Ni muhimu kila mtu awe huru kutoa mawazo yake, kuliko kunyamazishwa. Wanataaluma katika saikolojia wanatufundisha kuwa ukandamizaji au unyamazishaji, kwa maana ya "repression," una madhara makubwa. Sigmund Freud, Carl Jung, na wafuasi wao ni kati ya wanataaluma hao.
Watu wakiwa huru kujieleza, wanapata ahueni kisaikolojia, na hii ni muhimu kwa afya ya mtu binafsi na kwa afya ya jamii. Kuhusu madhara ya "repression," hata wahenga walitahadharisha, waliposema "kimya kingi kina mshindo mkuu."
Wakati huu, wa-Tanzania wanapita katika kipindi kigumu sana, kutokana na mvutano uliozuka baina ya wapinzani wanaotaka kufanya maandamano nchi nzima kupinga kile wanachoita udikteta, na papo hapo, polisi, serikali, na baadhi ya raia hawataki maandamano haya yafanyike. Wengine wamesema watafanya maandamano yao ili kuyapinga yale mengine.
Ninaona hili si suala gumu. Wote wanaotaka kuandamana wapewe fursa ya kufanya hivyo, ili mradi wahakikishe kuwa maandamano yao ni ya amani, kama inavyotaka sheria. Sioni tatizo iwapo maandamano ya wapinzani yatafanyika sambamba na maandamano ya hao wengine.
Kitu rahisi ni waandaaji wa maandamano ya aina zote kukaa na polisi na kukubaliana utaratibu wa maandamano hayo. Kwenye mji kama Dar es Salaam, kwa mfano, wapinzani wanaweza kufanya maandamano yao Kinondoni, na hao wengine wakafanya maandamano yao Ilala. Sio lazima maandamano ya aina mbali mbali yafanyike katika mtaa huo huo na wakati huo huo. Jambo la msingi ni kutafuta namna ya kuwawezesha watu kuandamana kwa amani, kama katiba na sheria zinavyotamka.
Waandaaji wanaweza kujipanga kuhakikisha kuwa maandamano yao ni ya amani. Kwa mfano, waandaaji wa maandamano wanaweza kuwateua viongozi wengi wa maandamano. Kila kiongozi atakuwa na watu wake, kama vile kumi au hata ishirini, ambao ana wajibu juu yao, Hao wanakuwa pamoja wakati wa maandamano. Na kiongozi mwingine anakuwa na watu wake. Hata wakiwa waandamanaji elfu tano, hii inawezekana. Ninachopendekeza hapa ni utaratibu kama ule wa nyumba kumi kumi alioanzisha Mwalimu Nyerere, ambapo kila nyumba kumi zina kiongozi wake.
Sababu ya kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa maandamano hayaingiliwi na watu wasiohusika, kama vile vibaka. Wakati huo huo, polisi wawepo kusaidia kutoa ulinzi, kama inavyotaka katiba na sheria.
Maandamano ni haki ya wananchi wote. Ni muhimu kwamba tutafute kila njia ili kuhakikisha haki zisihujumiwe. Badala ya kuzuia maandamano na kuwatisha watu, jambo ambalo linajenga uhasama katika jamii, naona ni bora kukaa na kutafuta njia ya kuwezesha watu kutekeleza uhuru na haki zao na papo hapo kuhakikisha kuwa amani inadumishwa. Ninaamini kuwa hayo yote yanawezekana. Kwa ki-Ingereza tungesema kuwa hayo malengo mawili sio "mutually exclusive."