Kinana, CCM Wanapanga Njama za Kumvua Lissu Ubunge
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO (CHADEMA) TAARIFA KWA UMMA KINANA, CCM WANAPANGA NJAMA ZA KUMVUA LISSU UBUNGE MAHAKAMANI!!!
Dar es Salaam, 31 Mei 2013...
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimelaani vikali njama za
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana kufufua kesi
ya uchaguzi dhidi ya Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA), Mh. Tundu Lissu. Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa CHADEMA Dr. Wilbroad
Slaa amedai kwamba CHADEMA imekamata nyaraka zinazoonyesha kwamba Katibu
Mkuu wa CCM Kinana amewaelekeza waliowakuwa mawakili wa makada wa CCM
waliomfungulia Mh. Lissu kesi ya kupinga matokeo ya Uchaguzi wa Ubunge
katika Jimbo la Singida Mashariki mwaka 2010 wafungue rufaa katika
Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ili kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Kanda
ya Dodoma iliyotupilia mbali kesi ya makada hao wa CCM dhidi ya Lissu.
Kesi ya Mahakama Kuu ilitupiliwa mbali tarehe 27 Aprili mwaka jana.
Dr. Slaa alisema kwamba lengo la njama za Kinana na CCM ni kuhakikisha
kwamba Mh. Lissu anafutiwa Ubunge ili asiweze kushiriki katika mchakato
wa Katiba Mpya kama mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba litakalojadili na
kupitisha rasimu ya Katiba Mpya baadaye mwaka huu. Dr. Slaa alisema:
“Kwa kipindi kifupi ambacho amekuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni na Mbunge, Mheshimiwa Lissu amekuwa mwiba mkali kwa CCM
na Serikali yake ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Amefumbua macho
ya mamilioni ya Watanzania kuhusu masuala makubwa ya kikatiba na
kisheria kwa hoja zake Bungeni. Uelewa wake mpana wa masuala hayo na wa
Kanuni za Bunge umekuwa kikwazo kikubwa kwa CCM na Serikali yake pamoja
na uongozi wa Bunge kupitisha mambo yao kinyume cha sheria, Kanuni za
Bunge na maslahi ya nchi yetu. Uwepo wake ndani ya Bunge na ujasiri wake
katika kutetea hoja mbali mbali umemzuia Spika wa Bunge na uongozi
mzima wa Bunge kuwaonea Wabunge wa Upinzani na hasa CHADEMA. Mtu huyu
amekuwa adui mkubwa wa CCM ndio maana Kinana anataka aondolewe Bungeni
ili asiwepo kabisa katika mjadala wa Katiba Mpya Bungeni.”
Kwa
mujibu wa Dr. Slaa, mara baada ya Mh. Lissu kuwasilisha hotuba ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni juu ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria
tarehe 3 mwezi huu ambapo aliishambulia Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
CCM kwa kuvuruga mchakato wa uundaji wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa
lengo la kuhakikisha Mabaraza hayo yanakuwa ya wanachama wa CCM tu,
Kinana alimwita wakili wa kujitegemea Godfrey Wassonga wa kampuni ya
mawakili ya Wassonga Associates Advocates ya mjini Dodoma na kumwelekeza
afungue rufaa dhidi ya Lissu katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
haraka iwezekanavyo. Siku nne baadaye yaani tarehe 7 Mei, 2013, Wakili
Wassonga alifungua rufaa hiyo katika Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa
ya Tanzania mjini Dodoma.
Ijapokuwa rufaa hiyo inaonyesha
kufunguliwa na Shabani Itambu Selema na Paschal Marcel Hallu waliokuwa
walalamikaji katika kesi iliyotupwa na Mahakama Kuu, Dr. Slaa alidai
kwamba watu hao hawahusiki kwa namna yoyote ile na kufunguliwa kwa rufaa
hiyo. “CCM na mawakili wao wanawatumia tu wanakijiji hawa bila hata
kuwapa taarifa au kuwashirikisha kwa namna nyingine yoyote. Huyu Shabani
Itambu Selema amekula kiapo mahakamani Dodoma kwamba yeye na mwenzake
ambaye bado ni Katibu Kata wa CCM huko kwao, hawakuambiwa chochote juu
ya kufunguliwa kwa rufaa hiyo. Hawakutoa maagizo yoyote kwa Wakili
Wassonga kufungua rufaa kwa niaba yao dhidi ya Lissu; hawajamruhusu
Wakili huyo kupinga maamuzi ya Mahakama Kuu iliyoridhika kwamba uchaguzi
wa Mbunge Lissu ulikuwa halali; hawajamlipa Wakili Wassonga kwa ajili
hiyo. Huyu Wakili anafunguaje kesi au rufaa bila kuambiwa au kulipwa na
‘wateja’ wake? Kama huku sio kukosa maadili ya kiuwakili ni kitu gani?”,
alihoji Dr. Slaa.
Kuhusu ushiriki wa Kinana katika sakata
hilo, Dr. Slaa alisema kwamba mara baada ya rufaa hiyo kufunguliwa,
Wakili Wassonga alimwandikia Katibu Mkuu huyo wa CCM barua yenye kumbu
kumbu Na. NO/KM/CCM/01/2013 kwa ajili ya “MADAI YA MALIPO YA AWALI YA
SHAURI LA RUFAA KESI YA UCHAGUZI JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI SHABANI
ITAMBU SELEMA NA MWENZAKE DHIDI YA MH. TUNDU LISSU.” Barua hiyo
inamkumbusha Kinana juu ya ‘makubaliano’ kati ya Wassonga Associates
Advocates na CCM kuhusu kusimamia kesi ya wanachama hao wa CCM dhidi ya
Mh. Lissu ambayo baadae ilitupiliwa mbali na Mahakama Kuu. “Baada ya
shauri husika nilipata maelekezo kutoka kwa wanasheria wa CCM kwamba
tukate rufaa Mahakama ya Rufaa kazi ambayo tumekamilisha.” Wakili
Wassonga anamweleza Kinana “... katika shauri la mwanzo nilikuwa nalipwa
na CCM Singida Mkoa na hawakumalizia malipo.” Barua hiyo imeambatana na
hati ya madai ya malipo (invoice) kwa ajili ya ‘malipo ya awali’ ya
shilingi milioni mbili.
Dr. Slaa alidai kwamba kazi ya Lissu na
wabunge wa CHADEMA ndani ya Bunge inawatisha CCM na Serikali yake ndio
maana sasa Kinana anataka Lissu aenguliwe kwa kutumia Mahakama ya Rufaa
ya Tanzania. “CCM inatapatapa, Bungeni hapakaliki kwa sababu ya hoja za
Lissu na Wabunge wengine wa CHADEMA. Kila siku Bunge linaahirishwa ili
kukwepa mijadala mikubwa juu ya matukio muhimu yanayoisibu nchi yetu.
Njama za kuizima CHADEMA kwa kuipunguzia muda wa kuzungumza Bungeni
zimeshindikana; mikakati ya kuvuruga hoja za CHADEMA kwa kuingilia
hotuba za Kambi Rasmi ya Upinzani na kutaka sehemu za hotuba hizo
zifutwe zimegonga mwamba; vitisho vya Spika Makinda na Naibu Spika
Ndugai kuwasimamisha wabunge wetu hazijafua dafu. Sasa tuna taarifa
kwamba Kinana anataka kuwahonga majaji ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania
mamilioni ya fedha ili wamfutie Kamanda wetu Lissu ubunge. Naye
atashindwa pia.”
Akizungumzia hati ya kiapo ya Shabani Itambu
Selema ambaye alihama CCM na kujiunga na CHADEMA baada ya kesi yao
kutupiliwa mbali na Mahakama Kuu mwaka jana, Dr. Slaa alisema:
“Tutaishangaa sana Mahakama ya Rufaa kama itaisikiliza rufaa hiyo hata
baada ya aliyekuwa mhusika wa kesi ya msingi kusema kwa kiapo kwamba
yeye na mwenzake hawajakata rufaa bali ni mambo ya Kinana na CCM yake!”
Dr. Slaa alisema itakuwa ajabu kwa Mahakama ya Rufaa kusikiliza rufaa
iliyofunguliwa zaidi ya mwaka mmoja tangu Mahakama Kuu ilipotupilia
mbali kesi ya msingi. “Kwa mujibu wa kifungu cha 115 cha Sheria ya
Uchaguzi, Sura ya 343, Mahakama ya Rufaa inatakiwa kusikiliza rufaa
dhidi ya uamuzi wa Mahakama Kuu ndani ya kipindi cha mwaka mmoja tangu
rufaa ilipofunguliwa. Huyu Kinana na CCM yake wamesubiri mwaka umepita
tangu Mahakama Kuu ilipokataa kufuta matokeo ya Lissu ndio wafungue
rufaa. Kama huku sio kukanyaga spirit ya Sheria hiyo ni kitu gani?”,
alihoji Dr. Slaa.
Aliongeza kuwa katika kesi ya Mbunge wa
Arusha Mjini (CHADEMA), Mh. Godbless Lema aliyekuwa anashtakiwa na
wanaCCM pia, Mahakama ya Rufaa ilipiga marufuku wapiga kura ambao
hawakunyimwa haki zao za kupiga kura kufungua malalamiko ya kupinga
matokeo ya uchaguzi mahakamani. “Hata wino wa Mahakama ya Rufaa katika
hukumu ya Lema haujakauka Kinana na CCM yake wanataka Mahakama ya Rufaa
iyale matapishi yake kwa kusikiliza rufaa ya wapiga kura wanaodai kwa
kiapo kwamba walielekezwa na wakubwa wao katika CCM kufungua kesi
iliyokataliwa na Mahakama Kuu na sasa rufaa imefunguliwa kwa maelekezo
ya Kinana bila hata wao kujulishwa au kushirikishwa kwa namna yoyote
ile.”
Dr. Slaa alisema kwamba rufaa ya sasa inathibitisha
kauli inayodaiwa kutolewa na Rais Jakaya Kikwete juu ya Tundu Lissu
wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita ambapo Kikwete alidaiwa
kuwaambia wanaCCM mjini Singida kwamba ni afadhali Dr. Slaa achaguliwe
kuwa Rais kuliko Tundu Lissu kuwa Mbunge! “Kwa kazi zake ndani na nje ya
Bunge Lissu amethibitisha umahiri na uzalendo wake kwa Tanzania na kwa
chama chetu. Ametetea wabunge na viongozi wetu dhidi ya njama za CCM
kuwachafua kwa kuwafungulia mashtaka ya uongo mahakamani; ametetea
Watanzania kila mahali nchini, na ameelimisha wananchi kwa hoja zake
Bungeni. Ni mmoja wa Wabunge hodari, jasiri na wachapa kazi katika Bunge
hili. Huyu ndiye Mbunge ambaye Kinana na CCM wanataka aondolewe Bungeni
kwa mbinu za kishetani za aina hii. Hatutakubali na tunawataka
Watanzania wasikubali!”
Rufaa dhidi ya Lissu bado haijapatiwa
namba ya usajili licha ya kwamba imeshalipiwa ada ya kuifungulia na
tayari imeshapokelewa na Masjala Ndogo ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania,
Dodoma. Aidha, rufaa hiyo haijapangiwa majaji wa kuisikiliza wala
tarehe ya kusikilizwa kwake haijapangwa.
--------------------------------------------------- Dr. Wilbroad P. Slaa KATIBU MKUU CHADEMA
No comments:
Post a Comment