Wednesday, November 30, 2011

Makafiri

Ingawa watu wengi wanaamini kuwa masuala ya dini ni hatari kujadiliwa, blogu yangu haina kipingamizi kwenye kujadili masuala hayo, kama ilivyo kwa masuala mengine. Kama kuna tatizo, tatizo haliko kwenye mada, bali tatizo ni wahusika, kama nilivyoandika hapa.

Leo napenda kuongelea suala ambalo limenikera kwa muda mrefu. Ni suala la watu kuwaita wengine makafiri. Nimeshasoma taarifa kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania ambazo zimenifanya niandike ujumbe huu.

Leo katika mtandao wa Facebook, nimeona taarifa kutoka Mbeya ambamo mtu analalamika kuwa kuna makafiri sana kule. Miezi kadhaa iliyopita, nilisoma taarifa kutoka Zanzibar, kwamba watu wa kijiji fulani walikuwa hawataki makafiri kwenye eneo lao. Ukipita mtandaoni, utaona kuwa jadi hii ya kuwaita wengine makafiri inajitokeza mara kwa mara miongoni mwa watu wa Visiwani.

Sijui hao wanaowaita wengine makafiri walipata wapi uwezo wa kufahamu undani wa watu wengine kiasi hicho. Nilidhani kuwa sote tunaosema tunamwamini Mungu tunafahamu kuwa mwenye uwezo wa kumhukumu binadamu, uwezo wa kujua yupi ni kafiri na yupi si kafiri, ni Mungu tu.

Hatujui ya Mungu, na bora tuwe wanyenyekevu. Hao wanaowaita wenzao makafiri huenda Mungu anawajua kuwa ndio makafiri wenyewe. Binafsi siwezi kumtambua kafiri, kwa sababu sina njia ya kuona yaliyomo moyoni au akilini mwa yeyote. Sithubutu kumwita yeyote kafiri, kwani nitaona kuwa kufanya hivyo ni kufuru, yaani kujifanya mimi ni Mungu.

6 comments:

Goodman Manyanya Phiri said...

Nimeipenda mada hii kwa sababu mbili

1. Ni ujinga mtupu kwamba dini haistahili kuongelewa.

2. Mambo ya kunyanyaswa kwa wengine kama makafiri yanikumbusha maneno nilieyasoma pahala kuhusu wasenge.

Maandishi yenyewe yalieleza kwamba baadhi ya wale wanaolaani vikali usenge nao ni wasenge wenyewe.


Lakini nikirudi nyuma kidogo juu ya neno "kafiri". Nilichoweza kukipata hadi leo ni kwamba chimbuko la neno hili halikuwa baya. Bali liliamanisha mswahili wa kwanza aliekuwa na dini yake ya mwanzo kabisa bila kutaka kuichang'anya na Uislam. Makafirki enzi hizo waliheshimika sana kama watu wenye kujigamba na kujiamini katika dini yao ya jadi.

Kwa namna ingine mtu anapokutaja wewe "kafiri" anakupa sifa kwani ingawaje Mwenyezi Mungu wetu ni mmoja tu hamna hata dini mmoja tu ni yenye ukweli wa kutupeleka Kwake, bali roho na moyo wake mtu binafsi.

Kwa hiyo uniite Kafiri usiniite Kafiri ukweli wa mambo ni kwamba tunajuwana mie na Mungu wangu niko wapi na imani yanug Kwake!

Anonymous said...

Profesa sijaingia muda mrefu kidogo ktk net Ihope unaendelea vizuri na majukumu.
Hili neno la "kafir"watu hulitumia kama kumtusi mtu lakini nyakati za zamani nadhani lilitumika kama kutofautisha watu waliokuwa wanamtambua mungu na mtume Muhammad(saw)na wale wasiomtambua.Vilevile neno hilo "kafar"yaani wasioamini mungu.

Lakini tukija ktk jamii yetu utakuta watu wanachuki za kisiasa na kutumia hili neno.Mimi nadhani watu wa visiwani walitakiwa kufahamu kwamba serikali ndio yenye matatizo na sio wananchi.Ni vizuri watambue hilo kwa maana hata nikisoma mtandao wao hutumia lugha sio nzuri.Hawana ufahamu ya kuwa hata huku bara watu vilevile wapo wachofu na hiyo serikali.

Naomba Profesa angalia hii clip ni fupi tu ina topic ya Kafir

http://www.youtube.com/watch?v=YhopfqEJLnQ

Khalfan Abdallah Salim said...

Japokuwa maoni yangu yamechelewa lakini si kitu.

Neno kafiri mzizi wake ni Kiarabu, likiwa na maana ya 'kukataa'. Katika Sheria ya kiislamu, Kafir ni mtu yeyote ambaye baada ya kubainishiwa ukweli juu ya Uislamu na mafunzo yake kwa dalili (au hoja) zilizowazi, akakataa kufuata Uislamu.

Neno hilo haitwi kila asiye Muislmu kama ambavyo waislamu wengi wanavyolitumia, bali ni jina lenye kubeba hukumu ya Kisheria, kuwa mtu huyu amekataa ukweli juu ya Mola na dini yake aipendayo baada ya kubainishiwa.

Ifahamike kuwa wapo 'waislamu' ambao kwa kukataa kwao kufuata Uislamu kama ulivyofunzwa au ulivyofundishwa na Mtume Muhammad na Qur'an yenyewe, nao hustahili kuitwa 'Makafiri' Kwa mfano; Waislamu wa Ahmadiyya, Waislamu wa Shia Rafidha, Ismailia n.k.

Natumai, maoni haya yamebainisha ufahamu wangu wa neno Kafiri.

Mbele said...

Ndugu Khalfan Abdallah Salim
Shukrani kwa ujumbe wako. Ukimsikiliza muumini wa dini nyingine, kama vile u-Hindu, atakuambia kuwa msahafu wake ndio haswa neon la Muumba. M-Kristu naye atasema kwa dhati kuwa Biblia ndio haswa neno la Muumba.

Kutokana na ukweli huo, mimi msimamo wangu ni kuwa watu wa dini zote waheshimiane kikamilifu. Pasiwe na kudharauliana kwa sababu ya Imani zetu tofauti. Pasiwe na kubezana wala kushinikizana kwa namna yoyote.

Neno kafiri ni tusi. Mtu ana dini yake, kwa nini aitwe kafiri? Mtu anamtambua na kumtii Mungu kwa mujibu wa dini yake, kwa nini aitwe kafiri?

Kuwaita watu makafiri ni kuwatukana. Hakuna dini inayoturuhusu kuwatukana wenzetu. Kuna wakati nilikuwa mwanachama katika mtandao wa Facebook ulioitwa Radio Imaan. Ulikuwa ni mtandao wa wa-Islam.

Baadhi yao waliniita kafiri. Niliwasihi kwamba mimi ni m-Kristu, nina dini yangu. Niliwaambia kuwa neon kafiri ni tusi.

Hawakuacha kuniita kafiri. Mmoja wao skaniita kuffar, ambayo nadhani ni maana ile ile.

Kama mtu anakuambia kuwa unamtukana, jambo la uungwana ni kuacha. Hii ndio njia ya dini ya kweli. Ukimkosea mtu, unaomba radhi na unafanya kila juhudi kutorudia kosa.

Kwa namna hiyo hiyo, mimi naziheshimu dini zote. Hao Ahmadiyya, Shia, Ismailia, na kadhalika nawaheshimu, sawa na ninavyowaheshimu waumini wa dini nyingine yoyote.

Ninawaheshimu watu wanaobadili dini. Nawaheshimu watu ambao hawana dini. Ninawaheshimu wanadamu wote, na naheshimu haki ya kila binadamu kuwemo katika dini yoyote, au kubadili dini, au kuishi bila dini.

Msimamo wangu ndio njia tuliyo nayo ya kuepusha magomvi na vita za kipuuzi ambazo zinaitwa vita za kidini.

Mwl. Zanjabeel said...

Hili neno kafiri likitamkwa kama lilivyo kafiri watu hulichukia sana na hata kujengeana uadui na chuki,, lakini neno hili iwapo litafasiriwa kwa lugha ya Kibantu utakuta linajenga dhana nzuri na maelewano kati ya mtu na mtu mfano tukisema neno kafiri maana yake ni mpinzani dhidi ya mtu na mola wake au mtu na mtu au mtu na kitu fulani... Mfano tukisema CCM ni mpinzani wa CHADEMA hakuna atakaye shituka na kupandisha jazba... Lakini tukisema CCM ni kafiri dhidi ya CHADEMA hapo utakuta watu wanaamsha jazba na kusema tumetusiwa... kwahiyo shida ni watu kufahamu kiundani maana ya neno kafiri.

Stanley shedrack said...

Kakaka mkubwa Hassan waweza ukawa sahihi kadri ya maelezo yako lakini wenzetu waislamu waliokua wengi wanatuchukulia sisi wakristo kama makafiri kwa maana dini yetu haibudu mungu wa kweli kifupi yaani dini yetu haifai kabisa.Na hapa nipo karibu na msikiti namsikia mtoa mawaidha anawakataza waislamu kushirikiana na watu wasiokuwa waislamu.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...