Walimu Tunduru walia na mazingira duni ya kazi 

 

CHANZO: Blogu ya Maendeleo ni Vita

Na Albano Midelo


Baadhi ya walimu katika sekondari ya Frankweston Tunduru

MAZINGIRA duni ya kufanyia kazi yaliyopo katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma yanatajwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazosababisha wilaya hiyo kuwa duni katika elimu ya msingi na sekondari.

Hayo yamesemwa na baadhi ya walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo katika mahojiano maalum ya kutambua kwanini wilaya hiyo inakuwa ya mwisho kitaaluma katika wilaya zote za mkoa wa Ruvuma ambazo ni Songea vijijini,Songea manispaa,Nyasa,Mbinga,Namtumbo na Tunduru.

Teresphol Ngonyani ni mwalimu wa sekondari ya Frankweston anazitaja sababu za wilaya hiyo kuwa ya mwisho kuwa ni pamoja na maslahi duni ya walimu wanaoishi na kufanya kazi katika mazingira magumu kama ya wilaya ya Tunduru hivyo walimu wamepoteza moyo wa kufanyakazi.

“Kama moyo wa mwalimu umekufa kufanyakazi hata serikali ingeleta wakaguzi kumi kila siku mwalimu hawezi kutoa elimu bora badala yake atatoa bora elimu na matokeo yake ndo tumeanza kuyaona kwa kuwa madhara ya walimu kugoma hayaonekani kwa urahisi kama ilivyo kwa madaktari kwa kuwa watu watakufa lakini walimu sasa wanatengeneza taifa la wajinga jambo ambalo ni hatari sana’’,alisisitiza.


Neema Mwakila mwalimu wa sekondari  Frankweston aliitaja sababu nyingine ambazo inaifanya wilaya ya Tunduru kuwa ya mwisho kitaaluma ni idadi kubwa ya wanafunzi kusomea katika chumba kimoja cha darasa ambapo hivi sasa kuna shule chumba kimoja kinakuwa na wanafunzi karibu 100 hali ambayo inasababisha ugumu katika tendo la ufundishaji na kujifunza.

Ally Chilowa mwalimu kutoka shule ya sekondari Mgomba anasema kutokana na mazingira duni ya kusomea yamesababisha wanafunzi wanaojiunga na elimu ya sekondari baadhi yao hupokelewa wakiwa hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu na kwamba wanafunzi wengi wanaosoma wana matatizo makubwa ya kusoma,kuandika na kuhesabu.

Edmund Ndunguru anasema mitihani yote ambayo inafanywa hivi sasa kuanzia shule za msingi na sekondari ni ya kiini macho kwa kuwa wizara inashusha wastani na kuonekana mambo ya  kisiasa kwa kuwa wanafunzi wanaofanya vibaya wanaongezewa alama ili waonekane wamepata alama nzuri,lakini katika hali halisi katika shule za msingi utafiti ukifanyika kuna idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu.

“Walimu kuanzia shule za msingi na sekondari katika nchi nzima nina uhakika wataalamu wangekwenda kufanya utafiti kwa kila darasa watakuta idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawajui kusoma,kuandika na kuhesabu hali hiyo inatokana na walimu kufa moyo wa kufundisha  kwa kuwa serikali imeshindwa kumjali mwalimu  kuanzia nyumba wanazoishi na maslahi yao’’,alisema mwalimu Teresphol Ngonyani.

Mwalimu wa shule ya msingi Mbarikiwa kata ya Ligunga tarafa ya Matemanga Ally Rashid kutokana na ubovu wa nyumba anayoishi ambayo inaweza kuanguka wakati wowote ameamua kuandika kwenye mlango “tatizo namba moja ni nyumba’’ hivyo serikali inatakiwa kushughulikia matatizo hayo kabla bomu la elimu halijalipuka anasema mwalimu huyo.

Terephol Ngonyani mwalimu wa sekondari ya FrankWeston ametaka serikali iache utani na walimu kwa kuhakikisha  inatekeleza madai yote ya walimu ambayo yanachangia kushusha kwa elimu.

Mwalimu Ally Chilowa  anasema Serikali ijitahidi  kuboresha maisha ya wananchi wake ili waweze kusomesha watoto wao hasa katika wilaya ya Tunduru ambayo wakazi wake wengi ni masikini wanashindwa hata kulipa ada na michango mbalimbali inayotakiwa shuleni.

Mwalimu Edmund Ndunguru anaishauri serikali iboreshe mfumo mzima wa ajira ya mwalimu, ili mwalimu awe na mwajiri mmoja badala ya hali ambayo ipo hivi sasa mwalimu anawaajiri zaidi ya watatu, anadai kuwa mwalimu ndiyo mtumishi wa umma ambaye ana hali mbaya ya maisha matokeo yake mwalimu anadharaulika katika jamii kutokana na maisha duni yanayosababisha kuwa na madeni mengi

“Mwalimu anayemlipa mshahara ni mwajiri mwingine,anayefanya naye mkataba wa kazi ni mwajiri mwingine na anayefuatilia utendaji kazi wake ni mwajiri mwingine,hivyo mfumo mzima wa elimu ufanyiwe marekebisho ili kufikia malengo ya millennia ambayo yanategemea sana elimu bora kwa watu wote’’,alisema.

Mwalimu Ally Chilowa anasema serikali inahusika moja kwa moja  na  kutoa fungu la pekee kwa walimu wanaoshi katika mazingira magumu ikiwemo wilaya ya Tunduru kwa kuwa waliahidi kutoa fungu ili walimu walimu wanaoishi katika mazingira magumu waweze kuishi maisha bora ambayo yatasababisha walimu kutoa elimu bora.

Kaimu Afisa elimu wilayani Tunduru Flavian Nchimbi amekiri miundombinu hafifu ya vyumba vya madarasa,nyumba za walimu na madawati ni miongoni mwa mambo ambayo yanachangia kuporomoka kwa elimu katika wilaya hiyo.

Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Tunduru Chande Nalicho amekiri mazingira duni katika wilaya hiyo yanachangia elimu duni na kwamba hivi sasa serikali inajitahidi kuboresha mazingira bora ya kufundishia kuanzia ujenzi wa vyumba vya madarasa,nyumba za walimu na kuongeza idadi ya walimu.

Halmashauri ya wilaya ya Tunduru ina jumla ya shule za msingi 145 kati ya hizo shule za serikali ni 144 na shule moja ni ya shirika la kidini ambapo shule za sekondari katika wilaya nzima zipo 23 kati ya hizo shule 21 ni za serikali na mbili ni seminari za shirika la kidini.

albano.midelo@gmail.com

Comments

Mbele said…
Kabla hatujaenda mbali, naomba nikumbushie kuwa hii Tunduru inayozungumziwa ina utajiri wa madini ya mbali mbali, ambayo hao wanaoitwa wawekezaji wanafaidika nayo, wakati wenyeji wa Tunduru wanasota hata walimu wanakosa nyumba.

Kuhusu utajiri wa Tunduru katika madini, kuna taarifa nyingi mtandaoni, kwa mfano soma hapa.

Popular posts from this blog

Kumbukumbu ya Kuzaliwa

Tenzi Tatu za Kale

Pesa za Majini