Monday, September 24, 2012

Tamasha la Vitabu "Twin Cities" Linakaribia

Tamasha la vitabu liitwalo Twin Cities Book Festival litafanyika tarehe 13 Oktoba mjini St. Paul, Minnesota. Litafanyika kwenye sehemu maarufu iitwayo State Fairgrounds. Hii ni mara ya kwanza kwa tamasha hili kufanyika nje ya mji jirani wa Minneapolis. Nimeshiriki tamasha hili kwa miaka kadhaa, kama nilivyoelezea hapa na hapa.

Mimi kama mwandishi wa vitabu nimeshalipia meza. Hapa pichani ni vitabu vyangu nitakavyopeleka kwenye tamasha. Sasa nangojea tu siku ije, nikajumuike na wadau mbali mbali katika nyanja za uandishi, uchapishaji, uuzaji, na uchambuzi wa vitabu.  Nangojea kuwashuhudia tena maelfu ya watu wa hapa wakiwa katika heka heka za kuangalia vitabu, kuvinunua, kuongea na waandishi, wachapishaji, wauza vitabu, na kadhalika.

Friday, September 21, 2012

Tanzania Inaendelea Kufedheheka

Hapa kuna ujumbe kutoka Jumuia ya Nchi za Ulaya. Ujumbe unalalamikia mauaji ya mwanahabari Daud Mwangosi. Papo hapo, kati ya mambo mengine, ujumbe unaikumbusha serikali ya Tanzania umuhimu wa uhuru wa vyombo vya habari, uhuru ambao umeendana na uhuru wa watu kujieleza. Ujumbe unaikumbusha serikali ya Tanzania kufanya kila liwezekanalo kudumisha na kuendeleza uhuru huo.

Suali langu ni hili: Kwa nini serikali ikumbushwe umuhimu wa kulinda haki za binadamu, kama vile hili ni suala gumu sana kulielewa na kulizingatia? Na kwa nini serikali yenyewe haikutambua mara moja umuhimu huo ikawa imechukua hatua muafaka, hadi ikumbushwe na nchi za nje? Hii ni fedheha kwa nchi yetu. Hapa nimeongezea tu taarifa ya suala ambalo nililiongelea siku chache zilizopita katika ujumbe huu hapa.

Ujumbe wa  Jumuia ya Nchi za Ulaya ni huu hapa:



Tuesday, September 18, 2012

Tamko Dhidi ya Serikali ya Tanzania Kuhusu Uvunjwaji wa Haki za Binadamu

Nadhani wengi wetu tunafahamu kuwa kuna tamko linalosambaa mitandaoni dhidi ya serikali ya Tanzania, ambalo watu sehemu mbali mbali duniani wanasaini ili hatimaye lipelekwe serikalini, kuishinikiza kuheshimu haki za binadamu. Tamko lenyewe ni hili hapa.

Heshima ya Tanzania inaendelea kuchafuka ulimwenguni kutokana tabia ya serikali hii. Hiyo ni habari ya kweli, sio uzushi. Leo, nimesoma taarifa kuwa mkurugenzi mkuu wa UNESCO ametoa tamko kuitaka serikali ya Tanzania iwajibike katika kuchunguza tukio la kuuawa mwanahabari Daud Mwangosi. Taarifa ni hii hapa.



Sunday, September 16, 2012

Mwenyekiti Mjengwa Amtembelea Mjane wa Daud Mwangosi


Ndugu zangu,

Leo jioni nilifunga safari kwenda kumwona mjane wa marehemu Daud Mwangosi. Anakoishi ni maeneo ya Mwanyingo hapa Iringa.

Mjane amerudi juzi jioni kutoka msibani Tukuyu. Itika, jina la mjane wa marehemu, anawashukuru kutoka ndani ya moyo wake, wale wote waliomchangia na wanaoendelea kumchangia fedha kama pole ya msiba mkubwa uliomkuta. Na wote waliokuwa naye katika wakati huu mgumu. "

Mungu ndiye atakayewalipa"- Anasema Itika Mwangosi, mjane wa marehemu. Amerudi kutoka msibani akiwa hana cha kuanzia. Leo pekee tumefanya jitihada ya ziada kuhakikisha maji hayakatwi kutokana na bili iliyochelewa kulipwa kutokana na msiba wa ghafla wa Daud Mwangosi . Kutokana na michango yenu, kesho Jumatatu familia italipa deni la maji lisilozidi shilingi laki moja na nusu.

Nilichokiona kwa mjane wa Daud Mwangosi ni uhalisia wa hali aliyo nayo sasa. Anafikiria jinsi atakavyomudu kuishi na kuitunza familia. Alifarijika sana aliposikia amechangiwa kiasi cha fedha kinachozidi shilingi milioni tano hadi sasa. Anaamini, kuwa ataweza kupata pa kuanzia ikiwamo kutumia ofisi ya marehemu Mwangosi kwa shughuli za biashara ndogo aliyoifikiria. Anafikiri pia kufuga kuku, maana nyumba anayoishi ina eneo kubwa.

Na katika kumsaidia kumwongoza kwenye shughuli hizi za ujasiri amali, Mama Mfugale, mmoja wa wajasiri amali maarufu hapa Iringa amejitolea kumpa ushauri na kumwelekeza mjane wa marehemu namna ya kwenda mbele. Na katika siku chache zijazo, mjane wa marehemu atafungua akaunti NBC ambapo pia fedha mlizomchangia zitaingizwa humo ifikapo mwisho wa mwezi huu.

Dada Janet Mwenda Talawa hivi majuzi aliwasiliana nami na alikuja na ushauri wa mjane wa marehemu apewe mafunzo ya ku-edit mikanda ya video ili aweze kuitumia vema studio aliyoachiwa na marehemu mumewe kwa shughuli za namna hiyo. Nilifikisha wazo hilo, na mjane wa marehemu ameonyesha utayari wa kujifunza.

Mwana wa kwanza wa marehemu Mwangosi aitwaye Nehemia, tayari amesharipoti shuleni Malangali, huko anasoma kidato cha nne, anajiandaa na mitihani ya mwisho mwezi Oktoba. Na mtoto Hertsegovina ( Pichani) yeye yuko darasa la saba. Kesho kutwa anaanza mitihani ya kumaliza elimu ya msingi. " Usimfikirie sana baba yako kwa sasa, fikiri kuhusu mitihani yako. Hata baba yako alitaka sana msome na mfike mbali"- Itika, mjane wa marehemu Daud anamwambia mwanawe aliyekaa kando yangu.

Naam, kama mzazi, unaingiwa na huzuni kubwa unapomsikia mzazi mwenzako aliyeondokewa ghafla na mwenziwake akiyatamka maneno hayo kwa mwanawe.

Kumsaidia mjane wa marehemu kwa sasa , ni kama hicho kilichofanywa na waliojitolea kutoa senti zao. Ndio, ni michango yenu ndiyo ambayo leo imemwezesha mjane wa marehemu awe na hakika ya kupata maji nyumbani kwake, na ndio itakayomsaidia kupata pa kusimamia kwa kuanzisha biashara, ili asije kukatiwa maji tena, na umeme pia. Na watoto nao wawe na hakika ya mlo wao. Ni matumaini yetu.

Maggid Mjengwa,
Iringa.
0788 111 765

CHANZO: MJENGWA BLOG

Tuesday, September 11, 2012

Waalimu wa Idara Yangu, Chuoni St. Olaf

Hapa ni picha iliyopigwa siku chache zilizopita ya walimu wa idara ya ki-Ingereza katika Chuo cha St. Olaf. Nimefundisha katika idara hii tangu mwaka 1991. Kuanzia mwaka 1976 hadi huo mwaka 1991 nilikuwa mwalimu katika idara ya Literature, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Chuo cha St. Olaf kinatoa shahada ya kwanza katika masomo mbali mbali.

Walimu wengi niliowakuta katika idara hii hapa St. Olaf wamestaafu. Waliobaki, ambao wamo pichani, ni watano tu, na mwingine, wa sita, hayupo katika picha hii. Nimekuwa mwalimu pekee kutoka Afrika tangu ule mwaka 1991, na sasa nami nimeanza kuwazia suala la kustaafu, ili nirudi Tanzania nikiwa bado na umri wa kuendelea na kazi za taaluma.

Monday, September 10, 2012

Ziara Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki, Songea

Kama nilivyoelezea tena na tena, napenda kutembelea vyuo ninapokuwa Tanzania. Soma kwa mfano, hapa. Ni fursa ya kujiweka sawa katika ufahamu wa nini kinachoendelea, changamoto zilizopo, mikakati ya kuboresha elimu ya juu. Napata fursa ya kujadiliana na wahusika namna ya kushirikiana na kuchangia vyuo hivi. Tarehe 21 mwezi Julai, mwaka huu, nilitembelea tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin, mjini Songea. Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustin ni mradi wa Kanisa Katoliki Tanzania. Ni mtandao ambao tayari una vituo sehemu mbali mbali za nchi. Kwa taarifa zaidi, soma hapa.

Hapa kushoto naonekana na Profesa Donatus Komba, makamu wa mkuu wa chuo hicho mjini Songea. Yeye ndiye alikuwa mwenyeji wangu siku ya ziara yangu, akinitembeza kila mahali na kunipa maelezo.








Hapa kushoto naonekana nikitia sahihi katika kitabu cha wageni.


Hapa kushoto ni jengo la utawala. Chuo cha Mtakatifu Augustin kina mipango mikubwa ya kupanua mtandao wake. Kwa upande wa Songea, tayari Seminari Kuu ya Peramiho imeshafanywa sehemu ya Chuo Kikuu, kwa masomo ya falsafa. Wanaofahamu taratibu za seminari za Katoliki wanajua kuwa tangu zamani, mapadri walitakiwa kusoma masomo ya kawaida tunayosoma sisi wengine, na baada ya hapo kwenda seminari kuu kusomea masomo ya teolojia na falsafa.  Basi Peramiho sasa ni sehemu ya Chuo Kikuu, kwa masomo haya ya falsafa.

Kanisa Katoliki jimbo la Songea limetoa majengo yaliyowezesha chuo hiki kuanzishwa. Chuo kina mipango ya kuongeza majengo. Nilionyeshwa sehemu mbali mbali, kama vile madarasa, kumbi kubwa, na maktaba. Nilivutiwa kusikia kuwa, mapadri wastaafu wamekuwa wakichangia hazina ya vitabu vyao katika juhudi za kuitajirisha maktaba.


Tayari, chuo kikuu cha Songea kinaendesha masomo ya aina mbali mbali. Mimi kama mwalimu wa "Literature" nilifurahi kusikia kuwa hilo ni somo mojawapo katika chuo hiki, na nilifurahi kukutana na mhadhiri wa somo hili.



Kwamba hiki ni chuo cha Kanisa Katoliki haimaanishi kuwa wanaosoma, kufundisha, au kufanya kazi hapo, ni wa-Katoliki tu. Chuo hiki kinawapokea watu wa dini na madhehebu mbali mbali. Angalia, kwa mfano, orodha ya wanafunzi wapya kwa mwaka huu.

Nilijifunza mengi katika ziara yangu hii, na hapa juu nimetoa dondoo chache tu.







Mdau jipatie taarifa zaidi kwa kuangalia video hii inayoelezea ufunguzi wa chuo hiki:

 

Sunday, September 9, 2012

Mwangosi Aliuawa Hivi: Simulizi ya Shahidi

Mwangosi aliuawa hivi
•  SIMULIZI YA SHAHIDI

na Mwandishi wetu

SEPTEMBA 2, 2012, polisi waliua kikatili mwandishi wa habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, katika Kijiji cha Nyololo, mkoani Iringa. Alikufa mbele ya Kamanda wa Polisi mkoani humo, Michael Kamuhanda, wakati polisi hao walipovamia ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ili kuwatawanya wasifungue tawi la chama chao katika kijiji hicho.
Mmoja wa watu walioshuhudia tukio zima, ni mwandishi wa Tanzania Daima, Abdallah Khamis. Ifuatayo ni simulizi ya kile alichokiona wakati polisi wanaondoa uhai wa Mwangosi.
SIKU hiyo asubuhi tulipata taarifa kuwa Kamanda wa Polisi mkoani humo (RPC), Michael Kamuhanda, alipanga kukutana na waandishi wa habari majira ya saa 2.30 ambapo waandishi walifika akiwemo Daudi Mwangosi.
Tukiwa katika chumba cha mikutano katika jengo la polisi Mkoa wa Iringa, Kamanda wa mkoa huo, alifika akiongozana na maafisa wake wawili na kuanza kutusomea taarifa ya zuio la mikutano ya CHADEMA iliyokuwa iendelee siku hiyo baada ya kupisha zoezi la awali la sensa.
Alitusomea zuio hilo na kutuambia hata viongozi wa CHADEMA wameshataarifiwa usiku wa Septemba Mosi. Tukamuuliza mbona taarifa za sensa zinaeleza kuwa kuna mafanikio kwa asilimia 95 na waliobaki wanatakiwa waende kwa viongozi wao? Akatujibu kuwa hilo ni agizo na linapaswa litekelezwe na CHADEMA.
Waandishi hawakuchoka kumuuliza maswali RPC na moja ya maswali yaliyoonekana kumkera kamanda huyo ni lile lililotoka kwa Daudi Mwangosi kuwa mbona wakati wa mwanzo walipozuia mikutano ya CHADEMA mkoani humo mikutano mingine ya CCM ndani ya mkoa huo na sehemu nyingine nchini ilikuwa inaendelea.
Swali lingine la Mwangosi lilimtaka kamanda huyo kutumia busara katika hali iliyopo kwa lengo la kuepusha maafa yanayoweza kutokea endapo angeendelea kushikilia msimamo wake kuwa hakuna mkutano wa aina yoyote utakaofanyika.
Baada ya maswali hayo, tulimuona Kamanda Kamhanda akiwa amekunja sura kama ishara ya kuchukizwa na maswali ya Mwangosi ambaye aliongeza swali lingine kwamba, “inaonekana Kamanda umechukia kutoka ndani ya moyo wako” na kamanda akajibu “ni lazima nichukie na nawachukia hawa CHADEMA kwa kuwa ninaipenda kazi yangu na pia ninakaribia kustaafu na sitaki kustaafu vibaya.”
Baada ya hapo maafisa waliokuwa na RPC waliandika ujumbe kwenye karatasi na wakamfikishia mkuu wao, na baada ya muda mkutano huo ulimalizika huku kukiwa na kauli za utani wa hapa na pale kati ya waandishi wa habari na baadhi ya askari juu ya kwenda kuripoti matukio ya siku hiyo.
Tulipokuwa nje ya jengo, Mwangosi, kwa kuwa ni mwenyeji wa mkoa huo, alikuwa akitaniana na mmoja wa askari aliyevaa kiraia, ambaye alimwambia kuwa, “huko hakutakuwa na kujuana na kuna uwezekano wa watu kufa.”
Mwangosi alijibu papo hapo kuwa hilo haliogopi kwa kuwa kifo ni ada ya mja yeyote na kwamba ataogopa kama mtu atamuahidi kuishi milele.
Baada ya hapo, kila mmoja alitawanyika katika eneo lake, na majira ya saa saba mchana baadhi ya waandishi walikutana ili kuanza safari katika Wilaya ya Mufindi kwa ajili ya kuripoti mkutano wa ndani wa CHADEMA na ufunguzi wa matawi.
Waandishi wa habari hao pamoja na mimi ni Godfrey Mushi (Nipashe), Olver Motto (Star Tv), Renatus Mutabuzi (ITV), Clement Sanga (Mwananchi), Joseph Senga (Tanzania Daima) na Tumaini Makene (Ofisa Habari wa CHADEMA).
Tulipofika katika mji wa Mafinga, tulipata chakula cha mchana kabla ya kwenda katika Kijiji cha Nyololo, na muda wote huo Mwangosi alikuwa hajaungana nasi.
Tuliondoka Mafinga kuelekea Nyololo huku mwenzetu Clement Sanga akiwasiliana na Mwangosi aliyesema yuko katika basi na angeungana nasi tukiwa Nyololo. Tulipofika pale tuliona askari wachache wakiwa wamesimama barabarani huku gari lao moja likiwa linajaza mafuta katika kituo cha mafuta kilichopo eneo hilo.
Tukiwa njia ya kwenda Mbeya, mita kama 100 kutoka katika mji wa Nyololo, kushoto kwetu tuliziona ofisi za CHADEMA zikiwa zimepambwa kwa bendera nyingi, na kulia kwake tuliona magari manne ya askari waliokuwa na silaha.
Baada ya kupita eneo hilo, gari moja la polisi lilikuwa likitufuata, na hapo tulishauriana kugeuza gari kurudi katika eneo la mji. Tulipofanya hivyo, na gari la polisi lilisimama.
Wakati tunarudi katika eneo la mji, tuliegesha gari pembeni. Baadhi ya waandishi wa habari waliingia mitaani kwa makubaliano kuwa baada ya dakika 10 tuwe tumerejea kwa ajili shughuli iliyotuleta - kushuhudia ufunguzi wa tawi hilo jipya la CHADEMA.
Muda huo ulipofika, tulirejea, lakini Mwangosi alikuwa hajaungana nasi. Baadaye tulianza kuona baadhi ya magari yakiwa na bendera ya CHADEMA yakipita moja baada ya jingine.
Kuwasili kwa Mwangosi eneo la Nyololo
Saa 10.22 Mwangosi aliwasili kwa basi ambalo sikumbuki kama ni Hood au Abood; na muda huo huo tukawaona askari wakiyatoa magari yao kutoka mafichoni na kuingia upande wa kulia wa mji wa Nyololo kwenye ofisi za kata za CHADEMA.
Wakati askari wakiwa wanapita walikuwa wakisema Dk. Slaa anatokea eneo la Wami. Waandishi wa habari wakawa wamejiandaa kwenda kwa kufuata njia hiyo.
Tuliegesha gari letu mbali. Mwangosi ambaye hakuwepo awali, akataka kuchukua pikipiki ili awahi. Kwa kuwa muda huo nilikuwa naye, nikamsihi kuwa hana haja ya kuingia gharama kwa kuwa gari la waandishi wa habari lipo. Akanielewa, na tukaingia katika gari hilo, huku akiwa amempakata Oliver Motto wa Star Tv.
Tulipoenda kama mita 50 hivi, tulikutana na msafara wa CHADEMA ukiwa unaelekea tunakotoka. Gari la waandishi wa habari na magari ya polisi yakalazimika kukaa pembeni kuyapisha, kisha wakaungana nao kuelekea katika ofisi za tawi za chama hicho.
Ofisi za tawi za CHADEMA katika mji huo wa Nyololo zipo mita zaidi ya 100 upande wa kushoto wa bararara ya kuelekea Mbeya. Awali polisi walikuwa wameegesha magari yao barabarani wakati CHADEMA wakielekea katika ofisi zao.
Hakukuwa na vurugu yoyote. Ghafla kiongozi wa polisi ambaye alikuwepo pale - tulimtambua kwa jina la Mnunka - aliwaamuru askari wake watoe ilani kwa kunyoosha bendera kubwa nyekundu juu na kuwataka CHADEMA waondoke katika ofisi zao. Tukapiga picha tukio hilo.
Wakati askari wakijiandaa kuwafuata wana CHADEMA katika ofisi zao, alitokea mtu aliyevaa shuka na kujifunga kitambaa kichwani ambaye baadaye alijitambulisha kama mkuu wa upelezi mkoa (RCO), akawaamuru wenzake waende katika ‘target’ lakini wasithubutu kutumia nguvu bila amri.
Hapa ndipo tulipoanza kupata wasiwasi ni nani anatoa amri kwa kuwa yule wa mwanzo, Mnunka alijiapiza kuwa wamechoka kuvumilia, na kwamba siku hiyo CHADEMA watawatambua. Hata tulipomuuliza maana ya kauli ile, hakutupa jibu la kueleweka.
Katika hali hiyo, mtu aliyejitambulisha kama ndie RCO alizungumza na viongozi wa CHADEMA, wao wakamwambia wako katika kikao cha ndani. Yeye akasema jukumu lake ni kuhakikisha usalama unakuwepo, na kwamba kama ni suala la kikao cha ndani hawawezi kuzuia.
Tulitaka kupata ufafanuzi wa masuala mbalimbali kutoka kwa RCO ambaye alikuwa akizungumza kwa simu na mtu ambaye baadaye ilikuja kubainika kuwa ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), akawa anamueleza kuwa hali ni salama. Alituahidi waandishi wa habari tuvute subira “kwa kuwa mwenye mkoa amewasili.”
Baada ya kuwasili kwa RPC Kamuhanda, Kamanda wa FFU, Mnunka alienda akamnong’oneza jambo. Pale pale, Kamuhanda akaonekana kukasirika. Akaagiza CHADEMA wasimamishe shughuli yao mara moja.
Tulitaka kujua tafsiri ya mkutano wa ndani kwa Jeshi la Polisi ni ipi, ni kwa wahusika kukaa ndani au ni ule mkutano utakaowahusisha wanachama peke yao kama ambavyo CHADEMA walikuwa wanasema pale. RPC akatujibu kuwa hilo halielewi na yeye si mwanasiasa.
Baada ya maelezo hayo, waandishi wa habari tulimbana RPC kwa maswali hata ikafikia hatua ya kamanda huyo kuanza kuwanyooshea vidole baadhi yetu, huku alimlalamikia Mwangosi kwamba kwanini hakushiba na majibu aliyopewa tangu asubuhi.
RPC akaniambia mimi kwamba nauliza maswali yanayopingana na mtazamo wa jeshi hilo; akamwambia Mutabuzi kuwa anamfahamu.
Baada ya hali hiyo, CHADEMA walimaliza mkutano wao katika ofisi za tawi na wakawa wanaelekea katika ofisi za kata. Gari lililotubeba lilikuwa nyuma ya gari la RPC ambaye baadaye dereva wake aliendesha kwa kasi kwenda mbele kutaka kuzuia msafara wa CHADEMA.
Lakini viongozi wa CHADEMA walikuwa wameshafika katika ofisi yao ya kata na tukashuka kwenda kushuhudia kinachoendelea. Hapo ndipo tulimkuta Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zanzibar, Hamad Yusuph na viongozi wengine wakisaini katika kitabu cha wageni.
Ghafla, RPC akatoa amri ya kuwakamata viongozi wa CHADEMA waliokuwa katika ofisi yao. Baada ya amri hiyo, wanachama wa CHADEMA waliokuwa pale wote walikaa chini wakinyoosha mikono juu.
Balaa linaanza kwa amri ya RPC Kamuhanda
Baada ya RPC kutoa amri hiyo, polisi walioipokea walianza kurusha mabomu ya machozi kuelekea sehemu waliyokaa wanachama wa CHADEMA. Mabomu hayo yalirushwa na kuumiza wengi, wakiwamo waandishi wa habari. Mimi nilipigwa na kitu chenye kishindo, nikajeruhiwa mkono wa kushoto na sehemu ya paja la mguu wa kulia.
Jitihada za polisi kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA zilifanikiwa. Baadhi ya watu na viongozi waliwekwa chini ya ulinzi, sisi tukiwa tunaendelea kufanya kazi yetu ya kukusanya taarifa ili kuhabarisha umma juu ya kile kinachoendelea katika eneo hilo.
Wakati hali hiyo ikiendelea, ofisi za kata za CHADEMA hazikuwa na mtu. Askari wakawa wanapiga mabomu kuelekea ndani ya ofisi hiyo tupu.
Tuliendelea kupiga picha tukio hilo. Ghafla askari mmoja akamgeukia mwandishi wa gazeti la Nipashe, Godfrey Mushi, akaanza kumpiga.
Baada ya kuona mwandishi huyo anapigwa, Mwangosi aliwasogelea askari akitaka kujua sababu za kumshambulia mwandishi wakati yupo kazini kama ambavyo askari hao walivyokuwa wakiwajibika.
Swali la Mwangosi likavuta askari wengine. Wakamzunguka na kuanza kumpiga kwa marungu, mateke na ngumi. Wakati hayo yakifanyika, RPC alikuwa pale anashuhudia.
Baada ya kuona kipigo kimekuwa kikali, Mkuu wa Kituo cha Polisi (OCS) cha Mafinga aliingilia kati kutaka kumnusuru Mwangosi.
Wakati Mwangosi akiwa anashambuliwa, mpiga picha wa gazeti la Tanzania Daima, Joseph Senga, naye alikuwa katika wakati mgumu baada ya askari kumdhibiti na kuanza kumpekua mifukoni, huku mwenyewe akijitahidi kujinasua mikononi mwao.
Mbali na mimi na Senga, muda huo hakukuwa na raia yeyote katika eneo lile, isipokuwa Godfrey Mushi wa Nipashe ambaye sina hakika kama alikuwa anafahamu kinachoendelea maana alikuwa amepigwa sana, yuko hoi.
Baada ya kuona kipigo kinazidi kwa Mwangosi huku Senga akiendelea kupiga picha, uzalendo ulinishinda, nikaamua kumfuata Kamanda wa Polisi mkoani humo aliyekuwa mita zisizozidi kumi ndani ya gari lake, akishuhudia tukio lile. Nikamuomba asaidie kumnusuru Mwangosi na kipigo kile.
RPC alishusha kioo cha gari lake, akaniangalia, kisha akafunga kioo, huku dereva wake akawa anapiga honi. Sikujua maana ya honi hiyo.
Baada ya kuona hakuna msaada wowote kutoka kwa RPC, nilisogea karibu kwa ajili ya kuendelea kupata picha ya tukio, ili umma ujue juu ya madhila yanayowapata waandishi wa habari mikononi mwa polisi.
Wakati nikiwa naendelea kuchukua picha, nilimwona askari mmoja akinyoosha mkono juu na mwingine aliyevaa kiraia akiwa ameshika bastola yake kuelekeza juu, huku wengine wakiwa wanaendelea kumpiga Mwangosi aliyekuwa anajitahidi kuinuka kwa kumshika mmoja wa askari wale.
Katika harakati za Mwangosi kujinasua, nilimshuhudia mmoja wa wale askari akiwa kama anainama akaelekeza mtutu wa bunduki usawa wa tumbo la Mwangosi aliyekuwa katika hali ya kutaka kusimama huku akipiga kelele “msiniuee, msiniuee…”
Mara nikasikia mlipuko mkubwa pale pale walipo; baadhi ya nyama zikarushwa na kutapakaa, nyingine zikanirukia mimi na kuchafua fulana yangu.
Kumbe walikuwa wamemlipua Mwangosi! Nikapiga picha ya mwili uliosambaratika na kukatika vipande vipande. Nikaona askari wale wanambeba askari ambaye naye alijeruhiwa na mlipuko uliomuua Mwangosi. Nikakimbia kujinusuru na askari wale.
Sikuona tena usalama wangu mbele ya polisi wake. Sikumwamini tena RPC kama angeweza kulinda maisha yangu. Nikatimua mbio kuelekea nisipopajua.
Nikiwa nakimbia nilichomoa kadi ya kamera kutoka katika kamera yangu ili nisipokonywe. Hapo ndipo nilipokutana na mwandishi mwingine, Francis Godwin, nikamwambia asielekee nilikokuwa natoka mimi – ambako ndiko alikuwa anataka kwenda - kwa kuwa Mwangosi ameshauawa na polisi!
Wakati naachana na Godwin, nilichukua simu yangu na kumpigia Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda, ambaye ndiye Mhariri Mtendaji wa gazeti hili kwa ajili ya kumpa taarifa. Bahati mbaya simu yake haikupokelewa.
Nikamfuata Makene (Tumaini, afisa habari wa CHADEMA) aliyekuwa amejikinga katika gogo, alikokuwa pamoja na Oliver Motto, nikawaambia eneo hili halitufai watatuua. Ndipo nikampigia simu Bakari Kimwanga, mwandishi wa gazeti la Mtanzania, nikamfahamisha kuwa Mwangosi ameuawa na polisi. Tukakimbilia porini kujificha, kila mtu akiwa analia kivyake.
Baada ya kukaa porini kwa muda, tuliamua kubadilisha nguo zetu ili tusitambulike kirahisi. Tukatoka mafichoni kuangalia hali ya usalama. Tukaanza kuwatafuta wenzetu ambao tulipoteana nao. Baadaye tulikodi teksi kuwafuata wenzetu ambao wakati huo walishakimbia kutoka eneo hilo la hatari.
Tukiwa katika hoteli ya MR mkoani Iringa, mwananchi mmoja alikuja kutueleza kuwa alifanikiwa kukusanya sehemu ya mwili wa marehemu Mwangosi pamoja na mabomu yaliyoachwa katika eneo la tukio na walipoangalia wakaona ni sehemu ya nyama ya utumbo iliyowekwa katika mfuko pamoja na mabomu ya machozi na kuyapanga yale mabomu juu ya meza ya hoteli hiyo na kuyapiga picha huku utumbo wa Mwangosi ukiendelea kuwa katika mfuko uliowekwa.
Hadi sasa sijajua endapo sehemu hiyo ya utumbo ilizikwa usiku ule mkoani Iringa au uliunganishwa na sehemu nyingine ya mwili wake uliotawanywa na bomu hilo kiasi cha kushindwa kujua kama ni mwili wa binadamu au ni ng’ombe aliyechinjwa tayari kwa mauzo.
Hivi ndivyo tulivyompoteza mwandishi mwenzetu, Daudi Mwangosi, akiwa mikononi mwa polisi.

Chanzo: TANZANIA DAIMA

Saturday, September 8, 2012

Mchezo wa "Pool," Lizaboni, Songea

Tarehe 21 Julai, wakati natoka Peramiho kurudi Songea, dala dala ilisimama kidogo kwenye kitongoji cha Lizaboni, ambacho ni sehemu ya Songea.

Hapo niliona mchezo wa "pool" unaendelea, nikapiga picha hii nikiwa ndani ya dala dala.

Friday, September 7, 2012

Kanisa Kuu la Peramiho

Hii ni picha ya kanisa kuu la Peramiho, ambayo nilipiga tarehe 21 Julai. Safari yangu ya Peramiho niliielezea hapa.

Wednesday, September 5, 2012

Nilizuru Nyumba za Ibada za wa-Hindu, India

Mwaka 1991 nilipata fursa ya kwenda India, kwa utafiti wa mwezi moja. Nilifikia katika taasisi ya American Studies Research Center, ambayo ilikuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Osmania, mjini Hyderabad. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuishi na wa-Hindi.

Siku moja, Afande Rana, mstaafu wa jeshi la India, alinichukua kwa piki piki yake, tukazunguka maeneo kadhaa ya Hyderabad. Alinipitisha katika nyumba kadhaa za ibada za wa-Hindu, kama inavyoonekana katika ukurasa huu.
 




Hapa kushoto tunaonekana mbele ya nyumba mojawapo ya ibada, tukiwa tumevaa vilemba.


Kwa bahati nzuri, ninasoma misahafu na maandishi mengine ya u-Hindu. Ninafahamu kiasi cha kuridhisha kuhusu historia ya dini hii, imani yake. Ni dini yenye miungu wengi, baadhi wanafahamika kwa kila muumini na kuabudiwa, na wengine hawafahamiki na kila muumini. Baadhi ya miungu hao wanachorwa wakiwa na umbo la wanyama. Kwa mfano mungu aitwaye Ganesha anawakilishwa na tembo, na mungu aitwaye Hanuman anawakilishwa na umbo la tumbili. Ndio maana hapa kwenye picha kushoto, ninaziangalia sanamu kwa uchaji.
 Hapa tuko mlangoni pa nyumba ya ibada. Tunapiga kengele, kabla ya kuingia. Sikuelewa maana yake, lakini nimesoma hivi karibuni kuwa huu ni utaratibu wa kuwafahamisha miungu kuwa umekaribia kuingia hapo.
Hapo kushoto naonekana nikitoa heshima katika nyumba hii ya ibada. Mhusika wa nyumba hii anaonekana akitabasamu, ingawa alijua kuwa mimi si m-Hindu. Ni ishara kuwa watu wa dini mbali mbali tunaweza kuheshimiana na kupendana bila tatizo.
Hapa naonekana nimekaa kwa heshima kabisa ndani ya nyumba ya ibada. Sikumbuki kama nilikuwa ninasali, au kama nilisali vipi, au labda nilikuwa nimegubikwa na mshangao kuwemo katika nyumba hii ya ibada ya dini ambayo sio yangu. Katika mazingira kama haya, mtu unaogopa kukiuka utaratibu, kwa hivi nadhani nilikuwa na woga fulani.
Hapa ninaonekana nikiendelea kutoa heshima katika nyumba hii ya ibada. Kwa kufanya hivyo, siamini kama nilikiuka imani yangu ya Katoliki. Niliwahi kukaribishwa misikitini katika mji wa Lamu. Niliingia kwa heshima zote, na bado mimi ni m-Katoliki. Nashukuru kupata fursa ya kuona nyumba hizo za ibada na hivi kujiongezea ufahamu kuhusu dini hizo. Kwa mtazamo wangu, hii ni njia moja ya kujenga maelewano na kuheshimiana miongoni mwa watu wa dini mbali mbali.

Tuesday, September 4, 2012

Itafakari Katuni Hii

Katuni hii nimeiona katika mtandao wa Facebook. Inamwonyesha mchora picha na mteja wake. Huyu mteja ni mu-Islam anayeonekana amekaa kwenye kochi, akiwa ameshika ua.

Mwangalie mteja huyu na halafu angalia picha iliyochorwa.

Nimeitafakari picha hii na bado naitafakari. Ninaona ina mengi ya kutufundisha. Je, mdau una maoni gani?

Monday, September 3, 2012

Nimekutana na Wanablogu Songea


Mwaka huu, kwa mara nyingine, nilifanikiwa kufika Songea, nikaonana na Ndugu Christian Sikapundwa, mmiliki na mwendeshaji wa blogu ya Tujifunze Kusini. Hii ilikuwa ni mara pili kukutana, kwani tulishakutana mwaka jana pia, kama nilivyoripoti hapa. Tulifurahi kukutana tena, tukabadilishana mawazo na kupiga michapo kuhusu mambo mbalimbali. Kwa vile sisi wote ni walim, tulikuwa na mengi ya kuongelea. Hapa kushoto tunaonekana tukijipongeza na kushukuru kwa kukutana.






Hapa kushoto tunaonekana tukiwa na mdogo wangu na binti yake.













Katika pita pita yangu kwenye eneo la Chuo Kikuu kipya cha Mtakatifu Augustin (SAUT),  tarehe 21 Julai, nilikutana na jamaa ambaye alijitambulisha kuwa ni Willy Migodela, mmiliki na mwendeshaji wa blogu ya mtandao-net. Nilifurahi kukutana naye, kwani mimi ni mmoja wa wadau wa blogu yake. Ni yeye aliyenitambua tulipoonana. Alisema kuwa alikuwa mwanafunzi katika darasa la uzamili la Profesa Mugyabuso Mulokozi, ambamo niliwahi kutoa mhadhara, kama nilivoelezea hapa. Wanafunzi wengine wa darasa lile wameshajitokeza kwangu na kujitambulisha, nami nafurahi sana.

Ndugu Migodela kwa sasa anafundisha chuoni SAUT. Nilikitembelea chuo hicho siku hiyo na Siku chache zijazo, Insh'Allah, nitaandika taarifa za ziara yangu hapo chuoni.

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Makala hii nimeshaichapisha mara kadhaa katika hii blogu yangu, na imewahi kuchukuliwa na kuchapishwa na mitandao mingine pia. Nimeona niiweke tena hapa.

 --------------------------------

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa. Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

 Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:  

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

Saturday, September 1, 2012

Ziara Kwenye Kanisa Kuu Peramiho

Tarehe 21 Juni nilitembelea Peramiho, mkoani Ruvuma. Peramiho ni kituo kikuu kimojawapo cha Kanisa Katoliki nchini Tanzania, tangu enzi za m-Jerumani, ambapo wamishenari walijenga kanisa hapa. Walianzisha hospitali, shule, vyuo vya ualimu, ufundi na uuguzi; shirika la uchapishaji, na mambo mengine muhimu kwa jamii. Hapa kushoto ni picha ya Kanisa Kuu linavyoonekana leo.








Pembeni mwa Kanisa kuna nyumba za mapadri na masista, na pia ofisi. Hata Abate/Askofu mstaafu anaishi hapa. Nilienda Peramiho ili kumwona, kwani sijawahi kumwona tangu mwaka 1970, nilipomaliza kidato cha nne katika Seminari ya Likonde, ambapo alikuwa mwalimu wangu wa Historia na ki-Ingereza. Niliambiwa amesafiri. Nje ya makazi yake nilipiga picha inayoonekana hapa kushoto, kwa kuvutiwa na sanamu ya Mtakatifu Benedikt. Maaskofu, mapadri, masista, na mabruda walioleta dini ya Katoliki Peramiho ni wa shirika la Mtakatifu Benedikt. Pamoja na dini, walijishughulisha na masuala ya afya, elimu, na ustawi wa jamii kwa ujumla.







Hapo kushoto naonekana ndani ya Kanisa. Kwa vile nililiona kanisa hili kwa mara ya kwanza nilipokuwa kijana mdogo, kuwepo tena hapa mahali kulinifanya nikumbuke miaka ya zamani.












Hapo hapo kwenye eneo la Kanisa Kuu niliona kijipango kinachoonekana kushoto, kikiwa na sanamu ya Bikira Maria. Kijipango cha aina hii tunakiita groto. Kwetu wa-Katoliki, groto ni sehemu ya ibada. Ingawa sio kanisani, huwezi kuwepo mahala hapo halafu ukawa unasogoa na marafiki zako au unatafuna njugu. Basi hapo niliona ni muhimu nipige picha pia, iwe kumbukumbu yangu.


Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...