa nchini. Kwa njia yeyote ili ili Watanzana wengi na hasa wasomaji wa Mwanahalisi, na hata majeshi yetu amba kimsingi ninafahamu walilipenda Gazeti la Mwanahalisi wamsikie kwa masikio yao wenyewe. Taifa linawekwa pabaya sana Rais anapofikia kutoa matamko ya upotoshwaji mkubwa kiasi hicho tena nje ya nchi.
Ndiyo maana tunaposema Idara ya Usalama wa Taifa, ni tawi la CCM, tunaushahidi. Kwa mfano, tunajua jinsi baadhi ya watendaji wajuu wa idara hiyo kama vile, Zoka na vibaraka wake wadogo akiwamo Ighondo, ni radical wa CCM, wenye ushabiki uliopitiliza.
Hata ukiangalia jinsi walivyotekeleza mpango wa utekaji wa Dk. Ulimboka, kwamba walifanya hivyo mbele ya macho ya Dk. Deogratias Michael, haraka utabaini kuwa utekaji huu ulifanywa kwa ushabiki wa kulinda CCM.
Ndugu waandishi wa habari, kutokana na yote hayo hayo sasa tunasema ifuatavyo: Kwamba jeshi la polisi lifanye kazi yake bila ushabiki wa kisiasa au shinikizo la wanasiasa.
Ndugu Waandishi,CHADEMA haiko tayari kuruhusu watu wenye maslahi binafsi kutuchafua mbele ya jamii. Katika hilo, tutapambana na yoyote bila kujali cheo chake, madaraka yake serikalini, fedha alizonazo au madaraka mengine.
Wakati polisi wakitekeleza hilo, tunamtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, ajitokoze hadharani kueleza umma juu ya mgogoro wake na Kibanda. Tunavyofahamu sisi, Kibanda aliteuliwa kuwa mjumbe katika kamati ya kubuni vazi la taifa. Lakini alijitoa na kusema aliyemteuwa yaani - Nchimbi - ambaye wakati huo, alikuwa waziri wa habari, utamaduni na michezo, ndiye aliyeshinikiza polisi kumfungulia kesi ya uchochezi mahakamani.
Hadi sasa hatujapata taarifa za wazi zinazoonyesha kama uadui wa wawili hawa uliisha, na kwamba Nchimbi sasa ndiye waziri wa mambo ya ndani, ambapo polisi wanawajibika kwake. Tuna mashaka kuwa uchunguzi wa tukio lililomkuta Kibanda unaweza kudhoofika.
Kutokana na hayo yote CHADEMA tunasema nini sasa:-
i) CHADEMA katika hatua hii ya awali, tunafuatilia kwa karibu sakata lote la ukamataji wa Lwakatare na kuona kama sheria za nchi, taratibu mbalimbali na misingi ya Haki za Binadamu inafuatwa kuikamilifu.
ii) Tunarudia tena madai yaliyotolewa mara nyingi na CHADEMA, kwa Rais kuandikiwa barua na Mwenyekiti wetu, Iundwe Judicial Commission of Inquiry (Tume Huru ya Kimahakama kuchunguza vifo vyote vyenye utata na sura ya kisiasa). Serikali inaogopa nini kuunda Tume hii huru ili ukweli Ujulikane? Iweje CHADEMA inayotuhumiwa Kupanga njama wanaishinikiza Serikali kuunda Chombo huru na Serikali ndiyo inayopata kigugumizi?

iii) Kwa wale walioumizwa na kujeruhiwa kama kina Ulimboka Kibanda na wengine, tunarudia Tamko letu la kuwa hatuna Imani na uchunguzi unaofanywa na Jeshi la Polisi kwa kuwa viongozi wa Jeshi hilo ni sehemu ya watu tunaowatuhumu kwa kuhusika kwa njia mbalimbali, na Ushihidi wa wazi na Taarifa mbili za Serikali kupingana yaani Taarifa ya Kamati yqa Nchimbi na Tume ya Haki za Binadamu. Tutaiaminije Polisi na Serikali kwa Taarifa ya Kamati ya Nchimbi? Mwendawazimu tu anaweza kuwa na imani baada ya Taartifa zile 3.
iv) Kuokana na upotoshwaji mkubwa, na kutokana na uhakika tulionao mkubwa Mwanahalisi ilifungiwa si kwa sababu yeyote ile, bali kutoka na kukomalia swala la Dr Uliomboka na hasa uhusika wa Ighondu, Afisa Usalama anayefanya kazi Ikulu chini ya Raisi mwenyewe. CHADEMA sasa tunaitaka rasmi Serikali ifungulie Gazeti nla Mwanahali kwa sababu hatuwezi kuendelea kuvumilia uikandamizaji huu wa uhuru wa Habari, ambao sasa unaelekea kuota mizizi nchini kwetu. Na kweli ninawaomba na kuwataka waandishi wote msimame imara, bila kujadili itikadi, au tofauti zetu zozote zile na kusimamia uhuru wa Habari. Tunataka vivyo hivyo, kwa wanaharakati mbalimbali. Waache hofu, eti wanaogopa kuhusishwa na vyama vya Siasa! Haki ni haki na haina rangi ya bendera ya chama chochote.
Ndugu Waandishi Nawashukuru sana
Imetolewa Makao Makuu ya CHADEMA, na,

Dr. Willibrod P. Slaa
KATIBU MKUU - CHADEMA

Tuesday, March 12, 2013

Mabucha, Mto wa Mbu

Nilipiga picha hii hapa kushoto kwenye mtaa mmoja wa Mto wa Mbu. Nilivutiwa na mwonekano huu: safu ya mabucha na pia akina mama wakiwa wamejitokeza tu hapo mlangoni  na kuelekea walikokuwa wanaelekea.

Nilitafakari suala la haya mabucha, ila sikupata fursa ya kuongea na yeyote kuhusu suala hilo. Sikuweza kujua kama wenye mabucha hayo ni akina nani.

Miezi mingi iliyopita, kulikuwa na taarifa za mgogoro Mto wa Mbu baina ya wa-Kristo na wa-Islam. Sikufuatilia undani wa tatizo, isipokuwa haikuwa taarifa njema, kwani migogoro si jambo jema.

Taarifa hii ilinigusa kwa namna ya pekee kwa sababu nilishafika Mto wa Mbu mara kadhaa na nafahamiana na baadhi ya watu wa pale. Mimi kama mgeni nilikuwa na hisia kuwa Mto wa Mbu ni mji uliotulia sana. Sikutegemea mgogoro wa aina ile. Hayo yote yalinijia kichwani wakati napiga picha hii.

Monday, March 11, 2013

Maktaba ya Karatu

Wadau wa blogu yangu hii watakuwa wanajua jinsi ninavyoleta taarifa za maktaba mbali mbali, hasa zile ninazopata fursa ya kuzitembelea. Mfano ni taarifa hii hapa.

Mwaka huu, tarehe 7 Januari, nilipata fursa ya kuiona maktaba ya Karatu. Nilikuwa njiani kuelekea kwenye uwanja wa mnada, lakini papo hapo nilitaka kuiona maktaba. Kuna kibao nilikiona wakati natembea, kikielekeza iliko maktaba.

Nilipofika hapo nilipiga tu hii picha, nikaendelea na safari yangu ya mnadani. Maktaba iko juu kwenye sehemu ya mwinuko ambao nadhani ndio juu kabisa pale Karatu. Sikuingia ndani. Nikifika tena Karatu, nitaweka kipaumbele kuingia humo na kuona ilivyo. 


Saturday, March 9, 2013

Matokeo Zaidi ya Mhadhara wa Faribault

African Folk Tales

When Joseph Mbele visited our class last week, one of the things he talked about is how folk tales can be so very valuable in learning about a culture. He said that's a way to understand what's important and what a culture sees as valuable and moral.  It made me very happy that I had already planned to make (force?) each student in my Humanities of South Africa class to present a South African Folk Tale to the rest of the class.

Joseph Mbele has a book of folk tales himself, which I am purchasing as soon as I get my next paycheck: Matengo FolktalesThese folk tales are from Tanzania, and I can't wait to read this.

Since we're studying South Africa, however, I found this book:
 Each student will get one folktale to present to the class through any means they choose:
storytelling
a skit (collaboration is encouraged)
a video/film
a powerpoint with appropriate pictures while telling...maybe even reading in that case
anything else they can think of.
Some of the stories include the following (Aren't the pictures spectacular!!??)





Nelson Mandela's Favorite African Folktales was published by W.W.Norton&Company in 2002.
I can't list all the contributors or artists, but the book is worth checking out.Everything is copyrighted, so I only gave you a little sampling here.
I can't wait to see what my students do with these stories! 


Thursday, March 7, 2013

Utalii wa Kiutamaduni Unakuza Uchumi Haraka



Hapa ni ndani ya kituo cha utamaduni cha jiji la Arusha
 Na Albano Midelo

UTALII wa kiutamaduni bado ni nadharia changa katika nchi za ulimwengu wa tatu ikiwemo Tanzania,kutokana na ukweli kuwa katika nchi hizo wamezoea kuona utalii wa asili wa kutembelea mbuga za wanyama.

Utalii wa kiutamaduni ni nadharia mpya hapa nchini ambapo serikali imeanza kuutambua utalii wa kiutamaduni na kuupa nguvu kubwa aina hiyo ya utalii miaka ya hivi karibuni,zamani vivutio vya utalii wa kiutamduni kama majengo ya kale,maeneo ya kihistoria na makumbusho hayakupewa mtazamo wa kiuchumi zaidi.

Maeneo hayo yalipewa mtazamo wa kielimu zaidi na kuundwa idara za mambo ya kale na idara ya makumbusho ambazo zote awali zilikuwa katika wizara ya elimu na utamaduni ambavyo viliwekwa kama vyanzo vya elimu zaidi kuliko vyanzo vya utalii kwa sababu wakati ule  watalaamu walifanya tafiti mbalimbali za mambo ya kale wakiwemo wakina Dk.Leakey


Hata hivyo baadaye kulikuwa na mabadiliko katika ulimwengu mzima hali iliyosukuma kuwepo kwa utalii wa kiutamduni na nchi zilianza kutoa kipaumbele katika utalii wa kiutamaduni ndiyo maana hapa nchini idara za mambo ya kale na makumbusho zilihamishwa kutoka wizara ya elimu na kuingia katika wizara ya utalii na maliasili.


 Utalii wa kiutamadini hivi sasa unakuwa na  hata mabadiliko ya utalii huo hayawezi kuonekana kwa haraka badala yake inatakiwa watalaamu kuwahamasisha wananchi kutambua fursa zilizopo katika aina hiyo ya utalii na kuzitumia ipasavyo fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo wao binafsi na Taifa kwa ujumla wake.


Ni vigumu sana kutenganisha utalii asili na  utalii wa kiutamduni kutokana na aina hizo mbili za utalii kuwa na mahusiano ya karibu.Watalii wanapoingia nchini wote wanavutika na utalii wa aina zote mbili  .


Mtalii anapokwenda kutembelea utalii wa asili kama mbuga za wanyama pia anaweza kupita katika maeneo yenye utalii wa kiutamaduni na kwamba fursa ya utalii wa kiutamaduni ni kubwa kwa wananchi wa kawaida kuliko aina nyingine za utalii.


Mhadhili msaidizi kutoka idara ya utalii wa kiutamaduni chuo kikuu kishiriki cha Tumaini Frank Kimaro anabainisha kuwa  utalii wa kiutamaduni unazungumzia jamii husika na kwamba jamii hiyo inaweza kufaidika kutokana na utalii wa kiutamaduni ambao unapatikana katika eneo husika hadi kufikia hadi ngazi ya kitaifa.

“Unaweza kuona aina hii ya utalii ni tofauti na utalii wa asili ambao tunaangalia zaidi mbuga za wanyama na maeneo ambayo yametengwa na serikali ambapo wahusika wakubwa ni serikali yenyewe na siyo watu binafsi,katika utalii wa kiutamaduni wahusika wakuu ni  wananchi wenyewe”,anasisitiza  na kuongeza


“Wananchi katika utalii wa utamaduni wanaweza kunufaika kuanzia kiwango cha familia, mtaa, kitongoji,kijiji,wilaya,mkoa na kitaifa kwa hiyo utalii wa kiutamaduni unatoa fursa kubwa sana ya ukuaji wa uchumi kuanzia kwa mtu binafsi hadi kwa taifa”


Licha ya utalii wa utamaduni kuonekana kumlenga zaidi mwananchi wa kawaida ,lakini kipato anachopata mwananchi huyo kwa kucheza ngoma au kuuza bidhaa za jadi na kazi nyingine za mikono kipato chake kimekuwa cha chini na kuwakatisha tamaa wananchi.


Kimaro anasema kuwa vitu anavyovifanya mwananchi katika utalii wa kiutamaduni vina thamani kubwa kuliko mapato anayopata na kwamba katika hali ya kawaida vitu vya utamaduni vina thamani kubwa  na vikiachwa kupotea haviwezi kupatikana tena na kwamba hakuna kiwango cha malipo kamili kwa shughuli za utalii wa kiutamaduni.


Hata hivyo Kimaro anasema kuwa  utalii wa kiutamaduni unaweza kubadilisha kiwango cha maisha ya watu kutokana na kupata kipato kutokana  na kazi hiyo kuwa shughuli mbadala ambayo inawasaidia wao kuwaongezea kipato cha ziada katika mapato yao.


Anabainisha kuwa kabila la wamasai katika msimu wa utalii wa kiutamaduni wanapata mapato karibu shilingi 30,000 kwa siku kutokana na aina hiyo ya utalii jambo ambalo linaonesha kuwa ni kipato kikubwa ukilinganisha na vijana wengine mijini ambao wanaingiza kipato kidogo sana.


Bidhaa zinazotokana na utalii wa kiutamaduni kama samani zilizotengezewa kwa miti pamoja na sanamu za kuchonga zimekuwa zinauzwa na watu binafsi kwa watalii na wageni wengine kwa bei za juu sana kwa mfano kiti kinachotengezwa kwa kutumia miti ya mianzi kinauzwa kati ya shilingi 200,000 hadi 300,000,


kofia inayotengenezwa kwa ukindu inauzwa kati ya shilingi 3500 hadi 5000,mkanda unaotengenezwa kwa ngozi  yenye shanga unauzwa kati ya shilingi 5000 hadi 10,000,kigoda kilichotengenezwa kwa mti wa kawaida kinauzwa kati ya shilingi 10,000 hadi 15,000 wakati kinyago cha kuchongwa kinauzwa kuanzia shilingi 20,000 hadi 500,000 kutegemea na ukubwa wa kinyago hicho.


Hata hivyo amesema bei ya mtengenezaji ni ndogo ambapo muuzaji wa mwisho ndiyo anayepata faida kubwa kwa kuwa anauza kwa bei ya juu zaidi  na kwamba mnunuzi wa kati anakwenda kutafuta vitu hivyo sehemu ambazo mzalishaji anauza kwa bei nafuu ili na yeye aweze kuuza kwa bei ya juu  ili kufidia gharama za usafiri, uchukuzi, uhifadhi na malazi.


Nafasi ya utalii wa kiutamaduni ni kubwa katika kukuza uchumi wa nchi  kutokana na ukweli kuwa utalii unachangia uchumi wa Tanzania katika kiwango kikubwa  na kuchukua nafasi ya pili hivyo utalii endelevu una nafasi kubwa katika kuleta maendeleo endelevu.


Kulingana na mhadhili huyo utalii huo pia una nafasi kubwa ya kuchangia uchumi wa watu binafsi kwa sababu utalii unatengeneza ajira za moja kwa moja na ajira ambazo sio za moja kwa moja ambapo  watanzania wengi hivi sasa wamejiajiri katika shughuli za utalii wa kiutamduni ambao wamefungua maduka ambayo wanauza vitu vya kiutamaduni vyenye bei kubwa zaidi katika soko la utalii.


“Soko la vitu vya utamaduni wa kitalii vinatoa ajira kwa watu wengi wakiwemo mwenye duka,mtengenezaji na msambazaji hivyo kufungua fursa za ajira za moja kwa moja kwa wananchi ambapo watu wengine wananufaika na utalii wa utamaduni kutoka kwenye migongo ya watu walioajiriwa  moja kwa moja katika sekta hiyo’’,anasisitiza.


Anawataja watu wanaonufaika katika sekta ya utalii wa kiutamduni kutoka katika migongo ya watu wengine kuwa  ni pamoja na watu wenye hoteli,nyumba za kulala wageni,watu wanaouza maji na vyakula mbalimbali na kwamba  utalii huo unafungua milango ya ajira.


Uchunguzi umebaini kuwa katika ulimwengu hivi sasa kuna nchi nyingi ambazo zimekuza uchumi wake kwa haraka kupitia utalii wa kiutamaduni zikiwemo Australia,Ujerumani,Uingereza pamoja na nchi nyingine nyingi za ulaya ambazo kutokana na ukosefu wa mbuga za wanyama wengi kama zilivyo katika Afrika wameamua kuendeleza utalii wa kiutamaduni zaidi kuliko utalii wa asili na kupata maendeleo makubwa kupitia aina hiyo ya utalii.


Kutokana na hali hiyo watanzania na wadau wote wa utalii wanatakiwa sasa kubadilika kimawazo na kifkra kutoka   katika aina ya utalii wa asili ambao ni kuangalia wanyamapori na na kuingia katika utalii wa kiutamaduni ambao ni wa kipekee kwa kuwa  hutofautiana  kutoka eneo moja kwenda eneo jingine na watalii kupata vitu vipya hivyo kuvutika zaidi .



albano.midelo@gmail.com, 0766463129.

CHANZO: Blogu ya Maendeleo ni Vita



Wednesday, March 6, 2013

Mafanikio ya Mhadhara Wangu Faribault

Nilishaleta taarifa kuhusu mhadhara niliotoa katika chuo cha South Central, Faribault. Mhadhara ulihusu kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mhadhiri aliyekuwa mwenyeji wangu, Rebecca Fjelland Davis, ameandika taarifa ifuatayo katika blogu yake, akaambatisha pia uchambuzi wa kitabu aliouandika kwenye mtandao wa Goodreads:

Joseph Mbele's book AFRICANS AND AMERICANS




Our class, "Culture and History of South Africa,"  read Africans and Americans: Embracing Cultural Differences last week. The author, Joseph Mbele came to visit us on Tuesday. It was unanimously considered a DELIGHT.

The book is a fast read, and Joseph Mbele writes in a conversational, welcoming style that sucks you right in, keeps you laughing, and keeps you reading. 

In person, Joseph proved to be one of the most brilliant, funny, warm, and gentle human beings I've ever met. My students loved him; the two hours with him flew past.


Africans and Americans: Embracing Cultural DifferencesAfricans and Americans: Embracing Cultural Differences by Joseph L. Mbele
My rating: 5 of 5 stars

This was the most delightful read about the differences between Africans and Americans and how we relate to each other. My students loved it, found it fascinating, and flew through it.


If you have students, friends, neighbors, classmates, ANYBODY you know from Africa, this book is for you. If you are traveling to Africa, like my students and I are, it's a MUST.

Best part? Now whenever I am late (no, that never happens), I can say I'm on AFRICA TIME.

View all my reviews

Monday, March 4, 2013

Wazazi Wamefurahia Kijana Wao Kwenda Tanzania

Siku kadhaa zilizopita, niliandika ujumbe wa shukrani kwa mafanikio ya kozi niliyofundisha Tanzania mwezi Januari juu ya mwandishi Ernest Hemingway. Nilikuwa na wanafunzi 29 wa chuo cha St. Olaf. Leo nimepata ujumbe kutoka kwa wazazi wa mwanafunzi mmojawapo, ambao ninauleta hapa. Nimebadili jina la mwanafunzi, na ninamwita Kijana:

Dear Professor Mbele --

We want to thank you so very much for all you have done for our son, Kijana! He absolutely loved the recent trip to Tanzania. We thank you for giving him the opportunity to experience the rich culture of your home country. Kijana came back a different person--a better person--for all he was able to experience. You have given him a very valuable gift. He also truly enjoyed learning about Hemingway. thank you again for taking Kijana and the other students on the adventure of a life time. We hope to meet you sometime! 

Sincerely, 

Father and Mother of Kijana.

----------------------------------------------------------------------------------------------------------------------
Sababu moja ya kuuweka ujumbe huu hapa ni kwamba ni kielelezo cha manufaa yanayoweza kutokana na huu utaratibu uliopo katika vyuo vingi vya Marekani wa kupeleka wanafunzi nchi za nje. Inafahamika kuwa, mbali na somo wanaloenda kusoma, au masomo wanayoenda kusoma, ni fursa kwa vijana kupanua upeo wao wa kuifahamu dunia na tamaduni zake. Ni maandalizi kwa vijana hao kwa maisha yao ya baadaye katika ulimwengu huu unaoendelea kufungamana kwa kasi katika mchakato wa utandawazi.

Insha Allah, nitatafuta fursa nyingine  nielezee faida ya programu hizi kwa nchi zinazowapokea hao wanafunzi, kama vile Tanzania.




Saturday, March 2, 2013

Kimahama Literature Centre, Arusha

Kati ya maduka ya vitabu yaliyoko Tanzania, kuna moja mjini Arusha liitwalo Kimahama Literature Centre. Sikumbuki ni lini nilianza kusikia jina la duka hili, ila nakumbuka kuwa miaka zaidi ya kumi iliyopita, uongozi wa duka hili ulinunua kutoka kwangu nakala za kitabu changu cha Matengo Folktales. Kama nakumbuka vizuri, walinunua nakala 20. Baadaye nilipata taarifa kuwa zote zimeuzwa.









Siku nyingine, miaka michache iliyopita, nilijikuta tena ndani ya Kimahama Literature Centre kama ilivyo kawaida yangu, kutembelea maduka ya vitabu. Meneja alikuwa mpya. Katika maongezi, nilipomwambia kuwa nimechapisha kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, alinunua nakala kadhaa kutoka kwangu.

Mwaka huu, niliona kitabu hiki kinauzwa hapo, nikapiga picha hiyo hapa kushoto. Kuwepo kwa kitabu hiki katika duka hili kuliwahi kuelezwa na mwanablogu Bwaya katika blogu yake.

Hizi ndizo baadhi ya kumbukumbu zangu za duka hili. Kitu kimojawapo kilichonigusa ni kuona wahusika wa duka la vitabu wakiwa ni wapenda vitabu. Ni muhimu sana kwa wauza vitabu kuwa wapenda vitabu. Vinginevyo ni kujidanganya. Nimegusia suala hili katika kitabu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii, kurasa 30-32.

Duka la Kimahama Literature Centre liko katika jengo hili linaloonekana pichani, ambalo linatazamana na hoteli ya Golden Rose. Ni usawa wa chini kabisa wa hilo jengo, hapa yalipopaki magari.

Friday, March 1, 2013

Yatokanayo na Mhadhara Wangu Mjini Faribault

Sikupenda kuelezea kirefu mafanikio ya mhadhara niliotoa katika chuo cha South Central, mjini Faribault kwa wanafunzi na maprofesa wanaojiandaa kwa safari ya Afrika Kusini. Niligusia tu kuwa mhadhara ulikuwa mzuri. Undani wa kilichotokea ni habari ambayo nataka niwaachie waliohudhuria waelezee.

 Kwenye ukurasa wa Facebook, Profesa Becky Davis aliweka picha ambayo nimeiazima hapa, na pia aliandika hivi:

Joseph Mbele spoke with us this morning. What a generous spirit, and what a delightful and humorous speaker!

 Kwa upande wangu, mihadhara ya aina hii ninaitoa mara kwa mara, kwenye vyuo, taasisi na jumuia mbali mbali hapa Marekani. Msingi wake ni yale niliyoandika katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Mialiko hii inatoka zaidi kwa waMarekani ambao wanapangia safari ya Afrika au wanashughulika kwa namna mmoja au nyingine na waAfrika, iwe ni barani Afrika au hapa hapa Marekani.

Watu hao, ambao ni wengi sana, wakishasoma kitabu hiki wanapata hamasa ya kunialika nikaongelee masuala husika na hapo tunapata fursa ya kwenda ndani na mbali zaidi ya pale nilipofikia katika maelezo yangu kitabuni. Nimewaheshimu wa-Marekani hao,  kwa ari yao ya kujielimisha kuhusu tofauti za tamaduni kama njia ya kuboresha mahusiano na pia kujihakikishia mafanikio katika shughuli zinazowajumuisha na tamaduni tofauti.

Napenda nimalizie kwa kutoa ujumbe kwa wengine. Kila ninapopata mwaliko wa kutoa mihadhara hiyo, nahikikisha nimejizatiti ipasavyo ili kutoa mchango wa kiwango cha juu. Kwa namna hiyo, nawapa faida wahusika, na kisha wao wanakuwa wapiga debe wangu. Msingi mkuu wa mafanikio ni juhudi na umakini.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...