Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:  

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii: Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.
-----------------------------------
Makala yangu hii hapa juu nimeshaichapisha mara kadhaa katika blogu hii. Ila nimeona niilete tena. Ikumbukwe tu kwamba wakati Mwalimu alipoandika, upinzani haukuwa makini na wenye nguvu kama ilivyo leo. Nyerere angekuwa hai leo, nina hakika angeungana na CHADEMA katika kupambana na ufisadi. Yeyote ambaye amefuatilia mawazo ya Mwalimu katika hotuba na vitabu vyake mbali mbali, atakubaliana nami kwa hilo.

Comments

Anonymous said…
MWALIMU NYERERE WALA HAKUOGOPA CCM ALIKUWA KIONGOZI NA JUKUMU LA KIONGOZI NI KUONYESHA NJIA ILIBIDI ATOE KITABU HICHO NA HAKIKUCHAPISHWA NCHINI KWANI KINGECHOMWA MOTO ALIKERWA NA UONGOZI WA RAIS MWINYI KWANI ALIPOJARIBU KUSHAURI ALIPUUZWA KUWA WAALIMU WENGINE WANAPENDA KUFUNDISHA TU HATA KAMA WATU WANAELEWA.UONGOZI WA MWINYI ULIONDOA SERA YA UJAMAA NA KUJITENGEMEA YA AZIMIO LA ARUSHA NA KUSIMIKA AZIMIO LA ZANZIBAR BILA SERA NYERERE ALIKUWA MWANA FALSAFA ALIWEZA KUTABIRI KESHO KUTWA ITAKUWAJE WANAOJIFANYA WANA WALSAFA WA TANZANIA HATA HIYO JUZI WAMEISHANGAA IKITOKEA NA WANAUPENDA UONGOZI TOFAUTI NA MTAZAMO WA NYERERE KUWA MWANAFALSAFA AKILAZIMISHWA KUONGOZA HUONGOZA KIPINDI KIFUPI NA KISHA KURUDIA KAZI YAKE YA UCHUNGUZI KAULI KALI ALIYOTOA MWL NYERERE NI PALE ALIPOONA MANJAGU[MAAFSA USALAMA WA TAITAFA WANAELEKEA KUCHUKUA NCHI CHINI YA NCCR MAGEUZI KIASI CHA KUSEMA HAWEZI KUIACHIA NCHI YAKE IONGOZWE NA MAMBWA] KUFIKIRI KUWA AKILINI MWAKE ALIKUWA ANAKITABIRIA CHAMA CHA CHADEMA UJIKO NI UWONGO MTUPU TUMEFIKIA HAPA TULIPO UDINI.UKANDA NA UKABILA KUTOKANA NA KAULI ZA KICHOCHEZI ZA CHADEMA NILITEGEMEA MAPROFESA WAWILI BAREGU NA KAHIGI WANGEJENGA CHAMA BORA SIVYO NI KAMA WAMEWEKEWA PLASTA MIDOMONI NI WALE WALE WALIOSHANGAA KUIONA JUZI IKITOKEA NDIO UTAWATEGEMEA KUKUTABIRIA KESHO KUTWA ITAKUWAJE NATUMAINI UTAONA KUWA NAKALA YAKO IMESOMWA IWAPO HUJARIDHIKA TOA MAONI YAKO SI YA NYERERE
Mbele said…
Ndugu Anonymous

Nakushukuru kwa kutembelea blogu yangu, kusoma ujumbe wangu, kuutafakari na kutoa maoni. Daima nawaheshimu watu wa aina hiyo. Ndivyo inavyotakiwa hapa duniani, iwapo kweli tunajali haki na uhuru katika masuala ya kutafuta habari na taarifa, kutafuta ukweli.

Mwalimu Nyerere hakuwa anakitabiria CHADEMA. Yeye hakuwa Mungu wala nabii. Isipokuwa, alielezea ndoto yake kwamba nchi ipate chama imara cha kuishinda CCM. Hakusema ni CHADEMA.

Kwa msingi huo, nilichotaka kusema ni kuwa kwa vile hali ilivyo sasa imedhihirisha kuwa CHADEMA ni chama imara, cha aina hiyo aliyokuwa akiiwazia Mwalimu, chenye msimamo wa kutetea maslahi ya nchi na rasilimali zake, naamini Mwalimu angekuwa upande wa CHADEMA.

Siamini kama angejiunga na CHADEMA, kwa sababu yeye alikuwa na imani na mwelekeo wa ujamaa. Hatuna chama cha kijamaa Tanzania. Hatuna chama cha mapinduzi. CCM inajinadi kuwa ni chama cha mapinduzi, jambo ambalo si kweli, kwani ni chama kinachohujumu mapinduzi.

Umesema nitoe maoni yangu, si ya Nyerere. Hapa tunapingana, kwani mimi huwa siweki mipaka katika jukumu la kutafuta taarifa na kuzisambaza, jukumu la kutafuta ukweli na kuusema. Siafiki wazo la kuzuia aina yoyote ya fikra, ziwe za Nyerere, zangu, au zako.

Kwa hivyo, kuleta maneno ya Nyerere kama nilivyofanya ni sahihi kabisa, kwa mtazamo wangu. Je, pengine sina maoni mimi mwenyewe, lakini nikaona kuwa haya ya Nyerere ni changamoto nzuri? Niache hata kuleta maoni ya wengine? Hii itakuwa ni kuhujumu uhuru ninaosemea.

Nimefanya sawa tu kuleta maneno ya Mwalimu Nyerere, ambayo sio yangu.

Hata hivi, napenda kuthibitisha kuwa maoni ya Nyerere mara kwa mara yamekuwa ndio maoni yangu, tangu nilipokuwa kijana. Ukipitapita katika blogu yangu hii, utaweza kuona ushahidi wa hilo.

Kuna pia kijitabu nimechapisha, kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii, ambacho ni mkusanyiko wa makala fupi mbali mbali. Kitabu hiki kinathibitisha bila wasi wasi jiinsi mawazo ya Mwalimu Nyerere yalivyochangia na yanavyoendelea kuchangia tafakari na misimamo yangu.

Mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Kuhusu wasomi hao wa CHADEMA, unaowasema kuwa hawajaleta mabadiliko katika chama chao, napenda nikukumbushe pia wasomi wa CCM. Mwaka 2010 wakati wa kampeni za uchaguzi, wagombea wote wa CCM walitoroka midahalo, wakiwemo wasomi wao.

Ilinishangaza kuona wasomi wanatoroka midahalo namna hii. Kwangu mimi kama msomi, nawajibika kusema kuwa kilichofanywa na CCM mwaka ule ni kitendo cha kijinga, chenye hatari kubwa kwa malezi ya watoto wetu, ambao ninapenda walelewe katika tabia ya kuheshimu elimu, mijadala, na mambo mengine yote ya kubadilisha mawazo.

Ningependa unipe mifano ya hizo unazoziita kauli za uchochezi za CHADEMA. Hapo umenikumbusha kilichotokea Arusha siku chache zilizopita, ambapo Mbunge Lema ametajwa na mkuu wa mkoa kuwa ni mchochezi. Ushahidi niliouona ni kuwa Mbunge Lema alienda kwenye chuo cha uhasibu akatuliza hali tete iliyokuwepo, pamoja na kufanikiwa kuwashawishi wanafunzi wasiandamane.

Halafu akaja mkuu wa mkoa akatibua mambo kwa matendo na maneno yake. Mkuu wa mkoa alijidhihirisha kuwa ndiye mchochezi, akawatibua watu na ikatokea hali tete. Sasa huyu mchochezi ndiye amepela mashtaka mahakamani kwamba Mbunge Lema ni mchochezi.

Kuna uzuri wa kuwa raia usiye na chama, kwani huna kipingamizi inapofika kwenye suala la kutafuta ukweli na kuusema. Siwajibiki kwa CHADEMA wala CCM.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini